Tafuta

Baba Mtakatifu Francisko ameadhimisha Ibada ya Misa takatifu kwa ajili ya kufunga Sinodi ya Maaskofu Ukanda wa Amazonia: Ametafakari kuhusu Sala na Kilio cha Maskini wa Amazonia! Baba Mtakatifu Francisko ameadhimisha Ibada ya Misa takatifu kwa ajili ya kufunga Sinodi ya Maaskofu Ukanda wa Amazonia: Ametafakari kuhusu Sala na Kilio cha Maskini wa Amazonia! 

Sinodi ya Maaskofu Ukanda wa Amazonia: Sala ya Maskini!

Maadhimisho ya Sinodi ya Maaskofu Ukanda wa Amazonia yameongozwa na Kauli mbiu: “Amazonia: njia mpya ya Kanisa na kwa ajili ekolojia fungamani”. Papa Francisko katika mahubiri yake amewaalika waamini kutafakari pamoja sala ya wahusika wakuu wa Liturujia ya Neno la Mungu Jumapili 30 ya Kipindi cha Mwaka C wa Kanisa yaani: Sala ya Farisayo, Mtoza Ushuru na Maskini.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Utamaduni wa kukutana, kujadiliana, kusikilizana na hatimaye kutoa mang’amuzi ya pamoja ni kati ya vipaumbe vya kwanza wakati wa maadhimisho ya Sinodi ya Maaskofu Ukanda wa Amazonia mintarafu mwanga wa Wosia wa Kitume wa Baba Mtakatifu Francisko: “Evangelii gaudium” yaani “Furaha ya Injili” na Waraka wa Kitume wa Baba Mtakatifu Francisko “Laudato si” yaani “Sifa iwe kwako” juu ya utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote”. Mambo makuu yaliyochambuliwa ni: ekolojia ya mazingira na utamaduni; ekolojia ya kisiasa na kiuchumi; elimu makini pamoja na tasaufi ya kiekolojia. Tema zote hizi zimesaidia kutengeneza “Instrumentum Laboris” yaani “Hati ya Kutendea Kazi” wakati wa maadhimisho ya Sinodi ya Maaskofu Ukanda wa Amazonia iliyofunguliwa na Baba Mtakatifu Francisko, tarehe 6 Oktoba 2019 kwa Ibada ya Misa Takatifu. Maadhimisho yote haya yamewawezesha Mababa wa Sinodi kutoa Hati ya Sinodi ya Maaskofu Ukanda wa Amazonia kwa Mwaka 2019.

Maadhimisho ya Sinodi ambayo imefungwa rasmi kwa Ibada ya Misa Takatifu, na Baba Mtakatifu Francisko kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican, Jumapili tarehe 27 Oktoba, 2019 yameongozwa na Kauli mbiu: “Amazonia: njia mpya ya Kanisa na kwa ajili ekolojia fungamani”. Baba Mtakatifu katika mahubiri yake ameialika familia ya Mungu, kutafakari pamoja sala ya wahusika wakuu wa Liturujia ya Neno la Mungu Jumapili 30 ya Kipindi cha Mwaka C wa Kanisa yaani: Sala ya Farisayo, Mtoza Ushuru na Maskini. Sala ya Farisayo ni sifa na shukrani kwa Mwenyezi Mungu kwa sababu yeye si kama watu wengine, wanyang’anyi, wadhalimu na wazinzi, anafunga mara mbili kwa juma, ingawa kwa utaratibu wa nyakati zile, alipaswa kufunga mara moja kwa mwaka. Alikuwa anatoa zaka hata na kiasi cha ziada, lakini kwa bahati mbaya akasahau Amri Kuu ya Upendo kwa Mungu na jirani.

Farisayo huyu anasema Baba Mtakatifu, alijiamini kupita kiasi kwa sababu ya kutimiza Amri, akajihesabia haki binafsi. Mtakatifu Paulo anasema, yote haya pasi na upendo ni kama shaba iliayo na upatu uvumao. Farisayo hajisikii kutoka undani wake kwamba, ni mhitaji, ana pungukiwa kwa kuwa na deni na badala yake anajihesabia haki. Amesimama kati kati ya Hekalu la Mungu, lakini anakita mawazo yake kwenye Ibada ya ubinafsi. Anamsamahau Mwenyezi Mungu na kumpuuza jirani yake. Kwa bahati mbaya anasema Baba Mtakatifu huu ndio uhalisia wa historia. Watu wenye nafasi katika jamii, ndio wa kwanza kujenga kuta za utengano na kuwasukumizia jirani zao pembezoni mwa vipaumbele vya maisha. Wana wadharau na kuwabeza wengine, wanapuuza hata tamaduni zao; kwa kufutilia mbali historia ya watu mahalia na matokeo yake, “wanajimwambafai” na kuanza kumiliki ardhi na kuanza kunyonya utajiri na maliasili.

