Papa Francisko Katekesi Kuhusu Fumbo la Sala: Sala Saa ya Yesu
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.
Baba Mtakatifu Francisko katika Mzunguko wa Katekesi yake kuhusu Fumbo la Sala amepembua na kufafanua kwa kina kuhusu: Sala na Fumbo la Utatu Mtakatifu kwa kujielekeza zaidi kwa Roho Mtakatifu anayewafunulia waamini kumhusu Kristo Yesu. Roho Mtakatifu anao uwezo wa kuchunguza hata Mafumbo ya Mungu. Ni Mungu peke yake anayemjua Mungu kabisa. Kanisa linamsadiki Roho Mtakatifu kwa sababu ni Mungu na kamwe haliachi kutangaza imani kwa Mungu mmoja: Baba, Mwana na Roho Mtakatifu. Kanisa ni Mama, Mwalimu na Shule ya Sala. Imani inapyaishwa kwa njia ya sala. Baba Mtakatifu ameelezea mitindo mbalimbali ya sala inayomwezesha mwamini kuzungumza mubashara na Mwenyezi Mungu. Anasema kuna Sala ya Sauti, Sala ya Fikara au Tafakari na Taamuli. Katika Katekesi kuhusu Mzunguko wa Fumbo la Sala, Baba Mtakatifu amepembua kwa kina na mapana kuhusu: umuhimu wa utume wa sala na changamoto zake katika maisha ya waamini. Amekumbusha kwamba, Kanisa lina dhamana ya kusali na kufundisha namna ya kusali vizuri zaidi. Kanisa ni shule kuu ya sala. Baba Mtakatifu amefafanua kuhusu Sala ya Taamuli na Mapambano katika Sala ya Kikristo” na kwamba, Sala si lelemama yataka nguvu ya ndani. Amegusia kuhusu fadhaa, uzembe na ukavu katika maisha ya sala!
Tumaini, Udumifu na Ujasiri katika sala ni mambo muhimu sana katika maisha ya sala! Baba Mtakatifu amesisitizia kuhusu udumifu katika upendo na sala. Sehemu hii ya Katekesi ilinogeshwa na Waraka wa kwanza wa Mtakatifu Paulo kwa Wathesalonike 5: 15-20 “Angalieni mtu awaye yote asimlipe mwenziwe mabaya kwa mabaya; bali siku zote lifuateni lililo jema, ninyi kwa ninyi na kwa watu wote. Furahini siku zote; Ombeni bila kukoma; shukuruni kwa kila jambo; maana hayo ni mapenzi ya Mungu kwenu katika Kristo Yesu. Msimzimishe Roho; msitweze unabii.” Udumifu katika upendo na sala ni mchakato unaokita mizizi yake katika sala ya moyo inayomkiri Kristo Yesu kuwa ni Mwana wa Mungu na hivyo kuomba huruma na msamaha kwa kutambua kwamba, binadamu ni mdhambi, daima anahitaji msamaha na huruma ya Mungu katika maisha yake. Hii ni sala inayopaswa kunogesha siku ya mwamini, kwa sababu sala hii ni sehemu ya vinasaba vya maisha yake!
Kama muhtasari wa hitimisho la mzunguko wa Katekesi Kuhusu Fumbo la Sala, Jumatano tarehe 16 Juni 2021, Kwenye Uwanja wa Mtakatifu Damas mjini Vatican, Baba Mtakatifu amefafanua kuhusu Sala ya Saa ya Yesu inayokita ujumbe wake katika Fumbo la Mateso, Kifo na Ufufuko wa Kristo Yesu kutoka kwa wafu! Hii ni Sala ambayo Kristo Yesu aliisali alipokuwa Bustanini Gethsemane. “Kisha wakaja mpaka bustani iitwayo Gethsemane; akawaambia wanafunzi wake, Ketini hapa muda niombapo. Akamtwaa Petro na Yakobo na Yohane pamoja naye, akaanza kufadhaika sana na kuhangaika. Akawaambia, Roho yangu ina huzuni nyingi kiasi cha kufa; kaeni hapa mkeshe. Akaendelea mbele kidogo, akaanguka kifudifudi, akiomba ya kuwa, ikiwezekana, saa hiyo imwepuke. Akasema, Aba, Baba, yote yawezekana kwako; uniondolee kikombe hiki; walakini, si kama nitakavyo mimi, bali utakavyo wewe.” Mk 14:32-36.
