Hija ya Kitume Romania: Bikira Maria anamtembelea Elizabeti
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.
Baba Mtakatifu Francisko kuanzia tarehe 31 Mei hadi 2 Juni 2019 anafanya hija ya 30 ya kitume kimataifa nchini Romania, inayoongozwa na kauli mbiu “Twende pamoja” ili kujenga na kudumisha umoja na mshikamano wa kitaifa; kwa kufuata nyayo za mashuhuda wa imani, waliomimina maisha yao kwa ajili ya Kristo na Kanisa lake! Baba Mtakatifu ameanza hija hii katika maadhimisho ya Siku kuu ya Bikira Maria kumtembelea Elizabeti, Siku kuu ya “Magnificat” yaani utenzi wa Bikira Maria. Huu ni utenzi wa sifa, shukrani na matumaini yanayobubujika kutoka kwa Mwenyezi Mungu, kwa ajili ya wale wasiokuwa na sauti tena!
Ni wimbo wa matumaini, unaopania kuwaamsha wafuasi wa Kristo Yesu katika ulimwengu mamboleo, ili kwa njia ya Bikira Maria, mwanafunzi wa kwanza wa Yesu, ili waamini nao pamoja na Bikira Maria waweze kutembea; waweze kukutana na jirani zao na hatimaye, kufurahia zawadi ya maisha! Hii ni sehemu ya mahubiri yaliyotolewa na Baba Mtakatifu Francisko Ijumaa, tarehe 31 Mei 2019 kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Yosefu, Jimbo kuu la Bucharest, Romania, wakati wa hija yake ya kitume nchini humo! Bikira Maria anamtembelea binadamu yake Elizabeti, tukio la kwanza kabisa kusimuliwa kwenye Maandiko Matakatifu. Toka huko, baadaye atakwenda mjini Galilaya, Bethlehemu, mahali atakapozaliwa Yesu, Mwana wa Mungu; Itawapasa kuokoa maisha ya Mtoto Yesu kutoka kwenye mkono katili wa Herode kwa kukimbilia Misri.
Kila mwaka, Bikira Maria alikuwa anakwenda mjini Yerusalemu kwa ajili ya kuadhimisha Pasaka ya Wayahudi na alitekeleza azma hii, hadi siku ya mwisho alimposindikiza Mwanaye wa pekee kwenye Njia ya Msalaba. Hizi ni safari ambazo zilihitaji ujasiri na uvumilivu mkubwa, kwani hata leo hii, Bikira Maria anatambua magumu na changamoto zinazowakabili wafuasi wa Kristo katika hija ya maisha yao hapa duniani. Katika changamoto hizi, Bikira Maria anakuwa ni dada katika safari na mwenza, anayetoa mkono kuwasaidia wale wanaoelemewa na ugumu wa safari. Kama Mama, Bikira Maria anafahamu fika kwamba, upendo unamwilishwa katika mambo ya kawaida katika maisha.
Ni Bikira Maria aliyethubutu kubadilisha Pango la kulishia wanyama, kuwa ni makazi ya Yesu, akamvika mtoto wake nguo za kimaskini, lakini akamwonesha wingi wa upendo! Kwa kumtafakari Bikira Maria, waamini wanaweza kuona nyuso za wanawake na wasichana wengi duniani! Hawa ni wanawake ambao kwa sadaka na majitoleo yao wanaweza kuandika historia ya maisha ya leo na kuanza kusuka ndoto ya kesho. Ni watu wanaojisadaka katika hali ya ukimya, uvumilivu na unyenyekevu mkuu, kiasi hata cha kuthubutu kujitwika mizigo mizito inayowaelemea watoto na familia zao katika ujumla wake. Hawa ni wanawake wanao amini kwa kutarajia yale yasioweza kutarajiwa.
Injili ya matumaini inajionesha wazi katika maisha ya wananchi wa Romania, licha ya changamoto na matatizo yanayoweza kuzima moto huu wa matumaini. Kwa kumwangalia Bikira Maria pamoja na wanawake wote wa shoka wanaojisadaka bila ya kujibakiza, watu wa Mungu wanaweza kuonja na kupyaisha tena Injili ya matumaini, inayojielekeza kwa ajili ya leo na kesho iliyo bora zaidi. Ni katika muktadha huu anasema Baba Mtakatifu Francisko, Bikira Maria anatembea na kuwaita Wakristo kutembea kwa pamoja! Bikira Maria alikutana na binamu yake Elizabeti ambaye umri wake ulikuwa umekwenda sana! Mwanamke huyu katika uzee wake, akiwa amejazwa na Roho Mtakatifu akapaaza sauti na kusema “Umebarikiwa wewe katika wanawake, kwa sababu ana heri yule anayesadiki.
Hapa Bikira Maria katika ujana wake anakwenda kumtembelea mwanamke mzee, akitafuta mizizi na katika uzee huu, anaibua unabii kwa ajili ya kijana huyu. Hapa ni mahali ambapo vijana na wazee wanakutana na kukumbatiana; kwa kuhamasishana, kila mtu kuweza kutoa ndani mwake kile kilicho bora zaidi. Baba Mtakatifu Francisko anasema, huu ndio muujiza unaofumbatwa katika utamaduni wa watu kukutana; mahali ambapo kila mtu anaheshimiwa na kuthaminiwa, kwa sababu kila mtu ni muhimu kwa kuufunua Uso wa Mungu! Ni watu ambao hawaogopi kufanya hija ya maisha kwa pamoja na pale linapotenda hili, Mwenyezi Mungu anawasili na kutenda miujiza kwa watu wake.
