Wanaharakati wa vyama vya kiraia wako mstari wa mbele katika kupigania ujenzi wa msingi wa haki jamii ulimwenguni. Wanaharakati wa vyama vya kiraia wako mstari wa mbele katika kupigania ujenzi wa msingi wa haki jamii ulimwenguni. 

Mchango wa Vyama Vya Kiraia Katika Kudumisha Haki Jamii, Utu, Ubinadamu na Udugu

Papa Francisko anawasihi viongozi wakuu wa Jumuiya ya Kimataifa kufuta deni la nje kutoka katika nchi changa duniani; kutekeleza kwa vitendo rufuku ya kutengeneza, kulimbikiza na kutumia silaha za maangamizi. Ni wakati wa kuondoa vikwazo vyote vya kiuchumi. Hati miliki kuhusu dawa ya chanjo dhidi ya Ugonjwa wa UVIKO-19, iondolewe ili kuokoa maisha ya watu wengi duniani.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Wanaharakati wa vyama vya kiraia (Asasi za Kiraia, AZAKI) wanatambulikana kama vyombo vya mabadiliko ya kijamii na wameendelea kujipambanua kuwa ni Mitume wa mabadiliko ya kijamii kwani wao ni wale watu ambao wanatambua mateso na mahangaiko ya watu wanaonyimwa haki zao msingi. Wanaharakati wa vyama kiraia katika mikutano yao ambayo Jumamosi tarehe 16 Oktoba 2021 imeingia katika awamu ya nne, wamekuwa wakidai kwa namna ya pekee kabisa: Ardhi, Makazi na Ajira (Terra, Domus & Labor) Hizi ni haki takatifu kwa watu wote bila ubaguzi kama zilivyofafanuliwa na wajumbe hawa walipokutana na kuzungumza na Papa Francisko mjini Vatican kati ya Mwaka 2014, 2016 na wakati wa hija ya kitume nchini Bolivia kunako mwaka 2015. Wanaharakati wa vyama vya kiraia wamekuwa mstari wa mbele kutetea haki msingi, utu na heshima ya binadamu kwa kukazia kwamba, umilikaji wa ardhi, makazi bora na fursa za ajira ni mambo msingi katika Mamlaka Matakatifu ya Ufundishaji katika Kanisa, yaani “Magisterium” yanayopata chimbuko lake kutoka katika Maandiko Matakatifu na Mapokeo ya Kanisa. Ardhi, Makazi na Ajira ni vigezo msingi vya haki jamii. Mikutano hii, imekuwa ni jukwaa linalowakutanisha watu kutoka katika medani mbalimbali za maisha ya binadamu kama sehemu ya mchakato wa ujenzi wa mshikamano na udugu wa kibinadamu.

Katika kipindi cha miaka saba, maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii wamekuwa wakipata nafasi ya kukutana na kuzungumza na Papa Francisko, ili kuwasilisha kilio chao! Hawa ni waathirika wakuu wa mfumo tenge wa uchumi kitaifa na kimataifa, unaopelekea baadhi ya watu kutengwa katika mchakato wa maendeleo fungamani ya jamii yanayojikita katika kukidhi mahitaji msingi ya binadamu! Wakati maambukizi ya Ugonjwa wa Virusi vya Korona, UVIKO-19 yalipokuwa yamepamba moto, walijadili na sasa wanaharakati hawa Jumamosi tarehe 16 Oktoba 2021 Waraka unaojulikana kama “Save Humanity and the Planet” yaani: “Okoa Ubinadamu na Sayari”. Baba Mtakatifu Francisko katika ujumbe wake kwenye mkutano huu wa Kimataifa kwa njia ya video anawasihi viongozi wakuu wa Jumuiya ya Kimataifa kufuta deni la nje kutoka katika nchi changa zaidi ulimwenguni; kutekeleza kwa vitendo rufuku ya kutengeneza, kulimbikiza na kutumia silaha za maangamizi. Ni wakati kwa Jumuiya ya Kimataifa kuangalia uwezekano wa kuondoa vikwazo vyote vya kiuchumi ambavyo, vimekuwa ni mzigo mkubwa kwa maskini sehemu mbalimbali za dunia. Jumuiya ya Kimataifa iangalie uwezekano wa kuondoa hati miliki kuhusu dawa ya chanjo dhidi ya Ugonjwa wa Virusi vya Korona, UVIKO-19, ili watu wengi zaidi waweze kupata chanjo hii, ili kuokoa maisha ya watu yanayoendelea kuputika kila kukicha.

Ombi ambalo linapaswa kufanyiwa kazi kwa haraka iwezekanavyo ni kuweka kiwango cha kima cha chini cha mshahara kwa wafanyakazi pamoja na kupunguza siku za kazi kwa wafanyakazi. Baba Mtakatifu anasema, wanaharakati wa vyama vya kiraia ni wasanii wa kijamii wanaosimama kidete na kwa ujasiri ili kuwajengea maskini matumaini kwa leo na kesho iliyo bora sanjari na kusimama kidete kulinda, kutunza na kutetea utu, heshima na haki zao msingi. Kamwe walimwengu hawawezi kujenga leo na kesho iliyo bora zaidi kwa kujikita katika upendeleo, utandawazi usiojali wala kuguswa na mahangaiko ya watu wengine; kwa kuendelea kuwanyonya na kuwadhalilisha watu. Ugonjwa wa Virusi vya Korona, UVIKO-19 umesababisha madhara makubwa katika maisha ya watu wengi duniani. Kwa nchi zile ambazo zimesikiliza na kutekeleza ushauri wa wanasayansi, zimefanikiwa kudhibiti maambukizi ya UVIKO-19 kwa kutambua kwamba, afya ni sehemu ya haki msingi za binadamu, ustawi na mafao ya wengi. Lakini watu wengi katika Nchi maskini zaidi wamefariki na wanaendelea kufariki kutokana na UVIKO-19; wametumbukia katika ukosefu wa fursa za ajira na hatimaye, umaskini.

