Hija ya Kitume ya Papa Francisko Slovakia: Salam na Matashi Mema
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. –Vatican.
Hija ya Kitume ya Baba Mtakatifu Francisko nchini Slovakia kuanzia tarehe 12 hadi tarehe 15 Septemba 2021 imenogeshwa na kauli mbiu “Pamoja na Bikira Maria na Mtakatifu Yosefu Njia ya Kwenda kwa Yesu”. Baba Mtakatifu Francisko, Jumatano tarehe 15 Septemba 2021 baada ya kusali pamoja na Baraza la Maaskofu Katoliki Slovakia na hatimaye, kuadhimisha Ibada ya Misa Takatifu kwenye Madhabahu ya Bikira Maria wa Šaštin amefunga vilago na kuanza kurejea mjini Vatican ili kuendelea na maisha na utume wake wa kufundisha, kuongoza na kuwatakatifuza watu wa Mungu. Baba Mtakatifu Francisko akiwa njiani kurejea mjini Vatican ametuma salam na matashi mema kwa viongozi wakuu wa nchi ya: Slovakia, Hungaria, Croatia, Bosnia-Erzegovina pamoja na Italia! Baba Mtakatifu katika ujumbe kwa Rais Zuzana Čaputová wa Hungaria amewashukuru kwa wema na ukarimu waliomwonesha wakati wa hija yake ya kitume nchini mwao. Amewahakikishia sala na sadaka yake na kwamba, anawaombea amani, ustawi na maendeleo na hatimaye, amewapatia baraka zake za kitume!
Baba Mtakatifu katika ujumbe wake kwa Rais János Áder wa Hungaria, amesema, amehitimisha hija yake ya kitume nchini Hungaria na Slovakia na kwamba, anaendelea kuwaweka chini ya ulinzi na tunza ya Mwenyezi Mungu, mwingi wa huruma na mapendo. Anawatakia heri na baraka tele! Kwa viongozi wa Croatia, Bosnia-Herzegovina amewatakia heri, baraka, amani na ustawi na maendeleo. Hatimaye, Baba Mtakatifu alipoingia kwenya anga la Italia, amemjulisha Rais Sergio Mattarella wa Italia kwamba, amerejea tena baada ya hija yake ya Kitume nchini Hungaria na Slovakia ambako amebahatika kukutana na watu wa Mungu, wenye wingi wa utajiri wa maisha ya kiroho. Baba Mtakatifu anapenda kuwasalimia watu wa Mungu nchini Italia sanjari na kuwahakikishia sala zake, ustawi na maendeleo. Mwishoni amewapatia baraka zake za kitume! Kabla ya kuondoka, Baba Mtakatifu amekagua gwaride la heshima na hatimaye, kuagana na viongozi wakuu wa Slovakia!