Kuna baadhi ya watu wanajiona kuwa ni watu wa maana zaidi kuliko wengine, hali inayoendelea hata katika Ukanda wa Amazonia. Kuna baadhi ya waamini wanaojidai kuwa ni wanaharakati wanataka kuhakikisha kwamba, Ibada na  Sala za watu kutoka Ukanda wa Amazonia zinabezwa na kupuuzwa na kusahau kwamba, Ibada ya kweli kwa Mwenyezi Mungu inajikita katika upendo kwa jirani! Hata Wakristo wanaoshiriki Ibada kila jumapili, nao wanajikuta wakitumbukia katika Ibada ya ubinafsi; kwa kuwadharau na kuwabeza wengine. Baba Mtakatifu anawasihi waamini kumwomba Mwenyezi Mungu neema ya unyenyekevu na kwa Kristo Yesu, neema ya kutosengenya, kuwalalamikia au kuwabeza wengine kwani hii ni tabia ambayo haimpendezi kamwe Mwenyezi Mungu.

Baba Mtakatifu anasema, Sala ya Mtoza Ushuru inakita mizizi yake katika shukrani kwa Mwenyezi Mungu, kwa kuorodhesha mapungufu na umaskini wake. Watoza ushuru walikuwa ni watu wenye uwezo mkubwa kiuchumi, lakini walikuwa ni wadhambi wa kutupwa, hali ambayo iliwakosesha ile furaha ya kweli katika maisha. Mtoza ushuru akajitambua kuwa ni mdogo sana mbele ya Mwenyezi Mungu. Na katika unyenyekevu huu, Mwenyezi Mungu anasikiliza sala yake. Hakuthubutu hata kuinua macho yake mbinguni kwani huko mbinguni ni makao ya Mungu. Alijipiga piga kifuani, chemchemi ya sala yake na wala hakuyakuza yale mambo yanayo onekana kwa nje. Sala ni fursa ya kumwachia nafasi Mwenyezi Mungu ili aweze kuangalia undani wa mtu, bila kificho wala kutaka kujihesabia haki, kwani hii yote ni kazi ya Shetani, Ibilisi, lakini mbele ya Mwenyezi Mungu yote ni mwanga na ukweli. Baba Mtakatifu ametumia fursa hii kuwasifu na kuwashukuru Mababa wa Sinodi ambayo katika kipindi chote cha maadhimisho ya Sinodi wamejadiliana katika:unyoofu, ukweli na uwazi; kwa kutoa kipaumbele cha kwanza kwa Mungu na jirani.

Sala ya Mtoza Ushuru ni kielelezo kwa waamini kwamba, wote wametindikiwa neema na wanahitaji wokovu wa Mungu ambaye ni mwingi wa huruma na mapendo, ikiwa kama mwamini atajitambua kuwa ni mdhambi na kwamba, Mwenyezi Mungu peke yake ndiye mwenye haki. Mtoza ushuru aliyeonekana kuwa mdhambi wa kutupwa, anaonekana kuwa ndiye mchamungu, kuliko hata Farisayo. Wanyenyekevu wa moyo wanakuzwa na kunyanyuliwa na Mwenyezi Mungu. Kila mwamini ndani mwake, kuna tabia ya kifarisayo na kama ya mtoza ushuru. Tabia ya undumila kuwili haifai hata kidogo! Waamini wawe na ujasiri wa kumwomba Mwenyezi Mungu neema ya kujitambua kuwa ni maskini na wahitaji wa huruma na upendo wa Mungu usiokuwa na kifani. Watambue kwamba, wao ni maskini wa roho na wanahitaji wokovu, ambao ni zawadi kutoka kwa Mwenyezi Mungu.

Baba Mtakatifu Francisko anasema, Sala ya Maskini na dua yake itafika hima mbinguni, lakini sala na dua ya mtu mwenye kiburi, inabaki hapa hapa duniani kwa kumezwa na ubinafsi. Imani ya watu wa Mungu, daima imeonesha kwamba, “maskini ni walinzi wa malango ya mbinguni”; wanaowafunguliwa watu malango ya maisha na uzima wa milele. Ni watu ambao wamekita maisha yao katika hali ya unyenyekevu na kumpatia Mwenyezi Mungu nafasi ya kwanza kama amana na utajiri wao wa maisha ya kiroho. Hawa ni mifano bora ya unabii wa Kikristo! Katika maadhimisho ya Sinodi ya Maaskofu Ukanda wa Amazonia, Mababa wa Sinodi wamepata nafasi ya kusikiliza kilio cha maskini; kutafakari hali ya maisha yao tete, yanayotishiwa na mifumo tenge ya maendeleo.

Shuhuda nyingi zimeonesha kwamba, inawezekana kabisa kuuangalia ukweli kwa njia tofauti kabisa kwa kujikita katika ukweli; kwa kuishi ulimwenguni, lakini kwa kutambua kwamba, mazingira ni nyumba ya wote inayopaswa kulindwa, kutunzwa na kuendelezwa. Malalamiko ya mtu aliyeonewa yanasikilizwa na Mwenyezi Mungu. Hata ndani ya Kanisa, kuna baadhi ya watu wameshindwa kusikia na kujibu kilio cha maskini. Baba Mtakatifu Francisko, mwishoni, anawaalika waamini kumwomba Mwenyezi Mungu ili awajaze neema kusikiliza na kujibu kilio cha maskini: Hiki ni kilio cha matumaini ndani ya Kanisa. Kwa kusikiliza kilio cha maskini na kukifanya kuwa ni sehemu ya sala ya waamini, kwa hakika, sala hii itafika hima mawinguni!

Papa: Misa Sinodi
27 October 2019, 13:31