Tafuta

Papa Francisko ataendelea kubaki bado hospitalini kwa mapumziko. Papa Francisko ataendelea kubaki bado hospitalini kwa mapumziko.  

Afya ya Papa Francisko Hospitalini: Bado Anaendelea na Mapumziko!

Dr. Matteo Bruni, Msemaji mkuuu wa Vatican amewaambia waandishi habari kwamba, Baba Mtakatifu Francisko bado ataendelea kuwepo hospitalini hapo kwa mapumziko zaidi. Kabla ya Sala ya Malaika wa Bwana aliwatembelea watoto wagonjwa wa Saratani Hospitalini hapo. Alipata nafasi ya kusali na baadhi ya watoto hao pamoja na kuzungumza na badhi ya madaktari na wauguzi.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.  – Vatican.

Kwa Sakramenti ya Mpako Mtakatifu wa Wagonjwa na Sala za Makuhani, Kanisa lote huwakabidhi wagonjwa na wazee kwa Kristo Yesu aliyeteswa, akafa na kutukuzwa ili awagange, awainue na kuwaokoa wale wote wanaoteseka. Na kwa hakika, Kanisa linawahimiza wajiunge kwa hiari na mateso na kifo cha Kristo ili kutoa mchango wao kwa mafao ya Taifa la Mungu. Mama Kanisa anapenda kutafakari mang'amuzi ya ugonjwa na mateso mintarafu huruma ya Mungu inayojionesha kwa namna ya pekee kwa Kristo Yesu ambaye ni kielelezo cha Msamaria Mwema. Kwa kuiga mfano wa Msamaria mwema katika kufundisha na kuponya kwa njia ya Mpako Mtakatifu wa Wagonjwa, Mama Kanisa ameendelea kutekeleza dhamana na utume wake kwa wagonjwa kwa njia ya Sala ya Makuhani na Mpako Mtakatifu wa Wagonjwa sanjari na huduma ya afya inayotekelezwa na taasisi mbalimbali zinazomilikiwa na kuendeshwa na Kanisa. Kwa njia ya Maadhimisho ya Sakramenti ya Mpako Mtakatifu wa Wagonjwa, Kanisa linawasindikiza waamini wake ili kukabiliana na Fumbo la Mateso na Kifo.

Waamini wajitahidi kuthamini Sakramenti hii kama kielelezo cha mshikamano wa maisha ya kiroho na Kanisa zima, kwa kutambua uwepo endelevu wa Kristo Yesu anayewaimarisha wafuasi wake katika imani, matumaini na mapendo akiwakumbusha kwamba, hakuna kitu kinachoweza kuwatenga na nguvu yake inayoganga, kuponya na kuokoa! Mpako Mtakatifu wa wagonjwa unakamilisha kufananishwa kwa waamini na kifo na ufufuko wa Kristo Yesu kutoka kwa wafu kama ilivyo pia katika Sakramenti ya Ubatizo. Kimsingi Mpako wa wagonjwa hukamilisha mipako mitakatifu iliyotia alama yote ya Kikristo yaani: muhuri wa maisha mapya; mapambano ya maisha ya Kikristo na Sakramenti ya Mpako wa Wagonjwa huimarisha mwisho wa maisha ya mwamini hapa duniani, kama ngome thabiti kwa ajili ya mapambano ya mwisho, kabla ya kuingia katika nyumba ya Baba wa milele! Rej. KKK 1514 – 1532.

Ni katika muktadha huu, Baba Mtakatifu Francisko anasema, kila mtu anahitaji “Mafuta ya faraja” kama siyo leo, basi ni kesho. Mafuta ya faraja ni zawadi inayoweza kutolewa na kila mtu katika hija ya maisha yake hapa duniani kwa njia ya kuwatembelea wagonjwa, kuwapigia walau simu kuwajulia hali zao; kwa kuwasaidia kwa hali na mali wale wanaoteseka na kuhangaika katika maisha yao! Baba Mtakatifu kabla ya Sala ya Malaika wa Bwana, Jumapili tarehe 11 Julai 2021 aliwatembelea watoto wagonjwa wa Saratani waliolazwa kwenye Hospitali ya Gemeli, ili kuwashukuru kwa sala na ujumbe wao wa matashi mema waliomwandikia hivi karibuni. Baadhi yao wakiwa wameandamana na wazazi wao, walikwenda kusali pamoja Sala ya Malaika wa Bwana, kwenye ghorofa ya kumi, hospitalini hapo. Baada ya sala, alisalimiana na madaktari pamoja na wauguzi aliokutana nao njiani. Jioni aliadhimisha Ibada ya Misa Takatifu na watu wachache wanaomhudumia hospitalini hapo. Dr. Matteo Bruni, Msemaji mkuuu wa Vatican amewaambia waandishi habari kwamba, Baba Mtakatifu Francisko bado ataendelea kuwepo hospitalini hapo kwa mapumziko zaidi.

Baba Mtakatifu amefurahishwa na ushindi wa Timu ya Taifa ya Italia dhidi ya Waingereza kwa kuwachakaza kwa matuta 3-2 kwenye Uwanja wa Michezo wa Wembley, Jijini London, Uingereza, Jumapili tarehe 11 Julai 2021. Ushindi huu umepokelewa kwa heshima na taadhima baada ya Italia kushinda Kombe la Ulaya kwa mara ya kwanza kunako mwaka 1968, yaani miaka 53 iliyopita! Lionel Messi, ndiye aliyeitoa Argentina kimasomaso baada ya kuifunga Brazil kwa bao kwa nunge moja kwenye uwanja wa Rio wa Maracana, ulioko nchini Brazil. Kwa mara ya kwanza Argentina ilishinda ubingwa wa “Coppa America” miaka 28 iliyopita. Baba Mtakatifu amegusia umuhimu na tunu msingi zinazofumbatwa katika michezo, tayari kupokea matokeo kama sehemu ya ushindani. Kwa njia hii, wachezaji, mashabiki na viongozi wataweza kupokea matokeo kwa mikono miwili, huku wakiwa na imani na matumaini ya kuweza kufanya vyema zaidi wakati mwingine bila ya kutafuta “mchawi”.

Papa Wagonjwa

 

13 July 2021, 15:30