Sherehe ya Bikira Maria Mama wa Mungu: Siku ya 58 ya Kuombea Amani Duniani
Na Padre Bona Maro, C.PP.S. Dar es Salaam
Utangulizi: Wapendwa Taifa la Mungu, leo ni mwaka mpya, tarehe 01/01/2025. Ni siku ya furaha, ni siku ya shangwe, ni siku ya shukrani kwa Mungu kwa kusafiri pamoja nasi kwa mwaka mzima tunaoumaliza. Herini na baraka tele kwenu nyote kwa mwaka mwaka mpya. Maadhimisho ya Siku ya 58 ya Kuombea Amani Duniani tarehe Mosi, Januari 2025 yananogeshwa na kauli mbiu “Utusamehe Makosa Yetu: Utupe Amani.” Huu ni mwaka wa Maadhimisho ya Jubilei kuu ya miaka 2025 ya Ukristo inayokita ujumbe wake katika roho ya matumaini. Hii ni siku ambayo Mama Kanisa anaadhimisha pia Sherehe ya Bikira Maria Mama wa Mungu; kwa kufungua Lango la Jubilei Kuu ya Miaka 2025 ya Ukristo: Mahujaji wa Matumaini! Tumrudishie Mungu sifa na utukufu kwa kutufikisha hadi siku hii ya leo. Leo ni siku ya nane katika Oktava ya Noeli, Mama Kanisa anaadhimisha Sherehe ya BIKIRA MARIA MAMA MUNGU. Tunapoanza mwaka, Mama Kanisa anaadhimisha sherehe hii ya Bikira Maria Mama wa Mungu, akitukabidhi sisi sote na mwaka huu mzima kwa Mama yetu Bikira Maria. Yeye ni Mama wa Mungu na pia ni Mama wa Kanisa linalosafiri. Yesu alitukabidhi kwa Mamaye ili kwa msaada wa maombezi yake tusafiri pamoja naye katika hija yetu hapa duniani kuelekea mbinguni kwa Mwanaye Yesu.
Katika sherehe hii kubwa, tumshukuru Mungu ambaye aliamua mwanaye apate mwili wa kibinadamu kwa njia ya Roho Mtakatifu ndani ya tumbo la Mama Bikira Maria. Kwa njia ya Mama yetu Maria, Yesu ameshiriki ubinadamu wetu ili nasi atushirikishe umungu wake. Tumwombe Mama yetu Bikira Maria azidi kutuombea kwa mwanaye katika mahitaji yetu mbalimbali ya mwili na roho ili sisi sote mwisho wa maisha yetu hapa duniani tuweze kupata tuzo ya kustahilishwa maisha ya Mbinguni kama Mama yetu Bikira Maria. Bikira Maria Mama wa Mungu, Theotokos (Mtaguso wa Efeso 431 AD). Fundisho la kwanza na la muhimu kabisa la Kanisa kuhusu Bikira Maria ni kwamba, “Bikira Maria ni Mama wa Mungu” Bikira Maria ni Mama wa Mungu kwa kuwa ni Mama wa Yesu Kristo ambaye ni Mwana wa Mungu, Nafsi ya pili ya Fumbo la Utatu Mtakatifu. Fundisho hili na ukweli huu unatoka katika Maandiko Matakatifu, kwanza kabisa wakati malaika Gabriel anampasha habari Bikira Maria kwamba atakuwa Mama wa Mungu, “Tazama utachukua mimba na kuzaa mtoto mwanamume na jina lake utamwita Yesu. Malaika akamjibu akamwambia, “Roho Mtakatifu atakujilia juu yako na nguvu zake aliye juu zitakufunika kama kivuli, kwa sababu hiyo hicho kitakachozaliwa kitaitwa kitakatifu, Mwana wa Mungu” (Lk 1:31, 35). Pia Bikira Maria anapomtembelea Elizabeth, Elizabeth anasema, “Limenitokeaje Neno hili hata Mama wa Bwana wangu anijilie mimi?” (Lk 1:43).
