Kauli Mbiu ya Siku ya 55 ya Kuombea Amani Duniani Jan. 2022
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.
Baba Mtakatifu Francisko anasema elimu maana yake ni mchakato unaowajengea wanafunzi matumaini ya kuondokana na ubinafsi wao; kwa kutambua, kuheshimu na kuthamini tofauti msingi zinazojitokeza, ili hatimaye kujenga na kudumisha: utamaduni wa ukarimu, mshikamano, mafungamano na hofu ya Mungu. Upyaisho wa mfumo wa elimu katika ulimwengu mamboleo utawasaidia watu wa Mungu kupambana na changamoto zinazojitokeza kwa wakati huu, ili kujenga leo na kesho yenye matumaini. Elimu ni upendo unaowajibisha na kurithishwa kutoka kizazi kimoja hadi kingine, ili kuondokana na ubinafsi unaopelekea watu kutokuthaminiana. Kuna haja ya kujenga umoja na mshikamano unaosimikwa katika kipaji cha kusikiliza, kujadiliana na maelewano.
Baba Mtakatifu Francisko ameridhia kwamba, Maadhimisho ya Siku ya 55 ya Kuombea Amani Duniani kwa Mwaka 2022 yanogeshwe na kauli mbiu “Elimu, Kazi Na Majadiliano Kati ya Vizazi: Chombo cha Ujenzi wa Amani ya Kudumu.” Baba Mtakatifu anatoa kipaumbele kwa mambo makuu matatu, ili kuwasaidia watu wa Mungu kuwa na usomaji wa kibunifu unaojibu mahitaji ya nyakati hizi, ili kujielekeza zaidi katika siku za usoni, kwa kuwaalika watu wote kusoma alama za nyakati kwa jicho la imani, ili kwamba, maelekeo ya mabadiliko yote hayo yasaidie kuamsha maswali mapya na yale zamani ili yaweze kuchambuliwa kwa pamoja. Je, ni kwa njia zipi elimu inaweza kuchangia ujenzi wa amani ya kudumu? Je, Kazi ulimwenguni, inakidhi mahitaji msingi ya binadamu katika haki na ukweli? Je, vijana wa kizazi kipya na wazee wanaonesha mshikamano kati yao? Je, wanayo matumaini ya leo na kesho iliyo bora zaidi? Je, Serikali za kijamii zimefanikiwa kuweka mwelekeo huu katika muktadha wake unaopania kudumisha amani na utulivu?