Tafuta

Misingi ya Mafundisho Jamii ya Kanisa inafumbatwa katika: Utu, heshima na haki msingi za binadamu aliyeumbwa kwa sura na mfano wa Mungu. Misingi ya Mafundisho Jamii ya Kanisa inafumbatwa katika: Utu, heshima na haki msingi za binadamu aliyeumbwa kwa sura na mfano wa Mungu. 

Misingi ya Mafundisho Jamii ya Kanisa: Utu, Heshima na Haki Msingi

Mafundisho Jamii ya Kanisa yanachota amana na utajiri wake kutoka katika Biblia na Mapokeo ya Kanisa na imani thabiti inayomwilisha Neno la Mungu katika matendo, kielelezo cha imani tendaji. Mambo msingi katika mchakato wa kudumisha haki msingi za binadamu: Amani katika ukweli, haki, upendo na uhuru. Hizi ni tunu ambazo ni urithi mkubwa kwa binadamu wote, zilindwe

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Mafundisho Jamii ya Kanisa yanapata chimbuko lake mintarafu kanuni na muundo wa elimu fahamu, taalimungu, hususan taalimungu maadili ambayo ni dira na mwongozo wa maisha ya watu. Yanachota amana na utajiri wake kutoka katika Maandiko Matakatifu na Mapokeo ya Kanisa na imani thabiti ambayo inamwilisha Neno la Mungu katika matendo, kielelezo cha imani tendaji. Mambo msingi katika mchakato wa kudumisha haki msingi za binadamu: Amani katika ukweli, haki, upendo na uhuru. Hizi ni tunu ambazo ni urithi mkubwa kwa binadamu wote kwani zinabubujika kutoka katika asili ya binadamu aliyeumbwa kwa sura na mfano wa Mungu hivyo zinapaswa kulindwa, kutetewa na kuheshimiwa na wote; kwa kuzingatia kwamba, haki inakwenda sanjari na wajibu; hakuna haki pasi na wajibu. Hii ni haki ya kuishi, kupata huduma bora ya makazi, afya, elimu, kuabudu, uhuru wa dhamiri, uhuru wa kuchagua mfumo wa maisha; haki za kiuchumi na kisiasa pamoja na uhuru wa kwenda unakotaka kwa kuzingatia sheria na kanuni zilizopo. Kanisa Katoliki lina amana na utajiri mkubwa wa Mafundisho Jamii ya Kanisa yanayopata chimbuko lake katika Waraka wa Kichungaji wa Baba Mtakatifu Leo XIII; Mambo Mapya; Rerum Novarum.

Mtakatifu Yohane Paulo wa Pili, katika Waraka wake kuhusu Masuala ya Kijamii Centesimus Annus, alifafanua kwa kina kuhusu asili ya haki msingi za binadamu; umuhimu wa kukuza na kudumisha upendo na mshikamano miongoni mwa Jumuiya ya Kimataifa, kama inavyojidhihirisha katika Waraka wake wa “Sollicitudo Rei Socialis” cheche ya uanzishaji wa vyama vya kitume kijamii vilivyokuwa vinapania kulinda na kutetea uhuru, utu na haki msingi za binadamu. Itakumbukwa kwamba, uhuru wa kidini na uhuru wa kuabudu ni muhtasari wa haki zote za binadamu. Dini zisaidie kujenga amani, upendo na mshikamano wa udugu wa kibinadamu na kamwe zisiwe ni chanzo cha vurugu, kinzani na vita. Kanuni maadili na utu wema ni sehemu muhimu sana katika maisha ya mwanadamu zinazopaswa kuheshimiwa ili amani na utulivu viweze kushika kasi, bila kusahau nafasi na dhamana ya uwepo wa Mungu katika maisha ya mwanadamu. Waamini wanapaswa kufahamu vyema kweli za imani yao ili wasiyumbishwe, bali wasimame kidete kuilinda na kuitetea kwa ajili ya ustawi, mafao ya maendeleo ya wengi.

Ni katika muktadha huu, Baba Mtakakatifu Francisko katika ujumbe ulioandikwa kwa niaba yake na Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican kwenda Dominique Quinio Mratibu wa Masuala Jamii, Baraza la Maaskofu Katoliki Ufaransa, anapenda kuwatia shime katika maadhimisho haya ya Majuma ya Kijamii Ufaransa Semaines Sociales de France” SSF “French Social Weeks.” Maadhimisho haya yalianzishwa kunako mwaka 1904 ili kutoa nafasi kwa Mama Kanisa kupembua masuala mtambuka ya kijamii kwa ajili ya ustawi, mafao na maendeleo ya wengi. Maadhimisho ya Majuma ya Kijamii Ufaransa yanaadhimishwa kuanzia tarehe 26-28 Novemba 2021 na Baba Mtakatifu anasema, anashiriki pamoja nao kwa mawazo na sala. Kauli mbiu inayoongoza maadhimisho haya “Tuthubutu Kuota Yajayo Kwa Kutunza Watu na Mazingira.” Baba Mtakatifu anawataka wajumbe kuzama zaidi katika ukweli wa maisha, kwa kuota ndoto sanjari na kuhakikisha kwamba, ndoto hii inatekelezeka na kuwa ni sehemu ya ukweli wa maisha!

Jamii inapaswa kuwa na ndoto ya pamoja kwa ajili ya kulinda na kutetea haki msingi za wanyonge ndani ya jamii, ili utu, heshima na haki zao msingi ziweze kusikika, ili hatimaye, utu na uzuri wa binadamu viweze kung’aa zaidi na kuondokana na wivu usiokuwa na mvuto wala mashiko. Waamini waendelee kuota ndoto kwa jamii inayopokea Ujumbe wa Injili kwa kumtangaza na kumshuhudia Mwenyezi Mungu, chemchemi ya upendo usiokuwa na kifani; upendo ambao umeshuhudiwa na Kristo Yesu aliyeteswa, akafa na kufufuka kwa wafu na sasa anaishi. Kushirikishana mawazo na mang’amuzi ya maisha ni sehemu ya utamaduni wa watu kukutana. Baba Mtakatifu Francisko anasema, maambukizi makubwa ya Ugonjwa wa Virusi vya Korona, UVIKO-19 ni changamoto inayohitaji mabadiliko ya mtindo wa maisha, ili kuwa na matumaini kwa leo na kesho iliyo bora zaidi. Ni wajibu na dhamana ya Wakristo kutangaza na kushuhudia Injili ya matumaini, inayoleta shauku ya utimilifu na mafanikio katika maisha kwa kuambata mambo makubwa kama vile: Ukweli, wema, uzuri, haki na upendo.

Yote haya yawe ni kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi na yanayosaidia kuboresha maisha kwa kukazia utu, heshima na haki msingi za binadamu. Baba Mtakatifu Francisko mwishoni anawaombea wajumbe wote ili Mwenyezi Mungu aweze kufungua akili na nyoyo zao, ili waweze kubadilishana mawazo yao, ili kupandikiza mbegu ya matumaini inayohitajika sana katika ulimwengu mamboleo. Ni matumaini ya Baba Mtakatifu kwamba, watasimama kidete kulinda, kutetea na kudumisha mazingira bora nyumba ya wote sanjari na kuendelea kuwalinda, kuwatunza na kuwatetea maskini na wanyonge ndani ya jamii bila kusahau maendeleo fungamani ya binadamu: kiroho na kimwili. Mwishoni, Baba Mtakatifu anapenda kuyaweka mafanikio ya mkutano huu chini ya ulinzi na tunza ya Bikira Maria!

Mafundisho Jamii

 

27 November 2021, 15:02