Tafuta

Cookie Policy
The portal Vatican News uses technical or similar cookies to make navigation easier and guarantee the use of the services. Furthermore, technical and analysis cookies from third parties may be used. If you want to know more click here. By closing this banner you consent to the use of cookies.
I AGREE
Miserere
Ratiba Podcast
Liturujia ya Neno la Mungu katika Dominika ya pili ya Kwaresima inatualika, “kufanya mabadiliko ya ndani.” Liturujia ya Neno la Mungu katika Dominika ya pili ya Kwaresima inatualika, “kufanya mabadiliko ya ndani.”  

Tafakari Dominika ya Pili Kwaresima Mwaka C wa Kanisa: Utu wa Ndani!

:Kugeuka sura kwa Bwana wetu Yesu Kristo kunatupa nguvu na matumaini ya kuchukua misalaba yetu, Kristo Yesu aligeuka sura ili kuwaimarisha Mitume wake alipokuwa anakaribia mateso, kifo na ufufuko wake, ili wawe imara katika imani matumaini na mapendo. Katika nyakati ngumu katika safari yetu ya maisha, hasa tunapochukua misalaba Yetu, kugeuka sura kwa Bwana wetu Yesu Kristo kunatupa nguvu ya kusonga mbele katika kubeba misalaba yetu kwa matumaini.

Na Padre Bonaventura Maro, C.PP.S., -Kolleg St. Josef, Salzburg, Austria.

Utangulizi: Wapendwa Taifa la Mungu, leo ni Dominika ya 2 ya Kwaresima, mwaka C wa Kanisa. Liturujia ya Neno la Mungu katika Dominika ya pili ya Kwaresima inatualika, “kufanya mabadiliko ya ndani.” Kipindi cha Kwaresima ni mwaliko wa mabadiliko ya ndani, kuacha maisha ya kale na kuanza maisha mapya. Bwana wetu Yesu Kristo anabadilika sura mlimani Tabor, tukio hilo laeleza juu ya Fumbo la Pasaka yaani mateso, kifo na ufufuko wake. Ni kwa njia ya ubatizo wetu nasi sote tunashiriki fumbo la pasaka yaani mateso kifo na ufufuko wa Bwana wetu Yesu Kristo na hivyo tunashirikishwa utimilifu wa ahadi ya Mungu kwetu yaani uzima wa milele. Katika Dominika ya leo, tumshukuru Mungu ambaye ni mwaminifu kwa ahadi na Agano alilofanya nasi wakati wote. Ili tufaidi ahadi yake ya uzima wa milele, tunaalikwa kuwa tayari kupokea mwaliko wa mabadiliko, mwaliko wa kutubu na kuiamini Injili. Tuombe pia neema ya kushiriki mateso pamoja na Kristo ili tushiriki pia utukufu pamoja naye. Somo la Kwanza: Ni kutoka Kitabu cha Mwanzo 15:5-12, 17-18. Somo la kwanza tulilolisikia, kutoka kitabu cha Mwanzo, Mwenyezi Mungu anamwita tena Abram (baadaye ataitwa Abraham) na anafanya naye Agano tena. Abram, anatajwa kama mtu wa kwanza baada ya Nuhu kuisikia na kuitii sauti ya Mungu. Abram alipoitwa (Mwanzo 12:1-9) atoke kutoka katika nchi yake na kwenda katika nchi ambayo Mungu alimwamuru, aliitika na kupokea mabadiliko, kutoka kuwa mpagani hadi kuwa na Imani thabiti kwa Mungu. Kama thawabu kwa utii na Imani, Mwenyezi Mungu anamwahidi Abram uzao (numerous descendants), ardhi (land) na baraka (Blessings). Abram anataka uthibitisho wa ishara, kwamba kweli Mungu atatimiza hayo yote. Mwenyezi Mungu anaweka Agano naye kwa kutumia ishara iliyofahamika sana. Katika tamaduni za wayahudi, watu wawili wakitaka kuweka Agano yaani makubaliano ya kudumu, walimkata mnyama vipande viwili, na kuviweka ardhini. Kisha walipita katikati ya vipande hivyo, ikiwa ni ishara kwamba iwapo mmoja kati yao angekiuka Agano lile basi na akatwe vipande viwili. Lakini hili ni Agano kati ya Mungu na Abram, ni Mungu aliamua kumchagua Abram na kufanya naye Agano na hivyo hakupaswa kupita kati ya vipande viwili vya mnyama. Agano hili kati ya Mungu nasi linathibitishwa kwa njia ya mateso kifo na ufufuko wa Bwana wetu Yesu Kristo.

