Papa Francisko: Kiini cha Katekesi ni Fumbo la Pasaka: Ekaristi!
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. –Vatican.
Katekisimu ya Kanisa Katoliki ni amana, urithi na utajiri wa imani; matunda ya Mafundisho ya kina kutoka kwa Mababa wa Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican. Hiki ni chombo mahususi cha kusaidia mchakato wa uinjilishaji wa kina; ukuaji na ushuhuda wa imani kwa Kristo Yesu na Kanisa lake. Ni chachu ya utakatifu wa maisha yenye mvuto na mashiko katika azma nzima ya uinjilishaji mpya unaofumbatwa katika ushuhuda wa maisha. Katekisimu ambayo ni muhtasari wa Imani ya Kanisa katika Fumbo la Utatu Mtakatifu, Kanisa na Mambo ya nyakati. Ni muhtasari wa adhimisho la Fumbo la Pasaka katika Sakramenti za Kanisa, Sakramenti za Kristo, Sakramenti za wokovu, imani na uzima wa milele. Lengo la maadhimisho ya Sakramenti za Kanisa ni kumtukuza Mwenyezi Mungu na mwanadamu kutakatifuzwa. Katekisimu ni muhtasari wa dira na mwongozo wa Maisha ya Kikristo na Adili unaofumbatwa katika Amri kumi za Mungu zinazopaswa kumwilishwa katika uhalisia wa maisha: kwa kuonesha upendo kwa Mungu na jirani, kama mhutasari wa Mafundisho makuu ya Kristo Yesu. Katekisimu ni muhtasari wa Maisha ya Sala kama ilivyokuwa kwenye Agano la Kale na Sala kuu ya Baba Yetu kama ilivyofundishwa na Kristo Yesu kwa kubeba mafundisho mazito katika maisha na utume wake.
Hii ni kazi iliyovaliwa njuga na Mtakatifu Yohane Paulo II kama chombo muhimu sana cha maisha na utume wa Kanisa katika kukabiliana na changamoto mamboleo. Ni katika muktadha huu, Baba Mtakatifu Francisko, Ijumaa tarehe 17 Septemba 2021 amekutana na kuzungumza na Wakurugenzi wa Tume za Katekesi kutoka kwa Mabaraza ya Maaskofu Katoliki Barani Ulaya ili kushirikishana uzoefu na mang’amuzi mintarafu Saraka Mpya ya Katekesi iliyozinduliwa Mwaka 2020. Baba Mtakatifu Francisko anasema, Katekesi inachota amana na utajiri wake katika maadhimisho ya Fumbo la Ekaristi Takatifu, kama ilivyokuwa katika Maadhimisho ya Kongamano la 52 la Ekaristi Takatifu Kimataifa yaliyonogeshwa na kauli mbiu “Visima vyangu vyote vimo kwako” Zab. 87:7, huko Jimbo kuu la Esztergom-Budapest, nchini Hungaria. Ni katika muktadha huu, Katekesi inakuwa ni chombo madhubuti cha uinjilishaji, ikiwa kama inajikita zaidi katika maadhimisho ya Fumbo la Ekaristi Takatifu. Hapa ni mahali muafaka pa uinjilishaji wa kina unaogusa mahitaji ya mtu mzima: kiroho na kimwili; mahali ambapo waamini wanakutana pamoja kushuhuda uwepo angavu na endelevu wa Mungu katika maisha yao!
Karamu ya Mwisho ilikuwa ni maandalizi ya maadhimisho ya Fumbo la Pasaka, yaani: mateso, kifo na ufufuko wake kwa wafu. Katekesi ni safari inayopata hitimisho lake katika maadhimisho ya Fumbo la Imani, baada ya kukutana na watu katika maeneo yao. Katekesi ni ushirikishanaji wa uzoefu na mang’amuzi ya Fumbo la imani kati ya waamini katika maisha na mahali pao pa kazi. Hii ni fursa ya kukutana na Kristo Yesu katika hija ya maisha yao, kwani wanaitwa na kutumwa kama wamisionari mitume. Kiini cha Katekesi ni Kristo Yesu aliyeteswa, akafa na kufufuka kwa wafu; Kristo Yesu anawapenda wafuasi wake upeo na kamwe hawezi kuwageuzia kisogo na kuwaacha pweke! Ni katika hali na mazingira haya, Baba Mtakatifu Francisko amenzisha “Utume wa Katekista.” Kimsingi, Makatekista wanaitwa kuwa ni wataalamu na wahudumu wa jumuiya ya waamini katika kutangaza, kushuhudia na kurithisha imani katika hatua mbalimbali za maisha ya waamini. Hatua ya kwanza ni kutangaza Injili, “Kerygma”, kufundisha maisha mapya katika Kristo Yesu sanjari na kuwandaa waamini kwa ajili ya kupokea Sakramenti za Kanisa na hatimaye, kuendelea na majiundo endelevu ili kila mwamini aweze kuwa tayari siku zote kumjibu kila mtu anayemuuliza habari za tumaini lililo ndani mwake; lakini kwa upole na kwa hofu. Rej. 1Pet.3:15. Makatekista wanapaswa kuwa ni mashuhuda wa imani, waalimu, wandani wa imani na walimu wanaofundisha kwa niaba ya Kanisa.
Yote haya yanaweza kutekelezwa kwa njia ya sala, masomo na ushiriki wa moja kwa moja katika maisha ya jumuiya yanayoweza kukuza utambulisho na uwajibikaji wake wote. Makatekista wawe ni mashuhuda na vyombo vya huruma na upendo wa Mungu; kwa njia ya ukarimu na ujirani mwema unaowawezesha kuonja kwa undani zaidi amana na utajiri wa Neno la Mungu, ili hatimaye, kuadhimisha vyema Fumbo la Ekaristi Takatifu linalowajalia waamini wote matunda mema. Watakatifu ambao wamejitambulisha kuwa ni wainjilishaji wakuu, wameonesha kipaji cha ubunifu kwa kutangaza na kushuhudia Injili ambayo imetamadunishwa katika hali, maisha na vipaumbele vya watu wa Mungu. Kwa hakika watakatifu hawa wametangaza Injili na kushuhudia utamadunisho wa imani. Ili kuweza kufikia katika hatua hii, kuna haja ya kujenga utamaduni wa kusikiliza kwa makini: historia na tamaduni za watu. Kristo Yesu, Neno wa Mungu ni Injili hai, amana na utajiri kwa watu wa Mungu Barani Ulaya. Huu ni mwaliko wa kuendelea kutoa kipaumbele cha pekee kwa Katekesi hai, inayogusa akili, nyoyo na maisha ya watu wa Mungu. Kipaji cha ubunifu kipewe msukumo wa pekee sanjari na kujiachilia chini ya maongozi ya Roho Mtakatifu. Baba Mtakatifu anawapongeza Makatekista wote wanaoendelea kujisadaka kwa ajili ya mafundisho kwa watoto na vijana wanaojiandaa kupokea Sakramenti mbalimbali za Kanisa.