Tafuta

Cookie Policy
The portal Vatican News uses technical or similar cookies to make navigation easier and guarantee the use of the services. Furthermore, technical and analysis cookies from third parties may be used. If you want to know more click here. By closing this banner you consent to the use of cookies.
I AGREE
Allegretto
Ratiba Podcast
2025.03.21 Tanzania:Misa kwa ajili ya Jubilei ya miaka 25 ya Askofu Mstaafu wa Jimbo katoliki la Bukoba, Askofu Methodius Kilaini(19 Machi 2025). 2025.03.21 Tanzania:Misa kwa ajili ya Jubilei ya miaka 25 ya Askofu Mstaafu wa Jimbo katoliki la Bukoba, Askofu Methodius Kilaini(19 Machi 2025). 

Tanzania:Miaka 25 ya Uaskofu wa Askofu Kilaini:Jubilei ni fursa ya toba na kuomba msamaha!

Jubilei ya miaka 25 ya Uaskofu imebeba shangwera ya miaka 77 ya kuzaliwa;miaka 53 ya Upadre aliopewa 1972;miaka 25 ya kuteuliwa na Mtakatifu Papa Yohane Paulo II kuwa Askofu Msaidizi wa Dar es Salaam na kuwekwa wakfu katika Jubilei ya 2000,Machi 18.Haya na mengine mengi yamo katika mahubiri ya Askofu Rweyongeza wa Jimbo la Kayanga,tarehe 19 Machi 2025 katika Kanisa Kuu la Bukoba kwa ajili ya Jubilei ya Askofu Kilaini.Vatican News inachapisha Mahubiri kamili.

Askofu Almachius Vincent Rweyongeza– Jimbo Katoliki - Kayanga, Tanzania.

Wapendwa wanafamilia ya Mungu: JUBILEI Ya 2025, Mahujaji wa matumaini. Tumsifu Yesu Kristo, Milele Amina. Kristo, Tumaini Letu/Tumaini letu, Kristo. Mungu ni mwema, kila wakati: kila wakati Mungu ni mwema. WAWATA: kwa upendo wa Kristo, Tutumikie na kuwajibika bila kuchoka. UWAKA: Nguzo imara ya Kanisa. VIWAWA: Vijana Mapendo, Daima kwa Vitendo. TYCS: Mapendo, Daima. UKWAKATA (Kwaya): Tumwimbie Bwana, Katika roho na kweli (Yh 4:23). UTOTO MTAKATIFU: Imani katika Msalaba, Kristo katika Upendo. MOYO MTAKATIFU WA YESU: Ufalme wako Ufike. FATIMA, Mama Maria: Mama wa Wote. WATUMISHI WA MISA: Mtumikieni Mungu, Kwa furaha (Zab 100:2). MIITO: Mimi hapa, Nitume Mimi (Isa 6:8).

Askofu Rweyongeza wakati wa mahubiri
Askofu Rweyongeza wakati wa mahubiri

Maandiko Matakatifu yanatambulisha siku ya leo yakisema: “Siku hii ndiyo aliyoifanya Bwana, Tutashangilia na kuifurahia” (Zaburi 118:24). Napenda nianze na taarifa fupi ya habari. Mwanzoni mwa miaka 60 nikiwa Darasa la Pili, Mwalimu wetu wa Hesabu alizoea kutumia dakika 10 za mwanzo wa Kipindi kutupa chemshabongo. Siku moja aliuliza swali mintarafu mahesabu ya kutoa, si kujumlisha, kuzidisha au kugawanya! Aliuliza: “Bwana mmoja alikuwa na bunduki, kwenye mti walikuwepo ndege 5. Akalenga shabaha na kuua ndege 2. Je, kwenye mti walibaki ndege wangapi?” Darasa letu lilikuwa na wanafunzi 45. Wanafunzi watatu tu walipata jibu sahihi. Kati ya wanafunzi hao 3, wawili ni mapadre, na mwingine alioa akamzaa Padre.

Wanafunzi hao ni Msgr Pius Rutechura Protase, Mzee Projestus Mutashobya Pastor amezaa Padre Innocent; na Askofu Almachius-Vincent Rweyongeza Andreas. Na mimi leo napenda nianze na chemshabongo: Mosi, “Kwa nini kwenye viwanja vya mpira watu hawasinzii mpaka kipenga cha mwisho kinapopulizwa, lakini Kanisani wanasinzia, na wengine kukoroma na wengine kutoka nje kabla ya baraka ya mwisho? Pili, kama wewe hujaanza kusinzia, “Je, unaona? Kama unaona unaona nini?” Bwana Yesu alipofika kijijini Bethsaida, watu walimletea kipofu mmoja, wakamwomba amguse. Yesu akamshika huyo kipofu mkono, akampeleka nje ya kijiji. Akamtemea mate machoni, akamwekea mikono, akamwuliza, “Je, unaweza kuona kitu?” Huyo kipofu akatazama, akasema, “Ninawaona watu wanaoonekana kama miti inayotembea” (Mk 8:22-26). Je, wewe unaona nini? Unaona kuta za Kanisa au unaona watu kama visiki vya miti wameketi? Ilikuwa ni usiku wa manane, wafungwa wawili gerezani walifungua dirisha la seli ili kupata hewa safi. Wote wawili walitazama nje. Waliona nini? Mmoja aliona giza, akanuna! Mwingine aliona nyota, akatabasamu! Wewe unaona nini leo hii? Mimi nitakuambia na kukuonesha ninachoona! Ninaona nyota mbili! Wahenga wetu wamesema: “Nyota njema huonekana asubuhi.” Leo asubuhi tunazo nyota mbili zimeonekana: Nyota ya kwanza, ni Mt. Yosefu, Mume wa Bikira Maria. Nyota ya Pili, ni Askofu Kilaini. Sasa karibuni tufanye tafakari fupi juu ya nyota hizi mbili:

Jubilei ya miaka 25 ya Askofu Kilaini
Jubilei ya miaka 25 ya Askofu Kilaini

NYOTA YA KWANZA NI MTAKATIFU YOSEFU, MUME WA BIKIRA MARIA, AKIWAKILISHWA NA SANAMU HII NZURI:

Tumshangilie Mtakatifu Yosefu kwa wimbo wake: Yosefu tunakutolea sifa na heshima. Wana wako elekea uwe kwetu mjima. Ewe mlinzi mwaminifu tunaomba kwako,Mlinde Baba Mtakatifu na kanisa lako. Leo Machi 19, Kanisa Katoliki ulimwenguni kama ilivyo ada ya kalenda ya Liturujia ya kila mwaka, kwa namna ya pekee, linamheshimu na kumwadhimisha Mtakatifu Yosefu, mume wa Bikira Maria na Baba Mlishi wa Yesu. Mtakatifu Yosefu anawekwa mbele yetu, ili tutafakari sifa lukuki za kutusaidia na kutuimarisha katika maisha yetu ya kawaida, na zaidi maisha yetu ya imani. Mt. Yosefu ni mume wa mzazi wa Mungu, ni Mlinzi wa Mkombozi, ni Mlinzi safi wa Bikira, ni Mlishi wa Mwana wa Mungu, ni Mtii, ni mwaminifu, ni Kioo cha uvumilivu, ni Mfano wa watu wa kazi, ni Mlinzi wa Mabikira, ni Msaada wa wenye shida, ni Matumaini ya wagonjwa, ni Kitisho cha mashetani, ni mlinzi wa Kanisa Takatifu na kadhalika.

Leo tutafakari sifa tatu za Mtakatifu Yosefu:

Sifa ya kwanza, Mtakatifu Yosefu alikuwa mvumilivu katika kukabiliana na changamoto. Maisha bila changamoto hayamkomazi mtu. Ndio maana wahenga wamelonga: “Bahari shwari haitoi manahodha stadi.” Mfano, Mosi, ujauzito wa Maria ulimpa Yosefu changamoto kubwa katika kuendelea na mahusiano, hivyo aliazimia kumwacha kwa siri ili kumlinda Maria asiuawe; Pili, Yosefu alipata changamoto ya kuwa mkimbizi na familia yake, alikimbilia Misri (Mt 2:13-15), Herode alipotafuta kumuua mtoto Yesu kwa sababu eti mtoto Yesu alikuwa tishio kwa utawala wake (Mt 2:16-18). Tatu, changamoto ya Yesu kupotelea hekaluni, ambako Mt. Yosefu na Bikira Maria walimtafuta mtoto Yesu kwa huzuni (Lk 2:41-52). Leo hii katika baadhi ya maeneo, tunasikia baadhi ya wazazi wakitelekeza familia zao, sababu ya changamoto mbalimbali, zikiwemo za kiuchumi, wivu wa kimapenzi, uasherati, michepuko, ushirikina, nk. Mtakatifu Yosefu leo anawaalika akina baba kuwa mfano bora wa malezi na matunzo kwa familia zao; kuwa wavumilivu kwani, “uvumilivu na subira hung’oa milima.” Na Bwana Yesu anasema, “Atakayevumilia mpaka mwisho ndiye atakayeokolewa” (Mt 10:22).

Sifa ya pili, Mtakatifu Yosefu alikuwa mnyenyekevu, msikivu na mtii. Tunasimuliwa kwamba walipokuwa katika uchumba, ndipo Bikira Maria kwa mpango wa Mungu alimchukua mimba Yesu. Fundisho kubwa tunalojifunza toka kwa Yosefu ni moyo wa usikivu na utii. Malaika alipomweleza, wala hakubisha (Mt 1:20-21). Leo hii, vijana wengi na familia nyingi ziko kwenye magomvi yasiyokoma, kwa sababu hakuna unyenyekevu na usikivu. Kwa mfano, katika familia na kaya wakati wa mlo hakuna usikivu, kila mmoja yuko bize na simu yake au radio au luninga akisikiliza na kuangalia michezo ya mpira, tamthiliya na picha za ajabu ― utupu! Papa Francis anashauri wakati wa milo simu zizimwe na kamera ziwekwe chini. Maana “mshika mbili mmoja humponyoka” Vijana wengi leo hawachumbii, wengi wanakutana mitandaoni, kwenye facebook na kumaliza kila kitu huko. Vijana wengi wamesahau kuwa, uchumba ni kipindi kitakatifu cha kuhabarishana, kufahamiana na kuombeana namna watakavyojenga familia: wakizaa, wakilea na kutunza watoto kadiri Mungu atakavyowajalia baraka ya kuzaa (Zab 127:3-5).