Kristo Yesu amefanya Agano Jipya na la Milele kwa Damu yake Azizi.
Kristo Yesu amefanya Agano Jipya na la Milele kwa Damu yake Azizi.

Ndugu zangu katika somo hili la kwanza tuna mambo matatu ya kujifunza. Kwanza: Imani thabiti kwa Mungu inatusaida kubadili mitazamo yetu (centrality of faith). Katika somo la kwanza, Abram alikua na imani thabiti kwa Mungu tangu alipoitwa mara ya kwanza (Mwanzo 12:1-9), akaacha ardhi, akaacha ndugu na jamaa zake, akaacha mali zake na akapokea mwaliko wa mabadiliko na kuanza maisha mapya. Katika somo tulilolisikia, Mungu anampa Abram ahadi ambazo kibinadamu zilionekana kama haziwezekaniki, lakini bado Abram aliamini. Ndugu wapendwa, katika maisha yetu, tunaalikwa kuwa na imani thabiti kwa Mungu wetu kama Baba yetu wa imani Abram. Imani ni kuwa na hakika ya mambo yatarajiwayo, ni bayana ya mambo yasioyoonekana (Ebr 11:1-3). Kuna nyakati tunaweza kuwa na imani haba juu ya utendaji kazi wa Mungu katika maisha yetu. Twaweza kuwa na shaka kama kweli yupo kati yetu kutokana na changamoto mbalimbali tunazopitia kila mmoja katika maisha yake ya ufuasi. Tunakua na hofu na mashaka kama kweli anatatimiza ahadi zake alizosema nasi, atajibu maombi na sala zetu kwa mahitaji yetu mbalimbali ambayo tumemwomba. Mara kadhaa tunaona kama changamoto zetu ni kubwa kuliko ahadi za Mungu. Ndugu mpendwa, Mungu anaona imani na matumaini yetu kwake. Anahitaji tu tubadili mitazamo yetu, tuweze kuwaza na kuona kwa jicho la kimungu, kwamba, yeye ni Mungu, yeye Baba yetu mwema, yeye ni mweza wa yote, yeye anajua yote na kwamba atatimiza ahadi zake kwetu kwa wakati wake. Imani ya Abram iwe imani yangu mimi na wewe. Abraham anaoneshwa nyota za angani, ishara ya baraka zisizohesabika. Ninakuombea imani thabiti ili wingi wa baraka zisizohesabika ziwe katika maisha yako, na kupitia wewe watu wengine wakauone mkono wa Mungu.

Waamini wanapaswa kuwa ni mashuhuda wa Agano Jipya na la milele
Waamini wanapaswa kuwa ni mashuhuda wa Agano Jipya na la milele

Pili: Mwenyezi Mungu amejifunua kwetu, amefanya Agano na kila mmoja wetu, anatudai uaminifu. (Definitive revelation of God and an invitation to covenantal faithfulness). Katika somo la kwanza tumesikia namna Mwenyezi Mungu alivyofanya Agano na Abram. Mwenyezi Mungu anajifunga katika Agano na Abram, anathibitisha hilo kwa ishara ya tanuru ya moshi na mwenge unaowaka ukapita kati ya vipande vya nyama kutoka kwa wanyama ambao Mungu alimwamuru Abramu kuwachinja. Mwenge ni ishara ya uwepo wa Mungu na vipande viwili vyaonesha kufungwa kwa Agano kati ya Mungu na Abram. Ndugu Wapendwa, Mwenyezi Mungu amejifunua kwetu kwa njia ya mwanaye mpenzi Yesu Kristo, ambaye kwa njia ya mateso, kifo na ufufuko wake, ameweka Agano jipya na la milele kati yake na sisi. Sisi sote kwanza kabisa kwa njia ya ubatizo wetu tunafanya Agano na Mungu, tunakuwa watoto wa Mungu na Mungu anakuwa Baba yetu. Agano hilo linatudai uaminifu. Ubatizo unatubadili, tunavuliwa utu wa kale na kuvikwa utu mpya, tukialikwa kuishi maisha mapya ndani ya Kristo. Katika kipindi hiki cha Kwaresima, kila mmoja anakumbushwa juu ya Agano alilofanya na Mungu na namna tunapaswa kuwa waaminifu kwa maagano hayo. Kila siku, Yesu anajifunua kwetu kwa njia ya Neno lake Takatifu, na kwa njia ya Sakramenti za kanisa. Anatutafuta kila tunaposhindwa kuishi vyema ukristo wetu. Anatukumbusha kuwa anatupenda na kamwe hafurahii kifo cha mtu mwovu. Anatualika kufanya mabadiliko na kuanza tena upya katika maagano tuliyofanya naye. Mungu anatupenda.

