Sherehe ya Familia Takatifu Mwaka C:Familia ni msingi wa maisha ya furaha na amani
Na Padre Paschal Ighondo – Vatican.
Tafakari ya Neno la Mungu, katika sikukuu ya Familia Takatifu ya Yesu, Maria na Yosefu. Ndivyo wimbo wa mwanzo unaofungua maadhimisho ya sherehe hii unavyoashiria ukisema hivi; “Wachungaji wakaenda kwa haraka wakamkuta Maria na Yosefu, na yule mtoto mchanga amelala horini” (Lk. 2:16). Sherehe hii inaweza kuadhimisha Jumapili katika Octava ya Noeli au tarehe 30 Disemba kama katika Octava hakuna Jumapili. Ni katika mwaka wa 1921, Baba Mtakatifu Benedicto XV ndiye aliyetangaza kuwa jumapili katika oktava ya kuzaliwa Yesu Kristo, au tarehe 30 desemba itakuwa ni sherehe ya Familia Takatifu. Katika sherehe ya Kristo Mfalme mwaka 1981, Baba Mtakatifu Yohani Paulo II katika waraka wa kitume “familiaris consortio” – Ushirika wa Familia, akieleza wajibu wa familia ya Kikristo kwa Kanisa na ulimwengu - alisisitiza umuhimu wa familia katika malezi ya watoto na ujenzi wa Kanisa na taifa akisema; Familia ni kitalu cha kanisa na jamii kwa ujumla. Ili jamii na Kanisa lifanikiwe ni lazima kuwe na msingi mzuri katika familia ambayo ndio inaathiri tabia, mwenendo na maisha ya wanajamii. Hivyo basi; Familia ni Kanisa la nyumbani. Familia ni shule ya sala. Familia ni shule ya upendo. Familia ni shule ya amani na mshikamano. Familia ni makao ya furaha na kitalu cha uhai.
Familia Takatifu ni ile ya kumpendeza Bwana, ni familia inayodumu katika pendo la Mungu, imejaa amani tele na baraka za mwenyezi Mungu. Familia ya Yesu, Maria na Yosefu inawekwa mbele yetu kuwa mfano wa familia zetu ambao kwao unatuonyesha namna zinavyoweza kuiishi vyema furaha ya upendo katika familia na tiba kwa zile zilizojeruhika kwa kukosa upendo kama anavyosisitiza Papa Francis katika Amoris laetitia – Furaha ya Upendo. Ndiyo maana, katika hitimisho la waraka wake juu ya ufuasi wa familia katika ulimwengu wa sasa, Baba Mtakatifu Yohani Paulo II aliziweka familia zote chini ya ulinzi na usimamizi wa Yesu, Maria na Yosefu. Lengo kuu la kuadhimisha sherehe hii ni kuziombea familia zote zikue na kuishi kwa mshikamano zikimpendeza Mungu, zikidumu katika pendo lake, ziweze kujaa amani tele na baraka za mwenyezi Mungu ziwe ndani mwao daima. Zaidi sana kujifunza na kuiga mfano bora wa hii familia kama tunavyoomba katika sala ya mwanzo; “Ee Mungu, umependa kutuonyesha mifano bora ya Familia Takatifu. Utujulie kwa wema tuweze kufuata mifano ya hiyo Familia Takatifu katika fadhila za nyumbani na kuungana kwa mapendo.” Tunaomba fadhila ya upendo ambayo ni kiini cha furaha ya familia kama maneno ya mwanzo katika waraka wa kichungaji wa Papa Francis juu ya maisha ya familia yanavyoashiria; Amoris letitia, furaha ya upendo. Kwamba katika magumu yote; upendo unaleta furaha.
Tunapoongelea familia hapa ni vyema tukafahamu maana halisi kadiri ya mpango wa Mungu kuwa; Familia ni muungano wa Mume na mke, unaofungamanishwa na upendo na tunda litokanalo na Upendo wao ni watoto ambao ni zawadi toka kwa Mungu na ndiyo inayowafanya waitwe wazazi; Baba na mama. Familia ni mpango wa Mungu (Mw. 1:26-28; 2:24). Tangu mwanzo aliwaumba mume na mke, Adamu na Eva, akawashirikisha uwezo wake wa uumbaji ili tunu ya uhai iendelee kuwepo duniani. Kumbe familia ni wito wa kuishi pamoja kwa wanandoa, kuendeleza kazi ya uumbaji na kuwezesha mwendelezo wa tunu ya uhai kwa kuzaa watoto, kuwalea na kuwaridhisha tunu zilizo njema. Familia ni kitovu cha uumbaji, shule ya kutambua mapenzi ya Mungu. Katika familia, Injili inapaswa kusomwa na kutafakariwa, liturujia inapata msingi wake kwa njia ya sala, nyimbo na sakramenti. Kiujumla, masomo ambayo mama Kanisa anatuwekea kuyatafakari katika sherehe hii yanatuongoza katika kutambua umuhimu na namna ya kuishi vyema maisha ya ndoa na familia.