Roho Mtakatifu ndiye anayewahamasisha waamini kutoka katika undani na ubinafsi wao; kutoka katika mambo madogo madogo yanayowafunga, na kuwafundisha kuwa na mwelekeo mpana zaidi wa kuweza kusema mazuri na kuwabariki wengine, hasa wale wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii. Hawa ndio wale watu wanaoteseka kwa baa la njaa; watu wasiokuwa na makazi maalum; lakini wanaweza kukumbatiwa na urafiki pamoja na upendo unaobubujika kutoka katika Jumuiya kwa: kuwapokea, kuwalinda, kuwaendeleza na kuwashirikisha katika uhalisia wa maisha yao. Utamaduni wa watu kukutana anasema Baba Mtakatifu unawahamasisha Wakristo kung’amua muujiza wa umama wa Kanisa anayejibidisha kuwatafuta, kuwalinda na kuwaunganisha watoto wake.
Ndani ya Kanisa, madhehebu mbali mbali yanapokutana, jambo la msingi linalopaswa kupewa kipaumbele hapa ni watu wa Mungu wanaotambua umuhimu wa kumsifu Mungu, asili ya mambo makuu katika maisha ya mwanadamu na wala si kabila au mahali anakotoka mtu! Wakristo wanapaswa kusema kwa nguvu zote heri aliyesadiki kwa sababu anao ujasiri wa kukutana na kujenga umoja! Bikira Maria anatembea na hatimaye, anakutana na Elizabeti. Bikira Maria anakuwa ni Madhabahu ya kuweza kusikiliza mapigo ya Mungu, madhabahu ambayo yamejengwa kati ya watu wa Mungu, anakoishi na kuwasubiria waja wake ili waweze kumwendea.
Hii ni changamoto kwa waamini kuondokana na woga usiokuwa na mashiko na kuanza kushika njia ya kumwendea, kwa sababu Mwenyezi Mungu yuko kati pamoja na waja wake na kwa sababu ni Mkombozi mwenye nguvu. Hii ni siri kuu ya maisha ya Wakristo, ndiyo maana hata Bikira Maria akafurahi na kumwimbia Mungu utenzi wa sifa, kwa kuwa ni Tabernakulo ya kwanza ya Neno wa Mungu aliyefanyika mwili, Kristo Yesu, Emmanueli yaani Mungu pamoja nasi. Mkristo anapata furaha yake katika Roho Mtakatifu. Bila furaha ya kweli, anasema Baba Mtakatifu, waamini wanakuwa na “ngazi” wanabaki kuwa watumwa wa huzuni na msongo wa mawazo.
Wakati mwingine, watu wanasingizia kuhusu ukosefu wa miundo mbinu pamoja na wingi, lakini shida kubwa iliyofichika ni ukosefu wa imani, hali inayomtumbukiza mwamini katika huzuni na wasi wasi moyoni na hatimaye, kujikatia tamaa ya maisha. Upofu wa maisha na hali ya kujifungia katika ubinafsi ni mambo ambayo yanakwenda kinyume cha ushuhuda wa imani na kusahau kwamba, waamini wanaye Mungu ambaye ni Baba yao na wala si watoto yatima! Mwenyezi Mungu ni Mkombozi mwenye nguvu, chemchemi ya furaha ya Bikira Maria, licha ya matatizo na changamoto ambazo waamini wanaweza kukutana nazo katika maisha. Huu ni mwaliko kwa waamini kuendelea kujiaminisha kwa Mwenyezi Mungu katika hija ya maisha yao pamoja na kuonesha upendo kwa jirani, kama walivyofanya mashuhuda wa imani na wafiadini nchini Romania wakati wa madhulumu dhidi ya Wakristo.
Watakatifu ni watu waliojiaminisha mbele ya Mungu na hawa ni sababu ya kumwimbia Mungu utenzi wa sifa na shukrani. Machozi yao yamekuwa ni chemchemi ya sala iliyopanda kwenda mbinguni kama moshi wa ubani na kwamba ni machozi haya ambayo yamerutubisha matumaini ya watu wa Mungu nchini Romania. Baba Mtakatifu amehitimisha mahubiri yake kwa kusema kwamba, Bikira Maria anatembea, anakutana na kufurahia maisha kwani yeye ni chemchemi ya baraka, mwaliko kwa waamini kuwa ni baraka kwa Romania. Waamini nchini Romania, wawe ni mashuhuda na wajenzi wa utamaduni wa watu kukutana kwa kubomolea mbali tabia ya kutojali wala kuguswa na mahangaiko ya wengine; tabia ya kujenga kuta za utengano, ili kwa pamoja watu wa Mungu nchini Romania, waweze kuimba utenzi wa nguvu ya huruma ya Mungu!