Tunakutana na Mungu katika: Neno, Sakramenti na Huduma kwa jirani
Tunakutana na Mungu katika: Neno, Sakramenti na Huduma kwa jirani

Tatu: Tunapokutana na Mungu tunakutana na nguvu yake inayotubadilisha (God’s transformative power). Abram jua lilipokuwa likichwa usingizi mzito ulimshika, hofu ya giza kuu ikamwangukia. Ikawa jua lilipokuchwa likawa giza, tazama tanuru ya moshi na mwenge unaowaka ulipita kati ya vile vipande vya nyama. Tanuru ya moshi na mwenge ni ishara ya uwepo wa Mungu. Ndugu Wapendwa, tunapokutana na Mungu, tunakutana na nguvu yake inayotubadilisha. Abram alikua katika wakati wa hofu na sintofahamu juu ya ahadi za Mungu kwake. Katika hali hiyo Mwenyezi Mungu anamtokea na hapo anathibitisha Agano na ahadi zake kwake. Sisi tunapokutana na Mungu, katika sala, katika ibada ya misa Takatifu, katika saa takatifu, tunakutana nguvu yake inayotuimarisha kusonga mbele hata nyakati ambapo mbele kunaonekana hakuna matumaini na mwanga. Nyakati ngumu za giza na mkato wa tamaa, Yesu anasimama bado katikati yetu, anatukumbusha kuwa yeye yupo nasi, anakwenda nasi katika njia yetu. Tuseme pamoja na mzaburi, “Katikati ya bonde la uvuli wa mauti, sitaogopa mabaya, kwa kuwa wewe Bwana u pamoja nami” (Zab 24:4). Anabadili kukata kwetu tamaa kwa kutupa tumaini jipya, anabadili huzuni zetu kuwa furaha tena, anabadili kutokuamini kwetu na kuwa na imani thabiti kwake, anabadili ugumu wa mioyo yetu na kuwa wenye matumaini kwake, anabadili udhaifu wetu kuwa kushinda kwetu na mwisho hali yetu ya unyonge ili ifanane na mwili wake wa utukufu.

Kung'ara kwa Kristo Yesu ni kielelezo cha utukufu na ukuu wake wa daima
Kung'ara kwa Kristo Yesu ni kielelezo cha utukufu na ukuu wake wa daima

Somo la Injili: Ni Injili ya Luka 9:28b-36. Somo la Injili Takatifu kutoka katika Injili kama ilivyoandikwa na Luka, latueleza tukio la Bwana wetu Yesu Kristo kugeuka sura. Katika Dominika ya kwanza ya Kwaresima tulimwona Yesu akijaribiwa jangwani, Mwinjili akitueleza juu ya ubinadamu (humanity) wa Bwana wetu Yesu Kristo ambaye kama sisi alijaribiwa na akashinda katika majaribu. Katika Dominika ya pili ya Kwaresma, Mama Kanisa anaweka mbele yetu tukio la kugeuka sura Bwana wetu Yesu Kristo, akitualika kutafakari juu ya Umungu wa Bwana wetu Yesu Kristo (Divinity). Kugeuka sura kwa Bwana wetu Yesu Kristo kunawapa mtazamo na picha mpya wanafunzi wa Yesu nasi sote juu ya utukufu wa Bwana wetu Yesu Kristo katika fumbo la Pasaka. Anatukumbusha kuwa hakuna utukufu pasipo mateso na kifo, hakuna utukufu pasipo msalaba. Yesu anageuka sura, kwanza kabisa ni kufunua mbele ya wanafunzi wake utambulisho wake kama Masiya, mwana wa Mungu. Pili, ni kumwonesha Yesu kama utimilifu wa sheria na manabii (uwepo wa Musa na Eliya). Tatu ni laeleza juu ya mateso kifo na ufufuko wake, fundisho ambalo mara kadhaa aliwafundishwa wanafunzi wake lakini hawakulielewa. Katika somo hili la Injili dominika ya Pili ya Kipindi cha Kwaresima Mwaka C wa Kanisa tuna mafundisho mawili ya kujifunza. Kwanza: Kwa nini Bwana wetu Yesu Kristo anawachukua Mitume watatu? (Why three disciples?). Bwana wetu Yesu Kristo aliwachukua mitume watatu, Petro, na Yohane na Yakobo akapanda nao mlimani kuomba. Bwana wetu Yesu Kristo alikuwa na Mitume kumi na wawili, kwa nini aliwachukua hawa Mitume watatu pekee?

