Tafuta

Baba Mtakatifu amewashukuru watu wa Mungu kwa moyo wa ukarimu na upendo waliomwonesha wakati wa hija yake ya kitume nchini Ugiriki. Baba Mtakatifu amewashukuru watu wa Mungu kwa moyo wa ukarimu na upendo waliomwonesha wakati wa hija yake ya kitume nchini Ugiriki. 

Hija ya Kitume ya Papa Francisko Cyprus na Ugiriki: Ekaristi: Shukrani na Moyo wa Sadaka

Baba Mtakatifu Francisko anasema, “EUCARISTIA” (εὐχαριστία) ni neno la Kigiriki linalomaanisha “Shukrani”. Kumbe, kushukuru ni sehemu ya vinasaba vya imani na maisha ya Kanisa. Roho Mtakatifu katika maadhimisho ya Fumbo la Ekaristi Takatifu anatenda kwa niaba yao, ili kuwa ni watu wa shukrani kwa Mwenyezi Mungu na zawadi ya upendo kwa jirani zao. Moyo wa shukrani.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Askofu mkuu Theodoros Kontidis wa Jimbo kuu la Athene mara baada ya Baba Mtakatifu Francisko kuadhimisha Ibada ya Misa Takatifu kwenye Ukumbi mkubwa “Megaron Concert Hall”, Jumapili tarehe 5 Desemba 2021 wakati wa hija yake ya Kitume nchini Ugiriki kuanzia tarehe 4-6 Desemba 2021 amemshukuru na kumpongeza Baba Mtakatifu Francisko. Maadhimisho ya Ibada ya Sakramenti ya Ekaristi Takatifu ni kwa ajili ya utukufu wa Mungu na wokovu wa watu wote. Uwepo wa Baba Mtakatifu Francisko kati ya watu wa Mungu nchini Ugiriki, umewawezesha kujisikia kuwa ni sehemu ya washirika wa Fumbo la Mwili wa Kristo yaani Kanisa, walioenea sehemu mbalimbali za dunia. Kwa namna ya pekee, Jumapili tarehe 5 Desemba 2021, kwa uwepo wa Baba Mtakatifu Francisko wamejisikia kuwa ni sehemu ya ushirika wa Kanisa.

Askofu mkuu Theodoros Kontidis amemshukuru na kumpongeza Baba Mtakatifu Francisko kwa kuadhimisha Ibada ya Misa Takatifu pamoja na watu wa Mungu nchini Ugiriki. Amemshukuru na kumpongeza kwa maisha na utume wake kama Khalifa wa Mtakatifu Petro kwa ajili ya Kanisa na Ulimwengu katika ujumla wake. Mafundisho na wosia wake ni dira na mwongozo wa kumfuasa Kristo Yesu. Watu wa Mungu nchini Ugiriki, wamemhakikishia Baba Mtakatifu kwamba, wanamwombea na wataendelea kumwombea katika maisha na utume wake, ili aendelee kuwaongoza watu wa Mungu mintarafu njia ya Injili.

Baba Mtakatifu Francisko mara baada ya Misa Takatifu amewashukuru watu wa Mungu nchini Ugiriki kwa mapokezi na ukarimu wote waliomwonesha wakati wa hija yake ya kitume nchini mwao. “EUCARISTIA” (εὐχαριστία) ni neno la Kigiriki linalomaanisha “Shukrani”. Kumbe, kushukuru ni sehemu ya vinasaba vya imani na maisha ya Kanisa. Roho Mtakatifu katika maadhimisho ya Fumbo la Ekaristi Takatifu anatenda kwa niaba yao, ili kuwa ni watu wa shukrani kwa Mwenyezi Mungu na zawadi ya upendo kwa jirani zao. Baba Mtakatifu amewashukuru na kuwapongeza viongozi wa Serikali ya Ugiriki, Maaskofu na wale wote waliojisadaka usiku na mchana ili kuhakikisha kwamba, hija yake ya kitume inafanikiwa kama ilivyo pangwa.

Baba Mtakatifu amewashukuru wale wote walitolea muda wao kwa ajili ya kuombea hija yake ya kitume nchini Ugiriki. Baba Mtakatifu anasema, anahitimisha hija yake ya kitume, huku akiwabeba wote katika sakafu ya moyo wake, kwa kuwakumbuka na kuwaombea. Amewaomba hata wao kumkumbuka na kumwombea katika maisha na utume wake kama Khalifa wa Mtakatifu Petro. Takwimu zinaonesha kwamba, Ibada hii ya Misa Takatifu imehudhuriwa na watu zaidi ya elfu ishirini.

Askofu mkuu shukrani
06 December 2021, 15:24