Tafuta

WAWATA kwa sasa inaandaa Mpango Mkakati wa Miaka mitano mintarafu ujenzi wa familia bora ndani ya Kanisa na jamii katika ujumla wake. WAWATA kwa sasa inaandaa Mpango Mkakati wa Miaka mitano mintarafu ujenzi wa familia bora ndani ya Kanisa na jamii katika ujumla wake.  

WAWATA: Mpango Mkakati wa Ujenzi Wa Tunu Msingi za Kifamilia

Familia ni Kanisa dogo la nyumbani, shule ya upendo, huruma, haki na ukarimu. Ni mahali patakatifu ambapo tunu msingi za maisha ya kiroho, kiutu na kitamaduni zinatangazwa, zinashuhudiwa na zinarithishwa, Maisha ya ndoa na familia ni wito kwa waamini wengi ndani ya Kanisa. Familia ni shule ya ubinadamu, mahali pa kujifunza kupenda na kupendwa; kusamehe na kusamehewa; kuwajibika pamoja na kuonesha mshikamano wa umoja na udugu wa kibinadamu.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S., - Vatican.

Mama Kanisa anaendelea kuwekeza katika maisha na utume wa familia, ili kusimama kidete kulinda, kutetea na kudumisha utu na heshima; ukuu na utakatifu wa maisha ya ndoa na familia, tayari kutangaza na kushuhudia Injili ya familia inayojikita katika: Uhai, huruma na mapendo. Familia za Kikristo hazina budi kusimama kidete kulinda na kutetea tunu msingi za maisha ya ndoa na familia dhidi ya: Ukoloni wa kiitikadi, vikwazo na kinzani zinazojitokeza katika maisha na utume wa familia katika ulimwengu mamboleo. Ikumbukwe kwamba, familia ni Kanisa dogo la nyumbani, shule ya upendo, huruma, haki na ukarimu. Ni mahali patakatifu ambapo tunu msingi za maisha ya kiroho, kiutu na kitamaduni zinatangazwa, zinashuhudiwa na zinarithishwa, tayari kuunda jamii inayowajibikiana na kushikamana kama ndugu wamoja. Maisha ya ndoa na familia ni wito kwa waamini wengi ndani ya Kanisa. Familia ni shule ya ubinadamu, mahali pa kujifunza kupenda na kupendwa; kusamehe na kusamehewa; kuwajibika pamoja na kuonesha mshikamano wa umoja, udugu na upendo. Wazazi na walezi wanapaswa kuhakikisha kwamba, wanasimama kidete kutoa malezi na majiundo makini kwa watoto wao, kwani hii ni dhamana ambayo kamwe haiwezi kutekelezwa na taasisi nyingine iwayo yote. Wazazi na walezi wawajibike kwa kuwa waaminifu kwa maisha na utume wao ndani ya familia.

WAWATA: Mpango Mkakati wa Ujenzi wa Tunu Msingi za Kifamilia
WAWATA: Mpango Mkakati wa Ujenzi wa Tunu Msingi za Kifamilia

Mafundisho Jamii ya Kanisa kuhusu maisha ya ndoa na familia yanajikita zaidi katika; kuragibisha sera na mikakati ya maisha ya ndoa na familia na kwamba, familia ya Kikristo inasimikwa katika upendo thabiti kadiri ya Mafundisho ya Kanisa; Changamoto ya idadi ndogo ya watoto wanaozaliwa; wanandoa wawe ni mashuhuda “Amoris laetitia” yaani “Furaha ya Upendo ndani ya familia.” Baba Mtakatifu Francisko katika Wosia wake wa Kitume: “Amoris laetitia” yaani “Furaha ya Upendo ndani ya familia anasema kama ilivyo katika mchakato wa uinjilishaji kuwa ni wajibu na utume wa wabatizwa wote, hivi ndivyo inavyopaswa kufanyika hata kwenye utume wa ndoa na familia. Utume wa familia unapania kunogesha upendo wa Mungu katika maisha ya kifamilia, kwa kuwajengea vijana uwezo wa kuanzisha familia zao. Wanafamilia washirikiane bega kwa bega na viongozi wao wa Kanisa ili kutangaza na kushuhudia: utakatifu, ukuu, ukweli, uzuri na changamoto za maisha ya ndoa na familia! Huu ni muda muafaka wa kusaidiana na kushikamana ili kusonga mbele kwa ari na moyo mkuu kwa kutambua kwamba, hata katika magumu na changamoto za maisha, Kristo Yesu bado anaendelea kuwepo katika Sakramenti ya Ndoa, ili kuwakirimia wanandoa: upendo, uvumilivu na matumaini kwa watu wote kila mtu kadiri ya hali yake ya maisha!

