Tafuta

Cookie Policy
The portal Vatican News uses technical or similar cookies to make navigation easier and guarantee the use of the services. Furthermore, technical and analysis cookies from third parties may be used. If you want to know more click here. By closing this banner you consent to the use of cookies.
I AGREE
MASIFU YA ASUBUHI KWA KILATINI
Ratiba Podcast
Huruma ya Mungu ndiyo mahangaiko ya upendo wake kwa binadamu dhaifu na mdhambi. Huruma ya Mungu ndiyo mahangaiko ya upendo wake kwa binadamu dhaifu na mdhambi.  

Tafakari Dominika IV Kwaresima Mwaka C: Huruma Na Upendo Wa Mungu Kwa Wadhambi!

Kimsingi, huruma ya Mungu inawawezesha waamini na watu wote wenye mapenzi mema, kuwa ni vyombo na mashuhuda wa haki, amani na upatanisho. Ikumbukwe kwamba, huruma ya Mungu ni kiini cha imani, maisha na utume wa Kanisa; ushuhuda makini wa Ufufuko wa Kristo Yesu. Bikira Maria, Mama wa huruma ya Mungu awasaidie waamini: kuamini na kuyaishi yote haya kama mashuhuda wa Injili ya huruma, furaha na mapendo! Huruma, Upendo na Msamaha!

Na Padre Bonaventura Maro, C.PP.S., - Kolleg St. Josef, Salzburg, Austria.

Utangulizi. Wapendwa Taifa la Mungu, leo ni Dominika ya 4 ya Kipindi cha Kwaresima, Mwaka C wa Kanisa. Dominika ya nne ya Kwaresima hujulikana kama, “Sunday Laetare” yaani Dominika ya Furaha. Tunafurahi kwa kuwa tumekaribia kuadhimisha fumbo la Ukombozi wetu, yaani mateso, kifo na ufufuko wa Bwana wetu Yesu Kristo Liturujia ya Neno la Mungu katika Dominika hii ya nne ya Kwaresima inatutafakarisha juu ya, “Furaha ya kupatanishwa na Mungu Baba Mwenye Huruma” Mwenyezi Mungu ni Baba yetu mwenye Huruma, hafurahii kifo cha mtu mwovu bali anatutaka kila mmoja kuacha mwenendo wake mbaya ili aishi. Anatupokea kila mara tunapotambua upotovu na udhaifu wetu na kuamua kufanya toba na wongofu wa ndani. Huruma ya Mungu ndiyo mahangaiko ya upendo wake kwa binadamu dhaifu na mdhambi. Mwenyezi Mungu anajisikia kuwajibika, kwa maana ya kwamba, anatamani kuwaona watu wake wakiwa na afya njema, furaha na amani tele nyoyoni mwao. Hii ni njia ambayo upendo wa huruma ya Wakristo unaopaswa pia kujimwilisha. Huruma ndiyo msingi thabiti wa uhai wa Kanisa. Kazi zake zote za kichungaji zinapaswa kufungamanishwa katika upole linalouonesha kwa waamini; hakuna chochote katika mahubiri na ushuhuda wake kwa ulimwengu kinachoweza kukosa huruma. Umahiri wa Kanisa unaonekana kwa namna linavyoonesha huruma na upendo. Huruma ya Mungu inafungua malango ya moyo ili kuonesha upendo na ukarimu kwa watu wanaoishi katika upweke na kusukumizwa pembezoni mwa jamii, ili kweli waweze kujisikia ndugu na watoto wapendwa wa Baba wa milele kama ilivyokuwa kwa Mwana mpotevu, shilingi na kondoo aliyepotea. Huruma ya Mungu inawawezesha watu kutambua na kuguswa na mahitaji msingi ya jirani zao hasa wale wanaohitaji kuonjeshwa faraja na upendo. Kimsingi, huruma ya Mungu inawawezesha waamini na watu wote wenye mapenzi mema, kuwa ni vyombo na mashuhuda wa haki, amani na upatanisho. Ikumbukwe kwamba, huruma ya Mungu ni kiini cha imani, maisha na utume wa Kanisa; ushuhuda makini wa Ufufuko wa Kristo Yesu. Bikira Maria, Mama wa huruma ya Mungu awasaidie waamini: kuamini na kuyaishi yote haya kama mashuhuda wa Injili ya huruma, furaha na mapendo.