Leo hii kijana anakutana na msichana Jumatatu, na ndani ya wiki, wameshaanza kuishi pamoja, bila hata wazazi wa pande zote mbili kufahamu; na wala kutoa kwa Paroko taarifa ya kuandikisha ndoa. Hawajali kufunga ndoa Kanisani. Na baada ya wiki, mbili unasikia talaka! Kulikoni? Mke hajui kupika, hajui kulima, hajui kuosha vyombo, kufua nguo na kunyosha nguo! Muda wote yuko saluni akipodolewa. Anataka kumuajiri mtumishi wa nyumbani amfanyie kazi ambazo mke anapaswa kumfanyia mme wake, na matokeo yake anaishia kupinduliwa! Tujifunze kwa Mt. Yosefu kusali: “Kabla hawajakaribiana” ina maana wakati wa uchumba wao, yaani kabla hawajaanza kuishi pamoja, walimwomba Mungu! Mt. Yosefu anaalika watu wote kuheshimu ndoa. Biblia inasema: “Ndoa inapaswa kuheshimiwa na watu wote, na haki zake zitekelezwe kwa uaminifu. Mungu atawahukumu waasherati na wazinzi” (Ebr 13:4; Biblia yenye Vitabu vya Deutrokanoni: Habari Njema). Tafsiri ya Biblia ya Kiafrika inasema: “Ndoa iheshimiwe na wote, na kitanda cha ndoa kisichafuliwe, kwani Mungu atawahukumu waasherati na wazinzi” (Ebr 13:4).

Jubilei ya miaka 25 ya Askofu Kilaini
Jubilei ya miaka 25 ya Askofu Kilaini

Sifa ya tatu, Mtakatifu Yosefu alikuwa mwaminifu. Alitimiza kwa uaminifu kamili wito wake wa kuwa mlinzi wa familia takatifu ya Nazareti, mpaka Mungu alipomuita akamwambia: “Mtumishi mwema na mwaminifu, ingia katika furaha ya Bwana wako” (Mt 25:21, 23). Papa Fransisko anasema: Kila mmoja wetu anaitwa kuwa mlinzi. “Wito wa kuwa mlinzi unamaanisha kulinda viumbe vyote, kuwa mlinzi inamaanisha kuheshimu kila kiumbe cha Mungu, na kuheshimu mazingira ambapo tunaishi. Kuwa mlinzi, inamaanisha kulinda watu - tusiwapoteze na kuwaua kama Kaini ― maana damu yao kamwe haibaki kimya, inalia na kupiga kelele toka udongoni (Mwanzo 4:8-12). Biblia inaendelea kusema: “Atakayemwua binadamu mwenzake, nitamdai (Mungu anasema) uhai wake. Amwagaye damu ya binadamu, damu yake itamwagwa na binadamu; maana kwa mfano wa Mungu, binadamu aliumbwa” (Mwa 9:5-7). Kuwa mlinzi inamaanisha, kujaliana katika familia: wanandoa kulindana, na baadaye kama wazazi kulea na kutunza watoto wao, na watoto baadaye kuwatunza wazazi wao. Ina maana kujenga urafiki wa kweli ambapo tunalindana kwa kuaminiana, kuheshimiana na kutendeana wema… Kila kitu tumekabidhiwa (Mwa 1:28) tukilinde na wote tunawajibika. Uwe mlinzi wa zawadi za Mungu. Muigeni Mtakatifu Yosefu, na umuombe akuombee.” Anapopotea ndugu, raia, jirani unaulizwa kama Mungu alivyomuuliza muuaji Kaini: “Ndugu yako Abeli yuko wapi? Kaini akamjibu kwa kiburi: “Mimi sijui! Je, mimi ni mlinzi wa ndugu yangu?” (Mwa 4:9).

Katika salamu za Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC) kwenye hitimisho la Kongamano la 5 la Ekaristi Takatifu Kitaifa, Dar es Salaam, mnamo Septemba 15, 2024 tulipaza sauti tukisema: “Tukiangalia hali ya sasa ya nchi yetu, tunaona tunu yetu ya udugu na amani imeshambuliwa. Hii inatokana na matukio yaliyotokea nyakati za karibuni, za watu kutekwa, kuumizwa na hata kuuawa. Tunajiuliza nini kimepotea kwenye tunu yetu hii? Taifa letu limekosea wapi? Sisi Maaskofu hatuamini kuwa makundi haya ya kihalifu yana nguvu kuliko vyombo vyetu vya ulinzi na usalama; hivyo tunaomba vyombo vyetu hivi, vitimize majukumu yao ili kurudisha heshima ya Taifa letu ya kuwa kisiwa cha udugu na amani. Ujumbe mwingine kuhusu uaminifu ni kutoka Mh. Diomaye FAYE (23.3.1980) umri wa miaka 45, Rais wa Senegal anasema: Kwa kweli sitaki picha zangu kupambwa katika ofisi zenu, kwa kuwa mimi siyo Mungu wala mtu mashuhuri, bali mtumishi wa taifa. Badala yake, tundikeni picha za watoto wenu, na kuzitazama kila mnapotaka kufanya maamuzi, na kila mara roho ya wizi inapowatembelea, ziangalieni vizuri picha za familia zenu na kujiuliza kama wanastahili kuwa familia za wezi walioliharibu taifa? Tumuige Mtakatifu Yosefu na tumuombe atuombee.

NYOTA YA PILI INAYONG’ARA MBELE YETU NA KATI YETU LEO ni Mhashamu Methodius Mutashoborwa Paulo Kilaini, Askofu Msaidizi Mstaafu wa Dar es Salaam, Askofu Msaidizi Mstaafu wa Bukoba, na Msimamizi wa Kitume Mstaafu wa Jimbo la Bukoba. Kwa baadhi yetu ni mara ya kwanza kumuona mubashara, akiadhimisha Jubilei ya miaka 25 ya Uaskofu. Mahali alipo asimame atupungie mkono – na tuimbe naye wimbo wake wa Shukrani kwa Mungu: Niseme nini Ee Bwana?Nitamke maneno gani kinywani? Nikushukuru jinsi gani? Nisimulie vipi mimi, mapito niliyopita kuja hapa (miaka 25 hii yote)? Ni kutukuze vipi Mungu? Niseme tu (Bwana) Mungu (wangu); Asante nakushukuru. Narudia (Bwana) Mungu (wangu); Asante nakushukuru.

Kwa mara ya kwanza kabisa nilikutana na Askofu Kilaini mwaka 1973 nikiwa kidato cha Tatu pale Seminari ya Rubya. Ni mwalimu wangu na mlezi wangu, nimemfahamu kwa kipindi cha miaka 52 sasa. Kwa hiyo ninahitaji masaa 52 kumzungumzia wasifu wake. Lakini tumekuja hapa kusherehekea Jubilei ya miaka 25. Kwa kuwa hatukuja hapa kwa ajili ya semina nitazungumzia maneno 10 tu, sipendi kuwakawiza:

Neno la 1: Jubilei ni Shukrani

Jubilei ni kushukuru. Mtafiti fulani amebaini vitu saba ambavyo hupokea na havishukuru:

         Mosi, tumbo hupokea chakula, lakini halishukuru.

         Pili, mpumbavu hupokea ushauri, zawadi, lakini hashukuru.

         Tatu, dampo hupokea takataka, lakini haishukuru.

         Nne, kidonda na uchafu hupokea nzi, lakini havishukuru.

         Tano, maiti hupokea sanda, lakini haishukuru.

         Sita, kaburi hupokea maiti, lakini halishukuru.

         Saba, Bahari hupokea maji ya mito iwe masika au kiangazi,  lakini haishukuru!

Tumekuja kuungana na Askofu Kilaini kumshukuru Mungu na kusherehekea Jubilei ndani ya Jubilei. Ni Jubilei ndani ya Jubilei; Jubilei ndani ya Jubilei.   Mosi, Jubilei ya miaka 25 ya Uaskofu imebeba shangwera ya miaka 77 ya kuzaliwa. Alizaliwa Mwaka 1948 Machi 30 akiwa mtoto halali wa Ndoa Katoliki ya Ta Paulo Mutegeki na Ma Asteria Kokutona. Anawashukuru wazazi kwa malezi bora. Wapumzike kwa amani. Tulisherehekea Jubilei yake ya miaka 75 ya kuzaliwa 2023. Mtunga Zaburi anasema: “Miaka ya kuishi ni 70, au tukiwa wenye afya, 80; lakini yote ni shida na taabu!” (Zab 90:10). Napenda nitumie maneno mazuri ya Mt. Yohane kukutakia afya njema: “Mpenzi wangu, nakutakia mafanikio mema ya kila aina; nakutakia afya njema ya mwili kama ulivyo nayo rohoni” (3 Yoh 1:2). Pili, Jubilei ya miaka 25 ya Uaskofu imebeba shangwera ya miaka 53 ya Upadre aliopewa mwaka 1972 Machi 18 huko Roma kwa mikono ya Kardinali Rossi akiwa na pacha wake Padre. Gaudios Rutakyamirwa, R.I.P. Amen. Tulisherehekea pamoja naye hapahapa Kanisa Kuu la Bikira Maria Mama Mwenye Huruma, Bukoba 2022, Machi 18 tukaimba pamoja naye wimbo alioimba siku yake ya Upadrisho: “Nitajongea Altare yako, furaha yangu na heri yangu siku zote.” Na daima anapokuwa Sakristia akijiandaa kuadhimisha Misa anaikumbusha nafsi yake mambo matatu akisema: “Ewe Padre wa Mungu: Adhimisha Misa hii kama kwamba: Mosi, Ni Misa yako ya kwanza, Pili, Ni Misa yako ya mwisho. Tatu, Ni Misa yako pekee. Sala hiyo anatakiwa asali kila mhudumu wa Altare na kila anayekuja kushiriki Misa, ili uone kuwa hii ni fursa ya kwanza, ya mwisho na ya pekee. Kwa nini basi, unakuwa na haraka? Lakini kwenye viwanja vya mpira huangalii saa?

