Mazungumzo ya Papa Francisko na Wayesuit Nchini Slovakia! Uhuru!
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. –Vatican.
Hija ya Kitume ya Baba Mtakatifu Francisko ya 34 Kimataifa nchini Slovakia kuanzia tarehe 12-15 Septemba 2021, imenogeshwa na kauli mbiu “Pamoja na Bikira Maria na Mtakatifu Yosefu Njia ya Kwenda kwa Yesu”. Baba Mtakatifu amefanya hija hii baada ya kuhitimisha kwa Ibada ya Misa Takatifu Maadhimisho ya Kongamano la 52 la Ekaristi Takatifu Kimataifa “52nd International Eucharistic Congress” (IEC) kuanzia tarehe 5 hadi 12 Septemba 2021 huko Jimbo kuu la Esztergom-Budapest, nchini Hungaria kwa kuongozwa na kauli mbiu “Visima vyangu vyote vimo kwako” Zab. 87:7. Akiwa nchini Slovakia, Baba Mtakatifu Francisko, Jumapili tarehe 12 Septemba 2021 alipata nafasi ya kuzungumza na Wayesuit wanaoishi na kufanya utume wao nchini Slovakia. Amegusia: Dhana ya ukaribu katika maisha na utume wa viongozi wa Kanisa; Utakatifu ni mwaliko kwa waamini wote na wala si kwa watu wachache tu ndani ya Kanisa! Majadiliano ya kidini ni fursa ya kukuza na kudumisha uhuru wa kuabudu; Sera na mikakati yake kuhusu huduma kwa wakimbizi na wahamiaji.
Baba Mtakatifu katika mazungumzo yake amesikitika kusema wakati alipougua na kulazwa hospitalini kuna baadhi ya watu hata viongozi wa Kanisa walidhani kwamba, ataaga dunia na hivyo kuanza kujiandaa kwa ajili ya kuitisha Baraza la Makardinali kwa ajili ya uchaguzi wa Khalifa wa Mtakatifu Petro, lakini, Mwenyezi Mungu ni mwingi wa huruma, bado yupo na anaendelea kuchapa kazi kama kawaida! Muuguzi mmoja kutoka Vatican ndiye aliyeokoa maisha yake, kwa sababu hawa ni watu wanaokaa karibu zaidi na wagonjwa ikilinganishwa na madaktari. Baba Mtakatifu anawataka Wayesuis kuwa karibu na Mwenyezi Mungu kwa kwa sala, tafakari na maadhimisho ya Sakramenti za Kanisa. Wajenge utamaduni wa ujirani mwema kati yao, kwa kuoneshana udugu wa upendo wa kibinadamu, tayari kujikita katika mchakato wa ujenzi wa Jumuiya ya waamini kama ushuhuda amini wa uwepo angavu wa Kristo Yesu. Wayesuit, wajitahidi kuwa karibu na Maaskofu wao mahalia, ili kutekeleza sera na mikakati ya shughuli za kichungaji inayotolewa na Askofu Jimbo. Wayesuit wajenge na kudumisha utamaduni wa kuwa karibu na watu wa Mungu; katika ukweli na uwazi, kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi.
Maaskofu na Mapadre wakumbuke kwamba, wameteuliwa kutoka miongoni mwa watu wa Mungu kwa ajili ya mambo matakatifu ya Mungu, lakini asili na hatima ya maisha yao ni watu wa Mungu wanaopaswa kuwahudumia kwa ari na mapendo. Kumbe, kimsingi, Wayesuit wajenge ukaribu na ujirani mwema na Mwenyezi Mungu, wao wenyewe, Maaskofu mahalia pamoja na watu wa Mungu katika ujumla wao! Kati ya Wayesuit, walikuwemo Mapadre wazee 20 waliopewa Daraja ya Upadre wakiwa mafichoni kutokana na madhulumu ya kidini nyakati zao. Walilazimika kufanya kazi ili kujipatia mahitaji yao msingi na kwamba, kazi za mikono ziliwasaidia kupata afya bora. Baba Mtakatifu anasema, imani ya Kikristo ni chachu ya umoja na udugu wa kibinadamu, changamoto na mwaliko kwa Wakristo kujizatiti zaidi katika ujenzi wa umoja kwa kuondokana na kinzani zilizopelekea majanga makubwa katika maisha ya watu. Slovakia imepitia historia na vipindi vigumu vya dhuluma na nyanyaso za kidini pamoja na ukosefu wa uhuru wa kuabudu. Uhuru wa kweli ni tunu msingi katika maisha ya binadamu.
