Tafuta

Siku ya kuwekwa wakfu wa kiaskofu Vincent Cosmas Mwagala,Askofu wa kwanza wa  Jimbo jipya la Mafinga,Tanzania tarehe 19 Machi 2024. Siku ya kuwekwa wakfu wa kiaskofu Vincent Cosmas Mwagala,Askofu wa kwanza wa Jimbo jipya la Mafinga,Tanzania tarehe 19 Machi 2024. 

Askofu Mwagala,Mafinga:huduma kisiwani Lampedusa ni shule ya maisha!

Katika kazi ya huruma na ukaribisho wa wakimbizi wanaopitia Tanzania,Askofu Mwagala anawahesabu kuwa kama watu wa Mungu wa Mafinga,huku akipata msukumo kutokana na usikivu wa ajabu wa watu wa Lampedusa mahali alipofanya utume wa makaribisho kabla ya kuwa Askofu:“Ninajivunia kuwa sehemu ya historia ya Lampedusa,ya jumuiya ya watu ambao,katika kutoa upendo,ni walimu wa maisha duniani.Ninaweza kusema shukrani zangu kwao tu.”

Na Paolo Affatato na Angella Rwezaula – Vatican.

Kuna historia nyingi duniani hasa zinazohusiana na uhamiaji, na makaribisho kila kona ya dunia, na zaidi katika sehemu za kufikia kama Pwani, mito, baharini  na maziwa. Ndugu wote hawa wahamiaji na wakimbizi wanahitaji msaada wa kukaribishwa, kulindwa, kuhamasishwa na kuunganishwa, kama ambavyo Baba Mtakatifu Francisko amesisitiza mara kadhaa. Ni katika mkutadha huo ambapo tunachapishwa  ushuhuda wa mmoja wa kiongozi wa Kanisa alioutoa  kwa Waandishi wa Habari wa Vatican katika Gazeti la Osservatore Romano ambaye anasimulia historia ya kusisimua kuhusu kukaribisha wahamiaji. Katika Muktadha wa Italia wa wahamiaji ni uzoefu wa Lampedusa ambao  unavuma leo hii katika moyo wa Afrika, unaojumuisha matunzo, faraja na matumaini yanayotolewa kwa wahamiaji. Katika harakati za mzunguko zenye maana kubwa, kuturudisha katika Bara la Afrika roho iliyokomaa katika miaka ya ukuaji wa kibinadamu na kiroho, kisha ya huduma ya kukaribishwa na kichungaji pamoja na wahamiaji.

Siku ya kuwekwa wakfu wa kiaskofu tarehe 19 Machi 2024
Siku ya kuwekwa wakfu wa kiaskofu tarehe 19 Machi 2024

Na huyo ni Vincent Cosmas Mwagala, ambaye leo hii ni Askofu wa Mafinga, jimbo jipya Katoliki nchini Tanzania lililomegwa kutoka katika Jimbo la Iringa.“ Uzoefu wa kichungaji nilioishi huko kisiwa cha Lampedusa ulinitambulisha daima na ilikuwa shule ya maisha” alisema. Hapo awali akiwa Padre  Vincent, Paroko Msaidizi wa Parokia ya Mtakatifu Gerlando na Padre msimamizi wa  kituo cha kwanza cha mapokezi, alitumia wakati wake wa miaka muhimu kwa mafunzo yake kama mwanamume na kama padre, urithi ambao sasa anaubeba na kuutumia katika utume wake kama Askofu.“Huko nilikutana na wanadamu mbalimbali, watu wa mataifa mbalimbali, lugha, tamaduni na dini, hasa kutoka Afrika Magharibi, lakini pia kutoka Asia ya Kusini. Kila mtu alihitaji neno na ishara ya faraja na joto la kibinadamu. Na ulikuwa ni ubinadamu uliojeruhiwa, ambao ulikuwa na safari ya kutisha nyuma yake, iliyojaa hatari, shida na ugumu,” alikumbuka.

