Hija ya Kitume Romania: Mahojiano Maalum na Papa Francisko!
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.
Baba Mtakatifu Francisko amehitimisha hija ya 30 ya kitume kimataifa nchini Romania ilioanza tarehe 31 Mei hadi 2 Juni 2019 iliyokuwa inaongozwa na kauli mbiu “Twende pamoja” ili kujenga na kudumisha umoja na mshikamano wa kitaifa; kwa kufuata nyayo za mashuhuda wa imani, waliomimina maisha yao kwa ajili ya Kristo na Kanisa lake! Baba Mtakatifu akiwa njiani kurejea kutoka Romania, Jumapili, tarehe 2 Juni 2019 amepata fursa ya “kuchonga na waandishi wa habari” waliokuwa kwenye msafara wake.
Katika mahojiano haya, Baba Mtakatifu amekazia: Wadau wa tasnia ya mawasiliano kuwa ni mashuhuda wa mawasiliano duniani; Umuhimu wa kuenzi tunu msingi za maisha ya ndoa na familia; Majadiliano ya kiekumene, ili kutembea kwa pamoja katika sala na huduma; uhusiano kati ya Vatican na Serikali ya Italia. Vijana na wazee wanapaswa kuendeleza mchakato wa majadiliano na mahusiano na kwamba, Jumuiya ya Kimataifa inapaswa kujenga umoja unaosimikwa katika udugu!
Baba Mtakatifu Francisko amekumbusha kwamba, Jumapili, tarehe 2 Juni 2019, Mama Kanisa ameadhimisha Siku ya 53 ya Upashanaji Habari Ulimwenguni, kwa kuongozwa na kauli mbiu "Kila mmoja wetu ni kiungo cha mwili wa Kristo" (Efe. 4:25): Kutoka Jumuiya ya mtandaoni kwenda kwenye Jumuiya halisi ya watu! Hii ni changamoto ya ujenzi wa Jumuiya halisi ya binadamu! Baba Mtakatifu amewataka wadau wa tasnia ya mawasiliano ya jamii kuwa ni mashuhuda wa mawasiliano kwa kuhakikisha kwamba, wanafikisha ujumbe unaokusudiwa kwa usahihi zaidi.Wanahabari watambue kwamba, huu ni wito ambao una umuhimu wa pekee sana katika ulimwengu mamboleo. Watu wa Mungu wasiishie tu kwenye mawasiliano ya mtandaoni, bali mawasiliano haya yakite mizizi yake katika uhalisia wa maisha ya watu!
Baba Mtakatifu anawataka wanandoa na familia kuhakikisha kwamba, wanatekeleza vyema dhamana na wajibu wao unaofumbatwa katika upendo wa kweli! Baba Mtakatifu anasikitika kusema kwamba, kuna baadhi ya wanandoa inabidi kutengana kwa sababu ya kazi. Hali hii inaweza kusababishwa na mambo mengi: ukosefu wa fursa za ajira katika nchi husika, sera na mikakati ya Jumuiya ya Kimataifa au hata wakati mwingine, athari za myumbo wa uchumi kitaifa na kimataifa zinazopelekea baadhi ya makapuni kufunga shughuli zao na kuhamia ugenini, ili kutafuta unafuu wa gharama za uzalishaji! Matokeo yake ni kilio cha wafanyakazi wengi wasiokuwa tena na fursa za ajira!
Baba Mtakatifu anasikitika kusema kwamba, hapa kunakosekana mshikamano wa upendo na udugu miongoni mwa wafanyakazi. Haya ni matokeo ya sera za mashirika ya fedha kimataifa na ukosefu wa sera za uchumi na maendeleo fungamani ya binadamu. Ameipongeza Romania kwa kulinda na kudumisha tunu msingi za maisha ya ndoa na familia. Ukosefu wa fursa za ajira ni matokeo ya sera za fedha na uchumi kimataifa, zinazojikita katika ulaji wa kupindukia, kwa kutafuta faida kubwa, bila kuzingatia utu, heshima na haki msingi za binadamu. Baba Mtakatifu anasema majadiliano ya kiekumene kati ya Kanisa la Kiorthodox la Romania na Kanisa Katoliki ni changamoto endelevu inayowataka waamini kujenga utamaduni wa kutembea kwa pamoja kama ndugu; kusikilizana na kusali kwa pamoja.
Huu ni uekumene wa damu unaofumbatwa katika ushuhuda wa tunu msingi za maisha ya Kikristo! Ni uekumene wa maisha ya kiroho, sala na huduma kwa maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii! Hawa ndio maskini, wagonjwa, wakimbizi, wahamiaji na watu wasiokuwa na makazi maalum. Ni dhamana na wajibu wa wanataalimungu kuhakikisha kwamba, wanayasaidia Makanisa, ili siku moja yaweze kuadhimisha Fumbo la Ekaristi Takatifu kwa pamoja, chemechemi ya sala na kumbu kumbu endelevu ya Fumbo la Pasaka, yaani: mateso, kifo na ufufuko wa Kristo Yesu kutoka kwa wafu, amana na utajiri unaofumbatwa katika ushuhuda wa maisha ya wafiadini na waungama imani.
Uekumene wa sala, uwawezeshe Wakristo kusali kwa pamoja kama ndugu wamoja! Jambo la msingi ni kuhakikisha kwamba, Wakristo wanatembea kwa pamoja katika umoja na udugu wa binadamu. Kuna changamoto zake, lakini, zisiwe ni sababu ya kuwakatisha waamini tamaa ya kudumisha majadiliano ya kiekumene! Sala ya Baba Yetu ni Sala ya Wakristo wote. Baba Mtakatifu anasema, wakati alipotembelea Kanisa na kusali kwenye Kanisa kuu la Wokovu wa watu wote, kwa pamoja walisali Sala ya Baba Yetu kwa kuzingatia protokali, kama ushuhuda wa kutembea kwa pamoja. Hata miongoni mwa waamini wa Kanisa Katoliki kuna wale wenye misimamo mikali ya kiimani, hawa nao wanapaswa kuombewa!
