Umuhimu wa Hija ya Kitume ya Papa Francisko Nchini Iraq 2021
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.
Baba Mtakatifu Francisko anasema, hija yake ya kitume ya 33 Kimataifa nchini Iraq ni kati ya hija ambazo zilikuwa hatari sana katika maisha na utume wake. Alitumia muda mrefu kusali na kutafakari. Akapima madhara na faida yake kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya watu wa Mungu ndani na nje ya Iraq. Akajiaminisha mbele ya Mwenyezi Mungu na kuomba ulinzi, tunza na usalama kutoka kwa Bikira Maria, Afya ya Warumi, akapiga moyo konde na kuamua kwamba, kuanzia tarehe 5 hadi 8 Machi 2021 angefanya hija ya kitume nchini Iraq na kweli akafanikiwa kwenda na kurejea salama salimini. Hija ikanogeshwa na kauli mbiu “Bali ninyi msiitwe Rabi, maana mwalimu wenu ni mmoja, nanyi nyote ni ndugu” Mt. 23:8. Baba Mtakatifu akawa ni hujaji wa toba, ili kumwomba Mwenyezi Mungu msamaha, tayari kuanza mchakato wa upatanisho wa Kitaifa nchini Iraq. Baba Mtakatifu akawa nchini Iraq kama hujaji wa amani ili kukoleza majadiliano ya kidini na kiekumene kama sehemu ya mchakato wa ujenzi wa udugu wa kibinadamu unaofumbatwa katika mshikamano. Akapata nafasi ya kukutana mubashara na Kanisa la mashuhuda wa imani, ili kunogesha hija ya matumaini.
Hii ni hija ya kwanza ya kihistoria kuandikwa na Baba Mtakatifu Francisko, kama Khalifa wa kwanza wa Mtakatifu Petro kutembelea Iraq licha ya changamoto pevu zilizokuwa mbele yake. Baba Mtakatifu anasema Hati ya Udugu wa Kibinadamu kwa Ajili ya Amani na Utulivu ni sehemu ya mchakato wa majadiliano ya kidini na matunda yake ni Waraka wa Kitume wa "Fratelli tutti": Yaani “Wote ni Ndugu”: Kuhusu Udugu na Urafiki wa Kijamii”. Malengo ya Waraka wa Kitume:"Fratelli tutti” ni kuhamasisha ujenzi wa mshikamano wa kidugu unaoratibiwa na kanuni auni, kwa kutoa kipaumbele cha kwanza kwa utu, heshima na haki msingi za binadamu. Hii ni dhana inayokumbatia maisha ya kifamilia, kijamii, kitaifa na kimataifa. Ili kufikia lengo hili, kuna haja ya kujenga na kudumisha tasaufi ya udugu wa kibinadamu kama chombo cha kufanyia kazi katika medani za kimataifa, ili kusaidia kupata suluhu ya matatizo yanayoikumba Jumuiya ya Kimataifa. Huu ni msaada mkubwa katika kupambana na changamoto mamboleo kama vile: Vita na kinzani mbali mbali; baa la njaa na umaskini duniani pamoja na athari za uharibifu wa mazingira nyumba ya wote.
Ni katika muktadha huu, tarehe 3 Juni 2021 kumefanyika mkutano kwa njia ya vyombo na mitandao ya kijamii kuhusu umuhimu wa Hija ya Kitume ya Baba Mtakatifu Francisko nchini Iraq. Kamati Kuu ya Utekelezaji wa Hati ya Udugu wa Kibinadamu ndiyo iliyoandaa mkutano huu kwa njia ya vyombo vya habarri na mitandao ya kijamii. Wajumbe wa Kamati hii ni pamoja na Kardinali Miguel Angel Ayuso Guixot, Rais wa Baraza la Kipapa la Majadiliano ya Kidini, Professa Mohamed Hussein Mahrasawi, Mkuu wa Chuo cha Al Azhar na Monsinyo Yoannis Lahzi Gaidi, Aliyekuwa Katibu muhtasi wa Baba Mtakatifu Francisko. Wengine katika kamati hii ni Jaji Mohamed Mahmoud Abdel Salaam, mshauri mkuu wa Mufti mkuu. Wajumbe wengine ni wale walioteuliwa kutoka Serikali ya Umoja wa Falme za Kiarabu, Baraza la Wazee wa Kiislam Umoja wa Falme za Kiarabu pamoja na watu maarufu katika tasnia ya habari Umoja wa Falme za Kiarabu.