Kung'ara Kwa Bwana: Lengo ni kuwaimarisha wafiasi wake katika imani
Kung'ara Kwa Bwana: Lengo ni kuwaimarisha wafiasi wake katika imani

Yakiwa yamebakia majuma kadhaa kabla ya kuingia katika mateso kifo na ufufuko wake, Yesu anawachukua hawa watatu kwa sababu zifuatazo. Sababu ya kwanza: Ili kuwaimarisha katika Imani matumaini na mapendo. Hawa ni Mitume ambao alikua nao mara nyingi (inner circle) na baadae walikuja kuwa na nafasi kubwa katika kanisa la kwanza kati ya Mitume wengine. Petro: Mtume wa kwanza ni Petro ambaye Yesu anamwimarisha katika Imani ili naye awaimarishe Mitume wengine. Petro anakuja kupewa wajibu mkubwa kwa ajili ya kanisa, hivyo alipaswa kuwa na Imani thabiti kwa Bwana wetu Yesu Kristo. Ni wazi kwamba Petro asingeweza kuliongoza kanisa na kuwaongoza wenzake kama asingekuwa na imani, matumaini na mapendo, kama angekua hajaimarishwa na kristo.Yohane: Mtume wa pili ni Yohane. Bwana wetu Yesu Kristo alimchukua Yohane kwa sababu alijua kuwa, Yohane ataishi muda mrefu na atakuwa Mtume wa mwisho kufa kati ya mitume wote. Hivyo Yohane alitakiwa kuwa na imani, matumaini na mapendo makubwa kwani alishuhudia vifo vya mitume wenzake wote na hivyo hakupaswa kutetereka. Ingawa alishuhudia vifo vya mitume wenzake wote, hakutetereka katika imani, matumaini na mapendo kwa Kristu. Yakobo: Yesu alimchukua Yakobo kwa sababu alijua Yakobo ndiye atakayekuwa wa kwanza kati ya mitume wote kufa kifo dini. Hivyo alipaswa kuwa na matumaini makubwa kwa Bwana ili wenzake waige kutoka kwake. Kweli Yakobo alikuwa ni mtume wa kwanza kufa kifo dini. Alikubali kuuwawa kuliko kumkana Kristu. Hii ni kwa sababu Yesu alimwimarisha. Wenzake waliofuatia walikufa nao kifo dini isipokuwa Yohane. Waliona mtangulizi wao Yakobo alikufa kifo dini hivyo nao waliimarika wakawa tayari kufa kifo dini kuliko kumkana Bwana.

Ibada ya Misa Takatifu ilete mabadiliko katika utu wa ndani
Ibada ya Misa Takatifu ilete mabadiliko katika utu wa ndani