Somo la kwanza ni la cha Yoshua Bin Sira (YbS 3:2-6, 12-14). Katika somo hili mwenye hekima anasema hivi; “Bwana amempa baba utukufu mintarafu wana, na kuithibitisha haki ya mama mintarafu watoto. Anayemheshimu babaye atawafurahia watoto wake mwenyewe, na siku ya kuomba dua atasikiwa. Anayemtukuza baba yake, ataongezewa siku zake; akimsikiliza Bwana, atamstarehesha mamaye. Mwanangu, umsaidie baba yako katika uzee wake; wala usipate kumhuzunisha siku zote za maisha yake. Akiwa amepungukiwa na ufahamu umwie kwa upole, wala usimdharau iwapo wewe u mzima sana; Kwa maana sadaka apewayo baba haitasahauliwa, na badala ya dhambi itahesabiwa kwa kukuthibitisha.” Hivi ndivyo maisha ya familia yanavyopaswa kujengwa kwa mahusiano mazuri kati ya wanafamilia yaani wazazi na watoto, wakiishi kwa amani na mapendo, huku wakimcha Mungu. Ni katika muktadha huu mzaburi katika wimbo wa katikati asema hivi; “Heri kila mtu amchaye Bwana, aendaye katika njia zake. Taabu ya mikono yako hakika utaila; Utakuwa heri, na kwako kwema. Mkeo atakuwa kama mzabibu uzaao, vyumbani mwa nyumba yako. Wanao kama miche ya mizeituni, wakiizunguka meza yako. Tazama, atabarikiwa hivyo, yule amchaye Bwana, Bwana akakubariki toka Sayuni. Uone uheri wa Yerusalemu, siku zote za maisha yako” (Zab. 128: 1-5).
Somo la pili ni la waraka wa Mtume Paulo kwa wakolosai (Kol 3:12-21). Katika somo hili Mtume Paulo anatoa wosia kwa kila mwana familia na miongozo ya namna ya kuishi vyema maisha ya kifamilia; wake kuwatii waume zao, waume kuwapenda wake zao na kutokuwa na uchungu nao, na watoto kuwatii wazazi wao. Zaidi sana kwa akina baba, anawasihi kutokuwachoza watoto, wasije wakakata tamaa. Sheria kuu ni hii, kufuata fadhila anazotufundisha Kristo; kujivika moyo wa upendo, rehema, utu wema, unyenyekevu, upole, uvumilivu, kuchukuliana, na kusameheana, kutokulaumiana, kujijengea moyo wa kusameheana. Zaidi sana kuwa watu wa shukrani. Na zaidi sana kila mmoja ampendeze Mungu kwa kutimiza wajibu wake katika familia. Ka kulitumia neno la Kristo linalokaa ndani yetu, kwa hekima yake, tundishane na kuonyana kwa zaburi, na nyimbo, na tenzi za rohoni; huku tukimwimbia Mungu kwa neema mioyoni mwetu. Na yote tufanyayo kwa neno au kwa tendo, tuyafanye katika jina la Bwana Yesu.
Injili ni ilivyoandikwa na Luka (Lk 2:41-52). Sehemu hii ya Injili inasimulia jinsi familia ya Yesu, Maria na Yosefu ilivyoshika amri na maagizo ya Mungu kuhusu siku za kuhiji, ibada na sala, kama vile kwenda “Yerusalemu kila mwaka, wakati wa sikukuu ya Pasaka”. Lakini pia inasimulia jinsi Yesu alivyobaki Hekaluni, nyumbani kwa Mungu Baba na jinsi wazazi wake walivyohangaika kumtafuta mpaka kumpata akiwa Hekaluni. Na baada ya kumpata walirudi naye Nazareti, “naye alikuwa akiwatii…akazidi kuendelea katika hekima na kimo, akimpendeza Mungu na wanadamu”. Kumbe tunaweza kutambua umuhimu wa ndoa na familia, kuwa hata Mungu alipoamua kushuka na kuwa karibu zaidi nasi watu wake, alikuja na kuishi katika familia.