Mahujaji wa Matumaini
Mahujaji wa Matumaini   (AFP or licensors)

Kwa kuadhimisha Pasaka, Waisraeli walifurahia na kukumbuka jinsi Mwenyezi Mungu alivyowakomboa kutoka utumwani katika mateso na kuwafikisha katika nchi ya ahadi (Yos 5:9a, 10-12). Nasi kwa kuadhimisha Fumbo la Pasaka, tunafurahia na kushangilia jinsi Mungu, Baba mwenye Huruma kwa njia ya Mwanaye wa Pekee Yesu Kristo anavyotupatanisha tena sisi wana wapotevu na Baba na kuturudisha tena nyumbani kwa Baba kwa kutupatia zawadi ya uhai na uzima wa milele (Lk 15:1-3, 11-32). Katika Dominika ya Nne ya Kipindi cha Kwaresima Mwaka C wa Kanisa, tumshukuru Mungu, Baba yetu Mwenye Huruma, ambaye ametupa tena uhai na uzima sisi ambao tulikua tumekufa kwa sababu ya dhambi (2 Kor 5:17-21). Tunaalikwa kutambua Huruma kubwa ya Mungu Baba yetu (Zab 34:1-6), na kuwa tayari kubadilisha mitazamo na maisha yetu ili tuupate uzima wa milele, tupate neema ya kuishi milele nyumbani kwetu, yalipo makazi yetu ya kudumu huko mbinguni. Somo la 1: Ni kitabu cha Yoshua 5:9a, 10-12. Somo la kwanza tulilolisikia, kutoka kitabu cha Yoshua, ni simulizi la Pasaka ya kwanza ya wana wa Israeli wakiwa katika nchi ya Ahadi. Katika Pasaka hii walisherehekea na kukumbuka jinsi Mungu mwenye huruma, licha ya historia yao na ukosefu wao wa uaminifu katika historia na mahusiano yao na Mungu tangu walipotoka tumwani Misri, bado Mungu anawafikisha katika nchi ya ahadi. Kabla ya kuadhimisha kumbukumbu hii muhimu walirudia tena Agano na Mungu kwa njia ya kutahiriwa, Agano ambalo Mungu aliweka hapo mwanzo na Abrahamu (Mwa 17:9-14).  Kumbe ili waweze kuadhimisha vyema Pasaka, sherehe kubwa ya kukumbuka ukombozi wao, walipaswa kujitakasa na kujipatanisha tena na Mungu. Kisha wanaadhimisha pasaka kwa kula mazao ya nchi, ishara ya kuwa, Mwenyezi Mungu amewakabidhi ardhi ile kuwa mali yao kabisa. Na mazao ya kwanza ndiyo waliyotumia kuadhimisha Pasaka yao ya kwanza. Pasaka hii yaonesha Mwanzo mpya, kutoka utumwani katika shida na mateso na taabu, kwenda katika utulivu na kufurahia tena kurudi nyumbani katika ardhi ambayo Mungu aliwaahidi Baba zao.

Injili ya Baba Mwenye huruma kwa watoto wake wote
Injili ya Baba Mwenye huruma kwa watoto wake wote   (VATICAN MEDIA Divisione Foto)