Tatu, Jubilei ya miaka 25 ya kuteuliwa na Mtakatifu Papa Yohane Paulo wa Pili kuwa Askofu Msaidizi wa Dar es Salaam na kuwekwa wakfu na Kardinali Pengo Mwaka wa Jubilei Kuu 2000 Machi 18, akisaidiwa na Askofu Nestor Timanywa wa Bukoba na Askofu Justin Tetmu Samba wa Musoma. Wapumzike kwa amani. Amina.  Askofu Kilaini, ni Askofu halisi, Askofu wa kweli, Askofu “Original”, maana yake ni Askofu Katoliki ambaye hakupiga kampeini au kuhonga, akitafuta uaskofu; au kwenda kulala usingizi fofofo, akaota ndoto, na kuamka ni Askofu akiwa amevalia mavazi ya kiaskofu na Biblia mkononi!!

Miaka 25 ya ya uaskofu wa Askofu Kilaini
Miaka 25 ya ya uaskofu wa Askofu Kilaini

Jubilei ya miaka 25 ya Uaskofu sio haba. Kwa ufupi, miaka hiyo imebeba majukumu yafuatayo:

Tangu Mwaka 2000 Machi 18 amekuwa Askofu Msaidizi, Jimbo Kuu la Dar es Salaam. Tangu Mwaka 2009, Desemba 5 Baba Mtakatifu Benedikto wa 16 alimuhamisha kutoka Jimbo Kuu la Dar es Salaam, na kuja kuwa Askofu Msaidizi wa Jimbo Katoliki la Bukoba, chini ya Askofu Nestori Timanywa, na baadaye chini ya Askofu Desderius Rwoma. Tangu Mwaka 2022, Oktoba 1, Askofu Rwoma alipostaafu, kwa sababu ya umri, na afya yake kuwa mgogoro, Askofu Kilaini aliteuliwa kuwa Msimamizi wa Kitume wa Bukoba, wakati huo akatunga sala na kuhamasisha waamini kusali na kumuomba Mungu kumpata Askofu Jimbo haraka wa kuongoza Jimbo la Bukoba. Sala hiyo iligusa watu wengi sana, ikasaliwa, na hatimaye akapatikana Mhashamu Askofu Jovitus Francis Mwijage, aliyepewa Daraja la Uaskofu 2024, Januari 27. Tumshukuru Mungu. Siku hiyohiyo, Baba Mtakatifu alikubali maombi yake ya kustaafu na akaweza kuimba wimbo wa Mtume Paulo: “Nimeumaliza mwendo, nimevipiga vita vilivyo vizuri na sasa nangojea kupewa tuzo la ushindi kwa maisha ya uadilifu, tuzo ambalo Mungu atanipa mimi siku ile, na wala si mimi tu, ila na wale wote wanaotazamia kwa upendo kutokea kwake” (2 Tim 4:7-8). Askofu Kilaini anawashukuru wote na nyote mliomsaidia kwa namna mbalimbali, akitumia maneno ya Mt. Paulo, Mtume akisema: “Ninamshukuru Mungu wangu kila ninapowakumbukeni; na kila ninapowaombeeni nyote, nasali kwa furaha, kwa sababu ya jinsi mlivyonisaidia katika kazi ya injili tangu siku ile ya kwanza mpaka leo”(Fil 1:3-5).

Neno la 2: Jubilei ni kutafakari maana ya kile tunachosherehekea.

Jina Askofu kadiri tunavyokuwa nalo leo, linatokana na neno la Kigiriki, “presbyteros”, ambalo tafsiri yake ni mwanamume mzee au mtu mzima ambaye alikabidhiwa mamlaka ya kiibada na uongozi katika Kanisa la mwanzo. Mt. Petro, Papa wa kwanza wa Kanisa alikuwa na haya ya kuwatahadharisha Maaskofu na Makuhani: “Mimi mzee miongoni mwenu wazee wenzangu, mimi ambaye nilishuhudia mateso ya Kristo na kushiriki ule utukufu utakaofunuliwa, nawasihi mlichunge kundi la Mungu mlilokabidhiwa; mlitunze si kwa kulazimika, bali kwa hiari kama atakavyo Mungu. Fanyeni kazi hiyo si kwa tamaa ya fedha, si kama mfanyakazi wa mshahara au kama ajira, bali kwa moyo wenu wote” (1 Pet 5:1-2). Askofu, pia ni tafsiri ya neno “Episcopus” ambalo ni neno la Kilatini lililotafsiriwa kutoka kwa Kigiriki “Episkopos” likimaanisha “mwangalizi, mlinzi, mchungaji, Askofu; na lilitumika katika Kanisa la mwanzo kwa viongozi wa majimbo. Askofu ni mwangalizi mwenye utimilifu wa Daraja Takatifu ambaye amewekwa wakfu kwa kupakwa mafuta matakatifu ya Krisma mara 4 (nne): Mara ya kwanza, alipakwa mafuta ya Krisma utosini wakati wa Ubatizo wake tarehe 17.4.1948 na Padre P.J.B. Lapioche, Namba ya Ubatizo ni LB. No. 18462 Kashozi Parish. Mara ya pili alipakwa mafuta ya Krisma usoni na Askofu wakati wa Kipaimara 17.3.1956; kwa njia hiyo, kufanywa rasmi askari wa Kristo wa kupambana na shetani na hila zake zote. Mara ya tatu, alipakwa mafuta ya Krisma viganjani na Kardinali Rossi 18.3.1972, wakati wa kupewa Daraja Takatifu la Upadre ili agawe matakatifu. Sacerdos - Kilatini cha Padre, “Baba”.

Sacerdos ni maneno mawili ya Kilatini:

Sacer ― hiki ni kivumishi kinachomaanisha kitu kitakatifu, na dans linatokana na kitenzi dare, ambacho maana yake ni kutoa, kugawa. Hivyo, tafsiri ya neno hili Sacerdos ni kwamba Padre ni mgawaji wa matakatifu. Anapakwa mafuta matakatifu ili agawe matakatifu. Padre amebarikiwa ili abariki. Kwa hiyo usiende kwa Padre au Askofu kumuomba pesa, piga magoti umuombe baraka, na siyo (upako)? Mara ya nne, alimiminiwa mafuta ya Krisma kichwani na Kardinali Pengo tarehe 19.3.2000 akakamilishwa katika ukuhani, akawa Askofu. Mwadhama Polycarp Kardinali Pengo tunaye leo kati yetu. Karibu sana na hongera yuko anatabasamu kuonyesha furaha yake. Maandiko Matakatifu yanasema “Hakuna mtu awezaye kujifanya mwenyewe kuwa kuhani mkuu. Kila mmoja huteuliwa na Mungu kuwa kuhani mkuu kama alivyokuwa Aroni” (Ebr 5:4).  Uaskofu wa Kanisa Katoliki si ajira, si ofisi ya kujitajirisha: Biblia inakutahadharisha ikisema: “Kumbuka kwamba, katika siku za mwisho kutakuwa na nyakati za taabu.

Watu watakuwa na ubinafsi, wenye tamaa ya fedha, wenye majivuno, wenye kujiona, wenye kumtukana Mungu, wasiowatii wazazi wao, wasio na shukrani na waovu; watatokea watu wasio na upendo moyoni, wasio na huruma, wachongezi, walafi na wakali; watachukia chochote kilicho chema; watakuwa wahaini, wakaidi na waliojaa kiburi; watapenda anasa kuliko kumpenda Mungu. Kwa nje wataonekana kama watu wenye kumcha Mungu, lakini wataikana nguvu yake. Jiepushe kabisa na watu wa namna hiyo” (2 Tim 3:1-5; rejea Mt 7:15-20; Lk 6:43-44). Askofu Kilaini si mtu wa mtindo huo. Tumpongeze, maana yeye amekuwa daraja la kweli, na anaendelea kutuunganisha na Mungu. Biblia inasema: “Wapenzi wangu, msisadiki kila mtu asemaye kwamba ana Roho wa Mungu, bali chunguzeni kwa makini, kama huyo mtu anaongozwa na Roho wa Mungu au la, maana manabii wengi wa uongo wamezuka ulimwenguni” (1 Yh 4:1). Kuna vipimo vya kawaida vitano vya kukusaidia kuchunguza kwa makini manabii wa uongo na maaskofu wa uongo, wa kujitengeneza, wanaochezea imani za watu, wakihubiri Yesu wa utajiri na miujiza, na si Yesu msulubiwa Msalabani anayealika watu watubu, waache dhambi na wapendane kama alivyotupenda.

Jubilei ya miaka 25 ya uaskofu wa Askofu Kilaini
Jubilei ya miaka 25 ya uaskofu wa Askofu Kilaini

Kipimo cha kwanza yeyote anayejigamba kukemea mashetani, kabla ya kumpeleka mgonjwa hospitalini, ili apimwe na kuona kama ana malaria, kisukari au presha, mpeleke mchungaji huyo akanyage katikati ya msafara wa siafu kwa dakika walau tano, na aanze kukemea siafu hao wasimpande mwilini. Tuone kama siafu watamtii nasi tuweze kumwamini.

Kipimo cha pili, yeyote anayejigamba kufufua wafu mkamsikiliza, mpeleke mochwari ya hospitali yoyote au basi, mpeleke makaburini awafufue wapendwa wetu kwanza (Yoh 12:1,9,17).

Kipimo cha tatu, yeyote anayejigamba kufanya miujiza ya uponyaji majukwaani, mpeleke ICU au chumba cha wagonjwa mahututi, aponye wagonjwa hao tulio na wasiwasi nao! (Mt 4:23-24; 8:16; 12:22; Mk 1:34; Lk 6:19; 9:11).

Kipimo cha nne, mtu yeyote anayejiita mungu mkamfuata, apelekwe baharini au ziwani atembee juu ya maji kama Yesu, na asizame (Mt 14:22-33; Mk 6:45-52; Yoh 6:16-21).