Tunapaswa kufanya nini katika sherehe ya Familia Takatifu? Awali ya yote ni kumshukuru Mungu kwa zawadi na tunu hii kubwa hivi. Pili ni siku ya kuwashukuru na kuwapongeza wazazi na Walezi. Kila binadamu yuko jinsi alivyo kwa msaada wa familia yake au za wengine. Hivyo hatuna budi kuwakumbuka wazazi wetu na kuwashukuru. Lakini zaidi sana kuwaombea walio wazee Mungu awaimarishe katika uzee wao, huku tukiwasaidia katika uzee wao ili tujipatie neema na baraka mbele za Mungu. Kwa wale waliotutangulia mbele za haki tuwaombee ili Mungu awapokee katika uzima wa milele. Kwa wana ndoa, sherehe hii iwe ni siku ya kila mmoja kumshukuru mwezi wako wa ndoa. Mkumbuke mme wako, mkumbuke mke wako na kumshukuru kwa upendo anaokuonyesha, kwa kukuvumilia na kukusamehe ulipomkosea. Maana maisha ya ndoa si mchezo yanahitaji uvumilivu. Lakini pia hii ni siku ya wazazi kuwashukuru na kuwapongeza watoto kwa maana wanayo nafasi kubwa sana katika ustawi wa familia. Watoto ni kiungo kikubwa sana cha wazazi, baba na mama na ni sababu ya furaha katika familia. Hivyo, wanafamilia mshukuruni Mungu kwa zawadi ya watoto aliowajalia kwa kuwalea vyema na kuwaridhisha tunu zilizo njema. Muwaombee na kuwakinga dhidi ya yule mwovu ili wapate mafanikio katika maisha yao. Kama ilivyokuwa kwa Yesu, nyakati zetu pia kuna maherode wengi wanaotafuta kuwauwa watoto.
Kama Yosefu na Maria, tuwakinge na kuwalinda watoto na maherode wa siku hizi, huku tukiwafundisha tunu zilizo njema na kuwajengea uwezo wa kutambua mema na mabaya, waweza kusema ndiyo kwa mema na hapana kwa mabaya. Ushauri, kwa ambao bado hamjaingia katika maisha ya ndoa na familia, fanyeni maandalizi ya kina, huku mkimwomba Mungu Roho Mtakatifu awape mchumba mwema. Kwa walio ndani ya ndoa, ziheshimuni ndoa zenu, mkijua kabisa ni tunu bora na ya pekee aliyowajalia mwenyezi Mungu, ishini kwa upendo. Jivikeni rehema, utu wema, unyenyekevu, upole, uvumilivu, uaminifu na roho ya kujisadaka, kutoa maisha yako kwa ajili ya familia yako, kuyasadaka mawazo yako, vionjo vyako, matamanio yako, haki zako, majukumu yako na mengine, kwa ajili ya familia yako. Uwe na muda na wanafamilia na mwenzako wa ndoa. Ikitokea mmekoseana, ombaneni msamaha, maisha yaendelee.
Zaidi sana ishini kwa ushirikiano. Kila mtu atimize majukumu yake katika familia. Jihadharini na itikadi zinazodai “uhuru na ukombozi wa mwanamke.” Kamwe mwanamke asitafute kuwa mwanamme, na mwanamme asitafute kuwa mwanamke. Ujinsia huu si muundo wa binadamu ni wa asili na unaendana na ubaiolojia na maumbile ya kila mmoja kadiri ya mpango wa Mungu na daima mtu akienda kinyume na mpango wa Mungu, matokeo yake ni majuto ni mjukuu. Basi tuzifanye nyumba na familia zetu kuwa ni nyumba za sala. Tumwombe Mungu azibariki ili ziwe mahali pema pa kuishi kwa furaha na amani. Ni katika tumani hili mama Kanisa katika sala ya kuombea dhabihu anasali hivi; “Ee Bwana, tunakuomba sadaka ya kututuliza tukikuomba kwa unyenyekevu, uzithibitishe kabisa familia zetu katika neema na amani kwa maombezi ya Bikira Maria Mama wa Mungu na Yosefu mwenye heri.” Na katika sala baada ya Komunio anahitimisha maadhimisho haya akisali hivi; “Ee Baba mwema, sisi unaotuburudisha kwa sakramenti za mbinguni, utuwezeshe kuifuata daima mifano ya Familia yako takatifu, na baada ya taabu za hapa duniani, tukakae nao milele.”