Kila mmoja wao alikuwa na uzoefu wake mwenyewe na historia za kusimulia: Nilitumia muda mwingi kusikiliza historia zao, mateso yao, kwa sababu walihitaji kushirikisha kile walichobeba mioyoni mwao. Kwa Neno la Mungu, basi, nilijaribu kumwachia kila mtu ujumbe wa faraja na matumaini,” alisema Askofu  Mwagala. Tendo la kuwa  Mwafrika aliliona kuwa ilikuwa ni sababu iliyozaa imani kwa wahamiaji: “ Kwa sababu hii hata polisi mara nyingi waliniita kushughulikia kesi nyeti zaidi au kutatua masuala tata katika uhusiano na wageni wa kituo cha mapokezi. Siku zote niliona uwepo wangu mahali hapo kama dhamira ya kukuza na kuwezesha udugu, mkutano, mazungumzo na maelewano kati ya watu wa tamaduni mbalimbali.” Na hivyo huko Lampedusa, kwenye kisiwa cha Mediterania ambako alikaa miaka kadhaa kama Padre wa fidei donum katika jimbo kuu la Agrigento (hali halisi ya kikanisa inayohusishwa na pacha kwa Tanzania), Askofu Vincent alijifunza “kuwatunza watoto wadogo, walio hatarini, kuliko waliotengwa, wa wale ambao wamepoteza kila kitu.

Hata jina. Hii ni kwamba Askofu alikumbuka tukio  moja analobainisha kuwa:“Miongoni mwa wakati wa kugusa zaidi ni wakati tuliposherehekea mazishi ya kijana ambaye hakujulikana, Mnigeria wa miaka thelathini na sita ambaye alikufa mnamo 2009 kupatikana akiwa maiti katika Mtumbwi ambao alikuwa anajaribu kuvuka nao kufika Ulaya na wezanke: “tulimwita Ezekiel Chidi, tukiwauliza wenzake walionusurika kwa kupata kipande cha karatasi alichokuwa nacho mfukoni.” Kwa mujibu wa Askofu Mwagala alibainisha kuwa: “ Wahamiaji wanakufa mara mbili:  kwanza kwa sababu maji huwazuia kupumua, pili kwa sababu husahauliwa kwa kunyimwa heshima ya kumbukumbu. Na hivyo bahari inakuwa makaburi ya kutojali, ambayo ndani yake kuna  majina, historia, ndoto na matumaini yamepotea.”

Hatuwezi kusahau, alisema, safari ya Baba Mtakatifu Francisko ambaye alifika kisiwa cha Sicilia tarehe 8 Julai 2013, katika ziara yake ya kwanza ya upapa, na kama vile mauaji ya tarehe 3 Oktoba 2013 ambapo watu 368 walikufa katika ufukwe  wa Lampedusa mahali ambapo  bado zinabaki kuandikwa kumbukumbu zetu. Kinachokuja akilini, basi, ni kwamba “bahari ni ishara  yenye nguvu sana, ambayo inakuwa kama aina ya kumbukumbu ya Auschwitz, bahari ambayo inakuwa mahali pa kutorudi  na ambayo manyoya ya uhuru hubakia yamenaswa milele, kupoteza pumzi na kumbukumbu,  kama ilivyoandikwa kwenye mlango wa kaburi la Lampedusa. Hapo makaburi ya wakazi wa kisiwa hicho yanachanganyika na yale ya wale waliojaribu kufika Ulaya kwa kuvuka Bahari ya Mediterania, lakini ambao walipoteza maisha katika safari hii ya matumaini.” “Kwa sehemu kubwa ni makaburi yasiyo na jina, lakini kila mmoja wao ana historia inayohitaji kurejeshwa, kulindwa, kukabidhiwa mikononi mwa Aliye Juu,” alibainisha Askofu wa Mafinga.

Na hii ni “kwa sababu sio tu kuhusu idadi" lakini ni kuhusu watu, wenye maisha ambayo yana mizizi katika nchi za mbali, kumbukumbu ambayo wanafamilia wao, na sisi pamoja nao, tunabeba mioyoni mwetu.” Ndio maana Askofu  Mwagala anathamini sana kazi ya subira ya kutafiti shuhuda za wale “wahamiaji waliozikwa bila jina”, ambao kumbukumbu zao zilizama baharini lazima zihifadhiwe hai kwa manufaa ya wote, kwa manufaa ya Ulaya na Afrika, kwa huduma ya kweli kwa wanadamu wote.” Leo hii katika nchi yake Tanzania, katika jimbo ambalo kuna maskini, waliotengwa, familia ambazo hazina uhakika wa chakula na haziwezi kumudu elimu au huduma ya afya, hisia za Askofu Vincent zinaakisi jamii nzima na hivyo alisisitiza kuwa: “Sisi ni Jimbo Jipya  na eneo lililotengwa na lile la Jimbo la Iringa. Tuna Parokia 19, Mapadre 56 na uhalisia mbalimbali wa maisha ya kuwekwa wakfu, (Watawa na vyama vya Kitume) lakini maisha ya Kanisa bado yanahitaji kupangwa, na yatakuwa yale ya Kanisa ambalo milango yake iko wazi, ambalo linakuwa msindikizaji wa  msafiri, anayetunza huduma wale wanaozindua kilio cha kuomba msaada.”

