Hija ya Kitume Romania: Blas ni mji wa mashuhuda wa imani!
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.
Baba Mtakatifu Francisko kabla ya kuhitimisha Liturujia Takatifu, Jumapili tarehe 2 Juni 2019 kwenye Uwanja wa Uhuru huko Jimbo Katoliki la Blaj, ambamo amewatangaza Maaskofu saba kutoka Romania kuwa Wenyeheri kwa kukazia: Uhuru na huruma ya Mungu, amemshukuru Mungu kwa ukarimu na mapokezi makubwa waliomwonesha watu wa Mungu kutoka ndani na nje ya Romania. Amewashukuru viongozi wa Serikali, Viongozi wakuu na waamini wa Kanisa la Kiorthodox la Romania na wale wote waliojisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili ya kuhakikisha kwamba, hija hii ya kitume inafanikiwa kadiri ya mpango wa Mungu.
Baba Mtakatifu, anawaombea neema na baraka kutoka kwa Mwenyezi Mungu ili aendelee kuwasimamia na kuwaelekeza katika maisha na utume wao! Baba Mtakatifu amemshukuru sana Kardinali Lucian Muresan, viongozi na waamini wa Kanisa Katoliki nchini Romania, kwa kuwawezesha wote hawa kushirikiana naye katika sala, ili kuendeleza mchakato wa uinjilishaji mpya unaofumbatwa katika ushuhuda wa upendo. Jimbo la Blaj, ni chemchemi ya ushuhuda wa imani, uhuru na huruma ya Mungu.
Baba Mtakatifu anawashukuru kwa dhati kabisa watoto wa Kanisa Katoliki lenye asili ya Kigiriki ambao kwa karne tatu, wamesimama kidete kutangaza na kushuhuda imani kwa ari kuu na ushupavu wa kitume! Bikira Maria awalinde kwa tunza yake ya kimama, wananchi wote wa Romania, ambao kwa miaka mingi wamejiaminisha chini ya ulinzi, tunza na maombezi ya Bikira Maria. Baba Mtakatifu mwishoni, mwa tafakari yake, amewaweka wote hawa chini ya Bikira Maria ili awaongoze katika hija ya imani, maendeleo ya kweli na fungamani; wawe na amani na hivyo waweze kuchangia katika ujenzi wa taifa lao linalosimikwa katika haki na udugu!
Katika Ibada ya Liturujia Takatifu, Baba Mtakatifu Francisko ametumia kiti ambacho kimechongwa kutokana na mbao za viti vya gereza na chuma cha madirisha ya gereza ambamo Wenyeheri hawa wapya, walisadaka maisha yao kama ushuhuda kwa Kristo Yesu na Kanisa lake. Hadi wakati wa kuanguka kwa Ukomonisti, Liturujia Takatifu iliyokuwa inasikika nchini humo ni ile iliyotangazwa na kurushwa na Radio Vatican.