Baba Mtakatifu anasema kuna uhusiano mzuri kati ya Serikali ya Italia na Kanisa Katoliki. Pale ambapo viongozi wanaomba kukutana na Khalifa wa Mtakatifu Petro, wanafuata taratibu, sheria na kanuni kwa kuzungumza na Katibu mkuu wa Vatican. Hivi karibuni, Baba Mtakatifu anasema amebahatika kukutana na kuzungumza na Waziri mkuu wa Italia Profesa Giuseppe Conte na kwamba, ombi la Matteo Salvini, Waziri wa Mambo ya ndani nchini Italia, hajawahi kuliona. Baba Mtakatifu anakaza kusema, anapenda kusoma Gazeti la L’Osservatore Romano kwani linatoa mwelekeo na tafsiri sahihi ya maisha na utume wa Kanisa. Si mshabiki wa magazeti ya vyama vya siasa na kwamba, haifahamu siasa ya Italia.
Baba Mtakatifu anasikitika kusema kwamba, rushwa ni kati ya saratani kubwa zinazopekenya ulimwengu wa siasa sehemu mbali mbali za dunia. Haki na usawa; tabia ya kuheshimiana na kuthaminiana kama binadamu; ukweli, uwazi na uaminifu ni tunu msingi zinazoboresha siasa safi. Papa anasema mwanasiasa bora ni yule anayetambua dhamana na wajibu wake kwa jamii; anayeaminika na kuthaminiwa na jamii; ni kiongozi anayejitaabisha kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi.
Mwanasiasa anapaswa kuwa mwaminifu katika ahadi zake kwa wananchi waliomchagua, daima akijitahidi kujenga na kudumisha umoja na mshikamano, tayari kuchochea mageuzi katika maisha ya watu; kwa kuwasikiliza na kutenda kwa ujasiri! Siasa safi inayojikita katika ujenzi wa amani inatambua karama za watu na inaendeleza majadiliano na watu kuaminiana na kuthaminiana kama ndugu. Ni jukumu la Kanisa kuwasaidia wanasiasa kuwa: wakweli, waaminifu, wastaarabu na watakatifu na kamwe wasiwe ni watu wanaochochea: chuki na uhasama; bali wawe ni vyombo na mashuhuda wa matumaini.
Papa Francisko anasema, anamheshimu sana Baba Mtakatifu Mstaafu Benedikto XVI, kwa sasa anasumbuliwa na uzee, anazungumza kidogo kidogo, lakini bado kichwani, yuko vyema kabisa. Baba Mtakatifu Mstaafu Benedikto XVI ni amana na hazina ya Mapokeo hai ya Kanisa yanayoendelea kurutubisha maisha na utume wa Kanisa. Wazee wanaota ndoto na vijana wanatoa utabiri, kumbe, wanapaswa kushirikiana na kushikamana. Wazazi na walezi wanafurahia sana mafanikio ya watoto wao. Mababu na Mabibi wasipopewa nafasi katika jamii, wanatumbukia katika msongo wa mawazo.
Baba Mtakatifu anasema, Jumuiya ya Kimataifa haina budi kukuza na kudumisha mshikamano wa udugu kwa kutembea kwa pamoja, ili kuvunjilia mbali utandawazi usiojali wala kuguswa na mahangaiko ya wengine. Ni wakati wa “kufyekelea mbali” uchoyo, ubinafsi na utaifa usiokuwa na mvuto wala mashiko kwa ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Akipokea ”Tuzo ya Carlo Magno”, Baba Mtakatifu Francisko, aliutaka Umoja wa Ulaya kuwa ni chemchemi ya maisha na matumaini kwa watu wake; kwa kuwasaidia maskini na wale wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii sanjari na kuondokana na utamaduni pamoja na utandawazi usioguswa na mahitaji ya jirani zao.
Pamoja na mambo mengine, Baba Mtakatifu alikazia umuhimu wa kukuza na kudumisha uaminifu, ukweli, uwazi na utu wema; kwa kutoa kipaumbele cha pekee kwa tunu msingi za maisha ya ndoa na familia dhidi ya utamaduni wa kifo; kwa kuwajengea vijana matumaini ya kuwa na leo na kesho iliyo bora zaidi kwa kutengeneza fursa za ajira kuliko hali ya sasa. Baba Mtakatifu anatamani kuona Umoja wa Ulaya unaosimikwa katika haki msingi za binadamu; Injili ya uhai, upendo na mshikamano wa kidugu! Bara la Ulaya linaendelea kuzeeka kwa kasi kubwa, linapaswa kupyaisha na kusimama kwa miguu yake inayokita mizizi katika umoja na utandawazi wa mshikamano.
Ni wakati wa kujenga na kudumisha amani kwa kukataa sera na mikakati inayotaka kuligawa Bara la Ulaya. Historia iwe ni mwalimu atakayelisaidia Bara la Ulaya kusonga mbele kwa matumaini zaidi. Mwishoni, Baba Mtakatifu amewaambia waandishi wa habari kwamba, kutokana na hali mbaya ya hewa, ilimbidi kutumia gari kwa muda wa masaa mawili na nusu! Amevutiwa na hali na mazingira ya barabarani. Kwa kutumia barabara amejionea mengi na kwamba, anamshukuru Mungu kwa nafasi kama hii.Umefika wakati kwa Bara la Ulaya kurejea tena kwenye ndoto za waasisi wa Umoja wa Ulaya!