Manovisi 6 Wakarmeli wafunga nadhiri zao za daima tarehe 14 Desemba 2024,huko Teresianum,Roma miongoni mwao wapo watanzania wawili. Manovisi 6 Wakarmeli wafunga nadhiri zao za daima tarehe 14 Desemba 2024,huko Teresianum,Roma miongoni mwao wapo watanzania wawili. 

Shirika la Wakarmeli:manovisi 6 wafunga nadhiri za daima:unapoitwa itika kwa furaha

Bwana anapoita tusiogope kumfuata bali tusikie sauti yake.Ni maneno ya Ndugu Johanes Linus Mbago katiaka viunga vya Vatican News,Mwanashirika wa Shirika la Bikira Maria wa Mlima Karmeli aliyefunga nadhiri tarehe 14 Desemba 2024 katika Siku Kuu ya Mtakatifu Yohane wa Msalaba na wenzake 5 kutoka nchi tofauti zinazowakilisha shirika lake la Wakarmeli duniani kote.

Na Angella Rwezaula – Vatican.

Kila tarehe 14 Desemba ya kila mwaka, Mama Kanisa anamkumbuka kiliturujia Mkatatifu Yohane wa Msalaba, aliyezaliwa tarehe 24 Juni 1542 nchini Hispania na kifo chake tarehe 14 Desemba 1591. Yeye ni Padre Mwanzilishi mwenza na Mtakatifu Teresa wa Yesu au Avila katika kurekebisha Shirika la Wakarmeli maarufu kama Wakarmeli Peku. Yohane wa Msalaba alipokea Mwaliko wa Mtakatifu wa Teresa, akiwa wa kwanza kati ya wanaume, na akaweza kweli kusimamia mabadiliko hayo katika taabu, kazi na dhuluma nyingi sana. Maandishi yake yanaonesha wazi alivyopanda Mlima wa Mungu kupitia usiku wenye giza wa roho, huku akijitafutia maisha ya kujificha na ndani ya Kristo na akikubali mwali wa upendo wa Mungu umwashe kwa ndani. Na ndiyo maana ni kazi nzuri sana  na ya kina ya kujitafiti kwa Wakarmeli. Mtakatifu Yohane wa Msalaba anaheshimiwa sana kama Mtakatifu na Mwalimu wa Kanisa, na ameandika sana masuala ya kiroho.

Mtakatifu Yohane wa Msalaba:siku kuu yake ni kila tarehe 14 Desemba
Mtakatifu Yohane wa Msalaba:siku kuu yake ni kila tarehe 14 Desemba

Ni katika muktadha huu wa siku kuu yake na zaidi katika miito ya Kanisa ambapo chimba chimba za Vatican News, zilifanya mahojiano na mmoja wa wanashirika ambaye hivi karibuni katika siku kuu hiyo na wenzake 5 kutoka mataifa ya Tanzania, Congo, Madagascar na India walifunga nadhiri za  daima. Yafuatayo ni maelezo ya mmoja wapo  kwa kifupi ya wito wake.

Wakati wa litania ya watakatifu
Wakati wa litania ya watakatifu

Naitwa Ndugu Yohanes Linus Mbago wa Mtoto Yesu wa shirika la ndugu wa Bikra Maria wa Mlima Karmeli. Baba anaitwa Linus Simon Mbago na mama anaitwa Davidica Erenest Mbugano. Mimi ni mtoto wa kwanza kati ya watoto saba, wakiume wanne na wakike watatu. Nilizaliwa mwaka 1992 katika Parokia ya Mtakatifu Yohane Mbatizaji-Pawaga , jimbo katoliki Iringa. Nilibatizwa mwaka 1996 katika Parokia ya Bikra Maria Consolata –Mshindo na kupokea sakramenti ya Kipaimara mwaka 2005 katika Parokia ya Mtakatifu Yohane Mbatizaji-Pawaga jimboni Iringa. Safari yangu ya wito ilianzia katika familia, kwani wazazi toka nikiwa mdogo walinihimiza sana kuwa mwaminifu , kusoma kwa bidii na kuridhika na mahitaji ninayo yapata nyumbani. Mwaka 2001 nilianza masomo yangu katika shule ya Msingi Itundu na kuhitimu mwaka 2007.

