Hija ya Kitume ya Papa Francisko Nchini Iraq: MAHOJIANO MAALUM
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.
Baba Mtakatifu Francisko anasema, hija yake ya kitume ya 33 kimataifa nchini Iraq ni kati ya hija ambazo zilikuwa hatari sana katika maisha na utume wake. Alitumia muda mrefu kusali na kutafakari. Akapima madhara na faida yake kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya watu wa Mungu ndani na nje ya Iraq. Akajiaminisha mbele ya Mwenyezi Mungu na kuomba ulinzi na usalama kutoka kwa Bikira Maria, Afya ya Warumi, akapiga moyo konde na kuamua kwamba, kuanzia tarehe 5 hadi 8 Machi 2021 angefanya hija ya kitume nchini Iraq kwa kunogeshwa na kauli mbiu “Bali ninyi msiitwe Rabi, maana mwalimu wenu ni mmoja, nanyi nyote ni ndugu” Mt. 23:8. Baba Mtakatifu amekuwa ni hujaji wa toba, ili kumwomba Mwenyezi Mungu msamaha, tayari kuanza mchakato wa upatanisho wa Kitaifa. Baba Mtakatifu amekuwemo nchini Iraq kama hujaji wa amani ili kukoleza majadiliano ya kidini na kiekumene kama sehemu ya mchakato wa ujenzi wa udugu wa kibinadamu. Amepata nafasi ya kukutana mubashara na Kanisa la mashuhuda wa imani, ili kunogesha hija ya matumaini.
Hii ni hija ya kwanza ya kihistoria kuandikwa na Baba Mtakatifu Francisko, kama Khalifa wa kwanza wa Mtakatifu Petro kutembelea Iraq licha ya changamoto pevu zilizokuwa mbele yake. Baba Mtakatifu akiwa njiani kurejea mjini Vatican, Jumatatu tarehe 8 Machi 2021 alipata nafasi ya “kuchonga na waandishi wa habari 74 kutoka katika nchi 15. Kati ya waandishi wote hao, 14 kati yao kwa mara ya kwanza wameshiriki kwa karibu sana katika hija hizi za kitume. Huduma ya huruma na upendo kwa watu wa Mungu sanjari na mchakato wa ujenzi wa udugu wa kibinadamu ni mambo msingi katika majadiliano ya kidini na kiekumene, kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi anasema Baba Mtakatifu Francisko katika mahojiano maalum na wanatasnia ya mawasiliano ya jamii, waliokuwemo kwenye msafara wake kutoka Iraq. Amegusia jinsi alivyokosa maneno kwa kupigwa na bumbuwazi, alipoona na kushuhudia kwa macho yake jinsi Makanisa yaliyokuwa mazuri ambayo kwa sasa yamebaki kuwa magofu.
Baba Mtakatifu amezungumzia kuhusu: Hati ya Udugu wa Kibinadamu kwa Ajili ya Amani na Utulivu iliyotiwa saini kati ya Baba Mtakatifu Francisko na Dr. Ahmad Al-Tayyib, Imam Mkuu wa Msikiti wa Al- Azhar, ulioko mjini Kairo, nchini Misri, tarehe 4 Februari 2019 huko Abu Dhabi, Umoja wa Falme za Kiarabu. Ametia nia ya kutembelea Lebanon ili kuwafariji na kuwaimaarisha katika imani, matumaini na mapendo. Baba Mtakatifu amegusia pia majadiliano ya kidini na waamini wa dini ya Kiislam na kwamba, kwa sasa hana nia ya kutembelea Argentina. Licha ya hofu, wasiwasi na hatari kubwa ya maambukizi ya janga la Virusi vya Korona, UVIKO-19, kwa kusukumwa na dhamiri nyofu, ilimpasa kufanya hija hii ya kitume! Biashara haramu ya binadamu, viungo vyake pamoja na utumwa mamboleo. Baba Mtakatifu Francisko anasema, huduma ya huruma na upendo kwa watu wa Mungu sanjari na mchakato wa ujenzi wa udugu wa kibinadamu ni mambo msingi katika majadiliano ya kidini na kiekumene.
