Papa atuma salam za rambi rambi huko Laos kutokana na mafuriko makubwa
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. - Vatican.
Baba Mtakatifu Francisko amesikitishwa sana na maafa yaliyosababishwa na mafuriko makubwa yaliyotokeo huko mjini Xepian – Xe Nam Noy, baada ya bwawa kubwa lililokuwa linajengwa na Kampuni kutoka Korea ya Kusini kubomoka, Jumanne, tarehe 24 Julai 2018. Kadiri ya taarifa kutoka Laos, zaidi ya watu 6, 600 hawana makazi tena baada ya nyumba zao kubomolewa na mafuriko.
Baba Mtakatifu katika ujumbe ulioandikwa kwa niaba yake na Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican kwenda kwa familia ya Mungu nchini Laos, anasema, anapenda kuonesha umoja na mshikamano na wananchi wa Laos katika kipindi hiki kigumu na kwamba, anawaombea huruma na faraja kutoka kwa Mwenyezi Mungu, wale wote waliokumbwa na maafa haya. Kwa njia ya sala na sadaka yake anaungana na wale wote wanaoteseka kwa kukosa makazi. Baba Mtakatifu anawatia shime wale wote wanaoendelea kujisadaka kwa ajili ya kuokoa maisha ya wananchi wa Laos, kufanya hivyo kwa ari na moyo mkuu.