Ndugu zangu katika somo hili la kwanza tuna mambo manne ya kujifunza. Kwanza: Dhambi ilitutenganisha na Mungu Baba yetu Mwema. Taifa la Israeli walikua utumwani Misri kwa muda wa miaka 430, huko walikua mbali na Mungu, waliteseka na kunyanyasika, waliumizwa na walidharauliwa na kwa kuabudu miungu mingine walikua mbali na Mungu wao. Licha ya hayo, kwa kukosa uaminifu kwa amri na Agano walilofanya na Mungu, wengi hawakupata nafasi ya kuingia katika Nchi ya Ahadi licha ya kwamba Mungu alikwishawaahidi na kuwapa kila walichohitaji ili kuingia katika nchi hiyo. Ndugu wapendwa, dhambi inatutenga sisi na Mungu. Inaharibu mahusiano mazuri yaliyo kati yetu sisi na Mungu na matokeo yake mahusiano mema kati yetu sisi kwa sisi pia yanaharibika nasi tunakosa kufaidi ahadi ya Mungu wetu ya uzima wa milele. Kipindi cha Kwaresima ni muda kila mmoja kujitafakari, Je, nipo/upo mbali kiasi gani au karibu kiasi gani na Mungu? Je, nipo mbali kiasi gani mimi na roho yangu? Je, nafanya hija ndani ya moyo wangu na kukagua umbali au ukaribu nilio nao na Mungu wangu, au kati yangu mimi na wenzangu? Nipo mbali kiasi gani na familia yangu, Padre mwenzangu, mtawa mwenzangu, mwanandoa mwenzangu, Watoto wangu, wanajumuiya wenzangu, wafanyakazi wenzangu nk? Huenda vilema na udhaifu wangu vinaweka mbali siku baada ya siku na Mungu wangu kisha kuwa mbali zaidi zana na wale wote ninaoishi nao katika maisha yangu ya kila siku. Tukitambua dhambi inatutenga na Mungu tunafanya jitihada za kuzingatia moyoni na kuamua kwa haraka kurudi kwa Mungu Baba yetu mwema mwenye huruma.

Sakramenti ya Upatanisho ni chemchemi ya uhuru wa ndani
Sakramenti ya Upatanisho ni chemchemi ya uhuru wa ndani   (Vatican Media)

Pili: Mwenyezi Mungu mwenye huruma anatutoa katika utumwa na aibu ya dhambi. Yoshua anawaambia taifa la Israeli kwamba, “Mwenyezi Mungu siku hii ya leo ameiviringisha hiyo aibu ya Misri iondoke juu yenu” Tukio hili la kuadhimisha pasaka laonesha mwisho wa maisha ya mateso na utumwa na Mwanzo wa maisha mapya ndani ya Nchi ya Ahadi. Wanakumbuka siku Mwenyezi Mungu alipowakumbuka na kuwatoa katika utumwa na kuanzisha safari yao mpya ya ukombozi kuelekea katika nchi ya ahadi. Ndugu mpendwa, Mwenyezi Mungu mwingi wa huruma, anawapenda na kuawahurumia watu wake. Aliona na kuguswa na mateso ya watu wake waliokuwa utumwani Misri kama tulivyosikia katika somo la Dominika iliyopita (Kut 3:1-8a, 13-15), na kwa njia ya Musa akaanzisha safari ya ukombozi wa taifa lake. Ni mapendo yasiyo na mipaka ya Mungu kwetu sisi watoto wake, Mungu asiyependa tuabikie wala tupotee kwa sababu ya dhambi. Pasaka ya Mwaka huu wa Jubilei hii inatukumbusha mwanzo mpya wa maisha. Yatukumbusha thamani ya ukombozi wetu, kwa fumbo la Pasaka jinsi Mwenyezi Mungu alivyotukomboa sisi kutoka katika utumwa wa dhambi na mauti. Aliguswa na hali yetu dhaifu, hali ya kufa, hali ya utumwa wa dhambi na kifo na akaanzisha mpango mpya wa ukombozi wetu. Kumbe twapaswa kuishi maisha mapya kama wana wa Mungu ambao tunashiriki zawadi hii ya ukombozi kwa njia ya Ubatizo wetu. Pasaka yatukumbusha ahadi zetu za ubatizo na uaminifu kwa Mungu katika maagano tuliyofanya naye.

Baba Mwenye huruma: Kufanya Sherehe iliwapasa!
Baba Mwenye huruma: Kufanya Sherehe iliwapasa!   (Vatican Media)