Imekuwa ni fursa ya kukutana na kuzungumza na Ayatollah Ali Sistani ambaye ni kiongozi mkuu wa kiroho na kisiasa nchini Iraq. Katika mazungumzo yake na Kardinali Bechara Boutros Rai, Patriaki wa Kanisa la Wamaroniti Wakatoliki nchini Lebanon, alikuwa amemwahidia kwamba, panapo majaliwa angeweza kutembelea Lebanon. Baba Mtakatifu ametumia nafasi hii kumkaribisha na kumtambulisha Monsinyo Dieunonné Datonou, Mratibu mpya wa Safari za Kipapa na mlinzi wake maalum. Baba Mtakatifu amewashukuru na kuwapongeza waandishi wa habari waliokuwemo kwenye msafara wake nchini Iraq. Amewashukuru kwa uwepo wao licha ya kazi ngumu na mchoko. Jumuiya ya Kimataifa hapo tarehe 8 Machi 2021 imeadhimisha Siku ya Wanawake Duniani. Baba Mtakatifu amesema, “First Lady” wa Rais Barham Ahmed Salih Qassim wa Iraq katika mazungumzo yao, amemshikirika kuhusu nguvu na ujasiri wa wanawake katika mchakato wa kusongesha mbele uhai, historia, familia pamoja na mambo mbali mbali.
Hati ya Udugu wa Kibinadamu kwa Ajili ya Amani na Utulivu ilitiwa saini kati ya Baba Mtakatifu Francisko na Dr. Ahmad Al-Tayyib, Imam Mkuu wa Msikiti wa Al- Azhar, ulioko mjini Kairo, nchini Misri, tarehe 4 Februari 2019 huko Abu Dhabi, Umoja wa Falme za Kiarabu. Huu ni mwaliko na changamoto kwa waamini wa dini mbali mbali duniani, kuungana na kushikamana, ili kufanya kazi katika umoja na udugu wa kibinadamu, ili kujenga na kudumisha misingi ya haki, amani na maridhiano kati ya watu. Hati hii ni nguzo msingi ya haki, amani na upatanisho. Hati inakazia pamoja na mambo mengine kwamba: binadamu wote wameumbwa kwa sura na mfano wa Mwenyezi Mungu; wanatakiwa kusimama kidete kulinda, kutunza na kudumisha: uhai wa binadamu, mazingira nyumba ya wote, sanjari na kushikamana na maskini pamoja na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa vipaumbele vya jamii.
Baba Mtakatifu Francisko anasema Hati ya Udugu wa Kibinadamu kwa Ajili ya Amani na Utulivu ni sehemu ya mchakato wa majadiliano ya kidini na matunda yake ni Waraka wa Kitume wa "Fratelli tutti": Yaani “Wote ni Ndugu”: Kuhusu Udugu na Urafiki wa Kijamii”. Malengo ya Waraka wa Kitume:"Fratelli tutti" ni kuhamasisha ujenzi wa mshikamano wa kidugu unaoratibiwa na kanuni auni, kwa kutoa kipaumbele cha kwanza kwa utu, heshima na haki msingi za binadamu. Hii ni dhana inayokumbatia maisha ya kifamilia, kijamii, kitaifa na kimataifa. Ili kufikia lengo hili, kuna haja ya kujenga na kudumisha tasaufi ya udugu wa kibinadamu kama chombo cha kufanyia kazi katika medani za kimataifa, ili kusaidia kupata suluhu ya matatizo yanayoikumba Jumuiya ya Kimataifa. Huu ni msaada mkubwa katika kupambana na changamoto mamboleo kama vile: Vita na kinzani mbali mbali; baa la njaa na umaskini duniani pamoja na athari za uharibifu wa mazingira nyumba ya wote.
