Tafuta

Kitabu cha "Nostra Madre Terra" ni Mkusanyiko wa hotuba na tafakari mbali mbali zilizotolewa na Papa Francisko na Dibaji ya Kitabu imeandikwa na Patriaki Bartolomeo wa kwanza. Kitabu cha "Nostra Madre Terra" ni Mkusanyiko wa hotuba na tafakari mbali mbali zilizotolewa na Papa Francisko na Dibaji ya Kitabu imeandikwa na Patriaki Bartolomeo wa kwanza. 

Papa Francisko: Dhima ya Kikristo katika Ekolojia Fungamani!

Lengo la kitabu hiki ni kuonesha dhima ya Kikristo katika masuala ya kiekolojia. Kitabu hiki kinajulikana kwa jina la “Nostra Madre Terra” yaani “Dunia Mama Yetu”, Patriaki Bartolomeo wa kwanza wa Kanisa la Kiorthodox la Costantinopoli ndiye aliyepewa dhamana ya kuandika dibaji ya kitabu hiki, kinachokita maudhui yake katika mchakato wa kiekumene. Hii ndiyo Ekolojia fungamani!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Maadhimisho ya Sinodi ya Maaskofu Ukanda wa Amazonia imekuwa ni nafasi adhimu sana ya kutafakari kuhusu ekolojia fungamani kama sehemu ya utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote! Hii ni dhamana inayohitaji wongofu wa kiekolojia. Idara ya Uchapishaji ya Vatican, LEV imekusanya hotuba na tafakari zote za Baba Mtakatifu Francisko kuhusu mazingira na kuziandikia kitabu ambapo kwa sasa kiko madukani. Lengo la kitabu hiki ni kuonesha dhima ya Kikristo katika masuala ya kiekolojia. Kitabu hiki kinajulikana kwa jina la “Nostra Madre Terra” yaani “Dunia Mama Yetu”, Patriaki Bartolomeo wa kwanza wa Kanisa la Kiorthodox la Costantinopoli ndiye aliyepewa dhamana ya kuandika dibaji ya kitabu hiki, kinachokita maudhui yake katika mchakato wa kiekumene. Kwa ufupi kitabu hiki kinajadili kuhusu umoja wa familia ya binadamu katika muktadha wa utunzaji bora wa mazingira unaofumbatwa katika maendeleo fungamani ya binadamu kama njia muafaka ya kupambana na changamoto za athari za mabadiliko ya tabianchi.

Utunzaji bora wa mazingira hauna budi kwenda sanjari na Injili ya uhai kama njia muafaka ya kulinda, kudumisha na kuendeleza haki ya mtu kuishi dhidi ya utamaduni wa kifo. Utunzaji bora wa mazingira ni chanda na pete na ulinzi wa uhai wa binadamu kwani haya ni mambo yanayotegemeana na kukamilishana. Baba Mtakatifu anagusia kwa namna ya pekee maji kama sehemu ya haki msingi za binadamu. Kitabu hiki ni muhtasari wa tafakari ya maisha ya kiroho mintarafu utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote. Hapa kuna chimbuko la taalimungu ya kiekolojia. Ni kitabu kinachotoa kipaumbele cha kwanza kwa upendo kwa Mungu na jirani, ili kujenga na kudumisha misingi ya haki jamii, upendo na mshikamano wa dhati unaofumbatwa katika kanuni auni, ili kupambana na baa la umaskini linalosigina utu, heshima na haki msingi za binadamu. Huu ni mwaliko wa kuomba msamaha kutokana na ubinafsi, uchoyo na utandawazi usioguswa na mahangaiko ya wengine, ili kuanza mchakato wa toba na wongofu wa ndani, tayari kuambata na kukumbatia wongofu wa kiekolojia.

