Tafuta

Hotuba ya Baba Mtakatifu Francisko kwa wajumbe wa warsha juu ya afya ya umma na mtazamo wa kiulimwengu. Hotuba ya Baba Mtakatifu Francisko kwa wajumbe wa warsha juu ya afya ya umma na mtazamo wa kiulimwengu. 

Hotuba ya Papa Francisko Kwa Wajumbe Wa Warsha ya Afya ya Umma: UVIKO-19

Papa amegusia: Afya ya Umma: Kilio cha maskini na kilio cha dunia, Maadili ya Kibaiolojia Ulimwenguni; Afya na Magonjwa, Chanjo dhidi ya UVIKO-19 na umuhimu wa Mchango wa Taasisi ya Kipapa ya Maisha. Afya ya umma na mtazamo wa kiulimwengu inagusa undani wa maisha ya mwanadamu, changamoto na mwaliko wa kusikiliza na kujibu kilio cha maskini na kilio cha dunia.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. –Vatican.

Askofu mkuu Vincenzo Paglia, Rais wa Taasisi ya Kipapa ya Maisha katika hotuba yake ya utambulisho wa wajumbe wa Warsha ya Siku tatu kuanzia tarehe 27-29 Septemba 2021 kwa Baba Mtakatifu Francisko amesema, Warsha hii inaongozwa na kauli mbiu “Afya ya umma na mtazamo wa kiulimwengu”. Hii inaonesha mwingiliano na mafungamano yaliyopo katika familia ya mwanadamu na kwamba, binadamu wote wameonesha udhaifu, hali ambayo imegusa hata kazi ya uumbaji. Warsha hii inawashirikisha wataalam ambao wamekuwa mstari wa mbele katika mapambano dhidi ya Ugonjwa wa Virusi vya Korona, UVIKO-19. Waathirika wakuu ni wazee, walemavu, wakimbizi, wahamiaji na watoto. Hii ni changamoto inayohitaji mshikamano wa udugu wa kibinadamu ili kuweza kuishughulikia kikamilifu. Waraka wa Kitume wa Baba Mtakatifu Francisko "Fratelli tutti": Yaani “Wote ni Ndugu”: Kuhusu Udugu na Urafiki wa Kijamii”  unakamilishana na Waraka wa Kitume wa “Laudato si” yaani “Sifa iwe kwako” juu ya utunzaji wa nyumba ya wote.” Hizi ni nyaraka ambazo zinawaongoza wataalam hawa katika majadiliano yao, ili kupata mwelekeo wa ulimwengu ujao. Warsha hii, kuanzia tarehe 27-28 Septemba 2021 inaendeshwa pia kwa njia ya vyombo vya mawasiliano na mitandao ya kijamii.

Ni katika muktadha huu, Baba Mtakatifu Francisko katika hotuba yake kwa washiriki wa Warsha hii amegusia kuhusu: Afya ya Umma: Kilio cha maskini na kilio cha dunia, Maadili ya Kibaiolojia Ulimwenguni; Afya na Magonjwa, Chanjo dhidi ya UVIKO-19 na umuhimu wa Mchango wa Taasisi ya Kipapa ya Maisha. Baba Mtakatifu anasema, “Afya ya umma na mtazamo wa kiulimwengu” ni tema ambayo inagusa undani wa maisha ya mwanadamu, changamoto na mwaliko wa kusikiliza na kujibu kilio cha maskini na kilio cha dunia. Ugonjwa wa Virusi vya Korona, UVIKO-19 umewavuruga watu kiasi kwamba, hawatamani tena kusikiliza hotuba kuhusu gonjwa hili la hatari. Lakini ni muhimu kuendelea kufanya upembuzi yakinifu, ili kuweza kuchukua hatua madhubuti, baada ya kusikilizana kwa makini, ili kupata wongofu wa ndani na hatimaye, kuiwezesha Jumuiya ya Kimataifa kutoka katika janga hili la hatari. Maadili ya Kibaiolojia Ulimwenguni ni tafakari ambayo imeanza kuzaa matunda na kwamba, yanapaswa kuendelezwa zaidi, ili kujenga na kudumisha umoja, mshikamano na mafungamano katika familia ya binadamu.

