Papa ametuma Salamu za rambi rambi kufuatia ajali ya mgodi wa makaa huko Siberia
Na Sr. Angella Rwezaula – Vatican.
Baba Mtakatifu Francisk, Jumamosi tarehe 27 Novemba 2021 ameonesha masikitiko yake kufuatia na ajali ya mlipuko, iliyotokea kwenye machimbo ya mgodi wa makaa Listvyazhnaya, katika eneo la madini ya Kuznetsk, huko Siberia ya Mashariki. Ajali hiyo imesababaisha vifo vya watu 52. Katika telegramu iliyosainiwa na Katibu wa Vatican, Kardinali Pietro Parolin, Baba Mtakatifu ametuma salamu zake za rambi rambi kwa Rais wa Shirikisho la Urusi Bwana, Vladimir Putin na watu wote wa Urusi. Papa anawakikishia maombi yake kwa wale wote ambao wamefariki dunia na kwa wale ambao wanaomboleza kupoteza wapendwa wao ikiwa ni pamoja na walionusurika. Kwa wale wote ambao wamehusika katika kutoa msaada, Baba Mtakatifu anawaombea ili wapate nguvu na amani ya Mungu mwenyezi.
Ajali ya mgodi wa makaa
Ajali ya lipuko katika mgodi wa makaa umetokea Ijumaa tarehe 26 Novemba 2021, karibu saa 2.30 asubuhi, wakati shimo refu la machimbo ya makaa kulikuwamo na watu 285. Mara moja walianza kutoa msaada wa kuokoa watu 239, miongoni mwake 49 wamejeruhia. Mamlaka ya Urusi imeanza uchunguzi wa kutafuta sababu na wahusika wa ajali hiyo. Hata hivyo wamemweka mbaloni Mkurugenzi wa machimbo, na Makamu Mkurugenzi Mkuu wa kitengo ambaye kwa mujibu wa uchunguzi wanadaiwa kukiuka mahitaji ya usalama wa viwandani yanayohitajika katika vifaa vya uzalishaji hatari. Wakati huo huo, ilitangazwa kuwa, kati ya waathirika wa ajali hiyo, 46 walikuwa wachimba migodi na 6 wa timu za uokoaji. Shughuli ya kuwatafuta walionusurika iliendelea, na mmoja wao aliokolewa saa kadhaa baada ya mlipuko huo.