Tafuta

Baba Mtakatifu Francisko: Upatanisho ni Sakramenti ya furaha, huruma na upendo wa Mungu kwa binadamu Baba Mtakatifu Francisko: Upatanisho ni Sakramenti ya furaha, huruma na upendo wa Mungu kwa binadamu  Tahariri

Upatanisho ni Sakramenti ya Furaha, Huruma na Upendo wa Mungu

Baba Mtakatifu Francisko anawataka vijana kujenga mazoea ya kukimbilia Sakramenti ya Upatanisho, ili kuonja huruma na upendo wa Mungu katika maisha yao. Baada ya maungamo, vijana watumie muda kidogo ili kumshukuru Mungu aliyewaondolea dhambi zao! Upatanisho ni Sakramenti ya furaha, huruma na upendo wa Mungu, inayotoa kipaumbele cha kwanza kwa Mungu Baba

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. –Vatican.

Hija ya Kitume ya Baba Mtakatifu Francisko nchini Slovakia kuanzia tarehe 12 hadi tarehe 15 Septemba 2021 ilinogeshwa na kauli mbiu “Pamoja na Bikira Maria na Mtakatifu Yosefu Njia ya Kwenda kwa Yesu”. Baba Mtakatifu Francisko, Jumanne, tarehe 14 Sikukuu ya Kutukuka kwa Msalaba, alikutana na kuzungumza na vijana wa kizazi kipya nchini Slovakia, kwenye Uwanja wa Lokomotiva, Jimbo kuu la Košice. Baba Mtakatifu anawataka vijana kujenga mazoea ya kukimbilia Sakramenti ya Upatanisho, ili kuonja huruma na upendo wa Mungu katika maisha yao. Baada ya maungamo, vijana watumie muda kidogo ili kumshukuru Mungu aliyewaondolea dhambi zao! Upatanisho ni Sakramenti ya furaha, huruma na upendo wa Mungu, inayotoa kipaumbele cha kwanza kwa Mwenyezi Mungu. Mapadre waungamishaji wawe ni watu wenye huruma na mapendo na kamwe wasiwe ni wadadisi wa kutaka kuchokonoa hata yale yasiyowahusu. Mapadre waungamishaji wawe ni vyombo vinavyotoa: huruma na msamaha wa Mungu. Vijana wasikate tamaa wanapojisikia na kuona aibu ya kwenda kuungama dhambi zao, kwani hata katika hali na mazingira kama haya, Mwenyezi Mungu bado anawapenda na kuwajali jinsi walivyo!

Vijana wajenge utamaduni wa kujisamehe wenyewe kwani Mwenyezi Mungu anafurahi kuwaona watu wanaotubu na kumwongokea na anawangalia kama watoto wake wapendwa na wala si kama wadhambi! Sakramenti ya Upatanisho iwe ni chemchemi ya furaha mbinguni na amani duniani. Hii ni Sakramenti inayojikita katika: toba na majuto ya kweli yaani uchungu wa roho na chuki dhidi ya dhambi iliyoyendwa pamoja na kusudi la kutotenda dhambi tena baadaye. Maungamo ya dhambi, ili kuweza kujipatanisha na Mungu, Kanisa na jirani, baada ya utafiti wa dhati wa dhamiri. Na mwisho ni kutimiza malipizi. Hii inatokana na ukweli kwamba, dhambi nyingi husababisha madhara kwa jirani. Kumbe, kuna haja ya kujibidiisha kulipa hasara iliyojitokeza kama sehemu ya malipizi ya dhambi. Malipizi haya pia yanaweza kuwa katika mtindo wa sala, matoleo, matendo ya huruma: kiroho na kimwili pamoja na kufunga. Mitindo mbalimbali ya Kitubio inawasaidia waamini kufanana na Kristo Yesu ambaye amelipa dhambi mara moja na kwa daima. Malipizi yanawasaidia waamini kuteseka, kufa na hatimaye, kufufuka pamoja na Kristo Yesu na hivyo kuanza kutembea katika mwanga wa Kristo Mfufuka.

Ni katika muktadha huu, Dr. Andrea Tornielli, Mhariri Mkuu wa Baraza la Kipapa la Mawasiliano katika Tahariri yake kuhusu Upatanisho Sakramenti ya furaha amekazia umuhimu wa huruma na upendo wa Mungu unaobubujika kutoka katika Sakramenti ya Upatanisho. Baba Mtakatifu Francisko anasema, Mwenyezi Mungu daima anasamehe na kusahau na kwamba, huruma na upendo wa Mungu kwa mdhambi ndicho kiini cha Sakramenti ya Upatanisho. Waamini wajifunze kukimbilia huruma na upendo wa Mungu katika Sakramenti ya Upatanisho. Hata katika aibu yao ya kutenda dhambi, lakini bado Mwenyezi Mungu anawapenda na kuwathamini jinsi walivyo! Waamini na hasa vijana wa kizazi kipya, wajifunze kujisamehe kwanza, kwani hiki ni kielelezo cha upendo wa dhati! Kamwe waamini wasikate wala kujikatia tamaa ya kukimbilia katika Mahakama ya huruma na upendo wa Mungu, ili kuonja huruma ya Mungu inayoganga, kuponya na kuokoa! Huyu ndiye yule Baba Mwenyezi huruma ambaye anasimuliwa kwenye Maandiko Matakatifu, yuko tayari kuwapokea, kuwakumbatia na kuwakaribisha watoto wake wanaothubutu kutubu na kukimbilia huruma na upendo wake wa daima!

Sakramenti Upatanisho
16 September 2021, 16:31