Kipaumbele cha kwanza ni ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Mshikamano wa kidugu usaidie ujenzi wa mahusiano na mafungamano ya Jumuiya ya Kimataifa kama ilivyo pia miongoni mwa wananchi wenyewe. Ujasiri na ukarimu ni mambo yanayohitajika ili kufikia malengo ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Ayatollah Ali Sistani anasema, udugu wa kibinadamu unapata chimbuko lake katika kazi ya uumbaji inayowafanya kuwa ndugu na katika imani inayowaunganisha na kuwafanya kuwa ni ndugu wamoja. Usawa kama watoto wa Mungu ndilo jambo muhimu si tu katika masuala ya kidini bali hata katika utamaduni. Kwa Wakristo udugu huu umefunuliwa kwa njia ya Kristo Yesu, lakini imewachukua watu wa Mungu miaka mingi sana kuutambua na kuumwilisha udugu huu katika vipaumbele vyao vya maisha.
Hati ya Udugu wa Kibinadamu kwa Ajili ya Amani na Utulivu kama nguzo ya majadiliano ya kidini, inalenga kudumisha amani duniani. Ni sehemu ya utekelezaji wa maamuzi ya Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican, kama hata kuanzishwa kwa Baraza la Kipapa la Majadiliano ya Kidini. Hii ni hati ambayo imeandaliwa kwa sala na tafakari ya kina, ili kuweza kudhibiti: vita, uharibifu unaosababishwa na vitendo vya kigaidi, chuki na uhasama kati ya watu! Lengo ni kudumisha misingi ya haki, amani na maridhiano, chachu muhimu sana ya ustawi na maendeleo fungamani ya binadamu! Hakuna maendeleo ya kweli pasi na amani duniani. Hii ni hati inayopata chimbuko katika misingi ya imani kwa Mwenyezi Mungu mwingi wa huruma na mapendo! Iliandaliwa kwa usiri mkubwa. Lakini pamoja na faida zote hizi, Baba Mtakatifu Francisko mara kwa mara amekuwa akipokea shutuma kali dhidi yake na wakati mwingine inambidi kufanya maamuzi mazito! Haya ni maamuzi yanayotolewa baada ya sala, tafakari ya kina na ushauri.
Baba Mtakatifu Francisko anasema, “ametia nia” ya kutembelea nchini Lebanon ambako kuna mahangaiko makubwa ya watu wa Mungu. Kuna kinzani, migawanyiko na mipasuko. Ni mahali wanakohitaji toba, wongofu wa ndani na upatanisho wa Kitaifa. Baba Mtakatifu kupitia kwa Kardinali Béchara Boutros Raï, Patriaki wa Kanisa la Wamaroniti Wakatoliki nchini Lebanon, aliwaandikia watu wa Mungu nchini Lebanon Waraka wa matashi mema kwa Maadhimisho ya Sherehe za Noeli kwa Mwaka 2020. Lengo la Waraka huu, ilikuwa ni kutaka kuwafariji na kuwatia shime wakati Mama Kanisa alipokuwa anaadhimisha Sherehe ya Kuzaliwa kwa Kristo Yesu, Mfalme wa amani. Baba Mtakatifu pamoja na mambo mengine, alikazia kuhusu mateso na mahangaiko ya watu wa Mungu nchini Lebanon, Lebanon katika Maandiko Matakatifu, mwaliko kwa viongozi wa kisiasa na kidini pamoja na nia yake ya kutembelea Lebanon, pale hali itakapokuwa shwari.
Baba Mtakatifu Francisko katika Waraka wake kwa familia ya Mungu nchini Lebanon, anasema anasikitika sana kuona jinsi ambavyo wananchi wa Lebanon wanavyoteseka, walivyopokonywa hata ile hali ya kuishi kwa amani na hivyo kushindwa kuendelea kuwa ni mashuhuda na vyombo vya uhuru, amani na maridhiano kati ya watu. Kumbe, Baba Mtakatifu Francisko kusimama kitambo kidogo nchini Lebanon kama alivyokuwa ameombwa ingekuwa ni kutowatendea haki na heshima kutokana na matatizo, changamoto pamoja na fursa wanazokabiliana nazo. Lebanon imekuwa mstari wa mbele katika mchakato wa kuwapokea na kuwahudumia wakimbizi na wahamiaji. Baba Mtakatifu Francisko anasema amemtembelea na hatimaye kuzungumza na Ayatollah Ali Sistani, kiongozi mkuu wa kiroho na kisiasa nchini Iraq, ni kiongozi mwenye hekima na busara. Amemwelezea kuhusu nia ya hija yake ya kitume nchini Iraq kuwa ni hujaji wa toba, imani na matumaini; mambo ambayo yamemsukuma kutoka katika undani wake, kwenda kumsalimia. Kwa muda wa miaka kumi, Ayatollah Ali Sistani anapokea viongozi wa kidini tu!
