Tafuta

Matembezi ya Amani Assisi, Perugia, Italia: 1961-2021: I Care! Ninajali ni jina jipya la amani. Matembezi ya Amani Assisi, Perugia, Italia: 1961-2021: I Care! Ninajali ni jina jipya la amani. 

Matembezi ya Amani Assisi: 1961-2021: Utamaduni wa Amani Duniani

Matembezi ya Amani Assisi: Kwa muda wa siku tatu yaani kuanzia tarehe 8-10 Oktoba 2021 vijana zaidi ya 30, 000 wametembea umbali wa kilometa 24, huku wakiongozwa na kauli mbiu “I Care” yaani “Najali, Najali ni jina jipya la amani.” Najali na kushiriki katika mchakato wa utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote! Najali kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya vijana wpte!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Matembezi ya Amani Assisi, Perugia, Italia kwa mara ya kwanza yalianzishwa na Aldo Capitini (1961-2021) na mwaka 2021 yanatimiza miaka 60. Kwa muda wa siku tatu yaani kuanzia tarehe 8-10 Oktoba 2021 vijana zaidi ya 30, 000 wametembea umbali wa kilometa 24, huku wakiongozwa na kauli mbiu “I Care” yaani “Najali, Najali ni jina jipya la amani.” Najali na kushiriki katika mchakato wa utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote! Najali kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya vijana wa kizazi kipya! Najali ili kukoleza mchakato wa demokrasia shirikishi, na amani ya kweli! Sehemu kubwa ya washiriki wa matembezi haya ni vijana wa kizazi kipya wanaotaka kusimama kidete kulinda na kudumisha: utu, heshima na haki msingi za binadamu! Amani, usawa, demokrasia na udugu wa kibinadamu, ni tunu ambazo zinashambuliwa kila pembe ya dunia kama “mpira wa danadana.”

Ujumbe wa Baba Mtakatifu Francisko umesomwa kwa niaba yake na Askofu mkuu Domenico Sorrentino wa Jimbo kuu la Assisi-Nocera Umbra-Gualdo Tadino. Baba Mtakatifu katika ujumbe huu, amekazia umuhimu wa kulinda na kutunza mazingira nyumba ya wote, udugu wa kibinadamu na ujenzi wa utamaduni wa amani. Ujumbe wa Baba Mtakatifu Francisko katika maadhimisho ya Siku ya 54 ya Kuombea Amani Duniani kwa Mwaka 2021 ulinogeshwa na kauli mbiu “Utamaduni wa Utunzaji Kama Njia ya Amani”. Katika ujumbe huu, Baba Mtakatifu alizungumzia kuhusu madhara ya Ugonjwa wa Virusi vya Korona, UVIKO-19, majanga asilia, ukosefu wa uhakika wa usalama wa chakula duniani, hali ngumu ya uchumi kitaifa na kimataifa pamoja na wimbi kubwa la wakimbizi na wahamiaji duniani. Katika kipindi hiki kumeibuka pia utaifa usiokuwa na mashiko; chuki dhidi ya wageni, vita na kinzani mambo ambayo yanapelekea maafa na uharibifu mkubwa wa mazingira nyumba ya wote. Kumbe, utamaduni wa utunzaji bora wa mazingira ni dira na mwelekeo katika njia ya amani. Mungu Muumbaji ni kiini cha wito wa mwanadamu kutunza mazingira kama unavyofafanuliwa katika Maandiko Mtakatifu, yaani ulinzi wa Mungu kwa binadamu.

Kuna uhusiano na mwilingiliano mkubwa kati ya maisha na mafungamano ya kibinadamu pamoja na mazingira. Haya ni mambo ambayo kimsingi hayawezi kamwe kutenganishwa na udugu wa kibinadamu, haki na uaminifu kwa wengine. Baba Mtakatifu anakaza kusema, kuna tofauti kubwa kati ya utunzaji bora wa mazingira dhidi ya utandawazi usiojali wala kuguswa na mahangaiko ya wengine. Tabia ya kuvunjilia mbali utu, heshima na haki msingi za binadamu ni msingi wa uvunjifu wa amani na mwanzo wa utamaduni wa kifo unaokumbatiwa katika: kinzani, machafuko na vita! Inasikitisha kuona kwamba, hata baada ya mapigano na madhara yaliyosababishwa na Vita Kuu ya Kwanza na ya Pili ya Dunia, lakini bado kuna Mataifa yanayoendelea kuwekeza kiasi kikubwa cha rasilimali fedha kwa ajili ya kutengeneza silaha. Ni hao hao viongozi wa Serikali na Jumuiya ya Kimataifa wanaotangaza amani kwenye mikutano ya Kimataifa, lakini, wanajihusisha katika biashara haramu ya silaha duniani. Hii ni biashara inayowapa kisogo mamilioni ya watu wanaokosa mahitaji msingi na hivyo kubeza utu, heshima na haki msingi za binadamu.

Ni katika muktadha huu, Baba Mtakatifu anawahimiza vijana na watu wote wenye mapenzi mema kutia nia ya kutembea katika njia ya amani, ili kujenga utamaduni wa amani unaomwilishwa kila siku ya maisha na wala si mara moja tu kwa mwaka. Kwa msaada wa Mwenyezi Mungu, Baba anayewategemeza na kuwalinda watoto wake wote, watu wanaweza kujifunza kuishi kwa umoja na upendo kama ndugu! Kwa upande wake, Rais Sergio Mattarella wa Italia anasema, amani ni dhamana na wajibu unaopaswa kushughulikiwa kikamilifu na watu wote kwa kuwa na matumizi mazuri ya lugha sanjari na kuonesha mshikamano wa udugu wa kibinadamu. Hii ni changamoto ya kulinda, kuheshimu na kuendeleza mazingira nyumba ya wote. Matembezi ya Amani Assisi ni kielelezo cha matumaini ya watu wa Mungu katika utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote sanjari na uwajibikaji mkubwa! Mshikamano wa udugu wa kibinadamu, utu, heshima, haki msingi za binadamu; uhuru, demokrasia na amani ni urithi wa binadamu unaopaswa kutambuliwa na Umoja wa Mataifa!

Matembezi ya Amani

 

11 October 2021, 15:16