Hija ya Kitume Romania: Wenyeheri Maaskofu 7: Uhuru & Huruma!
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.
Askofu Iuliu Hossu, Askofu Vasile Aftenie, Askofu Ioan Balan, Askofu Valeriu Traian Frentiu, Askofu Ioan Suciu, Askofu Tit Liviu Chinezu na Askofu Alexandru Rusu. Maaskofu hawa walikamatwa na kutiwa nguvuni kati ya tarehe 28-29 Novemba 1948 hadi tarehe 25 Desemba 1989, utawala wa Kikomunisti ulipobwagwa chini. Hiki ni kikosi cha Watumishi wa Mungu, Maaskofu saba kwa Kanisa Katoliki lenye asili ya Kigiriki, waliotangazwa na Baba Mtakatifu Francisko kuwa Wenyeheri wakati wa hija yake ya kitume nchini Romania, tarehe 2 Juni 2019. Ibada ya Liturujia Takatifu imeadhimishwa huko Blaj na kuhudhuriwa na umati mkubwa wa familia ya Mungu kutoka ndani na nje ya Romania.
Baba Mtakatifu katika mahubiri yake wakati wa kuwatangaza wenyeheri saba, amefafanua kuhusu: Dhana ya dhambi na huruma ya Mungu isiyokuwa na mipaka; Utu na heshima ya binadamu; Nyanyaso na madhulumu dhidi ya Wakristo nchini Romania; umuhimu wa kudumisha uhuru na huruma ya Mungu pamoja na madhara ya ukoloni wa kiitikadi! Baba Mtakatifu anasema, kitendo cha Kristo Yesu kumponya kipofu aliyezaliwa hivyo, kulizua maswali mengi yenye ukakasi, kiasi cha kufafanua kwamba, kuzaliwa kwake kama kipofu si matokeo ya dhambi kama ilivyokuwa inasadikiwa katika Agano la Kale.
Baba Mtakatifu anakaza kusema, watu wanashindwa kuona muujiza wa Mungu aliomtendea mja wake kipofu na kudhani kwamba, ni tukio lisilokuwa na mashiko hata kidogo. Kipofu aliyeponywa anakuwa ni chanzo cha mafarakano ya kidini, kijamii na kifamilia kwa kushindwa kutambua utambulisho wa kipofu pamoja na kusigina huruma ya Mungu. Ni watu wanaodai kwamba, Mwenyezi Mungu kamwe hawezi kufanya muujiza Siku ya Sabato; eti kwamba, huyu, hakuzaliwa kipofu, alikuwa anajifanya tu!
Ni watu wanaoshindwa kutambua na kung’amua vipaumbele vya Kristo Yesu, kwa kukazia utu na heshima ya binadamu, ili kumrejeshea tena ile hali yake ya kuwa ni kiini cha huruma na upendo wa Mungu unaopania kumkomboa mwanadamu kutoka katika lindi la dhambi na mauti! Badala ya binadamu kupewa kipaumbele cha kwanza, wao wanataka kuweka mafao binafsi, kanuni na sheria zinazoelea kwenye ombwe, ili ziweze kukubaliwa na wote. Kristo Yesu, anamtafuta mtu mwenye historia na madonda yake, kwa kukazia mambo msingi ya maisha!
Baba Mtakatifu anasema hivi ndivyo inavyokuwa kwa sera na siasa ambazo zinajikita katika dhuluma na nyanyaso za watu; siasa zinazosigina imani na uhuru wa watu wa Mungu kwa mantiki ya kutaka kuwa na mamlaka ya kutawala watu, hali inayodhohofisha uwezo wa kufanya maamuzi, uhuru kamili pamoja na kupungua fursa ya ubunifu. Wakristo nchini Romania wameteseka, wakadhulumiwa na kudharauliwa, kiasi cha kushikishwa adabu. Hivi ndivyo ilivyokuwa kwa Maaskofu wafiadini, waliotangazwa na Mama Kanisa kuwa Wenyeheri.