Tatu: Kabla ya kusherehekea Pasaka, tunapapaswa kujitakasa kwa toba na wongofu wa ndani. Kabla ya kusherehekea Pasaka, Waisraeli walitahiriwa, ishara ya utakakaso na kustahilishwa ahadi za Mungu kama taifa teule la Mungu, ahadi ambazo Mwenyezi Mungu alimwahidi Abrahamu na uzao wake hata milele. Hivyo kwa kutahiriwa wakastahilishwa kuwa sehemu ya taifa teule la Mungu na hivyo kufurahia tukio kubwa la kumbukumbu ya ukombozi wao. Ndugu wapendwa, Mama Kanisa ametupatia kipindi cha Kwaresima, siku arobaini, muda wa kutosha ili tujiandae kila mmoja kusherehekea fumbo kubwa la ukombozi wetu yaani mateso, kifo na ufufuko wa Bwana wetu Yesu Kristo. Ni muda wa kujiandaa, muda wa kujitakasa ili tufufuke pamoja na Kristo kama wana wateule wa Mungu, tunaotarajia utimilifu wa ahadi ya Mungu, ahadi ya uzima wa milele. Tujitakase kwa njia ya Sakramenti ya Upatanisho mara nyingi iwezekanavyo. Tupokee pia Ekaristi Takatifu ili Yesu akae daima ndani mwetu, atakase mawazo, maneno, na Matendo yetu ili daima tuwaze na kutenda yale yampendezayo Mungu wetu. Nne: Kila tunapoadhimisha Ekaristi Takatifu, tunamshukuru Mungu kwa zawadi ya ukombozi. Taifa la Israeli walifanya Pasaka ya kwanza kwa kutumia mazao waliyoyapata wakiwa katika nchi ya Ahadi, ishara kwamba, nchi ile ilitoa mazao yake nayo ilikua ni mali yao kwa vizazi vyote. Ni ishara ya kwamba sasa walikua si wasafiri tena bali walipata makazi ya kudumu tena, walirejea nyumbani kwa Baba. Na baada ya kula pasaka ile, manna ambayo ilikua ikidondoka kwa miaka 40 haikudondoka tena, ishara ya utimilifu wa ahadi ya Mungu. Hawakuhitaji tena manna kwa kuwa walikua tayari katika nchi yenye utajiri wote. Ndugu wapendwa, kwa njia ya Bwana wetu Yesu Kristo Mungu ametupa utimilifu wa ahadi ya uzima wa milele. Ekaristi Takatifu ni adhimisho la karamu ya Bwana, tunaposherehekea fumbo la Pasaka, Kristo anayejitoa yeye bila kujibakiza kwa ajili ya uzima wa ulimwengu. Ametupa yote aliyokua nayo ili yawe yetu. Ametwaa hali yetu ya ubinadamu ili atushirikishe umungu wake.  Huu ni ukarimu wa Kimungu. Sisi sote tupo ndani ya kanisa, humo twapata utajiri wote. Humo kwanza tunabatizwa na kuwa Watoto wa Mungu, tunaondolewa dhambi ya asili ili tuwe warithi wa ahadi za Mungu pamoja na Kristo. Pili, tunapokea Sakramenti nyingine za kanisa za kutuimarisha katika safari yetu ya maisha hapa duniani. Tumamshukuru Mungu ambaye ametupa uhai na uzima wa milele kwa njia ya Bwana wetu Yesu Kristo.

Dhambi inaharibu mahusiano na Mungu pamoja na jirani
Dhambi inaharibu mahusiano na Mungu pamoja na jirani   (Vatican Media)

Somo la Injili: Ni Injili kama ilivyoandikwa na Luka15:1-3, 11-32. Somo la Injili Takatifu kutoka katika Injili ya Luka 13:1-9, ni simulizi ya mfano wa Yesu kuhusu Mwana mpotevu. Mfano huu watokana na manung’uniko ya mafarisayo na waandishi juu ya ukaribu wa Yesu kwa watoza ushuru na wenye dhambi, kwamba aliwakaribisha, na alikula nao chakula (Lk 15:1-3). Yesu anatoa mifano mitatu katika hii sura ya 15, kwanza, mfano wa kondoo aliyepotea (Lk 15:1-7) pili mfano wa sarafu iliyopotea (Lk 15:8-10) na kisha mfano huu ambao tumeusikia katika dominika ya leo wa Mwana mpotevu (Lk 15:1-3, 11-32). Katika mifano yote hii mitatu yatuonesha jinsi Mungu mwenye huruma anavyofanya jitihada (unconditional initiatives) kumtafuta mwanadamu aliyepotea na furaha ipatikanayo kwa mmoja aliyepotea anapoamua kuacha njia ya upotevu na kurudi nyumbani kwa Baba mwenye huruma. Kumbe mfano wa Mwana mpotevu wamtambulisha kwetu Mwenyezi Mungu, Baba mwenye huruma isiyo na mipaka, ambaye daima yupo tayari kutupokea tena, licha ya dhambi na udhaifu wetu, bado anatupokea, anatukaribisha, anatubusu, anatuvika pete na vazi jipya na kufanya sherehe. Kumbe Yesu nawafundisha mafarisayo na anatufundisha sisi sote kwamba kila mtu ana nafasi nyumbani kwa Baba na anakaribishwa kuukumbatia tena ufalme wa Mungu licha ya dhambi na udhaifu wetu, tunachotakiwa kufanya ni kutubu na kuanza maisha mapya.

