Hija ya Kitume ya Papa Francisko Slovakia: Jumuiya ya Warom: Utu!
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. –Vatican.
Baba Mtakatifu Francisko akiwa Jimbo kuu la Košice, Slovakia, Jumanne tarehe 14 Septemba 2021 amepata nafasi ya kutembea Jumuiya ya Warom wanaoishi huko Luník IX. Hili ni eneo la watu maskini ambalo kimsingi linakosa mahitaji muhimu kama vile: umeme, gesi na maji safi na salama kwa ajili ya matumizi ya binadamu. Jumuiya hii ilianzishwa kunako miaka ya 1970 na kwa sasa inahudumiwa na Wasalesian wa Mtakatifu Bosco. Takwimu zinaonesha kwamba, kuna watu zaidi ya 4, 300 wanaoishi katika eneo hili. Baba Mtakatifu Francisko kutembelea eneo hili limekuwa ni tukio litakalokumbukwa daima. Kutokana na ujio wa Baba Mtakatifu, kumekuwepo na maboresho makubwa katika eneo hili lakini, watu wa Mungu wanatamani kuona maboresho na upyaisho wa maisha ya kiroho, kiutu na kimadili, kwa ajili ya sifa na utukufu wa Mwenyezi Mungu. Baba Mtakatifu Francisko katika hotuba yake amehimiza kwa namna ya pekee kuhusu: Umoja na mshikamano kama watoto wa Mungu, walioumbwa kwa sura na mfano wake.
Watu wote wanapaswa kushirikishwa katika mchakato wa maendeleo fungamani ya binadamu, ili kulinda na kudumisha: utu, heshima na haki msingi za binadamu! Baba Mtakatifu amesema ndani ya Kanisa hakuna mgeni wala “mtu wa kuja” wote ni watoto wa Mungu walioumbwa kwa sura na mfano wake. Kanisa ni familia ya Mungu inayohamasishwa kujenga na kudumisha umoja, mshikamano na udugu wa kibinadamu, ili watu wote katika ujumla wao waweze kujenga familia kubwa ya binadamu. Na kwa njia hii, watu waweze kuipenda, kuiheshimu pamoja na kulipenda Kanisa ambalo kwa sasa limekuwa ni makazi yao. Hapa ni mahali ambapo watu wote wanapaswa kujisikia kwamba, wako nyumbani. Baba Mtakatifu anawataka wajitahidi kujenga na kudumisha tunu msingi za maisha ya kifamilia licha ya tofauti zao za mahali wanakotoka, tamaduni, mila na desturi zao, ili kuondokana na mawazo mgando yanayosimikwa katika maamuzi mbele.
Hii ni dhambi inayowapekenya hata Wakristo katika maisha yao, kwa kuwaangalia wengine kama maadui, bila ya kujibidiisha kuwafahamu na kusikiliza historia ya maisha yao. Kristo Yesu anasema msihukumu mtu msije mhakuhumiwa. Lakini, watu wengi “wamejichotea umaarufu kwa kupika majungu dhidi ya jirani zao”. Wamekwenda mbali hata kuwahukumu pasi na hatia, hali ambayo inachafua sifa njema, utu na haki msingi za binadamu. Ufahamu na utambuzi, unapaswa kufumbatwa kwa kutambua uzuri wa watoto wa Mungu walioumbwa kwa sura na mfano wake. Baba Mtakatifu anasikitika kusema kwamba, Jumuiya hii ya Warom imegeuka na kuwa kama “mpira wa danadana”. Ni Jumuiya ambayo imetwishwa maamuzi mbele, imehukumuwa bila huruma, imetengwa na kutendewa vibaya kwa mawazo na matendo. Na matokeo yake, Jumuiya hii imeendelea kudidimia katika umaskini wa hali na kipato. Changamoto ni kupyaisha utambuzi wa utu, heshima na haki msingi za binadamu, kwa kuondokana na maamuzi mbele na kuanza kujikita katika mchakato wa majadiliano na ushirikishwaji unaofumbatwa katika upendo wa dhati. Wanajumuia hii wapewe fursa za ajira ili kukidhi mahitaji yao msingi pamoja na kupendwa. Huu ndio ushuhuda uliotolewa na watu wanaoishi katika Jumuiya hii ya Warom.
Sera na mikakati ya shughuli za kichungaji inapaswa kutoa kipaumbele cha kwanza kwa utu, heshima na haki msingi za binadamu, kwa kuondokana na maamuzi mbele pamoja na tabia ya kuwahukumu wengine. Tabia ya ubaguzi inasababisha chuki na hasira na kwamba, njia ya amani inajengwa katika ushirikishwaji na utulivu; kwa kufahamiana na kupendana kama ndugu. Ikumbukwe kwamba, leo na kesho bora zaidi iko mikononi mwa watoto wanaopaswa kuwawajibisha katika kutunga sera na kufanya maamuzi magumu kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Licha ya changamoto na magumu yanayoweza kujitokeza, lakini kuna umuhimu wa kuunda Jumuiya shirikishi, ili kujenga utamaduni wa watu kukutana hata ndani ya Kanisa. Baba Mtakatifu amewashukuru wale wote wanaoendelea kujisadaka ili kuhakikisha kwamba wanawashirikisha watu katika mchakato wa maendeleo fungamani ya binadamu. Amewakumbuka pia wafungwa na wale wote wanaowasaidia kama sehemu ya shughuli zao za kichungaji.
Hii huduma itakayozaa matunda kwa wakati wake, kwa kujenga umoja na udugu wa kibinadamu sanjari na kupandikiza mbegu ya amani. Viongozi wa Kanisa wasiogope kwenda kuwatembelea na kukutana na watu waliosukumizwa pembezoni mwa jamii kwani huko kwa hakika watakutana na Kristo Yesu. Watambue kwamba, Kristo Yesu anaendelea kuwasubiri mahali penye mahitaji msingi ya binadamu; mahali ambapo huduma inatawala na wala si nguvu wala mabavu! Mwishoni, Baba Mtakatifu amewataka wanajumuiya Warom, kuachana na hofu na madonda yaliyopita na kuanza kujiamini, hatua kwa hatua, kwa kuaminiana na kusaidiana katika sala.