KUZALIWA KWA BWANA KUZALIWA KWA BWANA 

Sherehe ya kuzaliwa Bwana:Neno Akatwaa Mwili, Akakaa kwetu

Sisi tuifungue mioyo yetu tumpokee Yeye aliye Nuru iliyokuja ulimwenguni,atuangaze katika njia ya kwenda mbinguni.Ndiyo maana Mama Kanisa katika sala ya kuombea dhabihu kwa matumaini makubwa anasali:“Ee Bwana,ikupendeze sadaka ya sikukuu hii ya leo.Sadaka hii ndiyo fidia kamilifu ya kutupatanisha nawe,na pia ibada timilifu ya kukutolea wewe,ee Mungu."Heri kwa Siku kuu ya Kuzaliwa Mwokozi wetu Yesu Kristo.

Na Padre Paschal Ighondo – Vatican.

Tafakari ya neno la Mungu katika sherehe ya Krismasi. Katika adhimisho la sherehe ya Noeli, kuzaliwa kwa Imanueli Mungu pamoja nasi, Mama Kanisa ameweka Misa tatu; Misa ya usiku, Misa ya alfajiri na Misa ya mchana. Kila Misa ina sala, nyimbo na masomo yake. Tafakari hii ni ya masomo kwa ajili ya Misa ya mchana. Krismasi ni sherehe ya Umwilisho, Neno wa Mungu kutwaa mwili, kuwa mwanadamu na kukaa kwetu. Ni sherehe ya kuzaliwa Yesu Kristo, Mkombozi wa ulimwengu, Imanueli, Mungu pamoja nasi, Mfalme wa Amani kama tunavyoimba katika wimbo wa mwanzo; “Kwa ajili yetu mtoto amezaliwa, tumepewa mtoto mwanamume, na uweza wa kifalme utakuwa begani mwake, naye ataitwa jina lake Mshauri wa ajabu” (Isa.9:6). Naye mama Kanisa katika sala mwanzo anatuombea akisema; “Ee Mungu, ulimweka mwanadamu katika cheo cha ajabu, na tena ukamtengeneza upya kwa namna ya ajabu zaidi. Tunakuomba utujalie kushiriki umungu wake, yeye aliyekubali kushiriki ubinadamu wetu”.

Kazi ya mfalme ni kutawala na kuongoza. Kristo amekuja kutawala maisha yetu na kutuongoza kwa Mungu. Amekuja kuanzisha utawala wa Mungu duniani; utawala wa haki na amani, umoja na upendo. Ni Mungu aliyetwaa sura, umbo na mwili wa kibinadamu na kuzaliwa kati yetu kama mtoto mchanga. Kuzaliwa kwake ni mwanzo wa utimilifu wa ukombozi wetu kutimia, na nuru kuushukia ulimwengu. Ni kutimia kwa utabiri wa Nabii Isaya akisema; “Watu wale waliokwenda katika giza, wameona nuru kuu, wale waliokaa katika nchi ya uvuli wa mauti, nuru imewaangaza”. Nuru hii inamwangazia kila anayeipokea ili aweze kuona njia ya kwenda Mbinguni kwa Mungu Baba, maana kila anayeipokea Nuru hii, kwake huondolewa giza la dhambi.

Somo la kwanza ni la kitabu cha Nabii Isaya (Isa. 52:7-10). Katika somo hili Mungu anaahidi kuwarudisha tena Waisraeli Yerusalemu kutoka utumwani Babeli. Utumwa wao ni mfano wa hali ya dhambi, na ukombozi wao ni mfano wa ukombozi wa mataifa yote kutoka dhambini. Ni ujumbe wa matumaini kuwa amani imefika, vita sasa vimekwisha, utumwa umekwisha. Isaya anawaalika watu wafurahi akiwaambia; “Pigeni kelele za furaha, imbeni pamoja, enyi mahali pa Yerusalemu palipokuwa ukiwa”. Kwa nini wafurahi wakati wako utumwani? Kwa sababu mda sasa umewadia wa Mungu kutimiza ahadi yake ya kuwakomboa na ncha zote za dunia zitauona wokovu wa Mungu wao. Ujumbe huu ni utabiri wa ukombozi wa binadamu wote kutoka utumwa wa dhambi ambao nasi tunafurahia kuupata kwa kusherehekea kuzaliwa kwake Yesu Kristo.

