Tafuta

Malaika ni wajumbe na vyombo vya neema na baraka za Mungu kwa watu wake! Malaika ni wajumbe na vyombo vya neema na baraka za Mungu kwa watu wake! 

Malaika Ni Wajumbe Wa Neema Na Baraka Za Mungu Kwa Watu Wake!

Baba Mtakatifu Francisko anawaalika waamini kujiaminisha chini ya ulinzi na tunza ya Malaika wakuu ili matendo yao mema yaweze kuonekana mbele ya Mwenyezi Mungu. Kwa msaada wa Malaika hawa, waamini nao wajaliwe kuwa ni vyombo na mashuhuda wa neema na huruma ya Mungu. Mama Kanisa tarehe 29 Septemba anawakumbuka Watakatifu Malaika Wakuu! Walinzi!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. –Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko wakati wa Katekesi yake, Jumatano tarehe 29 Septemba 2021 amesema, Mama Kanisa kila mwaka ifikapo tarehe 29 Septemba anawakumbuka na kuwaenzi Watakatifu Malaika wakuu: Mikaeli, Gabrieli na Rafaeli, vyombo vya neema ya Mungu. Malaika wakuu wametajwa kwa namna ya pekee kabisa katika Maandiko Matakatifu na kila mmoja akitajwa kwa kazi maalum anayoifanya mbele ya Mwenyezi Mungu. Baba Mtakatifu anawaalika waamini kujiaminisha chini ya ulinzi na tunza ya Malaika wakuu ili matendo yao mema yaweze kuonekana mbele ya Mwenyezi Mungu. Kwa msaada wa Malaika hawa, waamini nao wajaliwe kuwa ni vyombo na mashuhuda wa neema na huruma ya Mungu. Baba Mtakatifu amesema Malaika mkuu Mikaeli ni mlinzi wa nchi ya Ufaransa. Awalinde na kuwasaidia kuwa waaminifu katika asili yao na awaongoze na kuwaelekeza katika mchakato wa ujenzi wa umoja wa Kitaifa na mshikamano wenye upeo mpana zaidi.

Malaika mkuu Mikaeli alipambana na Shetani, Ibilisi, awasaidie waamini katika mapambano dhidi ya Shetani, Ibilisi katika maisha yao. Malaika mkuu Gabrieli, ni mjumbe wa Habari Njema ya Wokovu awaletee watu wa Mungu Habari Njema ya Wokovu, Kristo Yesu, aliyemkomboa mwanadamu kutoka katika lindi la dhambi na mauti na awakirimie matumaini. Malaika mkuu Rafaeli, awashike mkono na kuwasindikiza katika safari yao ya kutafuta mafao ya wengi na katika mchakato wa uponyaji!

Mikaeli (Mikhā'ēl)  maana yake “Ni nani aliye sawa na Mungu? Huyu ni Malaika mkuu aliyepambana fika na Ibilisi, Shetani na kushinda, kiasi kwamba, yule nyoka mkubwa, aitwaye Shetani, Ibilisi audanganyaye ulimwengu wote, akatupwa hata katika nchi kama tunavyosoma kwenye Maandiko Matakatifu. Rej. Uf. 12:7. Malaika mkuu Rafaeli ni mlinzi wa watu wa Mungu kwa sababu yeye ni Jemedari mkuu. Rej. Dan. 12: 1.

Gabrieli  (Gaḇrīʾēl (גַבְרִיאֵל)) maana yake ni nguvu ya Mungu. Huyu ni kati ya Malaika wakuu saba wanaokaa siku zote mbele ya Mwenyezi Mungu kama alivyosema Malaika Gabrieli alipokuwa anajibizana na Zakaria kwa kumkumbusha kwamba, yeye alikuwa ni Gabrieli anayesimama mbele ya Mungu na ametumwa kumpasha Habari Njema ya kuzaliwa kwa Yohane Mbatizaji. Malaika mkuu Gabrieli ndiye aliyetumwa na Mungu kwenda mpaka mji wa Galilaya, jina lake Nazareti kwa Bikira Maria, ili kumpasha Habari Njema kwamba, atakuwa ni Mama wa Mungu. Kwa maneno machache, Malaika wakuu ndio wanaowafunulia watu siri za Mwenyezi Mungu. Rej. Lk. 1-19; Lk. 1:26-28.

Rafaeli ( רָפָאֵל, Rāfāʾēl” ) maana yake ni dawa ya Mungu inayoponya. Rafaeli ni kati ya Malaika watakatifu saba wanaopeleka sala za watakatifu, na kuingia mbele za utukufu wake aliye Mtakatifu. Mwenyezi Mungu ndiye anayepaswa kupewa heshima, utukufu na sifa. Rej. Tob. 12:15 na Ufu. 8:2. Mababa wa Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican wanasema katika liturujia ya hapa duniani, waamini wanashiriki, wakionja liturujia ya mbinguni, iadhimishwayo katika Mji Mtakatifu Yerusalemu, wanaouelekea kama wasafari, ambako Kristo Yesu ameketi mkono wa kuume wa Mwenyezi Mungu kama mhudumu wa patakatifu na wa ile hema ya kweli. Waamini wanaungana na wapiganaji wa jeshi la mbinguni kumwimbia Mwenyezi Mungu wimbo wa utukufu. Wakiwakumbuka kwa heshima watakatifu, wanatumaini kupata ushirika nao, wanangojea kwa shauku Mkombozi, Kristo Yesu, mpaka atakapojidhihirisha, Yeye ambaye ni uzima wao, ndipo nao watakapodhihirishwa pamoja naye katika utukufu. Rej. SC. 8.

Malaika Wakuu

 

 

29 September 2021, 15:35