Kardinali Miguel Angel Ayuso Guixot, Rais wa Baraza la Kipapa la Majadiliano ya Kidini katika hotuba yake elelezi amekazia kuhusu ushuhuda wa udugu wa kibinadamu wakati wa raha na shida mbalimbali. Kwa upande wa Iraq ni nchi ambayo bado ina makovu ya vita, ghasia na uharibifu mkubwa wa maisha na mali za watu. Hati ya Udugu wa Kibinadamu kwa Ajili ya Amani na Utulivu ilitiwa saini kati ya Baba Mtakatifu Francisko na Dr. Ahmad Al-Tayyib, Imam Mkuu wa Msikiti wa Al- Azhar, ulioko mjini Kairo, nchini Misri, tarehe 4 Februari 2019 huko Abu Dhabi, Umoja wa Falme za Kiarabu. Baba Mtakatifu Francisko anasema Hati ya Udugu wa Kibinadamu kwa Ajili ya Amani na Utulivu ni sehemu ya mchakato wa majadiliano ya kidini na matunda yake ni Waraka wa Kitume wa "Fratelli tutti": Yaani “Wote ni Ndugu”: Kuhusu Udugu na Urafiki wa Kijamii”. Huu ni mwaliko na changamoto kwa waamini wa dini mbali mbali duniani, kuungana na kushikamana, ili kufanya kazi katika umoja na udugu wa kibinadamu, ili kujenga na kudumisha misingi ya haki, amani na maridhiano kati ya watu.
Hati hii ni nguzo msingi ya haki, amani na upatanisho. Hati inakazia pamoja na mambo mengine kwamba: binadamu wote wameumbwa kwa sura na mfano wa Mwenyezi Mungu; wanatakiwa kusimama kidete kulinda, kutunza na kudumisha: uhai wa binadamu, mazingira nyumba ya wote, sanjari na kushikamana na maskini pamoja na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa vipaumbele vya jamii. Wakati wa hija yake ya kitume nchini Iraq, Baba Mtakatifu alibahatika kukutana na kuzungumza na viongozi wa kidini, kiserikali, wanadiplomasia pamoja na watu wa Mungu nchini Iraq katika ujumla wao. Baba Mtakatifu Francisko katika hotuba yake kwa viongozi wa Serikali, wanadiplomasia pamoja na viongozi wa asasi zisizo za Kiserikali aligusia mambo makuu yafuatayo: Janga la Virusi vya Korona, UVIKO-19, Madhara ya vita na vitendo vya kigaidi; Umuhimu wa majadiliano ya kidini na Kiekumene, ili kukoleza na kunogesha umoja na udugu wa mshikamano. Baba Mtakatifu Alikazia mchakato wa umoja, ushirikiano na mshikamano wa Jumuiya ya Kimataifa katika kukabiliana na changamoto mbalimbali zinazomwandama mwanadamu katika ulimwengu mamboleo.
Kimsingi, dini inapaswa kuwa ni kwa ajili ya huduma ya amani na udugu wa kibinadamu. Ndiyo maana tangu sasa tarehe 6 Machi ya kila mwaka, itakuwa ni Siku ya Kitaifa ya Kuvumiliana na Kuishi Pamoja “National Day of Tolerance and Coexistence”. Waamini wa dini mbalimbali wanapaswa kuheshimiana, kuthaminiana, kushirikiana na kusaidiana kama ndugu wamoja, kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Udugu wa kibinadamu ni jibu muafaka dhidi ya vita, ghasia na mipasuko mbalimbali ya kijamii. Majadiliano ya kidini na kiekumene na udugu wa kibinadamu ni msingi wa haki, amani na maridhiano kati ya waamini wa dini mbalimbali. Matumaini ya wapenda amani na maridhiano kwamba, Hija ya Kitume ya Baba Mtakatifu Francisko nchini Iraq itaendelea kuzaa matunda kwa wakati wake.
Kwa upande wake, Kardinali Louis Raphaël Sako wa kwanza, Patriaki wa Kanisa la Babiloni ya Wakaldayo, amesema kwamba, Hija ya Kitume ya Baba Mtakatifu Francisko pamoja na mambo mengine, ilijikita zaidi katika mchakato wa kutafuta na kudumisha misingi ya haki, amani na maridhiano kati ya watu wa Mungu nchini Iraq. Dini inapaswa kuwa ni daraja linalowaunganisha watu katika maelewano; chemchemi ya upatanisho, haki na amani. Elimu inayotolewa isaidie kunogesha mafundisho msingi ya dini hizi mbili, ili kuboresha maisha ya kiroho na kimwili, ili kujenga na kudumisha mahusiano, mafungamano, umoja na mshikamano wa kidugu. Viongozi wa kisiasa wanapaswa kusimama kidete kutafuta na kudumisha ustawi, maendeleo na mafao ya wengi; kwa kusimamia utu, heshima na haki msingi za binadamu.
Wakati huo huo, Jaji Mohamed Mahmoud Abdel Salaam, Katibu mkuu wa Kamati Kuu ya Utekelezaji wa Hati ya Udugu wa Kibinadamu katika hotuba yake elekezi, amekazia umuhimu wa umoja, ushirikiano na mshikamano wa udugu wa kibinadamu katika kukabiliana na changamoto mamboleo zinazoendelea kujitokeza kila kukicha! Vita, vitendo vya kigaidi, machafuko ya kisiasa na kidini ni kati ya mambo yanayogumisha mustakabali wa maisha ya watu wa Mungu nchini Iraq. Hija ya Kitume ya Baba Mtakatifu Francisko ilikuwa ni kwa ajili ya kujenga na kudumisha umoja na mshikamano wa watu wa Mungu nchini Iraq.