Dominika ya IV ya Majilio. Dominika ya IV ya Majilio. 

Dominika ya IV ya Majilio:Mariam akaondoka siku hizo,akaenda hata nchi ya milimani kwa haraka!

Jamani NOELI ipo mlangoni…tunafanyaje!nguo,vyakula,vinywaji,muziki,zawadi, likizo…sawa! Pamoja na hayo tunyooshe viungo vyetu,tutoke vitandani mwetu, majumbani mwetu na sehemu zetu tunakoishi hasa kutoka katika mazoea na tabia mbaya badala yake tuungane na Maria KUTEMBEA KWA HARAKA, tusijicheleweshe njiani shetani anatuvizia,tuchangamke…mwendo wetu uwe wa imani thabiti “unayo heri aliyesadiki kwa maana yatatimizwa aliyoambiwa na Bwana.”

Na Padre Joseph Herman Luwela - Vatican.

Karibu Ndugu msikilizaji wa Radio Vatican katika Kipindi cha Liturujia ya Neno la Mungu, Domika ya IV ya Kipindi cha Majilio Mwaka C wa Kanisa. Mpendwa msikiliza ni ukweli usiopingika kwetu sisi tuaminio katika Kristo Bwana, Matazamio yetu ni makubwa, hamu ya mioyo yetu haielezeki, tuna kiu nafsini tukisubiri shangwe kuu inayotujia hivi punde kwa njia ya pango la Bethlehem…  Kisha Gabriel (nguvu ya Mungu) kuzungumza na Maria akimpa habari njema ya kuwa Mama wa Aliye juu na kwamba shangazi yake Eliza ni mjamzito Maria hakusubiri, alinyanyuka akajitupia mtandio wake na kutoka nje, huenda alisimama mlangoni akiitazama kwa mbali milima ya Yuda aliyopaswa kuivuka, halafu akavuta pumzi ndefu na kuzishusha na huku akimuomba Mungu moyoni mwake alizianza hatua kwa haraka!

Njia ni ngumu lakini hachoki, moyoni anasukumwa na mambo mawili, dogo ni la udadisi “Ni kweli? Shangazi yangu ni mgumba na umri umeenda yaani ajuza sote tunajua, halafu mzee, iweje jambo hili? Ngoja niwahi nikajionee” akaongeza hatua… lakini kubwa lilikuwa moyo wake wa kuhurumia na kusaidia “Ikiwa ni kweli mjamzito na ninavyomfahamu shangazi lazima anahitaji msaada, hana mtu zaidi ya mzee mwenzie Kuhani Zakaria acha niwahi…”  Anakwenda haraka.

UFAFANUZI

Mama wa huruma na mwenye kujali hivi anawezaje kudharau sala na maombi tunayotamani yafikie kiti cha enzi kwa njia yake? Mkristo mkumbatie Mama Maria katika yote na ushuhuda wako utakuwa dhahiri. Macho yake ni maangavu na mepesi kuona changamoto zetu na kuzishughulikia.. kutoka kwa binti huyu Sayuni tunafundishwa kujali, kupenda na kusaidia na sio tu kusema “Pole sana! Mungu akutie nguvu! hata hili litapita! tunakuombea!” au huko mitandaoni tunaweka changamoto ya mwenzetu halafu tunaandika “usipite bila kukomenti ‘amen’”. Safari ya Mama Maria ni maandamano ya kwanza kabisa ya Ekaristi Tak, ya pili ikiwa safari ya Bethlehem kwenye sensa, tumbo lake la uzazi likiwa Wonyesho (Monstrance) halisi akiipeleka faraja ya Mungu kwa ndugu zake. Asante Maria kwa zawadi ya Ekaristi, uzima wa roho zetu.. kwa njia yako tunapokea furaha, amani na ushindi…