Mashuhuda wenye mvuto na mashiko katika maisha ya ndoa na familia
Mashuhuda wenye mvuto na mashiko katika maisha ya ndoa na familia

Baba Mtakatifu anawataka wanandoa na familia kuwa ni mashuhuda wenye mvuto na mashiko kwa vijana, ili hatimaye, vijana waweze kuona na kushuhudia kwa macho yao wenyewe uhalisia wa maisha ya ndoa na familia na kwamba, kufunga ndoa ni jambo linalowezekana na wala si ndoto ya kufikirika. Mama Kanisa anawahitaji wadau mbalimbali watakaoshirikiana naye katika kutangaza na kushuhudia Injili ya familia katika ulimwengu mamboleo. Ikumbukwe kwamba, Ndoa ni Sakramenti ya huduma inayowapatia wanandoa utume maalum wa ujenzi wa Kanisa. Wao wanatekeleza Ukuhani wa waamini wote katika Sakramenti. Familia ni Kanisa dogo la nyumbani, kumbe wazazi wanapaswa kuwa ni watangazaji na mashuhuda wa imani kwa ajili ya watoto wao, kwa maneno, lakini zaidi kwa matendo, ili kuwasaidia na kuwaelekeza watoto katika miito mbalimbali ya maisha. Upendo wa dhati unaobubujika kutoka katika familia una nguvu sana katika maisha na utume wa Kanisa. Kwa njia ya Sakramenti ya Ndoa, wanandoa wote wanakuwa ni amana na utajiri wa Kanisa. Baba Mtakatifu Francisko anawataka waamini waendelee kuwa ni vyombo na mashuhuda wa upendo wenye huruma unaobubujika kutoka kwa Kristo Yesu na Kanisa lake ili hatimaye, familia ziweze kukabiliana kikamilifu na changamoto mamboleo za: Ukata, ukosefu wa fursa za ajira, malezi tenge, ukosefu wa makazi ya kudumu, talaka, unyanyasaji, afya pamoja na umri mkubwa mambo yanayopelekea kumong’onyoka kwa kanuni maadili na utu wema.

Mpango Mkakati wa Ujenzi wa Tunu Msingi za Familia Bora Tanzania
Mpango Mkakati wa Ujenzi wa Tunu Msingi za Familia Bora Tanzania

Ni katika muktadha huu, hivi karibuni, Jumuiya ya Wanawake Wakatoliki Tanzania, WAWATA, imebainisha vipaumbele vyake kuwa ni: Malezi ya kifamilia ili kuunda jamii inayosimikwa katika maadili na tunu msingi za maisha ya kikristo; Pili ni Mwaliko wa kuwajali na kuwahudumia maskini na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa vipaumbele vya kijamii; Tatu ni utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote na Nne ni kutembea kwa pamoja kama sehemu ya ujenzi wa Kanisa la Kisinodi! Katika mahojiano maalum na Radio Vatican, baadhi ya wajumbe walikuwa na haya ya kusema: Stella Kahwa, Mwenyekiti WAWATA Jimbo kuu la Dar es Salaam na ambaye pia ni Katibu mkuu WAWATA, Taifa anasema, WAWATA kwa sasa inaandaa Mpango Mkakati wa Miaka mitano mintarafu ujenzi wa familia bora ndani ya Kanisa na jamii katika ujumla wake. Huu ni mpango mkakati unaopania pamoja na mambo mengine kutoa mafunzo ya awali na endelevu shuleni na kwenye makundi mbalimbali ya watu wa Mungu nchini Tanzania, kwa kukazia tunu msingi za maisha ya ndoa na familia, kanuni maadili na utu wema. Huu ni mwaliko kwa waamini na watu wote wenye mapenzi mema kuunga mkono juhudi hizi za WAWATA kwa kujikita katika tunu msingi za ndoa na familia. Kwa upande wake, Betrice Mkwela, Mwenyekiti WAWATA Jimbo Katoliki la Lindi, amekazia kuhusu uongozi kuwa ni huduma na kwamba, familia zijengwe kwenye msingi wa sala, maadili mema, utu na heshima ya binadamu. Wanawake watambue kwamba, wao ndio waalimu wa kwanza kwenye familia. Familia imara na thabiti ni chemchemi ya Kanisa imara na taifa lililo bora kimaadili.

Mpango Mkakati wa Familia

 

28 December 2024, 15:13