Tafuta

Chama Cha Kitume Kimataifa cha "Foi et Lumière International" kinaadhimisha Jubilei ya Miaka 50 tangu kuanzishwa kwake kunako mwaka 1971. Chama Cha Kitume Kimataifa cha "Foi et Lumière International" kinaadhimisha Jubilei ya Miaka 50 tangu kuanzishwa kwake kunako mwaka 1971. 

Jubilei ya Miaka 50 ya Chama cha "Foi et Lumière: Huduma Afya ya Akili

Sherehe ya Pasaka ya Bwana ya Mwaka 1971 mjini Lourdes, Chama cha Kitume cha Kimataifa cha “Foi et Lumière” kikaanzishwa kwa ajili ya huduma ya wagonjwa wa afya ya akili pamoja na ndugu, jamaa na marafiki zao. Chama hiki kikawa ni chemchemi ya furaha, upatanisho, umoja na mshikamano wa udugu wa kibinadamu. Chama hiki kimetoa matumaini kwa watu wengi duniani.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. –Vatican. 

Maadhimisho ya Jubilei ni kipindi muafaka cha neema na baraka ili kutambua na kukiri neema ambazo Mwenyezi Mungu amewakirimiwa waja wake katika kipindi cha Miaka 50 ya maisha na utume wa Chama cha Kitume cha “Foi et Lumière” kutoka Ufaransa. Hii ni fursa ya kuangalia yajayo kwa imani na matumaini sanjari na kujiaminisha katika maongozi ya Roho Mtakatifu, ili kuendelea kuzaa matunda yanayolisaidia Kanisa katika maisha na utume wake. Ilikuwa ni katika maadhimisho ya Sherehe ya Pasaka ya Bwana ya Mwaka 1971 mjini Lourdes, Chama cha Kitume cha Kimataifa cha “Foi et Lumière” kikaanzishwa kwa ajili ya huduma ya wagonjwa wa afya ya akili pamoja na ndugu, jamaa na marafiki zao. Chama hiki kikawa ni chemchemi ya furaha, upatanisho, umoja na mshikamano wa udugu wa kibinadamu. Chama hiki kimetoa matumaini kwa watu wengi waliokuwa wamekata na kujikatia tamaa, kwa sababu ya kukataliwa na jamii na hata wakati mwingine na Kanisa lenyewe!

Huu ukawa ni mwanzo wa kuzaliwa kwa vyama vyenye mwelekeo wa huduma kwa wagonjwa wa afya ya akili sehemu mbalimbali za dunia. Daima ujumbe wao umekuwa ni upendo na ukarimu, kiini cha Habari Njema ya Wokovu kwa maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii. Hii ndiyo Injili ya upendo inayosimikwa katika fadhila ya unyenyekevu, imani na matumaini thabiti! “Maana, ndugu zangu, angalieni mwito wenu, ya kwamba si wengi wenye hekima ya mwilini, si wengi wenye nguvu, si wengi wenye cheo walioitwa; bali Mungu aliyachagua mambo mapumbavu ya dunia awaaibishe wenye hekima; tena Mungu alivichagua vitu dhaifu vya dunia ili aviaibishe vyenye nguvu; tena Mungu alivichagua vitu vinyonge vya dunia na vilivyodharauliwa, naam, vitu ambavyo haviko, ili avibatilishe vile vilivyoko; mwenye mwili awaye yote asije akajisifu mbele za Mungu.” I Kor 1:26-29. Hayo yamesemwa na Baba Mtakatifu Francisko, Jumamosi tarehe 2 Oktoba 2021 alipokutana na wawakilishi wa Chama cha Kitume cha Kimataifa cha “Foi et Lumière” kutoka Ufaransa.

Chama hiki anasema Baba Mtakatifu ni ushuhuda wa kinabii kwa ajili ya huduma kwa maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii hata katika ulimwengu mamboleo. Ikumbukwe kwamba, tofauti msingi kati ya watu ni amana na utajiri na wala isiwe ni sababu ya kuwadharau, kuwanyanyasa na kuwatenga watu wengine ndani ya jamii. Chama hiki ni kielelezo cha huduma ya kiekumene inayosimikwa katika huduma ya umoja na upendo wa udugu wa kibinadamu, chemchemi ya mchakato wa upatanisho na mwaliko wa toba na wongofu wa ndani. Miaka 50 si haba, lakini, Kanisa bado linahitaji huduma hii kwa maskini, kumbe, kuna haja ya kuhakikisha kwamba, Jumuiya zao zinakuwa ni mahali pa watu kuonja ukarimu, kumwendeleza mwanadamu na kufurahia maisha. Kwa wazazi wenye watoto wenye mtindio wa ubongo na matatizo ya afya akili, wawe ni alama ya matumaini badala ya wazazi hawa kujifungia katika undani wao kutokana na simanzi na msongo wa mawazo. Baba Mtakatifu ametumia fursa hii kuwahamasisha Wakristo sehemu mbalimbali za dunia kuwa ni chumvi na mwanga wa mataifa, kwa kutoa kipaumbele cha kwanza kwa maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii.

Wakristo wajenge utamaduni wa upendo, mshikamano na urafiki, ili kukuza na kudumisha mchakato wa upatanisho na amani, hususan kwenye maeneo ambayo yana vita, kinzani na mipasuko ya kijamii. Mababa wa Kanisa tangu mwanzo kabisa wa tafakari zao, wameliona Kanisa kuwa kama ni mashua inayosafiri ili kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu kwa watu wa Mataifa kwa kutambua kwamba, Kanisa kimsingi ni Sakramenti ya wokovu. Ndani ya mashua kuna Mitume wenye uzoefu na mang'amuzi ya mapungufu yao ya kibinadamu, wasi wasi na mashaka, lakini kwa pamoja wanajisikia wamoja katika imani wakimzunguka Yesu Kristo. Katika maisha na utume, Kanisa limejikuta lilikabiliana na mawimbi mazito, kiasi hata cha baadhi ya waamini kudhani kwamba, Kristo Yesu, ameuchapa usingizi na kamwe hajali kile kinachoendelea ndani na nje ya Kanisa. Bila kushikamana na kuandamana na Kristo Yesu katika hija ya maisha ya kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu, wafuasi wa Wakristo watajisikia wapweke, waoga na wenye wasiwasi mkubwa. Na kwa nguvu zao wenyewe, hawawezi kufua dafu! Wanapokumbuka kwamba, Kristo Yesu yuko pamoja nao, wakimwita anaitikia na kuwaokoa. Huu ndio uzoefu na mang’amuzi yaliyojitokeza tangu kuibuka kwa janga la Ugonjwa wa Virusi vya Korona, UVIKO-19. Huu ni wakati wa kujikita katika imani na matumaini, ili kushinda wasi wasi na woga unaotanda katika maisha ya watu wengi duniani.

Papa Jubilei 50
02 October 2021, 17:01