Vipaumbele Vya WAWATA na Ujenzi wa Kanisa la Kisinodi
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S., Dar Es Salaam.
Hivi karibuni Halmashauri ya Utekelezaji Jumuiya ya Wanawake Katoliki Tanzania, WAWATA ilifanya mkutano wake, uliowajumuiya viongozi wakuu kutoka Majimbo mbalimbali nchini Tanzania. Mkutano huu ulianza kwa tafakari mintarafu mfumo wa maadhimisho ya Sinodi kwa kusikilizana katika roho pamoja na kujiweka katika hali ya kumsikiliza Roho Mtakatifu. Wajumbe walijifunza namna ya kutembea pamoja kama sehemu ya mchakato wa ujenzi wa Kanisa la Kisinodi yaani baina ya Wakleri, Watawa na Waamini walei. Wajumbe walipata nafasi ya kusikiliza mafunzo kuhusu biashara haramu ya binadamu. Sababu nzito zinazopelekea watu kujikuta wanatumbukizwa kwenye biashara haramu ya binadamu na viungo vyake sanjari na mifumo mbalimbali ya utumwa mamboleo ni umaskini wa hali na kipato, unaowawadanganya watu hawa kwamba, watapata fursa za ajira na hivyo kuondokana na hali yao duni. Lakini ukweli wa mambo, wanapofika huko wanakopelekwa, wanajikuta wakiwa wametumbukizwa kwenye biashara ya binadamu na viungo vyake sanjari na utumwa mamboleo kiasi kwamba, hawana tena uwezo wa kurejea nchini mwao.
Hawa ni watu wanaotoka katika maeneo ya vita, njaa na magonjwa; watu walioathirika kutokana na mipasuko ya: kiuchumi, kidini, kijamii, hali ngumu ya maisha pamoja na athari za mabadiliko ya tabianchi. Lakini, sababu kubwa zaidi ni watu kufilisika kimaadili na kiutu, kutokana na kuelemewa na uchu wa mali na utajiri wa haraka haraka na madaraka! Mapambano haya yamepewa kipaumbele cha pekee katika maisha na utume wa Baba Mtakatifu Francisko kwa wakati huu. Biashara ya binadamu si wazo la kufikirika bali ni hali halisi inayogusa mamilioni ya watu duniani. Hawa ni wale watu wanaotumbukizwa kwenye biashara na utalii wa ngono; biashara ya viungo vya binadamu; ndoa shuruti na kazi za suluba kwa watoto wadogo ambao wakati mwingine wanapelekwa mstari wa mbele kama chambo cha vita. Watoto hawa wakati mwingine wamekuwa ni kafara wa imani za kishirikina sehemu mbali mbali za dunia. Wakimbizi, wahamiaji na wale wote wanaotafuta hifadhi ya kisiasa mara nyingi wamejikuta hata wao pia wakitumbukizwa katika biashara haramu ya binadamu na mifumo mbali mbali ya utumwa mamboleo. Wajumbe walipata pia nafasi ya kusikiliza kuhusu ukatili wa kijinsia “GBV.” Mwishoni walijifunza kuhusu: Uongozi kwa ujumla: Wajibu wa viongozi, Jinsi ya kuendesha vikao; Namna ya kutatua migogoro; kuandaa mpango mkakati wa kazi; Utekelezaji wake pamoja na kufanya tathmini. Kama viongozi wanawajibika kulinda na kudumisha usalama wa walio hatarini; pamoja na Magonjwa yasiyo ambukiza.
