Tafuta

Baba Mtakatifu Francisko akiwa njiani kurejea mjini Roma, tarehe 6 Desemba 2021 amepata fursa ya kujibu maswali kutoka kwa waandishi wa habari waliokuwemo kwenye msafara wake. Baba Mtakatifu Francisko akiwa njiani kurejea mjini Roma, tarehe 6 Desemba 2021 amepata fursa ya kujibu maswali kutoka kwa waandishi wa habari waliokuwemo kwenye msafara wake. 

Hija ya Kitume ya Papa Francisko Cyprus Na Ugiriki: Mahojiano Maalum!

Papa Francisko akiwa njiani kurejea mjini Vatican alipata nafasi ya “kuchonga” pamoja na waandishi wa habari waliokuwa kwenye msafara wake. Baba Mtakatifu amegusia kuhusu: Majadiliano ya kiekumene, Tamko la Umoja wa Ulaya kuhusu Noeli, Demokrasia wimbi kubwa la wakimbizi na wahamiaji pamoja na shutuma dhidi ya Askofu mstaafu Michel Aupetit wa Jimbo kuu la Paris.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Hija ya Kitume ya 35 ya Baba Mtakatifu Francisko Kimataifa nchini Cyprus kuanzia Alhamisi tarehe 2 hadi Jumamosi tarehe 4 Desemba 2021 imenogeshwa na kauli mbiu “Tufarijiane Katika Imani.” Kuanzia tarehe 4-6 Desemba 2021 ametembelea nchini Ugiriki, hija ambayo ilinogeshwa kwa kauli mbiu “Jiwekeni Wazi Kwa Mshangao wa Mungu.” Hii ni sehemu ya ujumbe wa Baba Mtakatifu Francisko kwa maadhimisho ya Siku ya 36 ya Vijana Ulimwenguni. Jumatatu tarehe 6 Desemba 2021 akiwa njiani kurejea mjini Vatican alipata nafasi ya “kuchonga” pamoja na waandishi wa habari waliokuwa kwenye msafara wake. Baba Mtakatifu amegusia kuhusu: Majadiliano ya kiekumene, Tamko la Umoja wa Ulaya kuhusu Noeli, Demokrasia shirikishi, wimbi kubwa la wakimbizi na wahamiaji pamoja na shutuma dhidi ya Askofu mstaafu Michel Aupetit wa Jimbo kuu la Paris, Ufaransa. Makanisa yanajiandaa kuadhimisha Jubilei ya Miaka 1, 700 tangu Mtaguso wa Nicea ulipoadhimishwa kunako mwaka 325 na kilele cha maadhimisho haya ni mwaka 2025, tukio la pekee na muhimu sana.

Mwaka huo Wakristo wote wataadhimisha Pasaka ya Bwana siku moja, matendo makuu ya Mungu kwa waja wake. Kanuni ya Imani ya Nicea-Constantinopoli ni formula rasmi ambayo ilipitishwa na Mababa wa Mtaguso wa Kwanza wa Nicea (325) ikakamilishwa na Mtaguso wa kwanza wa Konstantinopoli (381) ili kubainisha imani sahihi ya Kanisa Katoliki dhidi ya uzushi, hasa wa Ario na wafuasi wake. Katika mazingira hayo, lengo kuu lilikuwa kwanza kabisa ni kumkiri Kristo Yesu kama Mungu kweli sawa na Baba, halafu kwamba Roho Mtakatifu anastahili kuabudiwa pamoja na Baba na Mwana (Utatu Mtakatifu). Mwaka 2025 Makanisa yataadhimisha Jubilei ya Miaka 1, 700 tangu kuadhimishwa kwa Mtaguso wa Nicea. Umoja wa Kanisa ulikuwa hatarini na hivyo pia kutishia amani na usalama hata katika masuala ya kisiasa. Baba Mtakatifu Francisko akizungumzia kuhusu Majadiliano ya Kiekumene amesema Jumamosi jioni tarehe 4 Desemba 2021 alipata nafasi ya kumtembelea Askofu mkuu Ieronymos II wa Kanisa la Kiorthodox la Athene na Ugiriki nzima. Katika hotuba yake anasema, aliomba msamaha wa Mungu na kwa Kanisa la Kiorthodox kuhusiana na  makosa mengi yaliyotendwa na Wakatoliki hata katika mapambano ya kudai uhuru nchini Ugiriki. Ameomba msamaha kutokana na historia ya kashfa ya utengano kwa kutambua kwamba, Mwenyezi Mungu anasamehe daima.