Ni katika muktadha huu katika wimbo wa katikati tunashangilia tukisema; “Mwimbieni Bwana wimbo mpya, kwa maana ametenda mambo ya ajabu. Mkono wa kuume wake mwenyewe, mkono wake mtakatifu umemtendea wokovu. Bwana ameufunua wokovu wake, machoni pa mataifa amedhihirisha haki yake. Amezikumbuka rehema zake, na uaminifu wake kwa nyumba ya Israeli. Miisho yote ya dunia, imeuona Wokovu wa Mungu wetu. Mshangilieni Bwana, nchi yote. Inueni sauti, imbeni kwa furaha, imbeni zaburi. Mwimbieni Bwana zaburi kwa kinubi, kwa kinubi na sauti za zaburi. Kwa panda na sauti ya baragumu, shangilieni mbele za Mfalme, Bwana” (Zab. 98 :1-6).

Somo la pili ni la waraka kwa Waebrania (Ebr. 1:1-6). Somo hili liweka wazi kuwa utabiri wa kale umetimia katika Yesu Kristo. Katika yeye utukufu wa Mungu umefunuliwa na ni katika yeye tu Mungu anaongea nasi katika nyakati hizi zetu. Tunasoma hivi; “Mungu, ambaye alisema zamani na baba zetu katika manabii kwa sehemu nyingi na kwa njia nyingi, mwisho wa siku hizi amesema na sisi katika Mwanaye, aliyemweka kuwa mrithi wa yote, tena kwa yeye aliufanya ulimwengu….Yeye kwa kuwa ni mng’ao wa utukufu wake na chapa ya nafsi yake, akivichukua vyote kwa amri ya uweza wake, akiisha kufanya utakaso wa dhambi aliketi mkono wa kuume wa ukuu huko juu.” Kumbe mtoto Yesu ni chapa ya Mungu. Tukitaka kumuona Mungu, basi tumuangalie mtoto Yesu kwa macho ya imani.

Injili ni kama ilivyoandikwa Yohane (Yh 1:1-18). Tukizitazama kwa makini Injili zote nne tunaona kuwa; Marko mwanzoni kabisa mwa Injili yake anaandika habari za kazi ya kuhubiri Yesu Kristo. Yeye hajishughulishi kabisa na habari ya kuzaliwa kwake. Mathayo na Luka wanaanza kwa habari za fumbo la umwilisho - Neno wa Mungu kutwaa mwili – kuzaliwa kwake Yesu. Lakini kila mmoja anaanza tofauti na mwingine. Yohane anaanza Injili yake kwa kutuonyesha nini kilikuwepo hapo mwanzo wa uumbaji, na nani walihusika katika uumbaji. Hapa tunafahamishwa kuwa Yesu ni Neno wa Mungu naye tangu mwanzo alikuwa Mungu. Kumbe “Yesu kwa asili alikuwa daima Mungu, lakini hakufikiri kwamba kule kuwa sawa na Mungu ni kitu cha kung’ang’ania kwa nguvu, bali kwa hiyari yake mwenyewe aliachilia hayo yote akajitwalia hali ya mtumishi akawa sawa na wanadamu, akaonekana kama wanadamu” (Flp. 2:6-7).

