Sherehe za Familia Takatifu:Familia ndio msingi wa malezi bora ya kikristo!
Na Padre Joseph Herman Luwela - Vatican.
Mpendwa msikilizaji na msomaji, Kanisa limechagua Dominika hii ndani ya Oktava ya Noeli iwe kama sherehe ya Familia Takatifu. Familia hii takatifu iliishi huko Nazarethi, familia hii ndiyo ni kielelezo na mfano wa maisha na malezi bora kwa familia zetu . Na leo hii basi tutafakari pamoja wazo hili kuwa familia ndio msingi wa malezi bora ya Kikristo, ndio chemchemi na tunu bora za Kikristo. Yatupasa basi tuige mfano wa familia hii iliyoishi huko Nazarethi.
Ufafanuzi
Si mara chache neno “familia” linatumika vibaya katika mazungumzo ya kila siku. Mathalani utasikia mtu akisema nina familia tano, au familia zangu mbili zinaumwa. Kumbe, anataka uelewe kuwa ana watoto watano, au watoto wake wawili wanaumwa. Mtoto au watoto si familia. Familia ni baba na mama na watoto katika ujumla wao na si kila mmoja peke yake. Wala hakuna familia halali yenye baba au mama wawili kwenye familia moja. Familia ya namna hii ni batili.
Familia Takatifu
Utaratibu wa kawaida wa kuwataja wana familia ni huu wa baba, mama na watoto, mama na baba; yaani Yesu, Maria na Yosefu. Kwa vile Yesu ni Mungu, lazima apewe nafasi ya kwanza. Maria au mama wa Mungu ni binadamu, lakini amepata upendeleo mkubwa wa kumzaa mwana wa Mungu, ndio maana anachukua nafasi ya pili. Yosefu ni baba mlishi wa Yesu , kwa hiyo anachukua hiyo nafasi ya tatu. Kwa makusudi Mungu aliamua mwanae azaliwe katika familia ya kibinadamu. Lengo halikuwa tu mwanae apate uhalali wa kijamii, yaani kuzaliwa katika ndoa si nje ya ndoa ; lakini pia aweze kujifunza kimaisha na matendo halisi ya familia , toka hatua ya mwanzo mpaka mwisho. Wazazi wa Yesu Kristo, Maria na Baba mlishi Yosefu, walikuwa na fadhila zote za kila mzazi. Imani, unyenyekevu, uvumilivu, uchaji, uthabiti, upendo n.k. Yesu alishuhudia jinsi hao wazazi wake walivyokuwa wakiziishi, na hivyo kujifunza toka kwao.
Familia Takatifu ni mfano kwa familia zetu
Katika Oktava ya Noeli kanisa limetuwekea leo sikukuu ya familia takatifu. Kanisa linataka familia zote za kikristo ziige maisha ya familia takatifu, hata kama hazitafikia ukamilifu huo, lakini jitihada za makusudi zifanyike kufikia lengo hilo. Akina baba wa familia wanapata mfano wao katika Yosefu. Yeye kwa uvumilivu na unyenyekevu mkubwa alifanya kazi yake ya useremala. Kutokana na kazi hiyo aliweza kumudu mahitaji muhimu ya familia . Akina baba tuwe wachapa kazi ili tuweze kuzitunza familia zetu. Mahitaji ya msingi kama nyumba, chakula, mavazi, elimu, matibabu na mengine, hayawezi kupatikana kama akina baba hatufanyi kazi. Na mbaya zaidi, ni wale akina baba wanaozikimbia familia zao. Akina baba tusikwepe majukumu yetu, tuwe wachapa kazi hodari, hakuna sababu ya kuwakimbia wake na watoto wetu.
Mama Maria ni kielelezo kizuri kwa akina mama wa ndoa. Jinsi mama Maria alivyokuwa mchapakazi, mwaminifu na mpendevu kwa familia yake, ndivyo inavyowapasa akina mama kuwa hivyo. Akina mama tusiwe watu wa kulalamika tu mara bwana haleti chumvi, wala nguo, wala sabuni, au mwingine kuishia kudai nguo mpya tu kila toleo linalotoka yeye anataka apate na bila hivyo basi ni ugomvi tu kila kukicha, lakini tujiulize pia ni nini mchango wako katika kuiboresha familia yako? Watoto tuna mfano toka kwa Yesu. Yatupasa kuwapenda, kuwaheshimu na kuwatii wazazi wetu. Yesu licha ya kwamba alikuwa Mungu, lakini aliwatii Yosefu na Maria. Watoto, muwe faraja na kitulizo kwa wazazi wenu. Onesheni shukrani zenu kwao kwa kutimiza yale wanayowaelekeza yasiyopingana na mapenzi ya Mungu. Wakati mwingine hamwezi kujua kwa nini wanawakataza hili au lile. Muwatii tu kwani daima wanawatakia mema. Ni baadaye tu mkiwa watu wazima mtakuja kutambua mapendo hayo ya wazazi wenu.