Kipimo cha tano, mtu yeyote anayejiita Yesu mkamfuata, asubiri Ijumaa Kuu mkamcharaze mijeledi akiwa uchi wa mnyama, avishwe taji la miiba, atundikwe msalabani kwa kumpigilia misumari mikononi na miguuni, achomwe ubavu kwa mkuki kuhakikisha amekufa, azikwe kaburini na kuweka mfuniko wa zege zito, tuone kama atafufuka siku ya tatu! Ili tumuamini na tumfuate.

Onyo: Wewe muumini usiwe malaya na mzururaji kwa wachungaji na dini tapeli zinazotumia dini kama miradi ya biashara. Kinachoponya mara zote ni imani yako kwa Mungu – si imani yako kwa mafuta, maji, mchanga, upako na makelele ya aleluya (soma Biblia         Mt 9:2; 9:22; 15:28; Mk 10:52; Lk 8:48; Lk 18:42).

Majukumu 3 ya Maaskofu

Maaskofu wamewekwa wakfu ili kutimiza majukumu matatu:  Mosi, “The Munus Docendi (Jukumu la kufundisha) katika ofisi ya mwalimu”; Pili, “The Munus Sanctificandi (Jukumu la Kutakatifuza) katika ofisi ya ukuhani; Tatu, The Munus Regendi (Jukumu la kuongoza) katika ofisi ya mchungaji, au mtawala, au mfalme au kiongozi.

Mosi, Jukumu la kufundisha, Askofu Kilaini ametumia majukwaa yote yaliyomo kwenye mazingira kufundisha na kutangaza Injili ya Kristo. Amefanya kazi hiyo akiwaiga watakatifu Anselm, Bonaventura, Thomaso wa Akwino, Augustini, na Alberto Mkuu ambao kabla ya kuandaa mafundisho yao walipiga magoti zaidi ya saa nzima mbele ya Msalaba wa Yesu Msulubiwa au mbele ya Tabernakulo wakisali na kumuomba Mungu Roho Mtakatifu (Yoh 16:12-15) paji la hekima. Na sio kama wanateologia wengi wa siku hizi, na wanamuziki wanaoandaa mambo yao katika maktaba kuonyesha ugwiji wao wakisoma vitabu hali wakijipoza kwa soda na chupa ya bia au glasi ya divai. Askofu Kilaini hamuhubiri Yesu mtamu, Yesu wa raha na starehe, Yesu wa mafanikio na utajiri, bali haogopi kumuhubiri Yesu wa Msalaba, Yesu Msulubiwa, Yesu anayealika watu watubu dhambi, wawapende maadui zao na kuwaombea wanaowaudhi (Mt 5: 43-48). 

Pili, Askofu ana jukumu la kutakatifuza. Askofu Kilaini ametimiza jukumu hili kwa kuadhimisha Sakramenti, yaani kutoa vipaji na sadaka kuombea taifa la Mungu, kuchochea miito ya kipadre, ya kitawa na ya kimisionari; kubariki wote wanaomuomba baraka kwa ajili yao na mali zao. Tatu, Askofu ana jukumu la kuongoza kama Mchungaji wa roho. Askofu Kilaini amekuwa kati ya kundi lake kama mtumishi atumikaye, amekuwa kama mchungaji mwema anayejua kondoo wake na kondoo wamjua. Papa Francis amekuwa akituasa na kusema “tuwe wachungaji tunaonukia harufi ya kondoo au kundi tunaloliongoza na kulisimamia”. Mahudhurio makubwa ya leo yanaonyesha jinsi sisi kondoo wake tunavyomjua na kumpenda; naye anavyotupenda.

Mwenyeheri Carlo Acutis kijana aliyetangazia ulimwengu miujiza ya Ekaristi Takatifu na matokeo ya Bikira Maria kwa njia ya mtandao, alizaliwa tarehe 3 Mei  1991, na akafariki tarehe 12 Oktoba 2006 akiwa na umri wa miaka 15, tu na mwili wake umezikwa katika Kanisa la (Santa Maria Maggiore, yaani Mtakatifu Maria Mkuu,) Assisi, Italia, na haujaoza. Alitangazwa Mwenyeheri mnamo tarehe 20 Oktoba  2020 huko Assizi. Na wakati huo huo atatangazwa kuwa Mtakatifu tarehe 27 Aprili 2025. Kijana huyu anayejulikana pia kama 'Mtume wa Ekaristi' alikuwa na msemo huu: We are born originals, but we die photocopy.” “Tunazaliwa katika uasilia wetu, na  tunakufa tukiwa vivuli.” Kwa maneno mengine: “Tunazaliwa kila mtu akiwa na swali lake la kujibu, tunakufa tukinakiri majibu ya maswali ya wengine.” “Tunazaliwa kila mtu akiwa na shamba lake la kulima, tunakufa tukipalilia mashamba ya wengine.” Shida ni wivu, kutojiamini, kujilinganisha na wengine, kuchezea muda, nk. Askofu Kilaini si mtu wa namna hiyo – amebaki “original.”

Neno la 3: Jubilei ni kufurahi; ni shangwera (Walawi 25:8-22; Lk 4:18-19)

Tumekuja kufurahi pamoja na Askofu Kilaini. Tumekuja kumuongezea maisha na sisi kujiongezea maisha. Biblia inasema: “Furaha ya moyo ni uhai wa mtu; furaha ndiyo inayompa maisha marefu. Jifurahishe na kuwa na utulivu wa moyo; weka huzuni mbali nawe. Maana huzuni imewaangamiza wengi, wala haina faida kwa mtu yeyote. Wivu na hasira hufupisha maisha, mahangaiko na wasiwasi humfanya mtu azeeke upesi” (Sira 30:22-24).

Neno la 4: Jubilei ni kukumbuka, ni kuacha alama:

Jubilei inakualika usipite duniani kama mshale upitavyo angani bila kuacha kumbukumbu. Orodhesha baraka ulizokilimiwa na Mungu na jinsi ulivyompenda Mungu na kumtumikia (1 Yoh 4:7-21) Mara nyingi tunapoenda kuwazika ndugu zetu, wengi wao wakiwa watu wazima, wenye umri mkubwa, husomwa wasifu wa marehemu. Wasifu wa baadhi yao hauchukui hata dakika mbili – utasikia msomaji anatusomea: Tarehe ya kuzaliwa, historia ya ugonjwa wake, utadhani alizaliwa ili kuugua, tarehe ya kuugua, ya kulazwa na ya kufariki. Kisha kuwashukuru madaktari waliohangaikia afya yake bila mafanikio. Na kuhitimisha: Bwana alitoa na Bwana ametwaa, jina la Bwana lihimidiwe! Mtafiti mmoja amesema: “Makaburi mengi yamejaa miili ya watu waliokufa na kuzikwa na ndoto zao, karama zao na mipango yao.”  Na mtafiti mwingine amesema: “Shetani hajishughulishi na mipango mizuri tunayokuwa nayo, alimradi haifanyiki leo”. Anatufundisha lugha hii: “bado kuna muda, bado najipanga, haraka haraka haina baraka! Bado ninatafuta mtaji kumbe shetani anamsahulisha hekima hii ya wahenga: Mtaji wa maskini ni nguvu zake mwenyewe bila jasho hupati!” Askofu Kilaini ni mtu wa kutafuta mafanikio na kuacha alama kama konokono. Tumuige, walau otesha mwembe au mparachichi au mzambarau. Alama hizi ni zaidi ya picha za ukumbusho, sanamu za ukumbusho; alama hizi ni zaidi ya mawe ya msingi kwenye majengo au minara ya kumbukumbu.

Miaka 18 iliyopita, kuna rafiki yangu alikuwa anaadhimisha Jubilei ya kuzaliwa kwake, akatuma kadi ina jina langu, na imeandikwa namba 5619 akimaanisha mimi nilikuwa Mwalikwa wa 5619. Chini yake ameandika tanbihi kwa wino mzito: “Tafadhali usije na zawadi, uwepo wako unatosha.” Kweli mtu huyo alikuwa na uwezo mkubwa kiuchumi. Hakuchangisha mtu yeyote kufanikisha sherehe, na hakupenda mtu amchangie kuonesha kuwa si ombaomba, anajitosheleza! Lakini mimi sikusita kumtumia meseji hii haraka sana: “Batilisha kadi yako uliyonitumia, niandikie kadi nyingine yenye maneno haya: ‘Zawadi ya pesa inapokelewa kwa mikono miwili, kwa ajili ya kusaidia yatima, kujenga vyoo kwenye shule ya msingi nilikosomea na kununua vifaa tiba kwa hospitali mbili wilayani mwangu.’” Hakujibu! Na hivyo sikwenda. Kuna baadhi yetu wana mishahara mikubwa, na biashara kubwa. Wanatumia mapesa hayo kujenga horofa wakati wana watoto wawili au mmoja, kupanua biashara, kujenga maduka, mahoteli, magesti; kununua magari, malori, meli, nk. Hizo si kumbukumbu – haziachi alama mioyoni mwa watu ni ubinafsi. Kumbuka: “mwembe hauli maembe yake.” Kama huwezi kujenga zahanati au hospitali, madarasa au nyumba za walimu, kuchimba visima vya maji; basi, wanunulie maziwa watoto wa shule zilizomo wilayani mwako walau kwa mwaka mzima au maisha yako yote, au wanunulie sare ya shule; walimu wanunulie suti, wavae vizuri; tembelea vituo vya walemavu uone mahitaji yao. Biblia inasema: “anayemsaidia maskini anamkopesha mwenyezi Mungu; Mwenyezi Mungu atamlipa kwa tenda lake jema” (Methali 19:17; rejea Tobiti 12:9)”.

