Dominika ya III ya Majilio,Mwaka C:tufanye nini basi?
Na Padre Joseph Herman Luwela - Vatican.
Mpenzi msikilizaji na msomaji wetu, hakika tumepambawa na huruma ya Mungu, Ni Dominika ya furahini (Dominica Gaudete), nabii Sefania katika somo I (3:14-18) anahubiri ‘hisia ya furaha, ‘imba ee binti Sayuni, piga kelele ee Israel kwa kuwa Bwana ameziondoa hukumu zako, amemtupa nje adui yako’. Wimbo wa katikati pia, ‘paza sauti piga kelele, maana Mt. wa Israel ni mkuu kati yako’ (Isa 12:2-6)… Unabii huu unatimia katika Kristo ambaye kwa kifo na ufufuko wake amemtupa nje adui mwovu na kuturudishia hadhi ya kuwa wana hivi kwamba hata Mt Paulo anaona hivyo-hivyo ‘furahini katika Bwana siku zote tena nasema furahini, Bwana karibu (Filp 4:4).
Tunapomsubiri mtu muhimu sana, bila shaka tunakuwa na furaha kubwa ndani ya mioyo yetu. Ndio maana punde anapokuja tu, kunakuwa na vigelegele, shangwe na nderemo. Mama mja mzito pia, huwa anamsubiri mtoto wake kwa furaha kubwa. Naye Abiria anayesubiri ndege au basi huwa na furaha fulani ndani ya moyo wake. Kabla ndege au basi haijafika kuna furaha inayokuwa imefichika ndani mwake. Kwa hiyo kuna furaha katika kusubiri. Kwa nini tufurahi leo? Ni kwa sababu tumekaribia sana kuadhimisha Noeli iliyo siku ya furaha hata kwa wasioamini… tunafurahi kwa sababu Mungu anakwenda kushuka kwetu katika ubinadamu wetu, anakuja ayachukue maovu yetu, anakuja ili afe na kwa kifo hicho sisi tupate uzima kisha tuwe nao tele (Yh 10:10b)… tunafurahi kwa sababu Mungu anakuja kuwa mtu ili mtu awe “mungu” (Mt. Anselmo)…….hapa ndipo tunaponogeshewa na Kauli mbiu ya Baba Mtakatifi Fransisko katika maadhimisho ya jubilee ya mwaka mtakatikfu 2025 inayosema “Matumaini hayatayariki.”
UFAFANUZI
Mpendwa tunafurahi kwa sababu Mtoto tunayemtarajia anakuja kuleta mageuzi ndani yetu, kubadili muono wetu, kurekebisha fikra zetu, kuzigeuza tabia zetu na kungazia akili zetu ili zimjue, zimpende, zimtumikie na mwisho zimfikie Mungu aliye asili ya kila lililo jema… tunafurahi kwa sababu Mungu katika Kristo anatujia na vifurushi vinavyong’aa vikibeba haki, uhuru na Amani… tunafurahi kwa sababu katika Kristo mwanadamu anatoka gizani, anatoka utumwani na kutembea kama mwana mpendwa katika uhuru kamili… Kuwa wakristo ni kuwa watu wa furaha. Dini yetu sio dini ya kuhuzunika, kulalamika na kulialia. Sote tunatamani kufurahi, furaha ya kweli ipo wapi? Yohane Mbatizaji analo jawabu anapoulizwa na makutano “tufanye nini basi?” anamtaka kila mmoja atimize wajibu wa kusaidia (kumpa kanzu asiye nayo na chakula pia), kutozidisha ushuru (mamlaka zione hitaji la ahueni kwa wananchi juu ya tozo mbalimbali kwa kubuni njia mbadala za kuongeza pato la serikali), askari wasidhulumu na wasiwabambikize watu kesi, wafanyabiashara wasidhulumu, sote tupendane… tutapata furaha.
Yohane Mbatizaji ni nabii wa ushuhuda, ‘huyo alikuja kwa ushuhuda, ili aishuhudie ile nuru, wote wapate kuamini kwa yeye. Huyo hakuwa ile nuru bali alikuja ili aishuhudie ile nuru’ (Yh 1:7-8). Nuru hiyo ni Kristo - mshumaa wa Pasaka, Nyota ya asubuhi.. Furaha yetu ni katika maisha hayo ya mwanga, yasiyo na kificho, hila wala giza.. maisha safi ya ukweli na utaua, uchaji na huduma.. maisha ya imani, matumaini na mapendo, uadilifu na uchamungu. Unywaji pombe kupindukia, mambo ya wanaume/wanawake kupita kiasi, uvutaji wa sigara na dawa za kulevya nk hakutupatii furaha ya kweli, yametuletea msongo wa mawazo, tumedhoofisha afya, tumekorofishana na wenzetu na kuwa wagomvi... Furaha halisi haipo katika mali, au vitu ila kwa kuwa na marafiki wengi, wema na wazuri… katika kulisikiliza neno la Mungu, kulishika, kuliishi na kutimiza mapenzi yake.
Furaha ni dalili ya uwepo wa ufalme wa Mungu katika moyo wa mtu. Mt. Paulo katika somo II (Filp 4:4-7) ili tufurahi tusijisumbue kwa neno lolote bali katika kila neno kwa kusali na kuomba pamoja na kushukuru. Tunaposali tunakutana na Mungu naye anatujalia mahitaji yetu, tunaposhukuru tunaonesha kujali na matokeo ya hayo mawili ni kujipatia moyo mwepesi wenye furaha takatifu. Mwisho, tufurahi katika Bwana kwa kuishi fadhila ya unyenyekevu kama Yohane Mb. Watu walipomshangaa wakiwaza-waza na kudhani yeye ni Masiha alijikatalia akasema ‘hapana’, Yeye hastahili hata kufungua tu kamba za viatu vya Masiha. Mimi na wewe tungejivuna tukidai sifa na utukufu. Majivuno ni mzizi wa dhambi unaotuweka mbali na Mungu sababu unatuondolea unyenyekevu. Yohane alipoulizwa yeye ni Kristo alikataa, akaambiwa ni Elia akagoma, akaambiwa ni nabii yule bado akakataa.
Mwisho akajitaja kama ‘sauti tu iliayo nyikani...’ Sauti ni muunganiko wa milio yenye ujumbe... ujumbe huo ukifika tu sauti nayo hufifia na kupotea na kinachodumu hapo ni ujumbe tu. Huenda ni ujumbe wa furaha au wa majonzi, kuwakuchoma moyo au kuhamasisha na hadhira huguswa kwa namna fulani. Yohane Mb ni sauti iliayo ikiandaa ujio wa Kristo, naye Yesu anapokuja Yohane anajivuta… ‘Basi hii furaha yangu imetimia, Yeye hana budi kuzidi, bali mimi kupungua’ (Yh 3:30).
Mara kadhaa maisha yetu yamejengwa katika mashindano tena wakati mwingine yasiyo na maana sana. Inafaa sana kuiga fadhila hii ya kujishusha kutoka kwa Yohane Mbatizaji. Ni unyenyekevu wa nafsi ndio uliomkweza hata Mama Maria Mt anapoimba Magnificat yake ‘kwa kuwa ameutazama unyenyekevu wa mtumishi wake kumbe tazama tokea sasa vizazi vyote watanisifu mwenye heri’ (Lk 1:48) na kweli, Maria anasifika kizazi baada ya kingine kuwa ni Mbarikiwa. Basi ndugu zanguni tuombe neema ya kufurahi katika Bwana furaha takatifu, naam “fanyeni yote ila msitende dhambi” (Mt. Augustine)…