Sababu ya pili: Kuwaandaa Mitume wake kwa ajili mateso kifo na ufufuko wake. Yesu anawachukua Mitume wake watatu ikiwa ni muda mchache kabla ya kuingika katika mateso, kifo na ufufuko wake. Mitume hawakumwelewa Yesu alikuwa ni Masiya wa namna gani. Waliwaza juu ya utukufu na heshima watakayopata baadaye wakiwa na Yesu kama Masiya. Yesu anawabadili mtazamo wao kwamba hakuna utukufu pasipo mateso na Msalaba. Kumbe nasi pia Yesu anajifunua kwetu akitukumbusha kila mara kwamba hakuna utukufu pasi na mateso, msalaba na kufa. Yeye ametuonesha mfano kwamba ni katika kufa ndipo tunapoupata uzima mpya, utukufu na uzima wa milele. Anatupa nguvu ya kuvumilia, pia anabadili mitazamo yetu hasa nyakati tunapokutana na magumu na mateso, tunapokutana na misiba na changamoto kubwa maishani. Sababu ya tatu: Ili tukio lile liwe ni ushuhuda wa kweli (Reliability of witness). Katika tamaduni za Wayahudi, ushahidi wa watu watatu ulichukuliwa kuwa ni ushahidi wa kweli juu ya tukio lililotokea. Kwa kuwachukua Mitume hawa watatu Yesu alitaka kuthibitisha kwamba tukio lile ni tukio la kweli na Mtume Petro anaeleza hili katika (2 Pet 1:16-19). Tukio hii liliwaimarisha Mitume baadaye katika jumuiya ya wakristo wa kwanza. Pili: Nini maana ya kugeuka sura kwa Bwana wetu Yesu Kristo katika maisha yetu sisi? (What is transfiguration to us?) Kama ilivyokuwa kwa Mitume, kwa nafasi ya kwanza, kugeuka sura kwa Bwana wetu Yesu Kristo kwetu sisi kwatufundisha mambo yafuatayo; Kwanza: Katika kila adhimisho la Misa Takatifu, Yesu anabadilika sura, anatubadili nasi pia tunaompokea (Transfiguration through transubstantiation). Katika adhimisho la Misa Takatifu, mkate na divai vinageuka na kuwa Mwili na Damu ya Bwana wetu Yesu Kristo. Tukio la kubadilika sura kama lilivyowaimarisha Mitume wa Yesu, sisi kila mara tunaposhiriki ibada ya misa Takatifu, kubadilika kwa mkate kuwa na divai kuwa mwili hai na mzima wa Bwana wetu Yesu Kristo, inatupa nguvu kwa kuwa kwa njia hiyo Yesu anakuwa daima kati ya watu wake.

Sakramenti za Kanisa ni kiini cha mabadiliko ya utu wa ndani
Sakramenti za Kanisa ni kiini cha mabadiliko ya utu wa ndani

Pili: Kila mara tunapopokea moja ya Sakramenti za Kanisa, nasi sote tunabadilishwa utu wetu wa ndani (transformation though church’s Sacraments). Ndugu Wapendwa tunapopokea moja ya sakramenti za kanisa tunabadilika sura. Sakramenti ya ubatizo, inatuondolea dhambi ya asili na dhambi nyingine zote, tunakuwa Watoto wa Mungu na Watoto wa kanisa, tunapokea roho mtakatifu na kuwa hekalu hai la Mungu. Vivyo hivyo sakramenti ya kitubio inatuondolea dhambi na kutufanya safi kabisa, inatupatanisha sisi na Mungu na kutupa amani na furaha rohoni. Tatu: Kugeuka sura kwa Bwana wetu Yesu Kristo kunatupa nguvu na matumaini ya kuchukua misalaba yetu (offers us a message of hope and encouragement).  Kristo Yesu aligeuka sura ili kuwaimarisha Mitume wake alipokuwa anakaribia mateso, kifo na ufufuko wake, ili wawe imara katika imani matumaini na mapendo. Katika nyakati ngumu katika safari yetu ya maisha, hasa tunapochukua misalaba Yetu, kugeuka sura kwa Bwana wetu Yesu Kristo kunatupa nguvu ya kusonga mbele katika kubeba misalaba yetu kwa matumaini kwamba ni kwa njia ya msalaba tutapata neema ya kuishi pamoja na Kristo katika uzima wa milele. Msalaba wangu ndio ngazi yangu ya kwenda mbinguni, sina budi kuumbatia, kuupenda na kuubeba kwa Imani na matumaini. Hakuna utukufu bila mateso na kufa, ndipo tufufuke pamoja na Yesu katika uzima wa milele. Nne: Tunahitaji nasi kupanda mlimani, ili tukutane na Mwenyezi Mungu (We need mountain top experience). Bwana wetu Yesu Kristo alipanda mlimani na alipokuwa katika kusali ndipo akageuka sura. Alikua katika mazungumzo na Mungu, alikutana na Mungu Baba yake akiwa katika sala, alipojitenga na kuongea na Mungu Baba yake. Ndugu Wapendwa, mlima wetu sisi ni mahali patakatifu, mahali tunapokutana na Mungu. Tunakutana na Mungu kila mara tunaposhiriki ibada ya misa Takatifu. Tunaalikwa kupanda na kuja katika mlima wa Bwana. Hapa tunakutana na Mungu naye anafunua kwetu mapenzi yake. Pia tunaalikwa kuwa na muda binafsi wa kuzungumza na Mungu. Kuwa na mazingira rafiki ya kuongea na Mungu, kuandaa nia na lengo binafsi, kwa ajili ya familia, ndugu, jamaa nk kila mara tunapokutana na Mungu. Tuwapo naye mlimani anajifunua kwetu, anashuka kati yetu na matokeo yake nasi tunang’aa. Maisha yetu yatang’arishwa na Yesu, mahusiano yetu, ndoa zetu, kazi zetu na yote tutakayoyafanya yatang’arishwa na utukufu wa Mungu.