Au kama hayo huyawezi, daima kumbuka kutoa moja ya kumi ya mshahara wako na mapato yako kama zaka yako ya kila mwezi kwa Paroko aendeleze Parokia yake, na kwa Askofu aendeleze Jimbo lake. Au kwa Imamu na Shekhe aendeleze Msikiti wake. Lakini fanya hivyo bila kutangaza kwenye vyombo vya habari kwa kutengeneza bango kubwa la hundi linalolingana mlango, ili kuonyesha kiasi ulichochangia. Biblia inasema: “Hakuna jema litakalomjia mtu anayedumu katika uovu au mtu anayekataa kutoa zaka” (Sira 12:3). Kumbukumbu ni jambo, au neno, au kitu chochote kinachogusa moyo wa mtu au mioyo ya jamii wakatabasamu na kukuombea baraka. Askofu Kilaini ameacha alama. Alama hizi ni urithi udumuo kwa vizazi vijavyo, kadiri Maandiko Matakatifu yanavyommwagia sifa kati ya wazee yakisema: “Sasa tuwasifu watu mashuhuri, wazee wetu na vizazi vilivyopita. Mungu aliwapa fahari kubwa, akawafanya wakuu tangu siku za kale. Walikuwako wale waliotawala falme zao, watu mashuhuri kwa nguvu zao; washauri waliojaa busara, watangazaji wa unabii. Baadhi yao waliacha jina jema duniani, na watu wakatangaza sifa zao mpaka leo. Wako na wengine ambao hawakumbukwi, ambao wametoweka wakawa kama hawakuishi. Walikuwa kana kwamba hawakupata kuzaliwa, kadhalika na watoto wao baada yao. Hao walipita duniani kama mshale upitavyo angani bila kuacha alama yoyote” (rejea Sira 44:1-3, 8-9). Askofu Kilaini ameacha alama zaidi ya moja, alama lukuki – Tumshukuru kwa kumpigia makofi ya aina tatu – makofi ya afya, makofi ya maua na makofi ya nyota.

Miaka 25 ya Uaskofu wa Askofu Kilaini
Miaka 25 ya Uaskofu wa Askofu Kilaini

Hebu tuorodheshe alama kumi:

Mosi, Askofu Kilaini alipoadhimisha miaka 25 ya upadre alikarabati Kilaini shule ya msingi nyumbani kwake na kujenga za Walimu. Pili, Askofu Kilaini alipoadhimisha Jubilei ya miaka 50 ya upadre alitumia zawadi yake ya pesa aliyopewa kumnunulia kiti-mwendo (Wheel chair) mtoto mlemavu Hilda Elizeus na kumuasili kama mtoto wake, akigharamia matunzo na elimu yake. Sasa mtoto huyo yuko kidato cha tatu. Tuzidi kumuombea heri na fanaka. Tatu, Askofu Kilaini ametoa vipindi vya Dini akielimisha umma juu ya Historia ya Uinjilishaji Tanzania na Kanisa kwa ujumla, alimaarufu chimbachimba Historia ya Kanisa. Nne, Askofu Kilaini ameandika vitabu vingi, kitabu kimojawapo ni cha Historia ya Uinjilishaji Kagera. Tano, Askofu Kilaini amejibu na anaendelea kujibu maswali ya papo kwa papo, tena kwa umahiri na ufasaha mkubwa – ni alama zidumuzo akilini na mioyoni mwa wasikilizaji.  Sita, Askofu Kilaini amesimamia na kuchochea uanzishwaji wa vituo vya Radio–Maria, Radio Mbiu, Radio Tumaini na TV Tumaini kwa ajili ya maendeleo endelevu ya mwanadamu, ni alama zidumuzo. Saba, Ukarabati wa Kanisa Kuu la Bikira Maria wa Huruma, uliokuwa umechukua miaka 15. Askofu Kilaini akiwa Askofu Msaidizi wa Askofu Nestori Timanywa alihamasisha waamini wakachangia pesa kubwa, Kanisa likakamilika na kutabarukiwa tarehe 6 na 7 Oktoba 2012, na kuhamisha mwili wa Mwadhama Laurean Rugambwa kutoka Kashozi na kuuzika Kanisa Kuu Bukoba.

Nane, tarehe 10 Septemba 2016 tulipata tetemeko na nyumba nyingi za Kanisa ziliharibika ikiwemo nyumba yake kule Bunena; na ile ya Askofu Jimbo, kule Ntungamo. Hivyo, Askofu Kilaini aliweza kuomba msaada nje na ndani ya nchi na kuupata, akausimamia na kisha kuandika ripoti sahihi ya mapato na matumizi. Na siyo taarifa ya kubabaisha inayoficha matumizi mabaya ya fedha. Tisa, Askofu Kilaini aliomba msaada Missio Aachen na kuomba ufadhili kutoka wanafunzi waliopitia Ihungo St. Thomas More Secondary School kujenga kanisa jipya na zuri hapo katika mazingira ya Shule ya Sekondari ya Ihungo, kwa sababu kanisa la zamani liliharibiwa vibaya na tetemeko. Kumi, Askofu Kilaini anapenda sana Jumuiya Ndogo Ndogo za Kikristo. Amefanya utume wake wa kuhubiri na kueneza Jumuiya Ndogo Ndogo za Kikristo (JNNK) Kiparokia, Kijimbo, Kitaifa na Kimataifa. Si mtu wa kuhubiria watu wanywe maji wakati anakunywa divai. Amewahubiria watu kunywa maji naye anakunywa maji. Amewahubiria watu JNNK – ameshiriki katika jumuiya, mfano pale kwako Bunena wewe ni mwanajumuiya hai wa Jumuiya ya Mt. Veronica na hata michango ya jumuiya unaitoa. Je, hiyo si alama hai? Maisha ni kitabu ambacho kimeandikwa kurasa mbili ukurasa wa kwanza kumeandikwa tarehe ya kuzaliwa, ukurasa wa mwisho kumeandikwa tarehe ya kufa aijua Mungu tu. Katika kitabu unajaza kurasa hizo kwa matendo ya upendo ukizingatia tu amri kuu ya mapendo. Watu mbalimbali waweza kusoma yafuatayo.

Miaka 25 ya Uaskofu wa Askofu Kilaini
Miaka 25 ya Uaskofu wa Askofu Kilaini

Zifuatazo ni alama 25 ulizoziacha mioyoni mwa watu. Nitazitaja kwa mwendokasi:

1.     Ni Baba mwenye huruma kwa wengi, ambaye ukimuelezea changamoto yako anayoweza kuibeba ataibeba na kukusaidia. Kama ni ngumu kwake, atakueleza wazi kwamba hii hapana siiwezi, na atakutafutia mtu wa kukusaidia kuitatua changamoto hiyo.

2.     Ni mtu ambaye anaenda na wakati licha ya umri wake wa miaka 77. Amejitahidi kufanya utafiti na kutumia vizuri sana mtandao (internet) kwa kuchimbua mambo ambayo baadhi ya vijana hawayafahamu hasa katika Kanisa. (Ni kama Askofu Bernadin Mfumbusa wa Kondoa).

3.     Ni Baba anayejitoa kwa matukio ya wengine, amekua mstari wa mbele kushiriki na kushirikiana na waamini katika matukio ya kijamii hasa anapokuwa na nafasi (Ni kama Askofu Almachius Rweyongeza wa Kayanga).

4.     Ni mwenye hekima na busara; mpenda amani; Kutojikweza licha ya kujaliwa akili na busara nyingi; Mahusiano mazuri na watu wa aina zote na kumudu vizuri lugha nyingi Kihaya, Kiswahili, Kiingereza, Kilatini, Kiitaliano, Kifaransa, Kijerumani, Kireno, nk.

5.     Askofu Kilaini ni Askofu ambaye anaweza akachangamana na mtu yeyote na yuko tayari kumsikiliza, na mtu anapotoka kwake anakuwa amesuuzika rohoni mwake. Anajishusha ili AWEZE kumhudumia.

6.     Askofu Kilaini, haiba yake “ni kama sumaku kwa watu wote”. Watu WENGI sana amewagusa sana katika mafundisho yake mbalimbali kama vile Historia ya Kanisa: Maswali na majibu, mahubiri mazuri sana ambayo yanawagusa wengi.

7.      Askofu Kilaini ni mvumilivu sana, hata kama mtu amekwaruzana naye, haweki kinyongo, anamwiga Bwana wake Yesu Kristo kusamehe.

8.     Askofu ni baba wa imani na matendo.

9.     Askofu Kilaini anawajali sana wanyonge na yuko tayari daima kuwahudumia kwa kile ambacho kiko ndani ya uwezo wake.

10.  He is a living saint. Ni mtakatifu anayeishi kati yetu.

11.  Mwinjilishaji asiyechoka kwa njia ya radio. Kwa muda wote Baba Askofu Kilaini ametumia radio kama chombo cha uinjilishaji bila kuchoka. Anafanya tafiti za historia ya Kanisa, na teolojia kwa ujumla kufundisha na kujibu maswali na dukuduku za waamini. Kwa mfano, ameinjilisha sana kupitia radio Mbiu na Radio Maria, Radio Tumaini na Tv Tumaini..

12.  Ni mtu mwenye nidhamu kubwa ya kufuata ratiba. Amefanikisha mambo mengi na kuboresha mengi kwa sababu ya kipaji chake cha kujali thamani ya kutunza muda. Baba Kilaini, kwa wastani, hufika sehemu ya tukio dakika 15 hadi 20 kabla ya muda uliopangwa kuanza kwa tukio hilo. Kwa sababu hii amewawezesha watu wengi kuwahi wakijiambia: Askofu Kilaini huwa hachelewi.

13.   Kipaji cha kujihabarisha kila wakati. Kwa Baba Kilaini, uzee sio kikwazo cha kukosa taarifa na ujuzi. Anayo matumizi mazuri ya mtandao wa “internet”, kipaji kinachomfanya kubaki sambamba na yanayojiri duniani na kanisani.

14.   Baba Askofu Kilaini ni mchungaji wa watu anayekuwa daima kati ya watu na anapendwa sana na watu wa aina zote na kila mmoja haogopi kumfikia kwa lolote.

15.  Ni jasiri na mvumilivu, anaweka pembeni changamoto zake za afya, hata katika nyakati zozote ngumu, yeye ni tabasamu na kufariji wengine.