Baba Mtakatifu anakiri kwamba, amepata heshima kubwa kutoka kwa mtu wa Mungu ambaye kweli ameonesha unyenyekevu mkubwa. Ni kwa njia ya wazee wenye hekima kama hawa na kama ilivyo kwa watakatifu kusambaza hekima na busara yao kwa watu wa Mataifa. Wazee kama hawa ni muhimu katika kukuza na kudumisha udugu wa kibinadamu. Udugu na ujirani mwema ni ushuhuda wenye mvuto na mashiko kuliko kashfa zinazoweza kutendeka ndani ya Kanisa. Bwana Nelson Castro, Daktari na Mwandishi wa Habari ambaye amewahi kuandika kitabu kuhusu “Magonjwa ya Marais Duniani” ni rafiki wa karibu wa Baba Mtakatifu Francisko. Amewahi kumwomba, aandike kitabu kuhusu “Magonjwa ya Mapapa” katika kipindi cha miaka ya hivi karibuni. Tayari mahojiano waliyofanya, yameandikiwa Kitabu, ingawa yeye mwenyewe bado hajakiona. Baba Mtakatifu anasema, Mwenyezi Mungu akimwita kwenye maisha na usingizi wa milele, atazikwa na kubaki Jimboni Roma.
Kwa muda wa miaka 76 ameishi nchini Argentina haoni sababu msingi ya kurudi tena huko. Kunako mwaka 2017 kulikuwa kumepangwa hija ya kitume nchini Argentina, lakini kulikuwa na maandalizi ya uchaguzi mkuu, kumbe haikuwezekana. Nia njema ya kutembelea Argentina bado ipo na muda ukifika atakwenda. Kabla ya kupanga hija, anasali, anatafakari, anaomba ushauri na hatimaye kufanya maamuzi. Safari ya Iraq ni matokeo ya maombi kutoka katika ngazi mbalimbali za uongozi nchini Iraq. Amejitafutia habari kuhusu Iraq, mateso, changamoto na fursa zilizopo; mambo ambayo yalimwezesha kufanya maamuzi magumu ya kutembelea Iraq. Umri umekwenda na kwamba, katika hija hii ameonekana kuchoka zaidi, kumbe umri wa miaka “84 si haba kama kiatu cha raba”.
Kongamano la 52 la Ekaristi Takatifu Kimataifa litafanyika mwezi Septemba 2021 huko Jimbo kuu la Esztergom-Budapest, nchini Hungaria kwa kuongozwa na kauli mbiu “Visima vyangu vyote vimo kwako” Zab. 87:7. Baba Mtakatifu anasema, anatarajia kushiriki maadhimisho haya sanjari na kutembelea mji mkuu wa Bratislava, ulioko nchini Slovakia. Lakini, ni safari zinachukuliwa uamuzi baada ya kuzingatia mambo msingi na ushauri kutolewa. Kanisa huko Mashariki ya Kati linakabiliwa na changamoto nyingi zinazopaswa kufanyiwa kazi. Kwa sasa hakuna nia ya kuadhimisha Sinodi. Lakini wimbi kubwa la wakimbizi na wahamiaji kutoka Iraq ni changamoto pevu. Watu wana haki ya kutohama na kubaki nchini mwao! Pili, watu wanayo haki kimataifa ya kutafuta: usalama, hifadhi na maisha bora zaidi. Kwa nchi ambazo zimekuwa na sera bora za kuenzi familia kama ilivyo nchini Ufaransa zimeendelea kuwa na idadi nzuri ya watoto wanaozaliwa kila mwaka. Lakini kuna nchi ambazo zimeingiliwa na ukame wa watoto wanaozaliwa, kiasi cha kuwa na idadi kubwa ya wazee, hatari kwa siku za usoni, kwani itabidi kugharimia wageni watakaotoa nguvu kazi na kulipia pensheni za wazee. Hii ni hatari kubwa kwa Italia anasema Baba Mtakatifu Francisko.
