Siku kuu ya Kutabarukiwa kwa Kanisa la Mt. Yohane Laterano 2019
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.
Kila mwaka ifikapo tarehe 9 Novemba, Mama Kanisa anaadhimisha Siku kuu ya Kutabarukiwa kwa Kanisa kuu la Mtakatifu Yohane wa Laterano lililoko mjini Roma. Baba Mtakatifu Francisko anatarajiwa kuongoza Ibada ya Misa Takatifu kuaniza saa 11:30 jioni kwa saa za Ulaya. Katika Ibada hii ya Misa Takatifu, atakikabidhi kikosi cha shughuli za kichungaji Jimbo kuu la Roma dhamana ya utekelezaji sera na mikakati ya shughuli za kichungaji katika kipindi cha mwaka 2019-2020. Kwa namna ya pekee, watu wa Mungu Jimbo kuu la Roma wanaitwa na kuhimizwa kusikiliza na kujibu kilio cha wananchi wa Roma na vitongoji vyake. Baba Mtakatifu atabariki mimbari mpya, mahali muafaka pa kutangazia Neno la Mungu katika Liturujia ya Kanisa. Hivi karibuni, Baba Mtakatifu Francisko kwa njia ya barua binafsi “Motu Proprio” “Aperuit Illis” ameanzisha “Dominika ya Neno la Mungu” itakayokuwa inaadhimishwa kuanzia sasa kila mwaka, Jumapili ya III ya Kipindi cha Mwaka wa Kanisa.
Ni matumaini ya Baba Mtakatifu kwamba, Jumapili hiyo itakuwa ni fursa kwa watu wa Mungu kujenga utamaduni wa kusoma, kutafakari na kumwilisha Neno la Mungu katika uhalisia wa maisha yao. Ni nafasi adhimu kwa Kanisa kutangaza, kushuhudia na kusambaza Neno la Mungu. Huu ni muda muafaka wa kuombea umoja wa Wakristo pamoja na kudumisha majadiliano ya kiekumene na kidini pamoja na Wayahudi. Baba Mtakatifu anawashauri waamini: kusoma Neno la Mungu, kulisikiliza na hatimaye, kujitahidi kulimwilisha katika uhalisia wa maisha yao. Katika maadhimisho ya Fumbo la Ekaristi Takatifu, Neno la Mungu lipewe kipaumbele cha kwanza, kwa kuandaa mahubiri kuhusiana na Maandiko Matakatifu pamoja na kutoa huduma kwa Wasomaji wa Neno la Mungu. Hapa, Wasomaji wa Neno la Mungu wanapaswa kuandaliwa vyema, ili waweze kulitangaza kwa ukamilifu, kama ilivyo kwa wahudumu wa Ekaristi Takatifu kwa wagonjwa na wazee parokiani. Hii ni siku ambayo wasomaji watakabidhiwa Biblia Takatifu, ili waendeleze tafakari hii katika uhalisia wa maisha yao, daima wakijitahidi kusali na kulitafakari Neno la Mungu.
Kanisa kuu la Mtakatifu Yohane wa Laterano ni Mama ya Makanisa yote ulimwenguni na kichwa cha Makanisa yote ya Jimbo kuu la Roma, lililowekwa wakfu na Papa Silvester kunako tarehe 9 Novemba mwaka 324, na kuwekwa chini ya ulinzi wa Kristo Mkombozi wa dunia. Baadaye, liliwekwa pia chini ya ulinzi wa Mtakatifu Yohane Mbatizaji na Mwinjili Yohane. Haya ni matunda ya uhuru wa kidini, uliotolewa kwa Wakristo kuabudu kadiri ya dini na imani yao na Mfalme Costantino kunako mwaka 313. Kumbu kumbu zinaonesha kwamba, hili ni Kanisa la kwanza kujengwa mjini Roma na baadaye, kuanzia mwaka1565 Makanisa yakaanza kujengwa sehemu mbali mbali ndani na nje ya Roma. Kanisa hili ni kielelezo cha Kanisa moja, takatifu, katoliki na la mitume. Ni alama ya upendo na mshikamano na Khalifa wa Mtakatifu Petro, ambaye kwa sasa ni Baba Mtakatifu Francisko, ambaye, anawaalika waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema kumsindikiza kwa sala na sadaka zao, katika maisha na utume wake kama Khalifa wa Mtakatifu Petro.
Kanisa hili ndilo Makao makuu ya Jimbo kuu la Roma, ambalo, Baba Mtakatifu ndiye Askofu wake mkuu. Kumbe, hii pia ni alama ya utakatifu wa Kanisa, licha ya watoto wake, wakati mwingine, kuogelea katika dimbwi la dhambi! Hii ni changamoto na mwaliko wa kujenga Kanisa hai, yaani Jumuiya ya Kikristo katika msingi ambao ni Kristo mwenyewe. Kanisa ni mahali ambapo waamini wanakusanyika kusikiliza Neno la Mungu na kushiriki kikamilifu katika Fumbo la Ekaristi Takatifu, ili waweze kuwa ni vyombo na mashuhuda wa ukweli na upendo kati ya watu wanaoishi nao, kwa kudumisha umoja na udugu wa kibinadamu unaotengeneza sadaka safi na yenye kumpendeza Mungu. Waamini wanahimizwa kuyalinda na kuyatunza Makanisa yao, kwani huu ni urithi na utajiri mkubwa wa maisha ya kiroho, kitamaduni na kihistoria pamoja na kutambua kwamba, hata wao wenyewe, miili yao ni Mahekalu ya Fumbo la Utatu Mtakatifu.