Kwa upande wake Mama Evaline Malisa Ntenga Makamu wa Rais wa Wanawake Wakatoliki Ukanda wa Bara la Afrika ambaye pia ni Mwenyekiti WAWATA Taifa alikuwa na haya ya kusema: Kwa Upendo Wa Kristo! Kauli mbiu ya Sinodi ya XVI ya Maaskofu: “Kwa Ajili ya Kanisa la Kisinodi: Umoja, Ushiriki na Utume.” Tutumikie na Kuwajibika! Jumuiya Ndogo Ndogo za Kikristo - Miaka 50 ya kujenga Kanisa kama familia ya Mungu. Napenda kuchukua fursa hii kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa zawadi ya Uhai na kwa zawadi ya Utume wa Wanawake Wakatoliki Tanzania. Kwa namna ya pekee na kwa moyo wa unyenyekevu niwashukuru sana wenyeji wetu Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC) kwa mapokezi - Ahsanteni sana. Ni furaha na baraka kubwa kuwa pamoja nanyi siku ya leo tunapokutana kwa ajili ya mkutano huu muhimu pamoja na mafunzo. Mtakubaliana nami kuwa ni nafasi ya kipekee kuweza kukutana viongozi wote watano, mpigie Mungu makofi. Tunamshukuru Mungu aliewasafirisha salama na kutuweka pamoja, natambua wengine mmefika usiku sana, poleni. Tunapoanza rasmi mkutano huu, tuwe na tafakari na moyo wa shukrani kwa nafasi hii ya kukutana, kusikilizana, kumsikiliza Roho Mtakatifu, kujadiliana, kujifunza, na kujiimarisha katika utumishi wetu kama sehemu ya mchakato wa ujenzi wa Kanisa la Kisinodi. Ndugu zangu, uongozi wetu unapaswa kuwa mfano bora wa utumishi wa kujisadaka, unyenyekevu, na utendaji wenye maadili. Katika Waraka wa Kitume wa Baba Mtakatifu Francisko "Fratelli tutti": Yaani “Wote ni Ndugu”: Kuhusu Udugu na Urafiki wa Kijamii “tunakumbushwa kwamba “Hakuna anayekombolewa peke yake” (Fratelli tutti, 32). Hii inatualika sisi kuwa viongozi wanaoishi kwa kutanguliza udugu na mshikamano. Tukatae migawanyiko na kukosa umoja, kwani hayo yanazuia lengo letu kuu la kuwahudumia wale waliotuchagua.
Kipaumbele chetu cha kwanza ni malezi ya familia. Wosia wa Kitume wa Baba Mtakatifu Francisko: “Amoris laetitia” yaani “Furaha ya Upendo ndani ya familia”, unatufundisha kwamba: “Familia ni mahali ambapo tunajifunza kuishi pamoja, kuleta umoja na mshikamano” (Amoris laetitia, 315). Tunao wajibu wa kuwa mstari wa mbele katika kuhakikisha tunajenga familia zenye upendo, uvumilivu, na maadili mema. Kwa njia hii, tutatoa mchango bora kwa jamii na kuandaa kizazi kinachofuata kutekeleza wajibu wao kwa uaminifu. Sisi hapa kama viongozi watano watano ni familia moja. Tujichunguze, kuna upendo kati yetu? Mwulize Jirani yako kuna upendo baina yako na wenzako wanne? Kuna umoja? Kuna kusameheana? Ama ni unafiki na “uchawa”? Salamu yetu ya kwa upendo wa kristo – tutumikie na kuwajibika ni aidha haitumiki, ama imepoteza ladha, ama tunaikanyaga!!Tafakari. Katika malezi ya familia kati yetu kuna vilio. Kama sio kutoka kwa wenza ni watoto, kama sio watoto ni ndugu wa damu, ama wazazi. Malezi kwa Watoto wetu na wajukuu yamesahaulika ama tumeyaondoa kwenye kipaumbele! Nani baina yetu hajasikia mwanafunzi wa darasa la pili kalawitiwa, ama kabakwa ama kaokotwa ameharibiwa na kuuwawa kikakili? Nani hajasikia usagaji kwenye mashule ya bweni na hata kutwa? Nani hajasikia kuhusu tabia ya ushoga? Tunaotumia mitandao ya kijamii tunaona Watoto wetu wa kike wanatangaza biashara – kawaida 20,000 – mparange 50,000. Mara ngapi tunasikia ameuwawa na mume kisa wivu wa mapenzi? Ama amepotea akakutwa maiti imefukiwa nje ya nyumba yake? Dunia inaelekea wapi? Ni wapi tumekosea? Mambo ya Walawi 18:22 – 23 Usilale na mwanaume mfano wa kulala na mwanamke, ni machukizo. Wala usilale na mnyama yoyote ili kujitia unajisi kwake, wala mwanamke asisimame mbele ya mnyama ili kulala nae, ni uchafuko. Warumi 1:27 – Wanaume nao vivyo hivyo waliyaacha matumizi ya mke ya asili, wakawakiana tamaa, wanaume wakiyatenda yasiyopasa, wakapata nafsini mwao malipo ya upotevu wao yaliyo haki yao.