Kumbe Injili hii ya Yohane inatufunulia asili, mwanzo, mamlaka, nguvu na uwezo na kazi alizozifanya Mungu mmoja katika Nafsi zake Tatu kwa njia ya Nafsi ya pili, Yesu Kristo, Mwanae wa Pekee, Neno aliyefanyika mwili akakaa kwetu. Mungu kwa Neno lake aliviumba viumbe vyote. Tunasoma hivi; “hapo mwanzo alikuwapo Neno, naye Neno alikuwako kwa Mungu, naye Neno alikuwa Mungu. Huyo mwanzo alikuwako kwa Mungu. Vyote vilifanyika kwa huyo wala pasipo yeye hakikufanyika chochote kilichofanyika. Ndani yake ndimo ulimokuwa uzima, nao ule uzima ulikuwa nuru ya watu” (Yh. 1:1-3). Yesu anatuletea uzima mpya kwa kutupatanisha na Mungu Baba.  Kwa Neno lake ametukomboa kutoka utumwa wa dhambi na nguvu za giza na kutupatia uzima na mwanga wa milele. Kumbe Injili hii inatupa majibu ya maswali; huyu aliyezaliwa ni nani?  Kwa nini amezaliwa katika mazingira na hali duni ya kibinadamu? Aliyezaliwa ni Mungu katika Nafsi yake ya pili, Mungu-Mwana, Yesu Kristo, Emanueli, Mungu pamoja nasi. Sababu ya kuzaliwa ni kumpatanisha wanadamu na Mungu Baba na kuudhihirisha upendo wake kwetu sisi. “Hili ndilo pendo si kwamba sisi tulimpenda Mungu bali kwamba yeye alitupenda sisi, akamtuma mwanae wa pekee kuwa kipatanisho kwa dhambi zetu” (1Yh. 4:10). Kuzaliwa kwake katika pango na hori la kulishia wanyama ni kutuonyesha udhaifu wetu, uchafu wetu unaosababishwa na dhambi.

Yesu mfalme wa amani amezaliwa kwetu ili kuleta amani miiongoni mwetu. Ujumbe huu wa amani si ujumbe wetu peke yetu bali ni ujumbe wa dunia nzima. Hivyo inatupasa kueneza amani kuanzia katika nafsi zetu, famili zetu, taifa na ulimwengu kwa ujumla. Yesu Kristo ni nuru amtiaye nuru kila mtu. Kazi ya mwanga ni kuangaza, ni kuleta mwanga palipo na giza. Kwa dhambi ya Adamu na Eva giza lilitanda ulimwenguni. Yesu amezaliwa ili kuleta mwanga palipo na giza, kwani yeye ndiye nuru ya mataifa. Nasi pia tunaalikwa kuwa nuru na mwanga kwa watu wote. Kama tulivyokuwa tunaimba wakati wa majilio, “Dondokeni enyi mbingu toka juu, na mawingu yammwage mwenye haki, nchi ifunguke na kumtoa Mwokozi”; Mbingu zimekwishafunguka na mawingu yamekwishammwaga mwenye haki na nchi imekwishafunguka kumtoa mwokozi, Kristo Yesu. Basi, na sisi tuifungue mioyo yetu tumpokee Yeye aliye Nuru iliyokuja ulimwenguni, atuangaze katika njia ya kwenda mbinguni. Ndiyo maana mama Kanisa katika sala ya kuombea dhabihu kwa matumaini makubwa anatuombea akisali hivi; “Ee Bwana, ikupendeze sadaka ya sikukuu hii ya leo. Sadaka hii ndiyo fidia kamilifu ya kutupatanisha nawe, na pia ibada timilifu ya kukutolea wewe, ee Mungu”. Na katika sala baada ya komunyo kwa matumaini anasali hivi; “Ee Mungu mwenye huruma, tunaomba huyo Mwokozi wa dunia aliyezaliwa akatufanye watoto wako, atujalie pia uzima wa milele”. Herini kwa Siku Kuu ya Kuzaliwa Mwokozi wetu Yesu Kristo.

Tafakari ya Noeli
23 December 2024, 15:58