16.  Ni mkarimu wa kushirikisha dunia nzima ukuu wa Mungu kupitia mtandao ya kijami na vyombo vya habari. Mwana historia aliyebobea, anajulikana sana katika kipindi cha CHIMBA CHIMBA.

17.  Amekirimiwa kipaji cha kuchambua mambo kwa haraka na kujieleza kwa ufasaha na mvuto unaogusa wengi kwa haraka.

18.    Ni kiongozi mwenye muono na makini katika kutunza fedha na mali ya Kanisa.   Nilipojiunga Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC) kama Katibu Mkuu Msaidizi aliniasa juu ya umuhimu wa kuiwekea Taasisi Akiba ambayo ni muhimu katika kuibua mipango na kuendeleza iliyopo. Hilo limenisaidia sana katika kusimamia Taasisi za Kanisa na kuongeza thamani ya ziada.

19.   Ni mpenda mawasiliano na mtunza kumbukumbu kidijitali: mara kadhaa amenishangaza na kuwashangaza wengi jinsi anavyoweza kutuma baadhi ya picha za miongo kadhaa, ambazo huturudisha katika kuthamini watu tuliofanya nao, na ambao wamegusa maisha yetu kwa namna mbalimbali.

20.  Ni muunganishi wa watu. Kwa njia ya mtando wa kidijitali ameunganisha wengi na kuchochea ufanikishaji wa maendeleo ya kiroho na kimwili.

21.  Ni mpenzi wa Sala, Hija na Maisha ya Watakatifu; hususan Bikira Maria, Mt. Yosefu na Mtakatifu Teresia wa Mtoto Yesu.

22.  Ni mvumilivu katika mateso na majaribu. Amepitia changamoto  nyingi ambazo hazikumfanya akate tamaa katika utumishi.

23.  Ni nadhifu na mtanashati. Havai kupindukia, ila avaapo anatoka vizuri (rejea Sira 19:29-30).

24.  Askofu Kilaini ni mtu wa Mungu. Ni mchamungu. Anajitahidi kumuiga Mungu na anatualika daima tumuige Mungu, si kumuigiza, kadiri ya Maandiko Matakatifu yasemavyo: “Mwigeni Mungu maana ninyi ni watoto wake wapenzi. Upendo uongoze maisha yenu kama vile Kristo alivyotupenda, na kwa ajili yetu akajitoa mwenyewe kama dhabihu yenye harufu nzuri sadaka impendezayo Mungu”

(Efe 5:1-2).

25.  Askofu Kilaini ni mtu wa watu, ni mtetezi wa wanyonge. Anatualika tumuige Ayubu ambaye alijigamba akisema: “Kwa vipofu nilikuwa macho ya kuwaonyesha njia, kwa viwete nilikuwa miguu yao. Kwa maskini nilikuwa baba yao, nilifanya bidii kutetea haki za watu nisiowajua” (Ayubu 29:15-16; rejea Met 31:8-9).

Miaka 25 ya Uaskofu wa Askofu Kilaini
Miaka 25 ya Uaskofu wa Askofu Kilaini

Neno la 5: Jubilei ya Askofu ni fursa ya kuombea Miito ya Upadre

Bwana Yesu alisema: “Mavuno ni mengi, lakini wafanyakazi ni wachache. Basi, mwombeni mwenye mavuno atume wafanyakazi wavune mavuno yake” (Mt 9:37-38). Hakuna jambo linalomtia nguvu Askofu yeyote kuona wazazi wanaopokea baraka ya watoto, wakiwalea vizuri na kuwatunza vizuri hali wakiwaelekeza kwenye miito mitakatifu ya Upadre kama Mzee Eli wa Agano la Kale alivyomwelekeza mtoto Samweli. Ni furaha iliyoje Askofu anapompadrisha Padre, kwani Padre ni msaidizi wa karibu sana wa Askofu. Jiulize familia yako imezaa Mapadre wangapi? Ukoo wako umezaa mapadre wangapi? Mtakatifu fulani amekuwa na haya ya kusema:

Neno la 6. Jubilei ni wakati wa kutiana moyo

Licha ya changamoto, maana utume unaendelea. Changamoto katika wito wowote ule zipo. Biblia inasema: “Ukifa moyo wakati wa shida, wewe ni dhaifu kweli” (Methali 24:24). Bwana Yesu naye anasema: “Ulimwenguni mtapata masumbuko/changamoto; lakini jipeni moyo? Mimi nimeushinda ulimwengu” (Yoh 16:33). Biblia inaendelea kusema: “Mwanangu, ukienda kumtumikia Mungu uwe tayari kupata majaribu. Uwe mnyofu wa moyo na nia moja; na usihangaike wakati wa taabu. Ambatana na Mungu wala usimwache kamwe, nawe utafanikiwa mwishoni mwa maisha yako. Uyapokee yote yatakayokupata, hata ukiaibishwa uwe na uvumilivu, maana dhahabu hujaribiwa kwa moto na watu wanakubaliwa na Mungu kwa tanuri ya aibu. Mtegemee Mungu, naye atakusaidia, shika njia nyofu na kumtumaini yeye” (Sira 2:1-6; rejea Ebr 12:5-8). Katika wito wa ukuhani, changamoto zipo. Lakini cha kufurahisha na kutia moyo ni kwamba furaha ya ukuhani na unabii inazidi changamoto! Licha ya changamoto hajawahi kujutia kwa nini alikuwa Padre na kwa nini alikuwa Askofu daima anamshukuru Mungu na kumtumikia kwa furaha. Maandiko Matakatifu yanatutia moyo yakisema: “Tuna hazina hii katika vyombo vya udongo, ili adhama kuu ya uwezo iwe ya Mungu… twaona shaka, bali hatukati tamaa; twaudhiwa, bali hatuachwi; twatupwa chini, bali hatuangamizwi… kwa kuwa tuna roho ile ya Imani…” (2 Kor 4:7-15). Nabii Yoeli anasema: “Hata aliye dhaifu na aseme: ‘Mimi pia ni shujaa’” (Yoeli 3:10). Changamoto ni mishale. Ukiambatana na Mungu utaikwepa! Hivyo usiogope! Wahenga wetu wamesema: “Ukiona nyani amezeeka, ameikwepa mishale mingi.” Changamoto hizo, mishale hiyo ni ipi ambayo Askofu Kilaini ameikwepa?

Mosi, mnamo tarehe 15 Novemba 1981 alipata ajali mbaya ya gari akiwa na umri wa miaka 33, alipogonga kichwa chake kwa chuma, na kichwa chote kikapasuka vipande. Bahati nzuri damu iliyovuja aliitapika akawa salama. Huo si muujiza? Alikaa Bugando-Mwanza mwezi mmoja, baadaye alienda KCMC Moshi kwa wiki mbili kwa sababu mishipa ya macho ilikuwa imeathirika sana. Madaktari wote walijaribu, lakini hawakufanikiwa kumtibu kila kitu, hivyo jicho moja alilipoteza.

Pili, kuna mshale wa kutekwa nyara kwenye ndege tarehe 26 Februari 1982. Hapa Askofu Kilaini kwa ufupi anasema: “Utekaji ni kitu kibaya sana kisicho cha kawaida. Baada ya kupata ajali mbaya na kukaa mwezi mmoja akisali Nyakijoga, Mugana katika kituo cha Hija cha Mama Maria, alikuwa amejisalimisha kwa Mungu. Hivyo, katika utekaji hakushtuka. Alikuwa tayari kufa akimshukuru Mungu kwamba alikuwa amemtayarisha.” Aliukwepa mshale huo.  Tatu, kuna changamoto au mshale wa kufanya kazi kwa jicho moja. Pale Roma mahospitali mbalimbali walijaribu kumponya wakashindwa, naye akapokea hali. Watu hudhania ana kengeza, kumbe kwa miaka 40 sasa amefanya kazi na jicho moja tu kwenye kompyuta, nalo ni dhaifu. Anaendelea kuukwepa mshale huo kwa tabasamu. Nne, changamoto za kuwa na kazi nyingi, na matatizo ambayo hupati suluhu hasa kama yalihusu watu. Mara nyingine kuona kama hueleweki, hata kupata upinzani kutoka sehemu ambapo ungetegemea kusaidiwa, huu mshale unaumiza sana, lakini ameukwepa kwa sala. Tano, kupata kiharusi, lakini anashukuru aliwapata akina Simoni wa Kirene na akina Veronika wakamsaidia, akapona – wote hao anawashukuru sana.

Neno la 7: Jubilei ni fursa ya kuchota mafundisho, 'Elimu haina mwisho'

Baba Askofu Kilaini ametualika hapa kutupa mafundisho saba yafuatayo:  Mosi, Jambo kubwa ni kwamba usikubali kubeba matatizo, changamoto, huzuni moyoni, na kuruhusu yaache alama mbaya moyoni, chuki au kinyongo, bali yaache uzoefu wa kushinda. Samehe saba mara sabini (Mt 18:22). “Usikubali kushindwa na ubaya, bali ushinde ubaya kwa wema” (Rum 12:21).

Pili, afya yake imekuwa mgogoro baada ya kupata ajali mbaya na kupata shida ya macho na kuwangwa kichwa. Katika hali hiyo Askofu Kilaini anakufundisha usibaki kulalamika juu ya kitu ambacho huwezi kugeuza, au kuanza kubabaika na kukimbilia njia za mkato, mfano kikombe cha Babu, upako, nk.; bali jifunze kutembea nacho, Mungu anakupa nguvu ya kumudu. Biblia inasema: “Furahini daima, salini kila wakati na kumshukuru Mungu kwa kila jambo” (1 Thes 5:16-18). Tatu, ukipata kilema chochote mwilini usijifiche, usinyongonyee na kuwa na aibu nacho. Yeye alipopata kiharusi, alipata misaada mingi na akaendelea na kazi hata pale ambapo uso wake ulikuwa hautamaniki. Aliamua kutojificha. Wakati huo alielewa wanavyojisikia watu wenye ulemavu hasa ulemavu ukiwa usoni. Askofu Kilaini anatualika tuzingatie Maandiko haya Matakatifu: “Atukuzwe Mungu na Baba wa Bwana wetu Yesu Kristo. Baba mwenye huruma na Mungu mwenye kuleta faraja yote. Yeye hutufariji sisi katika taabu zetu zote, ili nasi tupate kuwafariji wengine katika kila taabu kwa faraja hiyohiyo tunayopokea kutoka kwa Mungu” (2 Kor 1:3-7).

