Hija ya Kitume Romania: Papa aomba msamaha kwa dhambi ya ubaguzi
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.
Baba Mtakatifu Francisko kabla ya kuhitimisha hija yake ya 30 kimataifa nchini Romania iliyokuwa inaongozwa na kauli mbiu “Twende pamoja” ili kujenga na kudumisha umoja na mshikamano wa kitaifa; kwa kufuata nyayo za mashuhuda wa imani, waliomimina maisha yao kwa ajili ya Kristo na Kanisa lake, Jumapili tarehe 2 Juni 2019 ametembelea na kukutana na Jumuiya ya Warom na Wasinti; watu wasiokuwa na makazi maalum. Baba Mtakatifu katika hotuba yake amekaza kusema, Kanisa ni mahali pa watu kukutana; Utu na heshima ya binadamu ivunjilie mbali maamuzi mbele na ubaguzi; wananchi wadumishe mchakato wa upatanisho, haki na amani na wala si kulipizana kisasi na kwamba, wananchi waoneshe ujasiri wa kutembea kwa pamoja!
Kanisa ni mahali pa watu kukutana kama sehemu ya utambulisho wake wa Kikristo, kama walivyoshuhudia na kutangaza wenyeheri wapya. Mwenyezi Mungu na kiu na hamu ya kutaka kukutana na watoto wake katika urafiki, kwani Furaha ya Injili inatangazwa na kushuhudiwa katika furaha inayowatambulisha watu kwamba, wanapendwa na Mwenyezi Mungu. Waamini wawe na ujasiri wa kuangaliana mubashara na kama ambavyo Mwenyezi Mungu anawaangalia watoto wake, ili kusindikizana na kushikamana katika maisha na utume wa sala! Ubaguzi wa rangi ni kashfa ambayo imewakumba walimwengu wengi na kuwa hata Wakristo wamejikuta wakitumbukia na kumezwa na dhambi hii.
Baba Mtakatifu Francisko amechukua fursa hii kuomba msamaha kwa dhambi ya ubaguzi inayotendwa na Wamini wa Kanisa Katoliki sehemu mbali mbali za dunia. Waamini hawa wamewaangalia Warom na Wasint kwa jicho la Kaini badala ya lile la Abeli, kwa kushindwa kuwatambua, kuwathamini na kulinda utambulisho wao wa pekee. Kama ilivyokuwa kwa Kaini, hakujali wala kuonesha upendo kwa ndugu yake, kiasi hata cha kumgeuzia kisogo. Hali kama hii inarutubishwa na maamuzi mbele, chuki na uhasama; kwa maneno na matendo na matokeo yake, familia ya binadamu inashindwa kusonga mbele. Watu wawe na ujasiri wa kuona utu, heshima na haki msingi za binadamu kabla ya kufanya maamuzi mbele na ubaguzi.
Baba Mtakatifu anaendelea kufafanua kwamba, katika historia ya maisha ya mwanadamu, daima kumekuwepo na akina Abeli na Kaini; watu wema na wakatili, wakarimu na wenye “roho ya korosho”. Kuna utamaduni wa upendo na ule unaojikita katika chuki na uhasama! Hapa binadamu anapaswa kufanya maamuzi machungu; kwa kuchagua kati ya Abeli na Kaini; kuamua kufuata njia ya haki, amani na upatanisho au ile ya chuki na kulipizana kisasi. Lakini, ikumbukwe kwamba, njia ya amani inakita mizizi yake katika msamaha na kwamba, hakuna kisasi ambacho kinaweza kuzima kiu ya haki. Baba Mtakatifu anaitaka Jumuiya ya Warom na Wasinti kutambua kwamba, inayo mchango mkubwa katika kukuza na kudumisha tunu msingi za maisha, ndoa na familia; mshikamano, ukarimu na upendo; kwa kusimama kidete kuwalinda na kuwatetea wanyonge; kwa kuwaheshimu na kuwathamini wazee.
Hii ni Jumuiya inayoheshimu tunu msingi za maisha ya kiroho na hiyo kiu ya furaha ya maisha. Baba Mtakatifu anawaalika Warom na Wasint kutembea kwa pamoja ili kushiriki katika ujenzi wa jamii inayosimikwa katika utu kwa kuondokana na hofu na woga usiokuwa na mashiko; kwa kubomolea mbali kuta za utengano, ili kujenga tabia ya kuaminiana kwa kukuza uvumilivu, ili kuambata udugu. Watembee kwa pamoja kwa kukita mawazo yao katika utu, heshima na tunu msingi za maisha ya ndoa na familia pamoja na maisha ya sala.
Baba Mtakatifu amesema, mkutano huu na Jumuiya ya Warom na Wasint umehitimisha hija yake ya kitume nchini Romania, ambako amepokelewa kama hujaji na ndugu yao katika Kristo Yesu. Anarejea Vatican akiwa amebeba amana na utajiri mkubwa wa watu na matukio muhimu katika hija hii ya kihistoria na kwamba, ataendelea kuwakumbuka katika sala na sadaka yake.