Kumbe aya zote hizi japo sio kwa wazi kwamba zinaeleza kuwa Maria ni Mama wa Mungu, lakini zaeleza kuwa Maria ni Mama wa Yesu, na Yesu ni Nafsi ya Pili ya Fumbo la Utatu Mtakatifu, hivyo pasi na shaka yoyote Kanisa lafundisha kuwa Bikira Maria ni Mama wa Mungu. Kupitia Bikira Maria, Yesu, anatwaa hali yetu ya kibinadamu, anatwaa asili yetu ya kibinadamu. Kwa kuwa alikwishakingiwa dhambi ya asili (Imaculate conception), Bikira Maria anapata neema hiyo ya kumpa mwanaye mwili wa kibinadamu. Yesu Mungu, kwa njia ya Roho Mtakatifu anatungwa mimba katika tumbo la Bikira safi asiye na doa, hivyo Bikira Maria anakua Tabernaklo iliyomhifadhi mwana wa pekee wa Mungu, Neno wa Mungu. Mtakatifu Athanasius anatuambia, “Kama Yesu asingetwaa hali yetu ya kibinadamu, asingeweza kutukomboa.” Kumbe ilimpendeza Mungu kwamba Yesu atwae hali yetu ya kibinadamu, katika mambo yote awe sawa na sisi isipokua hakutenda dhambi. Hivyo kwa kumtambua Bikira Maria kama Mama wa Mungu, haituelezei tu fundisho juu ya umwilisho, bali ni fundisho juu ya ukombozi wote wa mwanadamu. Katika historia ya kanisa, kumekua na uzushi mwingi kuhusu fundisho hili muhimu la kanisa kama ilivyo pia kwa mafundisho mengine ya kanisa. Wapo wazushi katika karne ya 5AD wakiongozwa na Nestorius ambao walipinga kuwa Bikira Maria sio Mama wa Mungu, na hivyo walikua tayari kumwita Bikira Maria ni Mama wa Kristo (Christotokos) kwa kuwa waliamini kuwa Yesu alikua na nafsi mbili zilizotengana, yaani Mwana wa Maria na Mwana wa Mungu.
Kanisa latufundisha kuwa Yesu ni Mungu, kwa nafsi (Divine person), mwenye asili mbili (two natures) ambazo hazitenganishwi (Hypostasis) yaani Mungu kweli na mtu kweli. Hivyo katika Mtaguso wa Efeso mwaka 431 AD, Kanisa likatangaza fundisho hili rasmi kuwa Bikira Maria ni Mama wa Mungu, kwa sababu alimzaa Yesu nafsi ya pili ya Mungu. Bikira Maria ni “Theotokos” yaani, “Aliyembeba Mungu” (KKK 495) na siyo Christotokos kama alivyofundisha Nestorius. Sherehe hii yaadhimishwa kila mwaka ifikapo tarehe 01 Januari. Katika sherehe hii ya Bikira Maria Mama wa Mungu (Theotokos) tunajifunza mambo yafuatayo. Kwanza: Yesu ni Mungu kweli na Mtu kweli, anashiriki ubinadamu wetu. Sherehe hii ya Bikira Maria Mama wa Mungu yatukumbusha juu ya kweli ya Imani yetu kwamba Yesu ni Mungu kweli na Mtu kweli. Kwa kuzaliwa na Bikira Maria, Yesu anatwaa asili yetu ya kibinadamu na kukakaa kati yetu. Hii yatueleza umoja tulio nao kati yetu sisi na Krito, ambaye kwa fumbo la umwilisho, yeye hakuona haya kutuita sisi ndugu zake (Ebr 2:11). Ndugu mpendwa, tunapoanza mwaka, tumwombe Yesu ambaye alikubali kutwaa mwili katika tumbo la Bikira Maria na akakaa kwetu, atusadie na sisi kuwa tayari kumwilishwa katika maisha ya watu wengine. Wapo watu wengi kati yetu wanaoteseka, wagonjwa walio mahospitalini na majumbani, wapo watoto wanaoteseka miataani, wapo wanaotupwa majalalani na wazazi wao, wapo wanaotengwa na ndugu na jamaa zao kwa sababu ya ulemavu nk. Yesu anatukumbusha kuwa, tayari kuwa ndugu, kati yetu sisi kwa sisi kwa kuvunja kuta zote za utengano na ubaguzi kati yetu. Tumwombe Mama yetu Bikira Maria atuombee kwa Mwanaye ili daima tuwe tayari kujitoa sadaka kwa ajili ya wengine.