Maneno ya Eliza kwa Maria “umebarikiwa wewe katika wanawake naye Mzao wa tumbo lako amebarikiwa” pamoja na ya malaika “Salamu uliyepewa neema, Bwana yu pamoja nawe” kutengeneza sala bora ya Salamu Maria, pamoja na mama tunasali kwa Mungu aliye asili ya neema na baraka zote. Tazama walivyopendeza, ni akina mama wa kawaida lakini furaha yao imewazidi wengi, wakubwa, maarufu, wenye vyeo na matajiri sababu Roho wa Bwana yumo ndani mwao… maongezi yao sasa, hadi raha! wanazungumza heri, baraka, neema, sifa Maria akimsifu Mungu akisema “moyo wangu wamwadhimisha Bwana!”.. wanapoonana wanaelewana, hawajitazami wao kama wao, wanamsifu Mungu, Eliza anamsifu Maria, Maria anamwimbia Bwana… mama zetu wapendwa, ni hamu ya mioyo yetu mnapokutana muongee lugha ya Maria na Eliza, lakini bila bahati na kwa masikitiko yetu hamjafaulu kuzungumza mema kwa kiwango chao, huwa mnazungumza nini? mwajua wenyewe, tuombe neema vinywa vyetu vinene mema, vibariki visilaani, visali visisengenye, vinene ukweli visidanganye, na kwa njia ya maneno yetu Mungu asifiwe na wenzetu wafarijike.

Tendo la Maria kumtembelea Elizabeth lilisababisha “magwiji” wakutane kwa mara ya kwanza na kuchati wakingali bado matumboni… kikao cha “malegend”, mmoja nabii wa Mungu aliye juu na mwingine Mwana wa Aliye juu.. wanasalimiana, wanafurahiana, wanazungumza sio kwa midomo bali kwa mioyo yao, kwamba likizo yetu ndefu imeisha, muda wa majukumu umefika, tuungane mikono, twende zetu tukaandike upya historia ya ulimwengu… malezi bora ya watoto huanzia tumboni, tunavyowapokea, kuwalea na kuzungumzana nao, wanasikia na kuonja… furaha au majonzi ya mama mjamzito humuathiri mwanaye moja kwa moja.shime akina mama wote na akina dada tutunze uhai na kuthamini uhai, kamwe usikubari kuua mtoto aliye tumboni mwako au hata kwa Jirani yako uhai ni zawadi adhimu nay a kwanza kwetu kutoka kwa Mungu na hapa sote tunawajibika kutunza uhai huu kwa namna yoyote awe mwanaume au mwanamke.

Bikira Maria alimtembelea Elizabeti
Bikira Maria alimtembelea Elizabeti

Jamani NOELI ipo mlangoni… tunafanyaje! nguo, vyakula, vinywaji, muziki, zawadi, likizo… sawa!  Pamoja na hayo tunyooshe viungo vyetu, tutoke vitandani mwetu, majumbani mwetu na sehemu zetu tunakoishi hasa kutoka katika mazoea na tabia mbaya badala yake tuungane na Maria KUTEMBEA KWA HARAKA, tusijicheleweshe njiani shetani anatuvizia, tuchangamke… mwendo wetu uwe wa imani thabiti “naye heri aliyesadiki kwa maana yatatimizwa aliyoambiwa na Bwana” (Lk 1:45)… Ni mwendo wa haraka pamoja na Maria kuyafanya mapenzi ya Mungu kadiri ya somo II (Ebr 10:5-10) “dhabihu na toleo hukutaka… ndipo niliposema tazama nimekuja niyafanye mapenzi yako Mungu”... Mwendo wetu wa haraka pamoja na Maria ni matumaini ya kutimia kwa unabii wa somo I (Mik 5:1-4) kwamba Mtoto ajaye atasimama na kulisha kundi lake kwa nguvu za Bwana na mtu huyu atakuwa amani yetu”… tutembee kwa haraka pamoja na Maria kwa kushika amri, kulisikia, kulisoma na kulitafakari neno la Mungu, matendo ya huruma, kusameheana na zaidi sana kupendana sisi kwa sisi.

Dominika ya 4 ya majilio:
21 December 2024, 10:41