Kwa watu wengi wanataka kupigania uhuru, lakini wanapopewa uhuru huo na kujaliwa kuwa na amani na utulivu, wanaweza kujikuta wakitumbukia katika utumwa wa maisha ya kiroho. Uhuru wa Kiinjili uwawajibishe kutafuta na kuambata umoja wa Wakristo unaofumbatwa katika: maamuzi thabiti, udumifu na sadaka kama kielelezo cha imani. Uhuru wa kweli unawafumbata na kuwaambata watu wote bila ubaguzi. Kanisa linapaswa kuwa ni mahali pa kuwakutanisha watu kwa sala, tafakari, maadhimisho ya Sakramenti za Kanisa pamoja na kufanya mchakato wa mang’amuzi ya pamoja, ili kujikita katika uhuru wa Kiinjili, ili hatimaye kusonga mbele! Usawa wa kijinsia unaopigiwa kampeni na baadhi ya nchi na Mashirika ya Kimataifa unapania kuondoa tofauti za kijinsia, jambo ambalo ni hatari sana kwani litawatumbukiza watu wengi katika ukoloni wa kiitikadi, hali ambayo inadhalilisha utu, heshima na utambulisho wa binadamu. Umoja wa Mataifa unapaswa kusimama kidete kulinda na kudumisha haki msingi za binadamu mintarafu uhuru wa kidini na kidhamiri. Waamini wanapaswa kutambua kwamba, Kanisa ni Sakramenti ya Wokovu, watu wanapaswa kusikilizwa shida zao na kusaidiwa kadiri inavyowezekana.
Majadiliano ya kidini kati ya waamini wa dini mbalimbali ni nyenzo msingi ya kupambana na tabia ya ubinafsi, ili kujenga na kudumisha umoja, upendo na mshikamano na maridhiano kati ya watu, kila mtu akipewa nafasi ya kushuhudia imani yake! Kumbe, katika mchakato wa majadiliano ya kidini, Wakristo wanapaswa kumuungama Kristo Yesu aliyeteswa, akafa na kufufuka kwa wafu, chanzo cha imani, furaha na matumaini ya waja wake. Mwenyezi Mungu ni kiini cha majadiliano na watu wake na kamwe hajaacha kuzungumza na wanawadamu katika safari ya maisha yao hapa duniani, kama ilivyokuwa kwenye Agano la Kale hata leo hii, Mwenyezi Mungu anazungumza na binadamu kwa njia ya Kristo Yesu na Kanisa lake. Kristo ni ufunuo wa huruma na upendo wa Baba wa milele, aliyetumwa kumkomboa mwanadamu kutoka katika lindi la dhambi na mauti. Majadiliano ya kidini ni fursa ya kukuza na kudumisha uhuru wa kuabudu unaofumbatwa katika ushuhuda wa imani inayoheshimu tofauti-msingi kama utajiri na changamoto ya kujenga na kudumisha umoja, mshikamano na udugu kati ya watu wa Mungu.