Pili, tunaalikwa kuwajali na kuwahudumia wanyonge. Yesu mwenyewe alisema, “Yeyote atakaye kuwa mkubwa kati yenu, na awe mtumishi wenu” (Mathayo 20:26). Tujitahidi kusaidia na kuwapa sauti wale walioko pembezoni mwa jamii. Katika waraka “Fratelli Tutti,” Baba Mtakatifu anatukumbusha umuhimu wa huruma na upendo kwa wote, hasa kwa wale wasio na sauti (Fratelli tutti, 77). Huu ni mwito wa kiongozi wa kweli: kujitoa kwa ajili ya wengine na kusimama na wanyonge. Kipaumbele chetu cha tatu ni utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote. Waraka wa Kitume wa Baba Mtakatifu Francisko “Laudato si” yaani “Sifa iwe kwako” juu ya utunzaji wa nyumba ya wote” unatuhimiza kutunza “mazingira nyumba ya wote” kwa kuwa “Dunia, nyumba yetu, ina shida kubwa” (Laudato si, 61). Tunapowahamasisha waamini na jamii kwa ujumla, ni muhimu kutekeleza na kufundisha juu ya ulinzi wa mazingira, kupanda miti, na kuchukua hatua za kupunguza uchafuzi wa mazingira. Hii itasaidia kudumisha dunia yenye afya kwa vizazi vijavyo. Mwisho, lakini sio kwa umuhimu tunaalikwa kutembea pamoja kisinodi. Sinodi ni njia ya kusikilizana na kushirikiana katika roho moja. Kama Baba Mtakatifu Francisko alivyosema, “Sinodi si tukio au kipindi maalum, bali ni njia ya kutembea pamoja, kuelekea kuwa Kanisa la umoja na ushirikiano” (Wito wa Utakatifu, 6). Tuwe viongozi ambao wanatafuta kusikiliza na kuelewa mahitaji ya wale tunaoongoza, tukiweka mbele mazungumzo na mshikamano. Tuna watoa mada mbalimbali watakaotupa mengi ya kutuimarisha na ili tuujenge umoja wetu. Tujitahidi kuwa pamoja, tuache tofauti zetu, makundi na kuchuuliana katika madhaifu yetu. Tumshukutu Mungu kwa ajili ya kila mmoja wetu kwa kutambua, sote tumechaguliwa kwa ajili ya kuinjilisha. Sote, hakuna hata mmoja mkamilifu. Tofauti zetu ndio nguvu yetu – kila mmoja ana karama tofauti, tukiziunganisha pamoja tunaweza kuukamilisha mwili wa Kristo. Ni kwa nini nikaitwa mimi baina ya wengi? Ni nini Mungu anataka nifanye? Nafasi hii niliyopewa nitatoa hesabu gani? Je, kazi yangu ni kuwachafua wengine? Je, kazi yangu ni kupaka matope karama za wengine ama kuziombea ili Mungu aendelee kutukuzwa? Tukiweka vipaumbele hivi mbele, tutakuwa tunatimiza wito wetu wa utumishi na kutengeneza jamii bora yenye amani, upendo, na mshikamano. Nawatakia mkutano wenye tija, baraka, na mwongozo wa Roho Mtakatifu. Kauli mbiu ya Sinodi ya XVI ya Maaskofu: “Kwa Ajili ya Kanisa la Kisinodi: Umoja, Ushiriki na Utume.”