Baada ya toba na wongofu wa ndani kuna karamu ya Pasaka
Baada ya toba na wongofu wa ndani kuna karamu ya Pasaka   (Vatican Media)

Katika somo hili la Injili dominika ya Nne ya Kipindi cha Kwaresima tuna mafundisho matano ya kujifunza. Kwanza: Tunapaswa kufurahi pale wenzetu wanapotafuta wongofu na maisha mapya. Yesu mara kadhaa aliingia katika mgogoro na mafarisayo na waandishi kwa kuwa alikula na kushirikiana na wale walioonekana katika jamii ya Wayahudi kwamba walikua wenye dhambi. Watoza ushuru walihesabiwa kuwa wenye dhambi kwanza kabisa kwa kuwa walifanya kazi iliyokua haina usawa, walitoza watu zaidi ya kiwango na kuwanyanyasa pia watu. Pili walishirikiana na warumi ambao kwa muda mrefu waliwakandamiza wayahudi na hivyo moja kwa moja wakaonekana kama hawastahili kuupata ufalme wa mbinguni. Licha ya hayo, hawa walikua tayari kumpokea Yesu na mafundisho yake na kuupokea ufalme wake. Ndugu wapendwa, mara kadhaa mimi na wewe tunaweza kuwa na mtazamo kama huu wa mafarisayo na watoza ushuru. Pengine tunaishi na wenzetu katika jamii na jumuiya zetu hata katika familia zetu ambao pengine ni waregevu na wamerudi nyuma kiimani. Mara nyingi tunaishia pengine kuwanyooshea vidole badala ya kufanya jitihada katika kuwarudisha tena katika Imani thabiti. Pengine tunaweza kuwakatisha tamaa pia wale ambao wanafanya jitihada mbalimbali katika kujikwamua kutoka kwenye hali zao fulani za maisha, pengine kwa kujua historia zao tunaona kama hakuna uwezekano wowote kwao kuboresha chochote. Tufurahi pale mmoja anapoonesha jitihada katika kufanya mabadiliko katika maisha, katika masomo, katika mahusiano, katika biashara, katika ndoa, familia nk. Tusiwazibie njia wengine pale wanapotaka kupiga hatua flani katika maisha ya kiimani au maisha ya kawaida ya kila siku. Mungu atusadie ili tuwe tayari kufufahia na kushiriki katika mabadiliko na maendeleo ya wenzetu.

Waamini wanatumwa kutangaza na kushuhudia kweli za Kiinjili
Waamini wanatumwa kutangaza na kushuhudia kweli za Kiinjili   (VATICAN MEDIA Divisione Foto)

Pili: Mwenyezi Mungu ametupa kila neema na baraka ili tuishi na kumtumikia vyema kama wanawe. Katika mfano huu wa mwana mpotevu, tunamwona mwana mdogo akiomba sehemu ya mali yake iliyomwangukia. Baba mwema na mwenye huruma akawagawia wote vitu vyake (de dielien autois ton bion). Baba alitoa si tu mali yake, bali aliwapa vyote alivyokuwa navyo, aliwapa maisha yake yote (ton Bion). Ndugu wapendwa, Mwenyezi Mungu ametupa kila tunachohitaji ili tuweze kuishi maisha mazuri, maisha matakatifu yenye kumpendeza. Ametupa zawadi ya Mwanaye wa pekee Yesu Kristo, ambaye kwa njia yake sisi sote tumepata uzima na uhai tele. Ametupa zawadi ya mwili wake na Damu yake, ili tuwe daima hai, tupate nguvu na afya rohoni za kuweza kumtumika vizuri zaidi Mwenyezi Mungu ametupa sakramenti nyingine mbaimbali za kanisa, ambazo kwazo tunaboresha siku kwa siku mahusiano yetu na Mungu. Tunaalikwa katika kipindi hiki cha Kwaresima na katika maisha yetu, tutumia vyema neema na baraka hizi za Mungu ili tuishi maisha mema, maisha yanayompendeza Mungu.