Wakati wa kufunga nadhiri:Johanes
Wakati wa kufunga nadhiri:Johanes

Nilikuwa mtumishi wa altare kuanzia mwaka 2003 na hapo ndipo wito wangu ulipoanza kujipambanua, kwani mapadri wamisionari wa shirika la Bikra Maria consolata walitushirikisha sana katika kazi za kitume kama vile ujenzi wa makanisa vigangoni, pamoja na ujenzi wa chekechea na kazi nyingine za kitume na walitamani sana kupata mapdri wazawa. Basi mwaka 2006 nikaandika barua kwa paroko Sylvestro Bettinsoli (I.M.C) na kueleza tamanio langu la kuwa padre, hii taarifa aliipokea kwa furaha sana na kusema nilikuwa nasubiri hii taarifa na nilikuwa naona kama unachelewa na sikutaka nikwambie kama unawito japo mimi nilishaona toka muda murefu. Mwaka 2007 baada ya kuhitimu darasa la saba nikaenda kufanya mtihani Tosamaganga Katika seminari ndogo ya maandalizi ya Mtakatifu Yosefu Kafaso jimboni Iringa na kuanza malezi mwezi wa kumi na mbili 2007 na kumaliza mwezi wa kumi mwaka 2008, na kuchaguliwa kujiunga kidato cha kwanza mwaka 2009 katika seminari ya mtakafitu kizito(Seminari ya mafinga ) ambayo kwa sasa ipo Jimboni Mafinga, ambapo nilisoma hapo hapo hadi kidato cha sita na kuhitimu mnamo mwaka 2015.

Nilipo kuwa kidato cha nne nilipenda kuwa mtawa,  na hii ikanisukuma kuomba mashirika kama la Wakapuchini, Consolata, Damu Azizi ya Yesu na Mateso ya Yesu, na mashirika yote walinikubalia. Mnamo mwaka 2015 na 2016 nilifundisha katika shule ya sekondari Lukuvi-Iringa, wakati nikifundisha lile tamanio langu la kuwa mtawa lilinijia kwa mara nyingine, bila kusita nikamwambia Mungu sasa naomba shirika nitakalo jibiwa ndio hilohilo najiunga, nikaomba shirika la karmeli haikuchukua hata siku tata wakanijibu na wakaniambia niende mara moja kuanza malezi ya mwanzo katika parokia ya malolo jimboni Morogoro kwani wengine walikuwa wamesha anza hapo ndipo safari yangu ya wito katika shirika la karmeli ilipoanza, mwaka 2017 hadi 2018 nikafanya postulanti katika parokia ya Bikra Maria wa Mlima Karmeli-Kihonda Morogoro na mwaka 2018 hadi 2019 niliingia unovisi huko Malisho katika jimbo kuu Katoliki la Mbeya.

Wakati wa kufunga nadhiri za daima
Wakati wa kufunga nadhiri za daima

Tarehe 20 Julai 2019 katika sherehe ya Mtakatifu Elia nikapata vazi ya kikarmeli,  nakuchukua jina la kitawa Yohanes wa Mtoto Yesu. Mnamo mwaka 2019 hadi 2022 nikafanya masomo ya Falsafa katika Chuo kishirikishi cha Mtakatifu Augustino- Jordan, Jimbo Katoliki la Morogoro huku nikiwa naendelea na majiundo katika Seminari yetu kuu ya Mtakatifu Edith Stein- iliyoko Kola Morogoro. Mwaka 2022 baada ya kuhitimu masomo ya Falsafa, shirika likanituma, Roma nchini Italia, kwa  ajili ya masoma ya Taalimungu  katika Chuo Kipapa cha Shirika- Teresianum na sasa nipo naendelea na Mwaka wa Tatu wa Taalimungu. Kwa neema ya Mungu nimefunga nadhiri za daima tarehe 14 Desemba 2024 katika siku ya sherehe ya Mtakatifu Yohane wa Msalaba.

Picha ya pamoja walifunga nadhiri na walezi wao
Picha ya pamoja walifunga nadhiri na walezi wao

Ndugu msomaji mengine zaidi unaweza kuyasikiliza kati audio inayoambatana na makala hii.

Ushuhuda wa Linus Mbago
17 December 2024, 17:25