Mwanamke akipiga kura katika uchaguzi wa serikali za mitaa katika kituo cha Kambangwa jijini Dar es Salaam Tanzania tarehe 27 Novemba 2024. Mwanamke akipiga kura katika uchaguzi wa serikali za mitaa katika kituo cha Kambangwa jijini Dar es Salaam Tanzania tarehe 27 Novemba 2024. 

Tanzania:TEC yalaani mauaji yaliyotokea wakati wa chaguzi za Serikali za Mitaa 2024

Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania TEC,tarehe 28 Novemba 2024 lilitoa tamko lililosomwa na Mwenyekiti wa Tume ya Haki na Amani ya Baraza hilo,Askofu Mkuu Jude Thadeus Rwa’ichi (OFMCap)mbele ya waandishi wa habari.Katika tamko,linalaani baadhi ya mauaji yaliyofanyika kabla ya Uchaguzi wa viongozi wa serikali za mitaa 2024."Tanzania tunaelekea wapi kwa kujenga tabia hii?Kitendo cha mauaji ya wanasiasa,kinapaswa kulaaniwa na kuchukuliwa hatua kali za Kisheria."

Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania(TEC).

Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC) limetoa tamko tarehe 28 Novemba 2024, siku moja baada ya uchaguzi uliofanyika hivi karibuni. Ujumbe wao ulisomwa na Mwenyekiti wa Tume ya Haki na Amani ya Baraza hilo, ukiwa na kichwa: Mauaji yaliyotokea wakati wa uchaguzi wa Serikali za Mitaa Mwaka 2024. Tunachapisha tamko hilo kamili:

Nchi Yetu inapita katika machungu maumivu makubwa kwa kuona raia wakikatishwa uhai wao wakati wakiwa katika kupigania haki zao za msingi za kisiasa. Usiku wa tarehe 26 Novemba 2024 kuamkia siku ya uchaguzi tarehe 27 Novemba, wameuawa watu wawili, mmoja Tunduma na mwingine Manyoni. Na tarehe 27 Novemba 2024, jana ameuawa mtu mmoja Dar Es Salaam. Kanisa Katoliki na Jimbo Kuu Katoliki Dae Es Salaam tumesikitishwa sana na vitendo hivi vya kutoa uhai wa hawa wapendwa raia wenzetu. Tukumbukwe kuwa Mungu Muumba ndiye pekee mwenye mamlaka na uhai wa wanadamu wote. Hapa duniani hakuna aliye na haki ya kuondoa uhai wa mwingine. Tunaonya jamii ya watanzania, kuacha tabia hii ambayo imeanza. Hatuoni wenye kusimamia sheria na kulinda uhai wa raia wakilaani na kuonya. Tabia hii ya kuchukulia mauaji ya wanasiasa kama vifo  vya kawaida ni tendo lenye kupekekea kujengeka tabia ya kupoteza na kukosa ulinzi wa haki ya uhai kama ilivyo kwenye Ibara ya 14 ya Katiba ya Nchu yetu. Wapo waliokabidhiwa jukumu la kulinda Ibara hii. Tunapoona mauaji haya yakiongezeka, tunajiuliza maswali mengi ya uwajibikaji wa serikali kwa wananchi.

Mwanzoni mwa mwezi huu wa Novemba, kule Iringa na Bukoba waliuawa pia wanasiasa wawili. Tanzania tunaelekea wapi kwa kujenga tabia hii? Kitendo cha mauaji ya wanasiasa, kinapaswa kulaaniwa na kuchukuliwa hatua kali za Kisheria. Hakuna mwenye mamlaka ya kuua mwenzake. Kutekeleza ama kudai haki za kisiasa wakati wa uchaguzi sio vita ni ushindani. Vyombo vya Ulinzi vimepewa mafunzo na kuwekewa sheria za utekelezaji wa majukumu yake. Serikali inalo jukumu la kuonesha kuzingatiwa ueledi katika hali tuliyo nayo. Watu wasijisikie kutishwa na vyombo vya ulinzi wakati wa maandalizi na wakati wa uchaguzi. Ukatili dhidi ya wanasiasa ni tendo ovu lazima likomeshwe nchini mwetu. Sisi sote ni ndugu na watoto wa Mungu Baba muumbaji. Tuheshimu na Kutii Amri ya Mungu ya kulinda uhai wa mwingine. Tutubu na kuongoka.

Ndimi Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu la Da Es Salaam na Mwenyekiti wa Tume ya Haki na Amani ya Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania,

Jude Thadeus Ruwa’ichiMCap.

Imetolewa leo tarehe 28 Novemba 2024, Dar Es Salaam na Idara ya Haki na Amani ya Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania.

01 December 2024, 15:37