Wenyeheri hawa katika dhuluma, wakasimama kidete kutangaza na kushuhudia imani na upendo wao kwa watu wa Mungu; wakaonesha ujasiri na nguvu ya ndani, kiasi hata cha kuthubutu kukubali kifungo, kazi ngumu na mateso ya kila aina, bila kuligeuzia Kanisa kisogo kwa usaliti. Hawa ndio wachungaji na mashuhuda wa imani ambao wameacha amana, utajiri na urithi mkubwa kwa familia ya Mungu nchini Romania. Urithi huu kwa ufupi ni uhuru na huruma! Liturujia Takatifu imeadhimishwa kwenye Uwanja wa Uhuru, changamoto na mwaliko kwa familia ya Mungu nchini Romania kuchuchumilia na kuambata mchakato wa ujenzi wa umoja na mshikamano wa kitaifa unaofumbatwa katika utajiri wa tofauti msingi.
Hii ni amana na utajiri mkubwa unaobubujika kutoka katika maisha ya kiroho na kitamaduni, sehemu muhimu sana ya utambulisho wa Romania. Wenyeheri wapya walisadaka na kuyamimina maisha yao kama njia ya kukabiliana na siasa zilizokuwa zinakinzana na uhuru pamoja na haki msingi za binadamu. Jumuiya ya Kanisa Katoliki ikajikuta inakuwa na maisha magumu kutokana na utawala dhalimu uliojikita katika ukanimungu; Maaskofu na waamini wengi wakateswa na kunyanyaswa sana! Baba Mtakatifu amefafanua huruma kama amana na urithi mkubwa wa maisha ya kiroho kutoka kwa Wenyeheri wapya.
Hawa ni watu waliothubutu kuwa waaminifu kwa kutangaza na kushuhudia imani yao kwa Kristo Yesu na Kanisa lake, bila kutaka kulipiza kisasi kwa kuwaonesha watesi wao upendo wa Mungu. Wenyeheri wapya wakawa ni vyombo na mashuhuda wa msamaha na huruma ya Mungu; kwa ajili ya toba na wongofu wa ndani. Huu ni muhtasari wamashuhuda wa imani kwa Kristo na Kanisa lake: Ni ujumbe wa kinabii dhidi ya watesi wao na mwaliko wa kufanya toba na wongofu wa ndani. Kwa njia hii, wakashinda chuki na uhasama kwa kutanguliza upendo, msamaha kama kielelezo cha ujasiri wa imani ya Kikristo!
Baba Mtakatifu Francisko anasema, hata ulimwengu mamboleo kuna ukoloni wa kiitikadi unaopania kung’oa: utajiri na amana ya maisha ya kiroho, kitamaduni na kidini kwa kudharau: utu na heshima ya binadamu; uhai, ndoa na familia, kiasi cha kuwaacha watoto na vijana kukua na kukomaa pasi na mizizi ya maisha adili na matakatifu. Matokeko yake ni sera zinazopandikiza tamaa ya kupata mafanikio ya chapuchapu! Zinageuza watu wengi kuwa kama bidhaa ya kuuzwa na kununuliwa sokoni; wzinapandika mbegu ya chuki, uhasama na mipasuko ya kijamii pamoja na kung’oa mizizi na urithi wa jamii, badala ya kukuza na kudumisha maridhiano ya kidini.
Mwishoni, mwa mahubiri yake, Baba Mtakatifu anapenda kuwahamasisha Wakristo kusimama kidete kutangaza na kushuhudia Injili; kwa kupambana fika na ukoloni wa kiitikadi unaoendelea kuibuliwa kila kukicha. Anawataka wawe ni mashuhuda na vyombo vya uhuru na huruma ya Mungu inayofumbatwa katika udugu na majadiliano ya kiekumene, ili kujenga na kudumisha uekumene wa damu na hivyo kuvuka mipaka ya historia ya utengano, ili kudumisha umoja na ujirani mwema, hija ambayo inasindikizwa na Bikira Maria pamoja na maombezi ya wenyeheri wapya!