Kwa upande wake Padre Florence Rutaihwa, Mkurugenzi wa Kurugenzi ya Kichungaji Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania aliyemaliza muda wake aligusia kuhusu mchakato wa maadhimisho ya Sinodi ya XVI ya Maaskofu iliyokuwa inaongozwa na kauli mbiu “Kwa Ajili ya Kanisa la Kisinodi: Umoja, Ushiriki na Utume.” Huu ni mwaliko wa kuwashirikisha wengine katika safari ya Kisinodi, kwa kujenga urafiki na kuhakikisha kwamba, hakuna anayebaki pembezoni mwa vipaumbele vya kijamii. Ikumbukwe kwamba, kusikiliza ni hatua ya kwanza inayohitaji akili na moyo uliofunguka, bila upendeleo, wala kupuuza sauti za waamini walei: wanawake na vijana pamoja na watu waliowekwa wakfu. Kuwa na ujasiri wa kusikiliza hasa wale wenye maoni tofauti, maskini na wale waliotengwa na jamii. Huu ni mwaliko pia wa kuzungumza kwa ujasiri, ukweli na uwajibikaji; kwa kuzingatia mambo msingi; sanjari na Umuhimu wa vyombo vya mawasiliano ya jamii. Padre Florence Rutaihwa alikazia umuhimu wa ushiriki mkamilifu katika maadhimisho ya Fumbo la Ekaristi Takatifu, kama kielelezo makini cha kutembea kwa pamoja sanjari na ujenzi wa Kanisa la Kisinodi. Liturujia na hasa Fumbo la Ekaristi Takatifu lizame katika maisha ya waamini. Kuna haja ya kugawanya majukumu katika utume wa pamoja katika medani mbalimbali za maisha kama sehemu muhimu sana ya ujenzi wa Kanisa la Kisinodi. Waamini watambue kwamba, kwa njia ya Ubatizo, wamekuwa ni wamisionari, tayari kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu kwa watu wa Mataifa. Huu pia ni mwaliko wa kukuza na kudumisha majadialiano ya Kanisa na ndani ya Jamii, kwa kujikita katika uvumilivu na utulivu; umoja na ushirikiano. Majadiliano ya kidini ni muhimu sana katika kuimarisha umoja, upendo, haki na mafungamano ndani ya jamii.
Kanisa liwe tayari kujifunza kutoka katika medani mbalimbali za maisha: Kisiasa, Kiuchumi, Kitamaduni na kutoka katika asasi za kiraia kwa kuwatambua na kuwathamini maskini kwani hawa ni walengwa wa kwanza wa Injili na Wainjilishaji wakuu. Majadiliano ya kiekumene yanayo nafasi ya pekee katika ujenzi wa Kanisa la Kisinodi na mafungamano ya kijamii. Ni vyema waamini wakajifunza kuangalia matunda, changamoto na fursa mbalimbali zinazojitokeza. Kanisa la Kisinodi ni shirikishi na linalowajibika kwa kubainisha malengo na njia ya kuweza kuyafikia malengo haya. Kumbe, kuna haja ya kukuza na kudumisha ushiriki wa waamini katika uongozi ndani ya Kanisa. Katika ujenzi wa Kanisa la Kisinodi maamuzi hufanywa kutokana na mang’amuzi kwa msaada wa Roho Mtakatifu. Huu ni mwaliko kwa Kanisa kukuza na kudumisha uwazi na uwajibikaji sanjari na kukua katika utambuizi wa kiroho wa kijamii. Kumbe, usawa unajumuisha upokeaji wa mabadiliko, malezi na majiundo makini ya awali na endelevu, ili kuweza kuwaunda waamini kutembea kwa pamoja; kwa kusikilizana; kwa kushiriki kikamilifu katika maisha na utume wa Kanisa. Kuna haja ya kujikita katika utambuzi wa utumiaji wa mamlaka katika ujenzi wa Kanisa la Kisinodi.