Waamini wawe na ujasiri wa kuwashirikisha wengine utukufu wa Yesu
Waamini wawe na ujasiri wa kuwashirikisha wengine utukufu wa Yesu

Tano: Tuwe tayari kuwashirikisha wengine utukufu wa Mungu. Petro anapouona utukufu wa Mungu hakumbuki tena kwamba aliwaacha Mitume wengine. Anataka utukufu wa Mungu ukae nao peke yao kwa kupanga kujenga vibanda kule mlimani. Ndugu Wapendwa, tunapopata nafasi ya kukutana na Mungu, tusikae na huo utukufu wake sisi peke yetu. Kila mara mwishoni mwa ibada ya misa Takatifu, tunaalikwa kwenda, nendeni na amani. Tunatumwa kila mmoja kwenda kushirikisha utukufu wa Mungu kwa njia ya maneno yetu na Matendo yetu kama watu wapya tuliokutana na Mungu katika Neno lake na katika saktamenti. Je, maisha yangu yanadhihirisha utukufu wa Mungu kati ya wengine? Sita: Tunaalikwa kumsikia Yesu Mwana pekee wa Mungu. Wakiwa mlimani, sauti ya Baba ilisikika ikisema, “Huyu ni Mwanangu, mteule wangu, msikieni yeye” Mwenyezi Mungu anamtambulisha Yesu kama mwanaye mpendwa, utambulisho ambao aliutoa pia katika ubatizo wake. Wajibu wetu sisi wafuasi wa Kristo ni kumtambua daima Yesu kama mwana wa Mungu, Yesu ni masiya mkombozi wetu. Tuna wajibu wa kumsikiliza. Kwaresma hii itukumbushe wajibu wetu wa kuwa watii kwa Neno la Mungu, neno la Uzima. Ni kwa njia ya kumsikia Yesu na kupokea ujumbe wa Habari Njema, ndipo nasi tunaweza kuurithi uzima wa milele pamoja naye. Wakati ndio sasa. Siku ya wokovu ni leo. Somo la pili: Ni Waraka wa Mtume Paulo kwa Wafilipi 3:17-4:1. Katika somo la pili, (Fil 3:17-4:1), Mtume Paulo anawaonya Wafilipi wajihadhari na wale waliotaka kuwashurutisha wakristo wote washike bado torati ya wayahudi akiwasihi wafuate mfano wake. Katika jumuiya ya wakristo wa kwanza, kulikua na mgogoro kwamba ili kuwa Mkristo mmoja alipaswa kuwa kwanza myahudi, kufuata yote yaliyopaswa kwa dini ya kiyahudi na ndipo kuwa Mkristo. Mtume Paulo anafundisha kuwa, safari ya Mkristo inaanza pale anapobatizwa. Na inapaswa kukamilishwa kila siku kwa njia ya imani thabiti, hadi mwisho wa nyakati wakati Bwana wetu Yesu Kristo atakapokuja tena ambapo ataubadili mwili wetu wa unyonge ili ufanane na mwili wake wa Utukufu. Hitimisho. Katika Dominika ya Pili ya kipindi cha Kwaresima Mwaka C wa Kanisa, tumshukuru Mungu ambaye ni mwaminifu kwa ahadi na Agano alilofanya nasi wakati wote. Ili tufaidi ahadi yake ya uzima wa milele, tunaalikwa kuwa tayari kupokea mwaliko wa mabadiliko, mwaliko wa kutubu na kuiamini Injili. Tuombe pia neema ya kushiriki mateso pamoja na Kristo ili tushiriki pia utukufu pamoja naye.

Kwaresima D 2

 

15 Machi 2025, 09:04
Prev
March 2025
SuMoTuWeThFrSa
      1
2345678
9101112131415
16171819202122
23242526272829
3031     
Next
April 2025
SuMoTuWeThFrSa
  12345
6789101112
13141516171819
20212223242526
27282930