Majadiliano ya kidini hayana budi kusimikwa katika ukweli na uwazi; kwa kutambua na kuthamini utambulisho wa maisha ya kiroho sanjari na kudumisha katekesi makini ya kila mwamini katika dini yake bila ya kutaka kufanya wongofu shuruti. Majadiliano ya kidini ni fursa muhimu sana kwa waamini kuweza kutangaza na kushuhudia imani yao; kwa kuheshimu na kuthamini uwepo wa dini za watu wengine ndani ya jamii na kuwaelekeza katika hija inayowapeleka kwa Mwenyezi Mungu asili ya wema na utakatifu wote. Baba Mtakatifu anawataka Wayesuit kujenga utamaduni wa majadiliano katika ukweli na uwazi, bila ya kujificha katika maamuzi mbele ambayo ni hatari sana katika mshikamano na mafungamano ya kijamii. Baba Mtakatifu anasema, katika utume wake, amejikita zaidi katika Injili ya haki na amani; utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote; maskini, wakimbizi na wahamiaji. Kwa bahati mbaya, kuna baadhi ya waamini wanasahau kwamba, amekazia pia kuhusu mchakato wa utakatifu wa maisha. Upendo wa dhati ni njia inayoweza kuwapeleka waamini katika utakatifu! Waamini wanapaswa pia kusikiliza, kutafakari na kulimwilisha Neno la Mungu katika uhalisia wa maisha yao; wajitahidi kushiriki mara kwa mara Sakramenti za Kanisa; kwa kujitia uthabiti katika kusali, kujinyima pamoja na kutekeleza matendo ya huruma: kiroho na kimwili kwa wahitaji zaidi. Hii ndiyo changamoto inayotolewa na Baba Mtakatifu Francisko katika Waraka wake kitume “Gaudete et exsultate” yaani “Furahini na kushangilia, wito wa utakatifu katika ulimwengu mamboleo”.
Baba Mtakatifu anasema, utakatifu ni mwaliko kwa waamini wote na wala si kwa watu wachache tu ndani ya Kanisa! Huu ni mwaliko wa kuongeza jitihada za kukutana na Kristo Yesu katika maisha kwa njia ya toba na wongofu wa ndani, tayari kuambata: huruma na upendo wa Mungu katika maisha. Watakatifu ni watu wa kawaida kabisa, ni wadhambi waliotubu na kumwongokea Mungu, leo hii wamekuwa ni marafiki zake wa karibu! Watakatifu ni mashuhuda na vyombo vya huruma na upendo wa Mungu katika maisha yao! Kwa njia ya Sakramenti ya Ubatizo, Wakristo wote wamejichukulia dhamana ya kuanza safari ya utakatifu wa maisha! Watakatifu walikuwa na mapungufu na dhambi zao binafsi, lakini wakathubutu kukimbilia huruma na upendo wa Mungu katika maisha yao! Utakatifu ni hija ya maisha mbele ya Mwenyezi Mungu inayofumbatwa katika ujasiri, matumaini na uthubutu kwa kuamini kwamba, neema ya Mungu inaweza kuwaongoza kufikia hatima yake, yaani kuonana na Mwenyezi Mungu uso kwa uso! Baba Mtakatifu anawataka viongozi wa Kanisa na waamini katika ujumla wao kusoma alama za nyakati na kutenda kadiri ya mazingira na kamwe wasipende kufanya mambo kwa mazoea. Viongozi wa Kanisa wajifunze kujenga na kudumisha utamaduni wa uvumilivu, sala na yote mawili yamwilishwe katika Injili ya upendo!
Baba Mtakatifu Francisko anasema, Kanisa Katoliki katika sera na mikakati yake kuhusu huduma kwa wakimbizi na wahamiaji linapenda kukazia kwa namna ya pekee umuhimu wa: “Kuwapokea, kuwalinda, kuwaendeleza na kuwahusisha wakimbizi na wahamiaji” katika maisha ya jamii inayowapatia hifadhi. Hawa ni watu wanaokimbia vita, dhuluma, nyanyaso, majanga asilia na umaskini, changamoto na mwaliko kwa familia ya binadamu kusoma alama za nyakati, ili kujenga utamaduni wa upendo na mshikamano wa udugu wa kibinadamu! Hakuna sababu msingi ya kuwanyanyapalia wakimbizi na wahamiaji. Jumuiya ya Kimataifa ijifunze sababu msingi zinazowapelekea watu kukimbia makwao na athari zake, ili kujipanga vyema zaidi kukabiliana na wimbi kubwa la wakimbizi na wahamiaji duniani. Baba Mtakatifu alikaribishwa chakula cha mchana, lakini, hakuweza kupata nafasi ya kushiriki pamoja nao, na badala yake, alikwenda jikoni kuangalia chakula kilichokuwa kimeandaliwa kwa ajili ya Maaskofu na wageni rasmi!