Bikira Maria ni kielelezo cha Imani na utii kwa Mungu. “Ndiyo” ya Mama yetu Bikira Maria (Lk 1:38), anaposema “Tazama mimi ni mjakazi wa Bwana na iwe kwangu kama ulivyosema” yatufundisha juu ya utii, Imani, unyenyekevu na kujiachilia kabisa (Total surrender) kwa Mungu na mapenzi yake. Ndugu zangu, Bikira Maria anatufundisha kuwa daima tayari kusema ndiyo kwa mapenzi ya Mungu. Mapenzi ya Mungu si mapenzi yetu, yaweza kuwa kinyume kabisa na mipango na matarajio yetu. Tujifunze na kuomba neema ya Mungu ili tuweze kuyapokea mapenzi yake katika nyakati mbalimbali za maisha yetu. Pengine tunategemea mambo makubwa kwa mwaka huu, tuombe ili matarajio yetu, matamanio yetu, mipango yetu iwe kwa ajili ya sifa na utukufu wa Mungu, na pale ambapo mambo yatakuwa kinyume na matarajio yetu, tuyapokee na kuendelea kujikabidhi daima mikononi mwa Mungu. Tuwe tayari kusema, “ndimi mtumishi wa Bwana na iwe kwangu kama ulivyosema.” Tunapoanza mwaka pia ni wakati wa kukabidhi yote tutakayotenda kwa Imani na matumaini mikononi mwa Mungu tukiamini na kutumaini daima huruma na msaada wake na kutambua kuwa kwa nguvu, akili na uweza wetu hatutaweza kutenda jambo lolote jema, hatutaweza kufanikiwa tukiwa peke yetu. Tatu: Bikira Maria anatufundisha juu ya thamani ya uhai wa Mwanadamu. Tunapomheshimu Bikira Maria Mama wa Mungu, kanisa laadhimisha pia thamani ya uhai wa mwanadamu, na wito Mtakatifu wa kuwa Mama (Dignity of human life and Motherhood). Bikira Maria alimbeba Mwanaye Yesu Kristo katika tumbo lake, atufundisha thamani ya utu wa mwanadamu. Tunapoanza mwaka kwa kusherehekea sherehe hii kubwa, Bikira Maria anatukumbusha kuwa mabalozi wa kulinda uhai kwa gharama kubwa. Yeye alikuwa wa tayari kupokea wito wa kuwa Mama na akamtunza mwanaye tangu alipokua tumboni na akatembe naye katika safari nzima ya ukombozi wetu. Katika nyakati zetu hizi, wito huu mtakatifu umekuwa ukichezewa na kutothaminiwa kwa sababu mbalimbali. Kumekuwapo na wimbi kubwa la watu wanaoangamiza uhai kwa utoaji wa mimba na kutelekeza watoto wajalalani na mitaani. Tumwombe Bikira Maria Mama yetu atuombee kwa mwanaye ili tuepukana na dhambi hii ya kuangamiza uhai ambao kimsingi ni zawadi ya Mungu kwetu sisi wanadamu na hakuna yeyote aliye na mamlaka ya kuutoa au kuuharibu.
