Tafuta

Monsinyo Corrado Maggioni ameteuliwa na Papa Francisko kuwa Rais wa Tume ya Kipapa ya Makongamano Kimataifa. Monsinyo Corrado Maggioni ameteuliwa na Papa Francisko kuwa Rais wa Tume ya Kipapa ya Makongamano Kimataifa. 

Mons. Corrado Maggioni Rais wa Tume ya Makongamano ya Ekaristi Kimataifa

Mons. Corrado Maggioni ameteuliwa kuwa Rais wa Tume ya Kipapa ya Makongamano ya Ekaristi Takatifu Kimataifa na hivyo kuchukua nafasi ya Askofu mkuu Piero Marino aliyeongoza Tume hii tangu mwaka 2007 hadi mwaka 2021. Mons. Corrado Maggioni, S.M.M., kabla ya uteuzi huu, alikuwa ni Katibu mkuu msaidizi wa Baraza la Kipapa la Ibada na Nidhamu ya Sakramenti za Kanisa.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. –Vatican.

Tume ya Kipapa ya Makongamano ya Ekaristi Takatifu Kimataifa ilianzishwa rasmi na Papa Leo XIII kunako mwaka 1876 ili kusaidia mchakato wa kumwezesha Kristo Yesu: kufahamika, kupendwa na kutumikiwa kwa njia ya maadhimisho ya Fumbo la Ekaristi Takatifu kiini na kilele cha maisha na utume wa Kanisa. Kumbe, Makongamano ya Ekaristi Takatifu Kitaifa na Kimataifa katika maisha na utume wa Kanisa ni katekesi endelevu inayogusa: Fumbo la Ekaristi Takatifu, kiini na kilele cha maisha na utume wa Kanisa. Ekaristi Takatifu ni Fumbo la Mwanga linalobubujika kutoka katika Neno la Mungu linalohitaji: kutangazwa na kushuhudiwa kama kielelezo cha imani tendaji. Hili ni Fumbo linalohitaji usikivu wa kiibada na ukimya wa kitafakari uwezeshao Neno la Mungu kugusa akili na mioyo ya watu. Ekaristi Takatifu ni chakula cha maisha ya kiroho na kielelezo cha uwepo endelevu wa Kristo Yesu kati ya waja wake.  Ekaristi takatifu ni shule ya upendo, ukarimu, umoja na mshikamano wa dhati kati ya watu wa Mungu. Ekaristi Takatifu ni Sakramenti na shule ya Upendo; ni zawadi na sadaka ya Kristo Yesu Msalabani; kielelezo cha huduma inayomwilishwa na kuwasha mapendo kwa Mungu na jirani.

Hili ni Fumbo kubwa linalopaswa kuadhimishwa vyema; Kuabudiwa na Kutafakariwa kikamilifu. Mtakatifu Yohane Paulo II katika Waraka wake wa Kitume, “Kaa Nasi Bwana”: Mane, Nobiscum Domine”, anawaalika waamini kujenga utambuzi hai wa uwepo halisi wa Kristo Yesu, katika adhimisho la Ibada ya Misa Takatifu na katika Ibada nje ya Misa. Maadhimisho ya Kongamano la 52 la Ekaristi Takatifu Kimataifa “52nd International Eucharistic Congress” (IEC), kuanzia tarehe 5-12 Septemba 2021, huko Jimbo kuu la Esztergom-Budapest, nchini Hungaria yalinogeshwa na kauli mbiu “Visima vyangu vyote vimo kwako” Zab. 87:7. Baada ya maadhimisho haya, Baba Mtakatifu Francisko amemteuwa Monsinyo Corrado Maggioni, S.M.M kuwa Rais wa Tume ya Kipapa ya Makongamano ya Ekaristi Takatifu Kimataifa na hivyo kuchukua nafasi ya Askofu mkuu Piero Marino aliyeongoza Tume hii tangu mwaka 2007 hadi mwaka 2021 na hivyo kumaliza muda wake. Monsinyo Corrado Maggioni, S.M.M., kabla ya uteuzi huu, alikuwa ni Katibu mkuu msaidizi wa Baraza la Kipapa la Ibada na Nidhamu ya Sakramenti za Kanisa.

Monsinyo Corrado Maggioni alizaliwa mwaka 1956 huko “Brembate di Sopra” Bergamo, Kaskazini mwa Italia. Tangu mwaka 1990 alianza kutoa huduma kwenye Baraza la Kipapa la Ibada na Nidhamu ya Sakramenti za Kanisa. Katika maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 2000 ya Ukristo aliteuliwa kuwa Mratibu wa Ofisi ya Liturujia, Kamati kuu ya Jubilei na hivyo akapangiwa dhamana ya kuratibu sala za jioni kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican. Tarehe 5 Novemba 2014 Baba Mtakatifu Francisko akamteuwa kuwa Katibu mkuu msaidizi wa Baraza la Kipapa la Ibada na Nidhamu ya Sakramenti za Kanisa. Ni mjumbe wa “Pontificia Accademia Mariana Internationale” ni Jaalimu wa Liturujia ya Kanisa kwenye Taasisi ya Kipapa ya Liturujia katika Chuo Kikuu cha Mtakatifu Anselmi, Roma na katika Kitivo cha Taalimungu Chuo Kikuu cha Marianum, kilichoko pia mjini Roma.

Makongamano
28 September 2021, 15:50