Vijana wengi wamekumbwa na ugonjwa wa sonona na kwamba, kumekuwepo na ongezeko kubwa la watu wanaopekenywa kwa baa la njaa na utapiamlo wa kutisha duniani. Jumuiya ya Kimataifa isipochukua hatua makini, watu wanaofariki dunia kwa wakati huu kutokana na baa la njaa na utapiamlo wa kutisha wanaweza kuongeza maradufu. Takwimu kutoka Siria, Haiti, DRC, Senegal, Yemen na Sudan ya Kusini zinatisha sana. Umaskini na baa la njaa limeongezeka hata miongoni mwa nchi tajiri zaidi duniani. Huu ni wakati wa kusikiliza na kujibu kilio cha Dunia Mama na Maskini, kwa kuonesha upendo,  umoja na mshikamano wa udugu wa kibinadamu! Huu ni wakati muafaka wa kufanya mabadiliko katika sera na mikakati ya mfumo wa uchumi Kimataifa. Ni wakati wa kutafakari, kung’amua na kuchagua, kwani mfumo wa uchumi kimataifa umekuwa ni kielelezo cha dhambi jamii. Baba Mtakatifu anawaalika wakuu wa Jumuiya ya Kimataifa, Mashirika na Taasisi za Kimataifa, kuhakikisha kwamba, nchi changa duniani zinapata mahitaji yake msingi na chanjo dhidi ya UVIKO-19. Ni wakati wa kulinda na kutunza mazingira nyumba ya wote, kwa kuboresha mfumo wa uzalishaji na ugavi wa chakula duniani, ili watu wengi zaidi waweze kupata lishe bora kwa bei nafuu.

Ni wakati muafaka kwa watengenezaji, wauzaji na wasambazaji wa silaha zinazoendelea kusabisha vita, mipasuko ya kijamii na maafa kuacha mara moja. Ni wakati wa kuwekeza katika teknolojia rafiki kwa mazingira, kwa kuwawezesha hata watoto wa maskini kuweza kupata elimu, ujuzi na maarifa kwa njia teknolojia kubwa ya mawasiliano sanjari na ujenzi wa mshikamano na udugu wa kibinadamu. Ni muda wa kuondoa vikwazo vya kiuchumi duniani kote! Waachane na ukoloni wa kiitikadi na ukoloni mamboleo. Umoja wa Mataifa unapaswa kuheshimiwa kama chombo muafaka cha kusitisha vita. Kumekuwepo na mtindo wa baadhi ya nchi kuvamia nchi nyingine kwa kisingizio cha usalama! Baba Mtakatifu anawaalika viongozi wa kisiasa na kidini, kuwasaidia wananchi wanaotafuta: ardhi, makazi na kazi kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wao. Dini kamwe zisitumike kuchochea vita, vurugu na mipasuko ya kidini, bali madaraja ya kuwakutanisha watu kwa upendo. Ni wakati wa kutangaza na kumwilisha Injili ya Msamaria mwema kwa kuguswa na mahitaji msingi ya jirani zao. Lengo ni kujenga na kuimarisha haki jamii dhidi ya ubaguzi wa rangi na nyanyaso mbalimbali, ili kuwaganga kwa mafuta ya faraja wale waliovunjika na kupondeka moyo kwa kuwanywesha divai ya matumaini.

Baba Mtakatifu Francisko anasema, umilikaji wa ardhi, makazi bora na fursa za ajira ni mambo msingi katika Mamlaka Matakatifu ya Ufundishaji katika Kanisa, yaani “Magisterium” yanayopata chimbuko lake kutoka katika Maandiko Matakatifu na Mapokeo ya Kanisa. Mkusanyiko wa Mafundisho Jamii ya Kanisa ni mchango mkubwa uliotolewa na Mtakatifu Yohane Paulo II katika maisha na utume wake kama Khalifa wa Mtakatifu Petro. Yote haya ni kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya watu wote wa Mungu katika ujumla wao. Kuna haja kwa Jumuiya ya Kimataifa kuweka kiwango cha kima cha chini cha mshahara pamoja na kupunguza siku za kazi. Lengo ni kuwawezesha watu wengi zaidi kupata fursa za ajira. Mwelekeo wa sasa ni kwamba, kuna watu wengi wasiokuwa na fursa za ajira na wachache ndio tu waliobahatika. Mwishoni mwa ujumbe wake, Baba Mtakatifu Francisko anawaalika viongozi wakuu wa Jumuiya ya Kimataifa kusikiliza na kujibu kilio cha maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii. Hawa ndio waathirika wa mifumo tenge ya uchumi, ubaguzi na ukosefu wa usawa. Ni watu ambao wanateseka kutokana na matumizi mabaya ya madaraka pamoja na chuki dhidi ya wahamiaji na wageni. Watu wajenge utamaduni wa kusikiliza na kuwasaidia wengine, ili kwa pamoja, waweze kufanya safari ya matumaini!

Vyama vya kiraia

 

16 October 2021, 15:40