Nne: Bikira Maria Mama wa Mungu ni Mama yetu sote sisi tunaomwamini Yesu/ ni Mama wa Kanisa. Kwa nafasi ya pekee aliyo nayo Mama Bikira Maria, Mama wa Mungu, yeye anakuwa kwetu mama yetu sisi sote. Na hii ni kwa sababu, yesu mwenyewe akiwa pale msalabani alitukabidhi sisi sote kwa Mama Bikira Maria, “Mama tazama Mwanao” (Yoh 19:27). Hivyo Bikira Maria ni Mama wa sisi sote tulio ndani ya Kanisa linalosafiri. Tunaposherehekea sherehe hii kubwa kabisa katika kanisa tunaalikwa kutambua nafasi ya Mama yetu Bikira Maria katika historia ya wokovu wetu. Kanisa kwa kutambua hilo, limekua na ibada ya pekee kwa Mama yetu Bikira Maria. Tunaalikwa kila mmoja kuwa na ibada kwa Mama yetu Bikira Maria (Hyperdulia) ibada pekee kwa Mama yetu Maria, kwa kutambua nafasi yake katika historia ya ukombozi wetu. Zipo ibada mbalimbali kwa Mama yetu Bikira Maria kama vile kusali rozari takatifu, kusali kwa nia maalum kwa miezi ile ambayo kanisa limetenga kwa heshima ya Mama yetu Bikira Maria, tukimwomba asafiri nasi katika mwaka huu mzima, aliombee kanisa na viongozi wake, atuombee ulinzi neema na baraka kutoka kwa Mwanaye Yesu, atuombee amani, furaha, upendo na upatanisho katika familia, taifa letu na ulimwengu mzima. Tano: Mwaliko kuanza mwaka mpya na Mwenyezi Mungu. Tunaposherekea Sherehe hii ya Bikira Maria Mama wa Mungu mwanzoni kabisa mwa mwaka, tunajikabidhi kwa Mungu na kuwa tayari kusafiri naye. Katika somo la Injili Takatifu, tumesikia wachungaji walivyokwenda kwa haraka kumtembelea mtoto aliyezaliwa nao wakatoa habari waliyoambiwa juu ya huyo mtoto. Wachungaji wanafanya haraka kwenda kumtembelea mtoto Yesu aliyezaliwa. Bikira Maria tunaambiwa aliyaweka hayo yote akayatafakari moyoni mwake. Ndugu wapendwa, mwaka huu unapoanza tunaalikwa kumtembelea mtoto aliyezaliwa, na kumwomba akae nasi daima. Tunapotafakari juu ya mwaka uliopita tuna mengi yaliyo ndani ya mioyo yetu, yapo yaliyotuhuzunisha, yapo yaliyotufurahisha, yapo yaliyotukatisha tamaa, hapo yaliyotuinua. Tukiwa na Yesu, tutakua tayari kupokea nyakati na majira yote tutakayokutana nayo kama vile Mama Maria alivyoyapokea yote na kuyatafakari moyoni mwake. Katika yote Maria alikua mtulivu akimtumainia Mungu.
Sita: Bikira Maria ni ishara ya amani. Bikira Maria ni Mama wa Mfalme wa Amani. Ujio wa Yesu ulimwenguni ulileta utawala mpya wa Mungu kati ya watu wake, nao ulikua ni utawala wa haki na amani. Hivyo katika sherehe hii ya Bikira Maria Mama wa Mungu, Kanisa limeweka pia kama siku ya kuombea amani ulimwenguni (World day of peace). Tunapoanza mwaka, tunaalikwa kila mmoja wetu kuwa chombo cha amani. Kuwa balozi wa msamaha na upatanisho. Huenda mwaka ulipita tulisosana hapa na pale, tunaalikwa kuwa tayari kupokea msamaha na kutoa msamaha kwa wale waliotukosea na kwa wale tuliowakosea, zipo familia ambazo hakuna amani, wapo ndugu ambao wana ugomvi usiokwisha nk. Pia yapo maeneo mbalimbali ulimwenguni ambapo hakuna amani, hakuna mapatano, vita vya wenyewe kwa wenyewe, mapigano kwa sababa za kisiasa na uchu wa madaraka, tumwombe Yesu Mfalme wa Amani atujalie amani na mapatano ya kweli. Saba: Kumshukuru Mungu kwa makuu ambayo ametutendea. Wachungaji katika somo la Injili baada ya kumwona mtoto aliyezaliwa, wakarudi huku wanamtukuza Mungu na kumsifu kwa mambo yote waliyosikia na kuyaona kama walivyoambiwa (Lk 2:17-18). Ndugu zangu wapendwa, tunapoanza mwaka ni muda wa kusimulia na kutangaza makuu ambayo Mungu ametutendea kwa mwaka mzima ulioisha, tunatambua kuwa ni Mungu alitutendea mambo makuu, tumeona, tunashuhudia. Ni mbali tumetoka tangu Januari mpaka desemba, Hesabu baraka na neema alizokutendea, jinsi Mungu alivyokubariki, jinsi Mungu alivyokuinua, maisha yetu leo ni ushuhuda kwamba Mungu ni mwaminifu, tunaomba aendelee kutubariki maana kushukuru ni kuomba tena, na moyo usio na shukrani unafuta mema yote.