Nne, dini ya Kikristo ni dini ya Msalaba si ya sofa, ni ya muarobaini na mshubiri si ya soda na juisi; ni ya kijeshi si ya mahanjumati (Mt 16:24; Yh 15:18-27; 16:1-4). Hivyo acha kutangatanga katika imani na kuishi kama popo au kinyonga. Uwe na msimamo katika imani (Fil 2:1-11). Biblia inaonya ikisema: “Mtu aliye na mashaka, mwenye nia mbili na asiye na msimamo katika mwenendo wake wote, asidhani ya kwamba atapata chochote kile kutoka kwa Mungu” (Yak 1:7-8). Tano, leo Askofu Kilaini anaadhimisha miaka 25 ya Uaskofu akiwa amestaafu, lakini anaendelea na utume na uchungaji wa kuadhimisha Sakramenti na kuhubiri Neno la Mungu. Fundisho ni hili: “Unastaafu madaraka, lakini hustaafu huduma hadi nguvu za mwisho na pumzi ya mwisho.” Biblia inasema: “Wewe shikilia wito na wajibu wako, zeeka ukiwa kazini mwako” (Sira 11:20). “If you rest you rust!” “You are retired, but not tired.”

Mtafiti mmoja alisema: “Changamoto ya kustaafu ni namna ya kutumia muda wako bila kutumia pesa.” Sita, usiogope changamoto, maana “Wapandao kwa machozi watavuna kwa kelele za furaha” (Zab 126:5). Bwana Yesu alizipitia, naye anatuambia: “Ulimwenguni mnayo dhiki; lakini jipeni moyo; mimi nimeushinda ulimwengu” (Yoh 16:33). Mitume walizipitia nao wakasema: “Ni lazima sisi sote kupitia katika taabu nyingi ili tuingie katika ufalme wa Mungu” (Mdo 14:22). Mwandishi mmoja amesema: “Changamoto ni dalili za uhai pambana nazo, asiyekuwa na changamoto ni maiti!”Saba, Maandiko Matakatifu na Askofu Kilaini tunapata nasaha hizi: “Ulipe hadhi jina lako kwani litakubakia, litadumu kuliko hazina elfu moja za dhahabu” (Sira 41:12).     

Neno la 8: Jubilei ni fursa ya kufanya toba, kuomba msamaha

Askofu Kilaini ametualika tuungane naye kumaliza deni la toba kwa Mungu na kwenu nyote. Anasema katika miaka 25 ya Uaskofu amefanya makosa mengi na labda kuwaudhi wengi katika namna yake ya kutenda, maamuzi aliyofanya, na maneno aliyoyatamka. Mbele ya Mungu na mbele yetu sisi sote anaomba msamaha kwa moyo wa dhati kabisa. Yeye alijaribu kutimiza wajibu wake, lakini kama binadamu ana madhaifu mengi; na hivyo anahitaji huruma kutoka kwa Mungu na kutoka kwenu. Anapiga magoti mbele yake Rabuka na kusema – “Mea culpa, Mea culpa, Mea maxima culpa”: “Nimekosa mimi, nimekosa mimi, nimekosa sana, hivyo namuungamia Mungu Mwenyezi, nanyi ndugu zangu niombeeni kwa Bwana Mungu wetu.” Mungu mwenyezi akuhurumie akusamehe dhambi zako akufikishe kwenye uzima wa milele. Amina.

Neno la 9: Jubilei ya Uaskofu ni fursa ya kuishauri Serikali Sikivu (Ebr 13:17)

Tulipopata uhuru wa bendera 1961, Baba wa Taifa alikuwa na mtihani bado wa kupiga vita maadui watatu: Ujinga, Umaskini na maradhi. Je, tumefanikiwa kwa kiwango gani kupiga vita maadui hao?

Miaka 25 ya Uaskofu wa Askofu Kilaini
Miaka 25 ya Uaskofu wa Askofu Kilaini

Kuhusu adui ujinga

Kuna bango katika lango la Chuo Kikuu fulani huko Afrika ya Kusini linasomeka hivi: “Ukitaka kuangamiza taifa lolote bila kumwaga damu, huhitaji kutumia silaha za nyukilia. Njia nzuri ya kuangamiza taifa ni kuharibu mfumo wa elimu na maadili. Ruhusu mbumbumbu waonekane ‘wamefaulu’ na wasonge mbele hadi Vyuo Vikuu. “Matokeo yake yatajidhihirisha baada ya muda: mbumbumbu hao wakishafaulishwa kwa kupata vyeti feki, wagonjwa watafia mikononi mwa madaktari na manesi; majengo yataporomoka mikononi mwa wahandisi; pesa zitapotelea mikononi mwa wachumi, utu utapotea mikononi mwa viongozi wa dini na serikali, na haki itapotea mikononi mwa mahakimu na wanasheria.” Kuchezea elimu ni kuchezea amani, ni kuangamiza Taifa! Mungu alionya watu wake kupitia kinywa cha Nabii Hosea akisema: “Watu wangu wameangamia kwa kukosa maarifa” (Hosea 4:6). Juzi nilikutana na vijana wawili. Mmoja akawa anamuuliza mwenzake. Je, umeishapata ajira? Mwenzake alijibu: “Sijapata, sasa huu ni mwaka wa nane”. Huyo rafiki yake akadakia kwa mshangao: “Wewe umekosa ajira kabisa kabisa hata ajira ya ualimu umekosa?” Akamcheka sana! Akiwa na maana kwamba Ualimu ni ajira ya walioshindwa, sio wito hapa Tanzania!  Fani ya Ualimu iheshimiwe na Serikali, isinyanyapaliwe. Irudishiwe hadhi yake! Kumbuka Mwalimu ndiye komandoo wa adui ujinga. Asipoandaliwa vizuri tutashindwa vita ya kumshinda adui ujinga, na tutaendelea kuliwa na mataifa mengi. Wahenga wetu wamesema: “Wajinga ndio waliwao!”

Mwalimu hasa wa Shule za Awali na Msingi awe amepata ushindi wa alama za juu kabisa, na alipwe mshahara unaolingana au kuzidi wa wabunge na Waziri, kwa sababu anafundisha na kulea madaktari, maprofesa, waandisi, wachumi, viongozi wa dini na serikali, maaskofu na wanajeshi, waandishi wa habari, wafanyabiashara, nk.   Mimi naunga mkono mia kwa mia sera mpya ya elimu ya kusoma hadi darasa la 10 pamoja na amali. Naomba sera hii isimbane tu mtoto wa mkulima na mpiga kura, wakati mtoto wa Mheshimiwa Mbunge aliyepitisha sera hiyo akaenda kusomea nje ya nchi huko Marekani, Ulaya, Asia na Uchina akitumia mshahara wake mnono, marupurupu na kiinua mgongo, ambavyo havina kikokotoo! Walimu waondolewe kikokotoo kabisa! Narudia watumishi wa ngazi ya chini waondolewe kikokotoo. Pia Serikali inapoendelea na utekelezaji wa sera mpya ya elimu iruhusu shule binafsi ziwe na mitaala ya kimataifa, na shule binafsi ziingie ubia na shule za nje ya nchi au za kimataifa, kwani huko ndiko tutapata Mapadre, Watawa na Wachungaji wa kufanya utume popote duniani. Hata na watanzania wenyewe baadhi wataweza kusaka kwa urahisi ajira nje ya nchi kama tunavyowaona Wahindi, Wachina, Wakenya, Waganda, nk hapa petu.

Kuhusu adui umaskini 

Hayati Baba wa Taifa alitufundisha kuwa fedha sio msingi wa maendeleo, Nami pia nilifundisha siasa shuleni nikiwasisitizia wanafunzi wangu jambo hilo. Nilikuwa nimeiva kisiasa. Ili nchi yetu iendelee inahitaji mambo 4: Watu, Ardhi, Siasa safi, na Uongozi bora. Tanzania ya leo mikopo na misaada imekuwa ni msingi wa maendeleo! Siku moja niliota ndoto, raia fulani mwenye cheo cha Ukatibu Kata alikuwa na uchungu mkubwa, akakemea na kusema: “Acheni mikopo, taifa linauzwa!” Baada ya kusema hayo akanyanganywa ofisi, akanyanganywa baiskeli yake, na kutishiwa – “Ukiendelea na kidomodomo, tutakuja kufyeka shamba lako la mahindi na mchicha!”. Hiyo ilikuwa ndoto yangu.

Tujiulize: Je, tumezingatiaje mambo 4?

1)  Watu: Je, ni sawa kuhamisha watu toka makazi yao, badala ya kuhamisha wanyama? eti kwa ajili ya watalii na wawekezaji?

2)  Ardhi: uharibifu wa mazingira – kufyeka na kuchoma misitu; matumizi ya sumu kuua magugu. Ikumbukwe “Mbuyu ulianza kama mchicha, kama gugu”. Wananchi kunyanganywa ardhi na kupewa wawekezaji kwa mfano kwa ajili ya kilimo. Je, wananchi wa pale wananufaika kwa vipi? Kwa mfano tuna Kagera Sugar, bei ya sukari kilo moja Dar es Salaam ni sh 2,800/=; Mkoa wa Kagera ambako kuna mashamba ya miwa na viwanda vya sukari, kilo moja ya sukari sh 3,000/= huko Kyerwa. Dar es Salaam mfuko wa saruji sh 16,000/=, na kiwandani sh 12,000/=; Mkoa wa Kagera, Wilaya ya Kyerwa, mfuko wa saruji ni sh 26,000/=. Mbona Kagera inafanywa maskini kana kwamba wananchi wa kule si wa Tanzania?

