Ujumbe wa Papa: Mkutano wa Urafiki Rimini 2021: Ujasiri wa Mtu!
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. –Vatican.
Mkutano wa Urafiki kati ya Watu Nchini Italia huko Rimini: “Meeting per l’amicizia fra i popoli” unaofanyika kila mwaka sasa umeingia katika awamu yake 42 Kuanzia tarehe 20-25 Agosti 2021 kwa kunogeshwa na kauli mbiu “Il Coraggio di dire Io” yaani “Ujasiri wa Kusema Mimi.” Baba Mtakatifu Francisko katika ujumbe ulioandikwa kwa niaba yake na kutumwa kwa Askofu Francesco Lambiasi wa Jimbo Katoliki la Rimini, nchini Italia anawatakia heri na mafanikio mema! Katika ujumbe wake, Baba Mtakatifu anagusia kwa namna ya pekee kuhusu: Kipindi cha karantini ya kwanza ya Ugonjwa wa Virusi vya Korona, UVIKO-19, Ujasiri wa kushinda uwoga kwa kujenga na kudumisha utamaduni wa watu kukutana unaosimikwa katika ujasiri wa matumaini ya Kikristo unaobubujika kutoka kwa Kristo Yesu, aliyeteswa, akafa na kufufuka kwa wafu! Huu ni ujasiri wa furaha ya Injili unaokoleza mchakato wa ushuhuda na majadiliano katika ukweli na uwazi! Baada ya patashika nguo kuchanika kutokana na maambukizi makubwa ya Ugonjwa wa Virusi vya Korona, UVIKO-19 Mkutano wa Urafiki kati ya Watu Nchini Italia huko Rimini unafanyika mubashara kwa wajumbe kuhudhuria, huku wakizingatia uhuru unaowawezesha kufanya maamuzi makini, bila kuhatarisha uhuru huo! Kipindi cha karantini ya kwanza ya Ugonjwa wa Virusi vya Korona, UVIKO-19, kilitoa changamoto ya kuhakikisha kwamba, watu wanatumia vyema uhuru unaowawajibisha kama mtu binafsi. Watu wengi walishuhudia uhuru huo, kwa kuonana mubashara na Ugonjwa wa Virusi vya Korona, UVIKO-19!
Hawa ni watu waliokuwa na ujasiri wa kusema, “Tazama mimi hapa!” Watu hawa wakawajibika kikamilifu na kuondokana na ubinafsi pamoja na uchoyo unaowatala watu wengi katika ulimwengu mamboleo. Inasikitikisha kuona kwamba, uchu wa mali na madaraka vinatawala badala ya sadaka na majitoleo ya mtu binafsi, ili kujenga na kudumisha udugu wa kibinadamu na urafiki wa kijamii! Baba Mtakatifu Francisko anawaangalisha wakuu wa Jumuiya ya Kimataifa kusimama kidete kulinda, kutetea na kudumisha utu, heshima na haki msingi za binadamu. Ni mwaliko wa kuondokana na utandawazi usiojali wala kuthamini uwepo wa watu wengine ndani ya jamii na hivyo kuwatumia kama bidhaa dukani, inayoweza kuuzwa na kununuliwa wakati wowote ule! Watu wakiwajibika, wanakuwa ni vyombo na mashuhuda wa ujasiri wa matumaini. Ujasiri hasa miongoni mwa vijana wa kizazi kipya ni kielelezo cha sadaka na majitoleo makubwa hasa katika ulimwengu mamboleo. Hatari kubwa ni watu kushikwa na hofu pamoja na mashaka na kwamba, hofu na ujinga ni maadui wakuu katika ulimwengu mamboleo! Ujasiri wa kusema mimi hapa unabubujika katika mchakato wa watu kukutana, tayari kuwapokea na kuwakirimia wengine; kuwatambua na kuwaonesha ukarimu katika ukweli!
Ukweli huu ni Kristo Yesu, aliyeteswa, akafa na kufufuka kwa wafu. Kristo Yesu amekuwa ni chachu ya mabadiliko katika maisha ya watu wengi, kwa kuondokana na wasiwasi, hofu na mashaka na hivyo kuwa na mwelekeo chanya zaidi katika maisha. Hii ndiyo furaha ya uinjilishaji inayopendeza na kufariji. Daima wema hutaka kusambaa. Kila mara ukweli halisi na wa uhakika unapotambulika, kwa asili yake unatafuta namna ya kukua ndani ya watu na mtu yoyote aliyewahi kupata ukombozi wa ndani huwa mwepezi zaidi kutambua mahitaji ya wengine. Kadiri unavyokuwa, wema unaota mizizi na kuendelea kukomaa! Rej. EG 9. Baba Mtakatifu Francisko anasema kwamba, uzoefu na mang’amuzi haya yanasababisha ujasiri wa matumaini, ili kuguswa na upendo na matumaini ambayo kamwe hayawezi kudanganya. Imani ni kimbilio la watu wenye ujasiri inayowawezesha watu kugundua ndani mwao wito wa upendo, tayari kuonesha uaminifu kwa Mwenyezi Mungu ambaye ana nguvu kiasi cha kushinda udhaifu wa mwanadamu. Nguvu hii inajidhihirisha zaidi katika Kitabu cha Matendo ya Mitume: “Petro na Yohane wakawajibu wakawaambia, Kama ni haki mbele za Mungu kuwasikiliza ninyi kuliko Mungu, hukumuni ninyi wenyewe; maana sisi hatuwezi kuacha kuyanena mambo tuliyoyaona na kuyasikia.” Mdo 4:19-20. Ujasiri huu ni matunda na kazi ya Roho Mtakatifu.
Ujasiri wa matumaini ya Kikristo unabubujika kutoka kwa Kristo Yesu, aliyeteswa, akafa na kufufuka kwa wafu! Ni Kristo Yesu anayewawezesha waja wake kusimama kidete na kukabiliana na dhoruba za maisha. Baba Mtakatifu anawaalika wajumbe wa Mkutano wa Urafiki kati ya Watu Nchini Italia huko Rimini kufanya tafakari ya kina kuhusu uinjilishaji mpya kwa ajili ya uenezaji wa imani. Hii ni huduma ya kichungaji inayokolezwa na moto wa Roho Mtakatifu. Waamini wanapaswa kuwa mashuhuda wa mchakato wa uinjilishaji mpya. Kuna waamini wengi wanaomtafuta Mwenyezi Mungu kimyakimya, wakiongozwa na hamu ya kuuona Uso wake, hata kwenye nchi zenye utamaduni wa kale wa Kikristo. Hawa wote wanayo haki ya kuipokea na kuhibiri Injili bila ya kumtenga mtu yeyote yule. Lengo ni kuwashirikisha jirani zao ile furaha ya Injili, kwa kuwaelekeza kwenye upeo wa uzuri na kuwaalika wengine katika karamu tamu inayosheheni vinono! Kanisa linakuwa na kukomaa kwa njia ya ushuhuda wenye mvuto na mashiko! Rej. EG 14. Ujasiri wa Kiinjili uwawezeshe kusoma alama za nyakati, kugundua ishara na watu wapya, kwa mvuto wa Injili. Baba Mtakatifu anahitimisha ujumbe wake kwa kukazia ushuhuda na majadiliano katika ukweli na uwazi na kwamba, imani kwa Kristo Yesu ni zawadi kwa walimwengu wote!