Somo la Pili linatuonesha kuwa Mungu ni mwaminifu kwa ahadi zake, ahadi alizonena kwa vinywa vya manabii anazitimiza wakati ulipowadia utimilifu wa wakati (Gal 4:4-5). Tunamshukuru Mungu kwa kuwa ni mwaminifu, huenda kuna mambo mengi ambayo Mungu amenena nawe kwa mwaka uliopita. Mshukuru kwamba alitimiza, lakini kama bado hajakujibu, ndugu mpendwa fahamu kwa hakika kuwa, wakati utimilifu wa wakati utakapowadia, Mungu anakwenda kusema nawe juu ya ahadi zake kwako. Mungu wetu ni mwaminifu, akatimizie yote aliyonena nawe. Mwisho: Pokeeni Baraka za Mungu kwa mwaka huu mpya unaoanza. Ndugu wapendwa katika somo la kwanza (Hes 6:22-27), ni baraka na kikuhani inayotolewa na Mungu mwenyewe kwa Musa ili anene na Haruni na wanawe. Ndivyo Mungu anavyowabariki nanyi nyote mnapoanza mwaka huu mpya wa Bwana. Bwana awabariki na kuwalinda: Baraka ni upendeleo kutoka kwa Mungu mwenyewe, kama alivyotupendelea licha ya kwamba hatustahili, aendelee kutubariki tena kwa mwaka huu. Awalinde na kila hatari za mwili na za roho, awakinge na hila na mitego ya mwovu shetani. Bwana awaangazie nuru ya uso wake na kuwafadhili: Kuangazia uso maana yake furaha, vile kama wazazi wanavyoonesha uso wa tabasamu kwa watoto wao, ndivyo Mungu atakavyokuangazia nuru ya uso wake kwa mwaka huu mzima. Bwana akawafadhili, tunapoanza mwaka Mwenyezi Mungu, Baba anayejua mahitaji yetu (Providential Father) akatimize haja za mioyo yetu, mahitaji yetu mbalimbali ya kiroho na kimwili. Bwana akuinulie uso wake na kukupa amani: Mwenyezi Mungu anawajali na upo karibu kabisa na watu wake (God’s attention and intimacy).
Mwaka huu wa 2025 wa Jubilei kuu ya Miaka 2025 ya Ukristo ukawe mwaka wa kuimarisha zaidi ukaribu wetu na Kristo Yesu kwa njia ya Neno la Mungu, Sakramenti za Kanisa pamoja na matendo ya huruma ili naye awe karibu kabisa nasi, ili atuinulie uso wake wakati wa shida na taabu zetu zote. Bwana akupe amani, neno Amani kwa lugha ya kiebrania ni Shalom, katika mwaka huu mwombe Mungu akupe amani na utulivu ndani ya nafsi yako, ndani ya familia yao, na utulivu na amani kati yako na Mungu. Mungu mwenye rehema akawabariki ninyi nyote. Hitimisho: Katika sherehe hii kubwa, tumshukuru Mungu ambaye aliamua mwanaye apate mwili wa kibinadamu kwa njia ya Roho Mtakatifu ndani ya tumbo la Mama Bikira Maria. Kwa njia ya Mama yetu Maria, Yesu ameshiriki ubinadamu wetu ili nasi atushirikishe umungu wake. Tumwombe Mama yetu Bikira Maria azidi kutuombea kwa mwanaye katika mahitaji yetu mbalimbali ya mwili na roho ili sisi sote mwisho wa maisha yetu hapa duniani tuweze kupata tuzo ya kustahilishwa maisha ya Mbinguni kama Mama yetu Bikira Maria.