3) Siasa safi: sera, hoja, sheria, zinazopitishwa Bungeni kwa wingi wa makelele ya NDIYO, badala ya kupiga kura za siri zilizowaingiza Bugeni. Msemaji mmoja alikuwa anasema kwamba nyuma ya makelele hayo kuna fundi mitambo, ikiwa wanaosema HAPANA ni wengi, fundi mitambo anapunguza sauti ya vipaza sauti inakuwa ya chini. Ikiwa wanaosema NDIYO ni wachache, fundi mitambo anaongeza sauti! Hiyo ni siasa safi?

4) Uongozi Bora: kupata viongozi, kwa kuchanganya na kujumlisha kura halali, nusu halali na haramu – na kutangaza mshindi hata kama hapendwi na wananchi hiyo sio njia ya kupata viongozi bora – wanaoingia uongozi kwa kuiba kura, kuhonga au kuwapoteza wapinzani wao.

Kuhusu adui umaskini

- Tutamshindaje adui umaskini iwapo wananchi wanachezea muda, kushinda na kukesha kwenye mabaa, kushinda na kukesha kwenye viwanda vya mipira na TV? Napoleoni aliwaambia wanafunzi wake: “Muda unaouchezea ni fursa ya kuwa balaa baadae”.

- Tamaa ya pesa huleta umaskini. Biblia husema: “mtu apatae mali isiyo halali ni kama kware akusanyaye makinda ambayo hakuyaangua: wakati wa kilele cha ujana wake itamchopoka, na mwishoni atakuwa mpumbavu” (Yer 17:11). Biblia inaendelea kusema: “wale wanaotaka kutajirika huanguka katika majaribu na kunaswa katika mtego wa tamaa nyingi mbaya za kipumbavu, ambazo huwavuta mpaka kwenye uharibifu na maangamizi. Kwa maana kupenda sana fedha ni chanzo cha uovu wote” (1 Tim 6:9-10). Serikali ipige vita michezo ya kamali, bonanza, ‘pool’, kubeti, wachungaji wa uongo wanaohubiria watu utajiri kushuka kama mvua kwa kununua mafuta na maji ya upako, badala ya kufundisha watu kufanya kazi ya kilimo; kupiga vita ushirikina.

-Tutamshindaje adui umaskini iwapo wananchi wanaojiajiri kwa kuanzisha viwanda vidogovidogo wanakatishwa tamaa na TRA, kodi, tozo? Ambazo msemaji mmoja alisema; “Kula kadiri ya urefu wa kamba yako!”.

-Ili kumshinda adui maskini naomba serikali yetu sikivu na iliyo tayari kujifunza, iige mbinu anazotumia Rais Ibrahim TRAOE wa Burkina Faso ambaye alijiandaa mapema kwa kutokutegemea mikopo na USAID. Pia muigeni Mh Diomaye FAYE Rais wa Senegali, Trump alipokata misaada hiyo Marais hawa hawakubabaika wanaendelea kuchapa kazi kwa nguvu kwa ajili ya maendeleo ya wananchi wao.

Kuhusu adui maradhi

Ni mpaka lini serikali itaendelea kutumia pesa nyingi kuagiza au kushinikizwa chanjo toka nje? Je, madaktari wetu tuliowasomesha kwa kipindi cha miaka 64 ya uhuru, hawana uwezo kabisa kutengeneza chanjo zetu na madawa yetu wenyewe?

Kipindi cha UVIKO-19, KORONA kilituachia funzo gani? Miti shamba tuliyochanganya tukanywa, tukajifukizia tukapona ― je, mmeisahau? Baada ya Mh. Donald Trump kufunga misaada ya USAID tumejipangaje kukabiliana na adui maradhi, au tusalimu amri kwa kwa adui maradhi?

Waheshimiwa wabunge mpo? Je, mnasaidiaje mwananchi kupiga vita maadui ujinga, umaskini na maradhi?

Neno kwa Waheshimiwa Wabunge

1. Kuacha mtindo wa upitishaji hoja, sera, kanuni, nk. kwa wingi wa kelele za ndio badala ya kupiga kura za siri, na kuhesabiwa tukajua idadi ya waliopiga kura ya ndio Idadi ya waliopiga kura ya hapana, Idadi ya kura zilizoharibika.

2. Muigeni Mzee Ayubu wa Agano la Kale ambaye, “Uadilifu ulikuwa vazi lake, kutenda haki kulikuwa kama joho na kilemba chake. Kwa vipofu alikuwa macho ya kuwaonyesha njia, kwa viwete alikuwa miguu yao. Kwa maskini alikuwa baba yao, alifanya bidii kutetea haki za watu asiowajua. Alizivunja nguvu za watu waovu, akawafanya wawaachilie mateka wao” (Ayubu 29:14-17).

3. Mzee Ayubu anasema: “Mtu ni mtoto tu wa mwanamke; huishi siku chache tena zilizojaa taabu. Huchanua kama ua, kisha hunyauka. Hukimbia kama kivuli na kutoweka” (Ayubu 14:1-2). Sanda hazina mifuko ya kihifadhi fedha.

4. Mt. Petro, Mtume anashauri viongozi wote akisema: “Ongoza lile kundi la Mungu mlilokabidhiwa; mlitunze si kwa kulazimika, bali kwa hiari kama atakavyo Mungu. Fanyeni kazi hiyo si kwa tamaa ya fedha, bali muwe mfano kwa hilo kundi” (1 Petro 5:1-3).

5. Biblia inatuambia: “usichukizwe na kila kosa la jirani yako, wala usifanye chochote kwa mkikimkiki wa ghadhabu. Kiburi huchukiwa na Mungu na binadamu; udhalimu ni jambo la kuchukiza kwa wote wawili. Kwa sababu ya udhalimu, kiburi na kupenda utajiri, mamlaka ya taifa moja huchukuliwa na taifa linguine. Je, mtu aliyevumbi na majivu atajivunia nini? Hata alipo hai matumbo yake yananuka” (Sira 10:6-9).

6. Wabunge fanyeni ziara ya majifunzo / study Tour Burkina Faso na Senegali. Bibi yangu alikuwa anaimba methali hii: “Mtoto ambaye hatembei, hubaki nyumbani akimsifia mama yake kwamba ni mpishi bora duniani.”

Litania ya Pesa

1.     Pesa hununua chakula, hazinunui hamu ya chakula.

2.     Pesa hununua sahani, hazinunui utamu wa chakula.

3.     Pesa hununua kitanda, hazinunui usingizi.

4.     Pesa hununua jiko, hazinunui mapishi bora.

5.     Pesa hununua jembe, hazinunui moyo wa kufanya kazi.

6.     Pesa hununua simu, hazinunui ujirani mwema.

7.     Pesa hununua mitihani ya darasani, hazinunui mitihani ya maisha.

8.     Pesa hununua vitabu, hazinunui maarifa.

9.     Pesa hununua peni, hazinunui mwandiko mzuri.

10.    Pesa hununua vyeti, hazinunui ufundi.

11.    Pesa hununua bima, hazinunui usalama.

12.  Pesa hununua dawa / chanjo, hazinunui afya.

13.  Pesa hununua saa, hazinunui muda.

14.    Pesa hununua suti, hazinunui heshima au uungwana.

15.  Pesa hununua silaha za kivita, hazinunui amani.

16.  Pesa hununua makanisa, hazinunui imani.

17.  Pesa hununua pete, hazinunui uaminifu kwa maagano ya ndoa.

18.  Pesa hununua mavazi ya ibada, hazinunui uchaji.

19.  Pesa hununua rozari, hazinunui moyo wa kusali.

20.  Pesa hununua vipodozi, hazinunui urembo.

21.  Pesa hununua wigi, hazinunui nywele.

22.  Pesa hununua wapambe, hazinunui marafiki.

23.  Pesa hununua mke, hazinunui mapenzi.

24.  Pesa hununua hakimu, hazinunui haki.

25.  Pesa hununua mtumishi wa nyumbani, hazinunui malezi bora.

26.  Pesa hununua starehe, hazinunui furaha.

27.  Pesa hununua maji, hazinunui mvua.

28.  Pesa hununua mbolea, hazinunui rutuba.

29.  Pesa hununua tochi, hazinunui mwanga wa jua.

30.  Pesa hununua viatu, hazinunui miguu.

31.  Pesa hununua miwani, hazinunui macho.

32.  Pesa hununua chupa ya maziwa ya kunyonyesha mtoto, hazinunui titi / ziwa.

33.  Pesa hununua sabuni, hazinunui usafi.

34.  Pesa hununua nyumba, hazinunui makazi.

35.  Pesa hununua uwongo, hazinunui ukweli.

36.  Pesa hununua machozi, hazinunui huzuni.

37.  Pesa hununua kura, hazinunui utawala bora.

38.  Pesa hununua mchumba, hazinunui upendo.

39.    Pesa hununua pasipoti ya kwenda nchi yoyote, hazinunui pasipoti ya kwenda mbinguni au paradisini.

40.  Pesa hununua jeneza la kifahari, hazinunui uzima wa milele.

Miaka 25 ya Uaskofu wa Askofu Kilaini
Miaka 25 ya Uaskofu wa Askofu Kilaini

Neno la 10. Sasa waweza kupumua. Namalizia

Aliyesinzia na aamke. La kumi, tunaendelea na Adhimisho Takatifu la Misa ambalo ni chemchemi na kilele cha maisha yote ya Kikristo (KKK. Na. 1324). Na adhimisho hili la Misa linaongozwa na Askofu Method Kilaini nyota yetu ya leo aendelee kutuangaza tutoke katika giza la uongo na chuki, giza la udanganyifu na dhuluma; tuishi kwenye mwanga wa ukweli na haki, upendo na amani.

Askofu Almachius-Vincent Rweyongeza,

Jimbo Katoliki la Kayanga, Tanzania.

Katika Siku Kuu ya Mtakatifu Yosefu Mchumba wa Bikira Maria Mtakatifu tarehe  19 Machi 2025.

21 Machi 2025, 09:08
Prev
April 2025
SuMoTuWeThFrSa
  12345
6789101112
13141516171819
20212223242526
27282930   
Next
May 2025
SuMoTuWeThFrSa
    123
45678910
11121314151617
18192021222324
25262728293031