Baba Mtakatifu Francisko anasema, hii ni hija inayopaswa kufanywa na waamini wote katika ujumla wao, kwani umoja na nguvu na utengano ni udhaifu! Utunzaji bora wa mazingira unapaswa pia kuangaliwa katika Liturujia sanjari na Maadhimisho ya Mafumbo ya Kanisa. Kazi ya uumbaji ni zawadi kwa ajili ya watu wote. Kumbe, inapaswa kuwa ni chanzo cha binadamu kujipatia mahitaji yake msingi. Mwenyezi Mungu ametumia mkate na divai, kazi ya mikono ya mwanadamu kuwa ni kielelezo cha Fumbo la Ekaristi Takatifu, kielelezo cha Mwili wa Kristo!  Baba Mtakatifu Francisko katika Waraka wake wa Kitume: “Laudato si” yaani “Sifa kwako” juu ya utunzaji wa nyumba ya wote” anapenda kukazia umuhimu wa maendeleo fungamani yanayojikita katika kanuni maadili na utu wema, mwanadamu akipewa kipaumbele cha kwanza sanjari na kutafuta mafao, ustawi na maendeleo ya wengi. Sifa na utukufu kwa Mwenyezi Mungu ni matunda ya tafakari ya kina kuhusu kazi ya uumbaji inayomwajibisha mwanadamu:kuilinda, kuitunza na kuiendeleza kama njia inayofaa kwa ajili ya kuheshimu kazi ya uumbaji na Mwenyezi Mungu ambaye ndiye Muumba mwenyewe!

Waraka unakazia ushirikiano na mshikamano wa kimataifa unaojikita katika kanuni auni na maadili, ili kudhibiti madhara yanayoendelea kusababishwa na mabadiliko ya tabianchi; kwa kupambana na umaskini wa hali na kipato; ukosefu wa usawa pamoja na kuhakikisha kwamba, rasilimali ya dunia inatumika kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya wengi. Kila raia anahamasishwa kuchangia katika utunzaji bora wa mazingira kwa kutekeleza yale ambayo yako katika uwezo wake. Uharibifu wa mazingira unahitaji wongofu wa kiekolojia; kwa kuwa na mageuzi makubwa katika mtindo wa maisha kwa kuwajibika. Siku ya Kuombea Utunzaji Bora wa Mazingira kwa upande wa Kanisa Katoliki ilianzishwa rasmi na Baba Mtakatifu Francisko tarehe 10 Agosti 2015 kama sehemu ya mchakato endelevu wa maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya Huruma ya Mungu, kwa kuwataka waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema kusimama kidete kulinda, kutunza na kudumisha kazi ya uumbaji. Kwa kuthamini na kujali umuhimu wa utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote, maadhimisho haya yakachukua mfumo wa kiekumene.

Kilele cha maadhimisho haya ni hapo tarehe 4 Oktoba, katika Maadhimisho ya Siku kuu ya Mtakatifu Francisko wa Assisi, aliyejisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili ya maskini, amani na utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote. Hiki ni kipindi muafaka cha kumwimbia Mwenyezi Mungu utenzi wa sifa na shukrani kwa kazi kumbwa ya uumbaji sanjari na kujibu kwa vitendo kilio cha Dunia mama! Matukio kuhusu utunzaji bora wa mazingira katika kipindi hiki chote, yanapania pamoja na mambo mengine, kufafanua na kumwilisha katika uhalisia wa maisha ya watu taalimungu ya kiekolojia. Lengo ni kudumisha ukweli kuhusu utu,heshima ya binadamu, haki msingi pamoja na uelewa wa kazi ya uumbaji kadiri ya Mafundisho Jamii ya Kanisa. Baba Mtakatifu Francisko katika ujumbe wake anasikitika kusema kwamba, kazi ya uumbaji iliyokuwa nzuri machoni pa Mwenyezi Mungu na kuikabidhi kwa binadamu kama zawadi imeharibiwa kwa uwepo wa dhambi, ubinafsi na uchoyo unaotaka kuinyonya kwa uchimbaji wa madini na nishati ya mafuta; kilimo cha mashamba makubwa pamoja na ukataji ovyo wa misitu hali ambayo imesababisha kupanda kwa joto duniani pamoja na kuongezeka kiwango cha bahari.