Ni wakati wa kuimarisha urafiki wa kijamii; mambo msingi yanayobainishwa kwenye Waraka wa Kitume wa Baba Mtakatifu Francisko "Fratelli tutti": Yaani “Wote ni Ndugu”: Kuhusu Udugu na Urafiki wa Kijamii.” Kuna mwingiliano wa karibu sana katika familia ya binadamu na utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote! Kumbe, kuna haja ya kufahamu fika kuhusu baiyolojia, afya, dawa, maradhi, uchumi, elimu jamii, uelewa wa binadamu pamoja na ikolojia. Ni vyema pia Jumuiya ya Kimataifa ikaweka vigezo katika utekelezaji wake kwa kuzingatia: teknolojia, siasa, kanuni maadili na utu wema mintarafu mifumo ya afya, familia, kazi na mazingira. Mang’amuzi haya ni muhimu sana katika sekta ya afya kwa sababu afya na magonjwa yanategemea kwa kiasi kikubwa mazingira na maisha ya kijamii, mambo yanayohitaji umakini kwa kila upande. Hata leo hii bado Malaria na Ugonjwa wa Kifua kikuu unapelekea mamilioni ya watu kupoteza maisha; magonjwa ambayo yangeweza kudhibitiwa kikamilifu, kama kungekuwepo na utashi wa kisiasa. Janga la Ugonjwa wa Virusi vya Korona, UVIKO-19 linashughulikiwa kwa umakini mkubwa sanjari na kutengewa rasilimali fedha ya kutosha, ikilinganishwa na magonjwa mengine yanayoendelea kusababisha maafa kwa watu sehemu mbalimbali za dunia.

Baba Mtakatifu anasema, umefika wakati kwa Jumuiya ya Kimataifa kutoa kipaumbele cha pekee kwa magonjwa yanayoendelea kusababisha vifo vya watu wengi duniani, maboresho ya huduma ya maji safi na salama sanjari na uhakika wa usalama wa chakula. Mchakato wa utengenezaji na ugavi wa chanjo ya UVIKO-19 unapaswa kuzingatia usawa na haki ili kuimarisha afya na kuendeleza maisha ya binadamu. Dhana ya afya ikichukuliwa katika mapana yake, itawasaidia watu wengi kuwajibika, kwa sababu ya mwingiliano wake. Hali ya maisha ya mwanadamu ni matunda ya maamuzi yanayofanywa kisiasa, kijamii pamoja na kimazingira na maotokeo yake yanaangukia kwenye afya ya binadamu hali ambayo imeonesha ukosefu wa usawa. Maisha na afya bora ni tunu msingi ambazo ziko sawa kwa watu wote na zinafumbata utu, heshima na haki msingi za binadamu. Utambuzi huu unapaswa kutekelezwa kwa vitendo, kwa sababu maisha ya binadamu wote ni sawa! Utawala wa Kimataifa unahitajika ili kulinda na kudumisha afya ya watu wote wa Mungu. Hii inatokana na ukweli kwamba, hatari ya kushambuliwa na majanga ya magonjwa ni kubwa sana kwa sasa na kwa siku za mbeleni!

Taasisi ya Kipapa ya Maisha inaweza kuchangia, ili kufikia lengo hili. Hapa kuna haja ya kuhakikisha kwamba, ujumbe na maudhui yake yanawafikia walengwa bila ya “kuchakachuliwa.” Hivi ndivyo inavyopaswa kuwa katika uelewa wa Kikristo kuhusu maisha ya binadamu unaopata chimbuko lake kutoka katika Ufunuo wa Mungu, asili na hatima ya maisha ya mwanadamu, tangu pale anapotungwa mimba hadi mauti ya kawaida yanapomfika! Kimsingi maendeleo makubwa ya sayansi yanapaswa kuwa ni kwa ajili ya huduma ya binadamu na wala si binadamu kwa ajili ya huduma ya sayansi. Baba Mtakatifu anaupongeza “Mfuko wa Renaissance” kwa kusaidia kusambaza uelewa wa Mkataba wa “Rome Call for Artificial Inteligence” uliotiwa saini tarehe 28 Februari 2020 unaokazia pamoja na mambo mengine, umuhimu wa kuzingatia kanuni maadili na utu wema ulitiwa saini kati ya Taasisi ya Kipapa ya Maisha, Kampuni ya Microsoft, Kampuni ya IBM pamoja na Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa (Food and Agriculture Organzation of the United Nations"; kifupi: FAO).

Ni matumaini ya Baba Mtakatifu kwamba watu wote wenye mapenzi mema wataendelea kushirikiana kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi; kwa kusimama kidete kuwalinda na kuwatetea wanyonge na kwamba, maendeleo ni kwa ajili ya wote! Baba Mtakatifu amewapongeza wajumbe wa Taasisi ya Kipapa ya Maisha kwa mchango wao mkubwa kwenye Tume ya UVIKO-19 ya Vatican. Kumbe, kuna haja ya kuendeleza ushirikiano na mshikamano wa ndani katika Sekretarieti kuu ya Vatican ili hatimaye kuweza kuwa na mradi wa pamoja, unaowashirikisha watu wengi zaidi, sanjari na kutoa kipaumbele cha kwanza kwa wazee, walemavu na vijana. Taasisi ya Kipapa ya Maisha ni kwa ajili ya kulinda na kuendeleza Injili ya uhai.

Papa Afya ya Umma
27 September 2021, 15:04