Tafuta

Baba Mtakatifu Francisko amewashukuru watu wa Mungu nchini Slovakia kwa kufanikisha hija yake ya kitume nchini mwao na hasa zaidi waliomwombea. Baba Mtakatifu Francisko amewashukuru watu wa Mungu nchini Slovakia kwa kufanikisha hija yake ya kitume nchini mwao na hasa zaidi waliomwombea. 

Hija ya Kitume ya Papa Francisko Nchini Slovakia: Shukrani Nyingi!

Maadhimisho ya Fumbo la Ekaristi Takatifu, imekuwa ni fursa ya kumshukuru Mungu kwa wema na upendo wake. Papa Francisko kwa namna ya pekee amewashukuru viongozi wa Serikali na wale wote waliojisadaka ili kufanikisha hija hii ya kitume, lakini zaidi, wale wote waliomsindikiza kwa sala. Wote hawa amewabeba katika “sakafu ya moyo wake” kama alama ya shukrani.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. –Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko, wakati wa hija yake ya kitume nchini Slovakia kuanzia tarehe 12 hadi 15 Septemba 2021, baada ya kuadhimisha Ibada ya Misa Takatifu kwenye Madhabahu ya Bikira Maria wa Šaštin nchini Slovakia, Jumatano tarehe 15 Septemba 2021, amewashukuru watu wote wa Mungu waliowezesha kufanikisha hija yake ya kitume nchini Slovakia. Na kwa namna ya pekee kabisa katika maadhimisho ya Kitaifa ya Kumbukumbu ya Bikira Maria Mama wa Mateso Saba, maadhimisho ambayo yamewakumbatia watu wote wa Mungu nchini Slovakia. Bikira Maria wa Mateso Saba ni Msimamizi wa Slovakia. Maadhimisho ya Fumbo la Ekaristi Takatifu, imekuwa ni fursa ya kumshukuru Mungu kwa wema na upendo wake wa daima. Baba Mtakatifu kwa namna ya pekee amewashukuru viongozi wa Serikali na wale wote waliojisadaka usiku na mchana ili kufanikisha hija hii ya kitume, lakini zaidi, wale wote waliomsindikiza kwa sala na sadaka zao. Wote hawa amewabeba katika “sakafu ya moyo wake” kama alama ya shukrani.

Kwa upande wake, Askofu mkuu Stanislav Zvolenský wa Jimbo kuu la Bratislava, Slovakia, kwa niaba ya watu wa Mungu nchini Slovakia amempongeza na kumshukuru Baba Mtakatifu Francisko kwa kuwawezesha kutangaza na kushuhudia imani na ibada yao kwa Bikira Maria Mama wa Mateso. Slovakia inamshukuru kwa namna ya pekee kwa kuadhimisha pamoja nao Sikukuu ya Bikira Maria Mama wa Mateso Saba. Hija ya Kitume ya Baba Mtakatifu Francisko nchini Slovakia kuanzia tarehe 12 hadi tarehe 15 Septemba 2021 imenogeshwa na kauli mbiu “Pamoja na Bikira Maria na Mtakatifu Yosefu Njia ya Kwenda kwa Yesu”. Baba Mtakatifu amewawezesha watu wa Mungu nchini Slovakia kutangaza na kushuhudia imani na ibada kwa Bikira Maria na Mtakatifu Yosefu. Amesaidia kukoleza moto na ari ya majadiliano ya kidini na kiekumene kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya watu wa Mungu nchini Slovakia, ili siku moja, Wakristo wote waweze kushuhudia umoja kamili unaoonekana. Kwa vijana amewahimiza kuendelea kuwa na ndoto kubwa katika maisha yao, kwa kuukumbatia na kuuambata Msalaba wa Kristo Yesu.

Kwa uwepo na ushiriki wa Baba Mtakatifu Francisko katika matukio mbalimbali nchini Slovakia amewasha moto wa imani, matumaini na mapendo. Sasa ni wajibu na dhamana kwa waamini na watu wote wenye mapenzi mema kuendelea kuwasha moto wa imani, matumaini na mapendo kwa Mungu na jirani!

Papa Shukrani
15 September 2021, 13:30