Kuna uchafuzi mkubwa wa mazingira unaofanywa kwa kutupa ovyo taka za plastiki; mambo yanayotishia usalama wa maisha ya viumbe hai duniani. Huu ni muda wa toba na wongofu wa kiekolojia, ili kuanza mchakato wa kuwa karibu zaidi na mazingira nyumba ya wote, Kitabu cha Mungu kilichofunguliwa wazi mbele ya macho ya binadamu. Ni muda wa kutafakari kuhusu mtindo wa maisha, ili hatimaye, kufanya maamuzi yatakayosaidia kuboresha utunzaji wa mazingira; kwa kuwa na teknolojia na nishati rafiki kwa mazingira. Hiki ni kipindi cha kufanya matendo ya kinabii kwa kusikiliza na kujibu kilio cha vijana wa kizazi kipya wanaotaka kuona Jumuiya ya Kimataifa ikijizatiti kwa vitendo zaidi katika mchakato wa utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote. Patriaki Bartolomeo wa kwanza wa Kanisa la Kiorthodox la Costantinopoli, ambalo kwa mwaka 2019 limeadhimisha Siku ya 30 ya Kuombea Utunzaji Bora wa Mazingira nyumba ya wote, anasema, utunzaji bora wa mazingira ni sehemu ya vinasaba vya maisha ya imani kwa Wakristo inayofumbatwa katika maadhimisho ya Liturujia Takatifu.

Maisha na utume wa Kanisa unamwilishwa katika matukio mbali mbali yanayogusa na kumwambata mwanadamu katika ulimwengu mamboleo. Taalimungu ya kiekolojia inagusa pamoja na mambo mengine, umuhimu wa kujizatiti katika kukabiliana na changamoto zinazoibuliwa kutokana na uchafuzi wa mazingira ambao unaendelea kusababisha athari kubwa katika mabadiliko ya tabianchi. Utu, heshima na haki msingi za binadamu sanjari na utunzaji bora wa kazi ya uumbaji mintarafu Mafundisho Jamii ya Kanisa ni mambo msingi katika kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi. Mazingira ni sehemu ya kazi ya uumbaji ambayo imepewa nafasi ya pekee katika Liturujia Takatifu, hususan katika maadhimisho ya Fumbo la Ekaristi Takatifu, kielelezo makini cha muhtasari wa utimilifu wa nyakati. Hii ndiyo karamu kuu inayodhihirisha utimilifu wa utukufu wa Ufalme wa Mungu. Patriaki Bartolomeo wa kwanza wa Kanisa la Kiorthodox la Costantinopoli anakaza kusema, katika ulimwengu wa utandawazi na maendeleo ya sayansi na teknolojia, kinachopewa kipaumbele cha kwanza ni faida kubwa hata kama ni kwa hasara kwa utu na heshima ya binadamu.

Uchumi unapaswa kuongozwa na kanuni maadili, utu, mahitaji msingi ya binadamu; mshikamano unaosimikwa katika kanuni auni pamoja na haki. Haya ni mambo msingi na ni sehemu muhimu sana ya ushuhuda wa imani inayomwilishwa katika matendo. Waamini wajifunge kibwebwe katika kulinda na kutunza mazingira nyumba ya wote. Vijana waelimishwe kanuni, sheria na taratibu za utunzaji bora wa mazingira, kwa kukazia pia umoja na mshikamano, sehemu muhimu sana ya malezi na majiundo yao. Utamaduni wa ekolojia ya mazingira ni muhimu sana kama sehemu ya mchakato wa mapambano dhidi ya uharibifu wa mazingira nyumba ya wote!

Papa: Ekolojia
24 October 2019, 15:23