Hii ni Sala inayokita mizizi yake katika tabia, maisha na utume wa Kristo Yesu kwa sababu ni kielelezo cha majadiliano ya kina na Baba yake wa milele na huu ni utambulisho wake wa maisha. Sala ya Kikuhani iliyotolewa na Kristo Yesu inabeba ujumbe na maana ya pekee wakati alipokuwa anajiandaa kulipokea Fumbo la Msalaba yaani: Mateso, Kifo na Ufufuko wake. Fumbo la Pasaka ni kiini cha utangazaji na ushuhuda wa Habari Njema ya Wokovu, Kerygma “κήρυγμα”. Siku za mwisho za maisha ya Kristo Yesu mjini Yerusalemu zinapewa kipaumbele cha pekee na Wainjili kwa kuzama zaidi katika mateso, kifo na ufufuko wake, kwa ajili ya wokovu wa walimwengu wote kwa kushinda dhambi na mauti. Kristo Yesu alijiandaa kikamilifu kuiadhimisha Pasaka yake kwa kuzama katika sala Bustanini Gethsemane. Roho yake ilikuwa na huzuni kiasi cha kufa! Ni katika muktadha huu, Kristo Yesu “akasema, Aba, Baba, yote yawezekana kwako; uniondolee kikombe hiki; walakini, si kama nitakavyo mimi, bali utakavyo wewe.” Kristo Yesu kwa kumwita Mwenyezi Mungu “Aba, Baba” anaonesha imani na mahusiano ya ndani kabisa.
Huu ni muda ambao Yesu mwenyewe alihisi uwepo wa giza nene katika maisha yake. Hata akiwa ametundika juu Msalabani, Kristo Yesu aliendelea kusali, huku akijiaminisha kwa Baba yake wa mbinguni. Juu ya Msalaba, Kristo Yesu alisali na kuwaombea watu wote bila ubaguzi hata kama wote walimgeuzia kisogo wakati wa mateso na hatimaye kifo chake. “Na walipofika mahali paitwapo Fuvu la Kichwa, ndipo walipomsulibisha yeye, na wale wahalifu, mmoja upande wa kuume, na mmoja upande wa kushoto. Yesu akasema, Baba, uwasamehe, kwa kuwa hawajui watendalo.” Lk 23:33-34. Katika mateso na mahangaiko makubwa, Kristo Yesu akasali Zaburi pamoja na wale wote waliosahaulika na kusukumizwa pembezoni mwa jamii. “Mungu wangu, Mungu wangu, Mbona umeniacha? Mbona U mbali na wokovu wangu, Na maneno ya kuugua kwangu? Zab. 22: 1-2.
Katika muktadha huu, Kristo Yesu alihisi kana kwamba, Mwenyezi Mungu amemwacha na hivyo akazama katika sala. Juu la Msalaba, Kristo Yesu akajitoa sadaka kwa Baba yake wa mbinguni, kwa ajili ya wokovu wa walimwengu na hatimaye akajiaminisha mikononi mwa Baba yake wa milele. Na hitimisho la Sala ya Saa tatu Msalabani ni kumwita tena Baba yake wa Mbinguni na kusema, “Ee Baba, mikononi mwako naiweka roho yangu.” Alipokwisha kusema hayo alikata roho.” Lk 23: 46-47. Wakati wa mateso hadi kifo chake, Kristo Yesu alijikita katika sala na hivyo anakuwa ni mfano na kielelezo bora cha maisha ya sala kwa waamini wake. Juu la Msalaba Kristo Yesu amesali na kuwaombea watu wote wa Mungu. Kwa ufupi kabisa, Mababa wa Kanisa wanasema, Saa yake ilipofika, Kristo Yesu alimwomba Baba yake wa mbinguni na kwamba, hii ni sala ndefu kuliko sala zote zinazotolewa na Wainjili. Ni sala inayokumbatia mpango mzima wa kazi ya uumbaji na wokovu; kifo na ufufuko wa Kristo Yesu kutoka kwa wafu.
Hii ni sala inayobaki kuwa ni sala binafsi ya Kristo Yesu inayokita mizizi yake katika Fumbo la Utatu Mtakatifu. Mapokeo ya Mama Kanisa yanaitaja sala hii kuwa ni Sala ya Yesu ya Kikuhani inayounganishwa na sadaka ya Kristo Yesu Msalabani na kumwendea Baba yake wa mbinguni ambaye amejiweka wakfu kwake. Ni sadaka inayojumuisha mambo yote katika Kristo Yesu. Ni sala inayosimikwa katika unyenyekevu na utukufu. Kwa ufupi hii ni Sala ya Umoja. Kristo Yesu wakati wa Karamu ya mwisho alisali sana na hata wakati huu anaendelea kusali na kuwaombea waja wake. Sala ya Saa ya Yesu inahitimisha kazi yake ya ukombozi kama Mwana mpendwa wa Mungu, Kuhani wa Milele. Hii ni sala inayotekeleza maombi makuu yanayofumbatwa katika Sala ya Baba Yetu yaani: Kushughulikia jina la Baba Mungu Mwenyezi, tamaa ya Ufalme na Utukufu wa Mungu; kutimizwa kwa mapenzi ya Mungu, mpango wa wokovu na ukombozi dhidi ya Shetani, Ibilisi. Hatimaye katika sala hii, Kristo Yesu anawafunulia waja wake ujuzi usiotenganishwa na Fumbo la Utatu Mtakatifu ambalo kimsingi ndilo Fumbo la Maisha ya Sala! Rej. KKK 2746 – 2758.