Kuna watoto kama Alan Kurdi wanafariki dunia wakiwa njiani kutafuta: hifadhi, usalama na maisha bora zaidi ughaibuni. Tafiti zinazonesha kwamba, hakuna uhusiano wowote kati ya wahamiaji na wakimbizi pamoja na vitendo vya kigaidi. Mara nyingi hivi ni vitendo vinavyofanywa na raia wa nchi hizo, ambao wamenyanyaswa na kubaguliwa na matokeo yake ni chuki na uhasama kwa jirani zao. Baba Mtakatifu anazishukuru nchi zile ambazo zimeendelea kutoa hifadhi kwa wakimbizi na wahamiaji. Lebanon inatoa hifadhi kwa wakimbikizi na wahamiaji zaidi milioni 2 kutoka Siria na Yordan inatoa hifadhi kwa wakimbizi na wahamiaji zaidi ya milioni moja na nusu. Kwa sasa Baba Mtakatifu hana mpango wa kufanya hija ya kitume nchini Siria, ingawa inabaki kuwa ni kati ya nchi ambazo tangu mwanzo amezipatia kipaumbele cha pekee katika maisha na utume wake.
Baba Mtakatifu anakiri kwamba, hija yake ya kitume nchini Iraq imemwezesha tena kukutana na watu mubashara na hivyo kupyaisha maisha na utume wake kama ilivyokuwa kwa Naamani jemedari wa Mfalme wa Shamu aliyeponywa ukoma wake na Nabii Elisha hata yeye amepyaishwa tena kutoka katika undani wa maisha yake. Viongozi wa Kanisa na waamini katika ujumla wao, wajifunze kujisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili ya Kristo na Kanisa lake bila kupenda sana kupokea “takrima”. Utamaduni wa kukutana na watu katika huduma ni chachu ya wokovu inayowasaidia viongozi wa Kanisa kuadhimisha Fumbo la Ekaristi Takatifu, kuwatangazia na kuwashuhidia watu Neno la Mungu pamoja na kuwaondolea dhambi zao. Baba Mtakatifu anasema ameguswa na shuhuda za watu wa Mungu nchini Iraq, watu ambao wamesiginwa na umaskini pamoja na vita, lakini, wako tayari kutubu na kumwongokea Mungu pamoja na kutoa msamaha kwa wale waliowatenda jeuri. Ni muda muafaka kwa waamini kujifunza kusamehe na kusahau, kiini cha Injili ya Kristo Yesu kwa wanafunzi wake.
Baba Mtakatifu anasikitika kusema kwamba, ameguswa sana alipoona Makanisa yaliyokuwa mazuri yamebomolewa na kubaki kuwa magofu, kiasi cha kupigwa bumbuwazi. Huu ni ukatili kupita kiasi unaochangiwa na biashara haramu ya silaha duniani. Silaha hizi ndizo zinazopandikiza mbegu ya chuki, uhasama na uadui kati ya watu. Wanawake wameteswa, wakanyanyaswa na kudhulumiwa utu, heshima na haki zao msingi nchini Iraq, lakini bado wameibuka kidedea. Kuna wanawake na wasichana wanaotumbukizwa kwenye biashara ya binadamu na utumwa mamboleo. Yote haya ni mambo yanayodhalilisha utu wa binadamu. Baba Mtakatifu Francisko anawaalika waamini na watu wote wenye mapenzi mema kusimama kidete kupambana na matendo haya maovu. Mambo haya yanatendeka hata Jijini Roma anaonya Baba Mtakatifu Francisko.