Kwaresima ni kipindi cha toba, wongofu na utakatifu wa maisha
Kwaresima ni kipindi cha toba, wongofu na utakatifu wa maisha   (Vatican Media)

Tatu: Tunapojitenga na Mungu na kutumia vibaya neema na baraka zake, tunapoteza urithi wetu wa uzima wa milele. Mwana mpotevu alipopata sehemu ya urithi wake iliyomwangukia, aliamua kukusanya vyote akasafiri na kwenda nchi ya mbali, akatapanya huko mali zake kwa maisha ya uasherati. Ni kama alimwua Baba yake, kwanza kwa kutaka uruthi wakati alikuwa bado hai, na pili kwa kuona kuwa hakuhitaji tena chohote kutoka kwa Baba. Mwana huyu mpotevu anawakilisha yeyote, mimi na wewe ambao mara kadhaa kwa kumwasi Mungu tunapoteza neema na baraka zake zilizo muhimu kabisa katika maisha yetu. Ndugu mpendwa, tunapaswa kutambua kuwa kila mmoja wetu ni mwana mpotevu. Mara kadhaa tunaweza kutafuta kuwa huru katika maisha yetu hata kwa kumwacha Mungu. Kwa uhuru wetu wenyewe twaweza kuchagua kuishi pasi na Mungu, kuishi maisha ya uregevu, maisha ya anasa na starehe, na kusahau kuwa maisha yetu, uhai wetu wa kweli upo katika kumtatuta Mungu, kuishi na Mungu an kufa tukiwa tumeungana na Mungu wetu. Pengine naweza kuvipa kipaumbele vitu na mambo mengine na kumsahau Mungu. Mwanaharakati maarufu nchi marekani, Martin Luther King aliwahi kusema, “Nimeshikilia mambo mengi sana mikononi mwangu na nimeyapoteza yote; lakini kila kitu ambacho nimeweka mikononi mwa Mungu bado ninakimiliki” Tunapofurahia zawadi ya ukombozi tulioupata kwa njia ya mwanaye mpenzi Yesu Kristo, tuombe neema ya kuyaweka mambo yote mikononi mwake, hata sisi wenyewe ili daima tumiliki yote pamoja naye.

Kwaresima ni kipindi cha sala na tafakari ya kina ya Neno la Mungu
Kwaresima ni kipindi cha sala na tafakari ya kina ya Neno la Mungu   (Vatican Media)

Nne: Mungu, Baba mwenye Huruma anatupokea na anafurahia tena pale tunapozingatia moyoni na kuamua kurudi kwake kwa toba. Baada ya kutapanya mali zake zote kwa maisha mabaya ya uasherati, njaa kuu iliikumba nchi ile. Njaa kali ni ishara ya ukavu rohoni, hali ya mtu aishiye mbali na Mungu aliye asili ya mema yote. Anazingatia moyoni, maana yake anaamua kurudi ndani kabisa ya moyo wake, anafanya tathmini na kuamua kuanza maisha mapya. Ametambua makosa na uasi wake dhidi ya baba na yupo tayari kurudi kwa Baba ambapo hakukosa kitu chochote. Anaporudi kwa Baba, baba anamkaribisha tena, anambusu, anamvalisha vazi jipya, na anamfanyia sherehe. Ndugu mpendwa, Mungu wetu mwenye Huruma anatupenda na yupo anatutafuta tena pale tunapopotea kwa sababu ya dhambi zetu. Katika mifano yote mitatu katika hii sura ya 15 Yesu anatuonesha jinsi Mungu anavyofanya jitihada kuturudisha kwake. Kipindi cha Kwaresma kila mmoja anaalikwa kufikiri moyoni mwake, kutathmini mahusiano yetu ya Mungu na kuamua kufanya mabadiliko ya ndani yaani Metanoia. Fikiri furaha kubwa niipatayo/uipatayo pale unapoambiwa, “Mwanangu, dhambi zako zote zimeondolewa, nenda kwa amani” baada ya sakaramenti ya kitubio. Ni Mungu anayekukumbatia, anakuvika taji, anakuvika pete, anafanya sherehe kwa kiroho tunakua hai tena. Mara kadhaa tunaweza kufikiri tu dhaifu, tunaweza kuwaza kuwa dhambi zetu ni nyingi na udhaifu wetu ni mkubwa na hivyo kuona mashaka juu ya huruma ya Mungu ipatikanayo kwa njia ya sakramenti mbalimbali za kanisa. Mwenyezi Mungu anatupokea sote kila mara tunapoamua kuacha maisha ya zamani na kuanza maisha mapya. Anatupokea, anatuvika vazi jipya, ishara ya kuzaliwa tena upya na anaturudishia tena hadhi ya kuitwa wanawe baada ya kuwa wafu kwa sababu ya dhambi.

