Papa ametuma salam za rambi rambi kwa kifo cha rais Bush
Sr. Angela Rwezaula - Vatican
Baba Mtakatatifu Francisko, ametuma salamu za rambirambi zilizotiwa saini ya Kardinali Pietro Parolin katibu wa Vatican kufuatia kifo cha Rais wa zamani wa Marekani Bwana George Herbet Walker Bush, aliyefariki hivi karibuni.
Salam hizo zimetumwa kwa Kardinali Daniel N. DiNardo Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu la Galveston-Houston ambapo Baba Mtakatifu anaonesha masikitiko yake na kuwahakikishia ukaribu na maombi kwa ajili ya familia ya Marehemu Bush. Anamkabidhi roho ya Rais Bus katika huruma ya upendo wa Mungu mwenyezi na kuwatakia baraka tele kwa wale wote wanao ombeleza kutokana na kifo chake na ili wawe na nguvu na amani.
Kifo cha Rais wa zamani wa Marekani George Herbet Walker Bush, na maisha yake:Tangazo la kifo chake katika vyombo vya habari zilitolewa na mtoto wake George W. Bush, ambaye pia alikuwa rais wa 43 nchini Marekani. George H. W Bush, alikuwa rais wa 41 wa Marekani na alikuwa madarakani kati ya mwaka 1989 na 1993. Kati ya mwaka 1989-1993, alihudumu kama Makamu wa rais wakati wa uongozi wa rais Ronald Reagan. Hadi kujiwa na mauti yake, Bwana Bush amekuwa akiugua kwa muda mrefu. Mwezi Aprili mwaka huu alilazwa hspitalini baada ya kupata maambukizi katika damu, lakini baadaye akaruhusiwa kuondoka hospitalini.
Kifo chake kimemjia, miezi saba, mara baada ya kifo cha mkewe Barbara. George HW Bush alikuwa nani? Alihudumu kwa muhula mmoja, kama rais wa 41 wa Marekani kati ya mwaka 1989 na 1993. Bush atakumbukwa sana kwa mchango wake wa kumaliza vita baridi, na kuimarisha sera ya diplomasia ya Marekani. Licha ya kuwa na umaarufu wa asilimia 90, mwanasiasa huyo wa chama cha Republican alishtumiwa na wapinzani wake kwa kushindwa kushughulikia mambo ya ndani hasa uchumi, na wakati wa Uchaguzi wa mwaka 1992, Bill Clinton alimshinda na kumwondoa madarakani. Alianza kujihusisha na masuala ya siasa na mwaka 1964, baada ya kuanza kujihusisha na biashara ya mafuta, na kufikia umri wa miaka 40, alikuwa Milionea. Aidha, alikuwa rubani wa ndege za kivita jeshi la Marekani na mwezi Septemba mwaka 1944 aliangushwa na wanajeshi wa Japan, wakati wa vita vya pili vya dunia.