Wahamiaji ambao wanatoka Kaskazini mwa Afrika kwenda Kusini mwa Afrika

Miongoni mwao kuna wale wahamiaji wa Kiafrika ambao hawaelekei kaskazini bali wanatafuta njia nyingine, daima kutoroka vita au umaskini, daima wakitafuta maisha bora.  Kwa miaka sasa Shirika la Kipapa la Habari za Kimisionari Fides, linabainisha kuwa “wahamiaji wengi kutoka mataifa ya Afrika wamekuwa wakielekea Afrika Kusini, nchi iliyoendelea zaidi kusini mwa Afrika. Katika vitongoji vya Afŕika Kusini, katika vitongoji vilivyokuwa vimetengwa kwa ajili ya watu weusi, kwa miaka mingi jumuiya kutoka mataifa yenye machafuko zaidi ya Afŕika Kusini mwa Jangwa la Sahaŕa wanameishi  kutoka: Zimbabwe, Msumbiji, Somalia na mataifa mengine ya Pembe ya Afŕika. Hawa wanafika baada ya safari  ngumu na hatari kama ile ya Kaskazini, iliyofanywa kwa njia ya muda kuvuka nchi ya Kenya, Tanzania, Zambia, Msumbiji.

Nyakati nyingine wahamiaji walisafiri kwa “boti za baharini” ambazo huishia kuzama katika Mfereji wa Msumbiji, ambao pia umekuwa makaburi. Na kisha, mara tu wanapofika katika marudio yao, mustakabali wa vurugu unawangoja: Waafrika Kusini weusi wanawachukulia kama washindani na hatari katika kutafuta ajira; wakati mwingine wao huanzisha visasi vikali sana, kwa misingi ya kikabila tu. Katika kazi ya huruma na ukaribisho wa wakimbizi wanaopitia Tanzania, Askofu  Mwagala anawahesabu kuwa kama watu wa Mungu wa Mafinga, huku akipata msukumo kutokana na usikivu wa ajabu wa watu wa Lampedusa mahali alipofanya utume wa makaribisho kwamba: “Ninajivunia kuwa sehemu ya historia ya Lampedusa, ya jumuiya ya watu ambao, katika kutoa upendo, ni walimu wa maisha duniani. Ninaweza kusema tu shukrani zangu kwao.”

Siku ya kuwekwa wakfu kwake tarehe 19 Machi 2024
Siku ya kuwekwa wakfu kwake tarehe 19 Machi 2024

Ikumbukwe Askofu Vincent Cosmas Mwagala, Askofu wa Jimbo katoliki la Mafinga Tanzania alizaliwa tarehe 11 Desemba 1973 huko Makungu, mkoani Iringa. Baada ya masomo yake ya Kikasisi kutoka Seminari kuu ya Mtakatifu Augustino, Peramiho, Songea kwa Falsafa aliendelezwa kwa masomo ya Taalimungu na akajipatia Shahada ya Uzamili kutoka katika Kitivo cha Kipapa cha Taalimungu, kisiwani Sicilia, huko Palermo. Alipewa Daraja Takatifu ya Upadre kunako tarehe 11 Julai 2007 kwa ajili ya Jimbo Katoliki la Iringa. Baba Mtakatifu Francisko, tarehe 22 Desemba 2023 aliunda Jimbo jipya la Mafinga, Tanzania kwa kulimega kutoka Jimbo Katoliki la Iringa jimbo hilo la Mafinga kuwa chini ya Jimbo kuu la Mbeya na wakati huo huo kumteua Askofu wake wa Kwanza ambaye  aliwekwa wakfu wa kiaskofu tarehe 19 Machi 2024 kwa ajili ya Jimbo hilo Mafinga.

Ushuhuda wa Askofu Mwagala, Jimbo Mafinga Tanzania
19 December 2024, 16:25