Huruma ya Mungu ni tunda la Kipasaka, mateso, kifo na ufufuko
Huruma ya Mungu ni tunda la Kipasaka, mateso, kifo na ufufuko   (Vatican Media)

Tano: Hatupaswi kujihesabia kuwa wenye haki kuliko wengine, sote tu na haki sawa nyumbani kwa Baba. Mwana mkubwa anaumia na kunung’unika kwa yale Baba aliyomtendea mwanaye mpotevu. Alimfanyia sherehe, akamvika vazi jipya, akamchinjia Mwanakondoo, na kumvika pete. Mwana mkubwa analalamikia huruma ya Baba kwa Mwana mpotevu. Lakini Baba anamhakikishia kuwa huruma ya Baba ni kwa wote, yeye si mtumwa, bali pia ni mwana wa pekee. Ndugu Wapendwa, mtazamo wa huyu mwana mkubwa ndio ulikua mtazamo wa Mafarisayo na waandishi, wananung’unika kuona huruma ya Mungu ikiwafikia hata wale waliokuwa wadhambi na dhaifu. Huruma ya Mungu ni ya milele. Inapatikana bure kabisa kutoka kwa Mungu kwa yule aliye tayari kuipokea na kukubali ifanye kazi ndani mwake. Tusiumia pale huruma ya Mungu inapofanya kazi ndani ya maisha ya wengine. Tumshukuru Mungu na kumfurahia Mungu anayetaka kila mtu aikumbatie huruma yake ili apate kuishi.

Waamini wanahamasishwa kuwa ni mashuhuda wa huruma na upendo
Waamini wanahamasishwa kuwa ni mashuhuda wa huruma na upendo

Somo la pili: Ni Waraka wa Mtume Paulo 2 Kor 5:17-21. Katika somo la Pili, Mtume Paulo anatufundisha kuwa, kwa njia ya Kristo sisi sote tumepita kutoka maisha ya utumwa na dhambi na kuanza maisha mengine mapya. Ni mpango wa Mungu kwamba sisi sote tuupate uzima wa milele, na hivyo kwa njia ya mwanaye Yesu Kristo anatupatia sisi sote upatanisho, sisi tuliotengwa hapo mwanzo na Mungu kwa sababu ya dhambi. Anatuasa kuwa hitaji la kujipatanisha na Mungu ni hitaji letu la kila siku, ni jitihada ya kudumu ili tuweze kupata neema ya kuurithi ufalme wa Mbinguni. Hitimisho: Katika Dominika ya Nne ya Kipindi cha Kwaresima Mwaka C wa Kanisa, tumshukuru Mungu, Baba yetu Mwenye Huruma, ambaye ametupa tena uhai na uzima sisi ambao tulikua tumekufa kwa sababu ya dhambi (2 Kor 5:17-21). Tunaalikwa kutambua Huruma kubwa ya Mungu Baba yetu (Zab 34:1-6), na kuwa tayari kubadilisha mitazamo na maisha yetu ili tuupate uzima wa milele, tupate neema ya kuishi milele nyumbani kwetu, yalipo makazi yetu ya kudumu huko mbinguni.

Baba Mwenye Huruma
28 Machi 2025, 14:50
Prev
April 2025
SuMoTuWeThFrSa
  12345
6789101112
13141516171819
20212223242526
27282930   
Next
May 2025
SuMoTuWeThFrSa
    123
45678910
11121314151617
18192021222324
25262728293031