Tafuta

Papa Francisko: Madhabahu ya Bikira Maria Mfariji wa wanaotesema nchini Romani ni mahali pa: Sala, Majadiliano ya Kiekumene; Umoja, Udugu, Toba na Wongofu wa ndani! Papa Francisko: Madhabahu ya Bikira Maria Mfariji wa wanaotesema nchini Romani ni mahali pa: Sala, Majadiliano ya Kiekumene; Umoja, Udugu, Toba na Wongofu wa ndani! 

Hija ya Kitume Romania: Papa: Tofauti msingi ni amana na utajiri

Baba Mtakatifu Francisko asema, Madhabahu ya “Șumuleu Ciuc” yaani Bikira Maria Mfariji wa wanaoteseka. ni mahali ambapo waamini wa dini na madhehebu mbali mbali ya Kikristo wanakutana kusali. Hiki ni kielelezo cha majadiliano ya kidini na kiekumene; mahali pa kukuza na kudumisha umoja na udugu; mahali pa kupyaisha ushuhuda wa imani unaomwilishwa katika matumaini!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko kuanzia tarehe 31 Mei hadi 2 Juni 2019 anafanya hija ya 30 ya kitume kimataifa nchini Romania, inayoongozwa na kauli mbiu “Twende pamoja” ili kujenga na kudumisha umoja na mshikamano wa kitaifa; kwa kufuata nyayo za mashuhuda wa imani, waliomimina maisha yao kwa ajili ya Kristo na Kanisa lake! Jumamosi, tarehe 1 Juni 2019, Baba Mtakatifu ameadhimisha Ibada ya Misa Takatifu kwa heshima ya Bikira Maria kwenye Madhabahu ya ““Șumuleu Ciuc” yaani Madhabahu ya Bikira Maria mfariji wa wanaoteseka yenye wingi wa utajiri wa historia na ushuhuda wa imani.

Hapa ni mahali ambapo waamini kutoka nchi jirani za Hungaria wanaungana na familia ya Mungu nchini Romania, ili kukutana, kusali na kumwomba Bikira Maria, Mama wa Mungu na Kanisa. Madhabahu ni Kisakramenti, ni Kanisa ambalo ni hospitali iliyoko kwenye uwanja wa mapambano! Hapa ni mahali ambapo panahifadhi kumbu kumbu ya waamini waaminifu, ambao kamwe hawachoki kutafuta chemchemi ya maji hai, ili kupyaisha tena matumaini yao. Madhabahu ni mahali pa sherehe na maadhimisho ya Sakramenti za Kanisa; ni mahali ambapo waamini wanamkimbilia Bikira Maria kwa machozi ya matumaini, wakimlilia huku bondeni kwenye machozi, ili aweze kuwasindikiza kwa Kristo Yesu, ambaye ni njia, ukweli na uzima!

Hii ni sehemu ya mahubiri yaliyotolewa na Baba Mtakatifu Francisko wakati wa Ibada ya Misa Takatifu kwenye Madhabahu ya “Șumuleu Ciuc” yaani Bikira Maria Mfariji wa wanaoteseka. Hapa ni mahali ambapo wahenga kwa nafasi mbali mbali wamekwenda kufanya hija, kila Jumamosi ya Mkesha wa Sherehe ya Pentekoste, ili kuimarisha imani yao kwa Mwenyezi Mungu na kukuza Ibada kwa Bikira Maria. Huu ni urithi wa watu wa Mungu kutoka Hungaria, lakini unatoa heshima pia kwa familia ya Mungu nchini Romania. Baba Mtakatifu anaendelea kusema kwamba, Madhabahu ya “Șumuleu Ciuc” yaani Bikira Maria Mfariji wa wanaoteseka. ni mahali ambapo waamini wa dini na madhehebu mbali mbali ya Kikristo wanakutana kusali.

Hiki ni kielelezo cha majadiliano ya kidini na kiekumene; mahali pa kukuza na kudumisha umoja na udugu; mahali pa kupyaisha ushuhuda wa imani unaomwilishwa katika matumaini! Ni mahali ambapo, waamini wanajisikia kuwa wako nyumbani kwa Mama, wametulia tuli, kama “maji mtunguni”. Wanajitambua kwamba, wao ni sehemu ya watu wa Mungu wenye utajiri unaofumbatwa katika tofauti za tamaduni, lugha na mapokeo, lakini wanaunganishwa na imani kwa Bikira Maria tayari kufanya hija ya pamoja ili kuimba utenzi wa huruma ya Mungu. Madhabahu ya Bikira Maria ni mahali ambapo waamini wanakimbilia ulinzi, tunza na maombezi ya Bikira Maria,  kwa Mwanaye mpendwa Kristo Yesu, ili wajanja wachache wasifanikiwe kuwapoka udugu kwa kuchochea kinzani na mipasuko katika medani mbali mbali za maisha.

Historia ya mambo yaliyopita lazima itunzwe na kuheshimiwa, lakini haiwezi kuwa ni kikwazo cha ujenzi wa mshikamano, umoja, udugu na utulivu. Baba Mtakatifu anaendelea kufafanua kwamba, hija maana yake ni ile hali ya kujisikia kwamba wameitwa na wanahamasishwa kutembea kwa pamoja, huku wakimwomba Mwenyezi Mungu awakirimie neema ya kuweza kubadilisha chuki na hali kutoamiana kuwa ni fursa ya ujenzi wa umoja na udugu unaovunjilia mbali tabia ya kujitafutia usalama na faraja binafsi na hivyo kuanza kutafuta maeneo mapya ambayo Mwenyezi Mungu anataka kuwapatia waja wake. Hija ni changamoto ya kutambua na kueneza ari na moyo wa kuishi pamoja, bila ya kuogopa kuchanganyikana na kukutana na wengine, kama majirani wema.

Hija maana yake ni kushiriki kikamilifu ule muujiza wa kupenda na kutambua udugu wa kweli, kwa kujiunga na msafara wa hija takatifu, ili kuandika historia ya pamoja! Ni mwaliko wa kutafuta ari na maana katika maisha, kwa kutambua kwamba, Mwenyezi Mungu yuko miongoni mwao, akihamasisha mshikamano, udugu pamoja na haja ya mambo mema, ukweli na haki. Hija ni mapambano yanayowawezesha wale waliobaki nyuma, kuwa ni wadau wa leo na kesho iliyo bora zaidi. Hii ni changamoto ya kuwa wajenzi wa mambo ya mbeleni, mwaliko kwa waamini kumwomba Bikira Maria, ili awasaidie kuwekeza katika mambo ya mbeleni.

Baba Mtakatifu anakaza kusema, hija kwenye Madhabahu ya Bikira Maria Mfariji wa wanaoteseka inawawezesha kutafakari Fumbo la Bikira Maria kuteuliwa kuwa ni Mama wa Mungu na ukubali wake uliosababisha mapinduzi makubwa ya upendo. Hii ni changamoto ya kuangalia upendeleo wa Mwenyezi Mungu kwa maskini kwa kuwaangusha wenye nguvu! Kama Bikira Maria, wawe tayari kukubali mpango wa Mungu katika maisha yao, ili kuanzisha mchakato wa upatanisho.Baba Mtakatifu amekamilisha mahubiri yake kwa kuwataka waamini na watu wote wenye mapenzi mema kutembea kwa pamoja, huku wakihamasishwa na tunu msingi za Kiinjili kujisadaka kwa ajili ya ndugu zao, ili kuwashirikisha furaha ya wokovu katika umoja na udugu!

Papa Madhabahu
01 June 2019, 16:43