Ndiyo, maana kauli mbiu ya Jubilei Kuu ya 2025 inasema: “SPES NON CONFUNDIT , yaani "Matumaini Hayatayariki: Mahujaji wa matumaini," ambapo inatoa mchango mkubwa katika muktadha wa familia kama taasisi msingi katika makuzi ya binadamu na jamii, hasa kwa mtazamo wa Kikatoliki. Huu hapa ni uchambuzi wa jinsi kauli hii inavyoimarisha familia. Kanisa Katoliki linafundisha kuwa familia ni msingi wa maisha ya kijamii, kiroho, na kimaadili. Familia ni mahali ambapo binadamu anapokea upendo wa kwanza, kujifunza maadili, na kuelewa nafasi yake katika mpango wa Mungu. Hii inajulikana kama “Kanisa la nyumbani”(Ecclesia Domestica), ambapo familia inajenga kiini cha imani, ibada, na malezi mema ya watoto. Kwa mtazamo huu, familia si tu kitovu cha maisha binafsi bali pia msingi wa kuimarisha jamii nzima. Kauli mbiu ya "Matumaini Hayatayaribiki au mahujaji wa matumaini" inahimiza familia na jamii kuendelea kushikilia tumaini hata wakati wa changamoto. Katika mazingira ya sasa ambapo familia nyingi zinakabiliwa na changamoto kama migogoro ya ndoa, mmomonyoko wa maadili, na changamoto za kiuchumi, kauli hii inaleta mwamko wa kuwa na matumaini thabiti.
Mchango wa Kauli Hii: Kujenga Imani na Ustahimilivu inawahamasisha wanandoa na wazazi kukabiliana na changamoto za maisha kwa kushikamana na Mungu kama msingi wa matumaini na suluhisho la matatizo yao. Kuhimiza Malezi Bora: Matumaini yanaimarisha juhudi za familia kuwekeza katika malezi ya watoto, kuwaandaa kuwa watu wa maadili mema na viongozi wa baadaye wa jamii. Kutoa Mwelekeo wa Kiroho: Familia zinapokumbuka kuwa Mungu ni chanzo cha matumaini yasiyoyumba, zinapata nguvu ya kujifunza na kumtegemea Yeye, hasa katika changamoto za kila siku. Familia na Jamii, Mtazamo wa Kanisa Katoliki unasisitiza kuwa familia ni "kiini cha asili cha jamii" (Katekisimu ya Kanisa Katoliki, 2207). Familia imara huzaa jamii thabiti, na jamii inayozingatia maadili hutoa mazingira bora kwa ukuaji wa familia. Kauli mbiu ya matumaini inachangia kwa:
Kuimarisha Mshikamano: Familia zenye matumaini zinaweza kushirikiana kwa karibu zaidi, kusaidiana katika changamoto, na kuleta mshikamano wa kijamii.
Kuhamasisha Haki na Amani: Familia imara hufundisha watoto thamani ya maadili kama haki, amani, na upendo, ambayo ni msingi wa jamii yenye maelewano.
Kukabiliana na Changamoto za Kijamii: Familia zinaposhikilia tumaini, zinakuwa na msimamo wa kupinga mmomonyoko wa maadili uonevu, uvunjifu wa haki na huchangia maendeleo endelevu ya jamii.nzima
“Matumaini Hatayariki” au hayakatishi tamaa ni wito wa kiimani kwa familia na jamii nzima kushikilia tumaini kwa Mungu kama chanzo cha maisha bora. Katika muktadha wa familia, kauli hii inasisitiza umuhimu wa kuilinda familia dhidi ya changamoto zinazoikumba, kuhakikisha kuwa inabaki kuwa msingi wa makuzi ya binadamu na chanzo cha maendeleo ya jamii. Familia, ikiwa imara katika tumaini, hujenga kizazi chenye nguvu kiroho, maadili, na kijamii.
Hitimisho: Basi ndugu zangu wapendwa katika Kristo, leo hii tunapoadhimisha sherehe ya Familia Takatifu, basi itukumbushe nyajibu zetu mbalimbali sisi tukiwa wana familia, natumaini kila mmoja wetu hapa anatoka katika familia, hakuna hata mmoja ambaye hajatoka kwenye familia, na wala hakuna ambaye ameshuka moja kwa moja toka juu. Basi yatupasa kuiga tunu hizi za familia takatifu ili ziwe kama kielelezo cha maisha bora kwa familia zetu sisi za kikristo.