Papa Francisko awataka waamini kuacha tabia ya unafiki, ili kuruhusu neema ya Mungu kupenya ndani mwao!
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.
Wokovu ni zawadi kutoka kwa Mwenyezi Mungu, inayomkirimia mwamini uhuru wa ndani, changamoto na mwaliko kwa waamini kuondokana na unafiki katika maisha kama walivyokuwa wanafanya Mafarisayo na Waalimu wa sheria. Hii ni sehemu ya tafakari iliyotolewa na Baba Mtakatifu Francisko Jumanne, tarehe 16 Oktoba 2018 katika Ibada ya Misa Takatifu kwenye Kikanisa cha Mtakatifu Martha kilichoko mjini Vatican.
Baba Mtakatifu anasema, watu wa kawaida walionesha upendo wa dhati kabisa kwa Yesu, kwani ujumbe wake ulikuwa unashuka hadi kugota katika sakafu ya nyoyo zao, tofauti kabisa na Mafarasayo, Masadukayo na Walimu wa sheria waliojenga wivu na chuki dhidi ya Yesu, kwa kujidai kwamba, wao walikuwa safi na mifano bora ya kuigwa!
Baba Mtakatifu anakaza kusema, kwa nje makundi ya watu hawa yalionekana safi sana mbele ya watu, lakini, usafi na utakatifu huu, haukugusa undani wa maisha yao, kwani walikuwa ni watu wenye mioyo migumu na Kristo Yesu aliwafahamu fika! Ni kutokana na mwelekeo huu, makundi haya yalikwazwa na matendo ya Yesu, pale alipowasamehe watu dhambi zao au kuwaponya wagonjwa siku ya Sabato, kiasi cha kurarua mavazi yao kama alama ya kashfa kwa Kristo Yesu kujiita Mwana wa Mungu. Kipaumbele cha kwanza kilikuwa ni Sheria na wala si mahangaiko na mateso ya watu wa kawaida!
Baba Mtakatifu anaendelea kufafanua kwamba, Yesu alipoalikwa na Farisayo mmoja, alikubali mwaliko, akaingia na kuketi chakulani, kwa sababu alikuwa ni mtu huru! Farisayo anakwazwa na matendo ya Yesu yanayovuka Sheria za Musa na kusahau kwamba, Yesu alikuwa huru na wala hakufungwa na Sheria! Yesu “anawatolea uvivu” kwa kuwalinganisha na makaburi yaliyopakwa rangi kwa nje yanang’aa lakini kwa ndani kuna mifupa ya miili iliyooza. Wao ni sawa na makaburi yasiyoonekana, ambayo watu wapitao juu yake hawana habari nayo!
Yesu anawataka Mafarisayo kusafisha kwanza maisha yao ya ndani, kwani ndani mwao wamejaa unyang’anyi na uovu. Kitu kinachopewa kipaumbele cha kwanza na Mafarisayo ni mwonekano wa nje na kwa hakika anasema Baba Mtakatifu ni “Madaktari wa mwonekano wa nje”. Mfano wa Msamaria mwema ni changamoto inayowataka kumwilisha Sheria na taratibu katika maisha ya kawaida badala ya kujikita katika kufunga na kutoa sadaka, mambo yanayoelea kwenye ombwe pasi na ushuhuda halisi katika maisha. Kwa maneno mengine, hawa ni wanafiki; watu wenye ndimi kali zinazoweza kuua; watu ambao wako tayari kulipwa ili kuwachafulia watu wengine majina yao au hata kuwafutilia mbali kutoka katika uso wa nchi.
Baba Mtakatifu Francisko anasema, nyuma ya pazia la ugumu wa moyo kuna matatizo makubwa, yanayoonesha kwamba, makundi haya yalikuwa ni ya watu wenye moyo na shingo ngumu, watu ambao hawakuwa tayari kubadilika. Kwa hakika mioyo ya watu wanafiki iko mbali sana na Kristo Yesu, hawa ni watu waliomezwa na kutopea katika malimwengu. Yesu anawaita wapumbavu na kuwashauri kukumbatia mambo ya adili, upendo kwa Mungu na jirani, kwa kuruhusu neema ya Mungu iweze kupenya katika sakafu ya nyoyo zao, kwani wokovu ni zawadi ya bure kutoka kwa Mwenyezi Mungu na kwamba, hakuna mtu anayeweza kujiokoa kwa nguvu zake binafsi!
Baba Mtakatifu anapenda kutoa angalisho kwa wakristo, wakleri au watawa wanaojikweza ili kuonekana kuwa ni watu wema na watakatifu, lakini, ndani mwao ni watu wenye mioyo na shingo ngumu, kuwa macho na makini zaidi, kwani ndani mwao hawana hata kidogo Roho ya Mungu, kwani wanakosa roho anayewajalia uhuru kamili. Waamini wajitahidi kufanya tafakari ya kina ili kukazia maisha ya ndani yanayofumbatwa katika sala, uhuru wa ndani pamoja na matendo ya huruma, ushuhuda wa imani tendaji!