Baba Mtakatifu Francisko anasema, pengine, waamini wanachoka mapema kusamehe. Lakini ni muhimu kwa waamini kuomba msamaha na huruma ya Mungu katika maisha yao. Bila ya msamaha, haki na upatanisho wa kweli, watu wengi wataendelea kupoteza maisha kutokana na vita, kinzani na mipasuko ya kijamii. Baba Mtakatifu ameomba msamaha kwa ajili ya wakimbizi, wahamiaji na wale wanaotafuta hifadhi ya kisiasa. Ameomba msamaha kwa niaba ya Wakatoliki ambao walishikamana na wakaloni kuwanyanyasa na kuwakandamiza ndugu zao. Ameomba msamaha pia kwa ajili ya wakimbizi na wahamiaji wanaopoteza maisha yao kila kukicha kwenye Bahari ya Mederrania. Sinodi ni chombo kilichoanzishwa na Mtakatifu Paulo VI kunako mwaka 1965 kwa ajili ya maisha na utume wa Kanisa, kwa kutaka kuwashirikisha watu wa Mungu katika mchakato wa kupanga, kuamua na kutekeleza mambo msingi katika maisha na utume wa Kanisa, dhana ambayo Baba Mtakatifu anapenda kulihamasisha Kanisa kwa nyakati hizi, kuivalia njuga kama sehemu ya utekelezaji wa maazimio ya Mababa wa Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican. Lengo ni kuliwezesha Kanisa kutembea kwa pamoja katika kuamua, kupanga na kutekeleza sera na mikakati ya Kanisa katika shughuli za kichungaji. Kwa sasa Kanisa Katoliki linaendelea kujielekeza zaidi katika maadhimisho ya Sinodi, ili iweze kuwa ni sehemu ya maisha na utume wake.

Mwezi Oktoba 2021 Jumuiya ya Umoja wa Ulaya ilichapisha Tamko ambalo lilikuwa linahimiza utumiaji wa lugha jumuishi, ili kuimarisha umoja wa usawa katika Jumuiya ya Ulaya. Huu ni usawa ambao unafutilia mbali tofauti za kijinsia na kwamba, ilikuwa ni marufuku kutumia majina ya Kikristo au Sherehe ya Noeli, kwa sababu watu wote si Wakristo na Noeli yenyewe inaadhimishwa kwa tarehe tofauti. Baba Mtakatifu amesema, hizi ni dalili za utawala wa kidikteta. Umefika wakati kwa Jumuiya ya Umoja wa Ulaya kuzingatia vipaumbele vilivyotolewa na waasisi wa Jumuiya ya Umoja wa Ulaya. Waasisi wa Jumuiya ya Umoja wa Ulaya, EU walikazia kwa namna ya pekee zawadi ya maisha ya binadamu na haki zake msingi sanjari na umuhimu wa ujenzi wa umoja, udugu na mshikamano unaosimikwa katika: ukweli na haki; msingi wa sera za kisiasa, kisheria na kijamii Barani Ulaya. Jumuiya ya Ulaya itaweza kudumu na kushamiri, ikiwa kama itaendelea kujikita katika uaminifu kwa mshikamano kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya familia ya Mungu Barani Ulaya badala ya baadhi ya nchi za Ulaya kutaka kujimwambafai, kwani matokeo yake ni mwanzo wa utekelezaji wa ukoloni wa kiitikadi.

Kutaka kufuta Noeli kwenye maisha ya watu wa Mungu Barani Ulaya anasema Baba Mtakatifu Francisko ni kosa la kumbukumbu “Anacronism.” Demokrasia shirikishi ni jambo muhimu sana kwa sabababu inawasaidia watu kufikia lengo la pamoja, kwani binadamu kama kawaida ni kiumbe jamii, ni wapekee lakini pia anawategemea viumbe wengine. Ukiritimba ni hatari sana kwa demokrasia ya kweli. Siasa inapaswa kuwa ni kwa ajili ya ustawi, mafao na maendeleo ya wengi ili kushirikishana na kwamba, maskini na wanyonge ndani ya jamii wanapaswa kupewa kipaumbele cha kwanza, ili wote kwa pamoja waweze kujielekeza kwenda mbele ili kufikia haki jamii. Juhudi zinapaswa kuelekezwa kwa ajili ya ushiriki wa wote. Ili kuweza kukabiliana na changamoto mamboleo. Wanasiasa wanaojitafutia umaarufu usiokuwa na tija wala mashiko ni hatari sana kwa demokrasia, kwani hawa ni wale viongozi wanaojitafutia umaarufu na wakati mwingine kwenda kinyume kabisa cha amali za kijamii na matokeo yake wanageuka kuwa ni madikteta “wakutupwa”. Viongozi wa namna hii hatari kwa sababu wanataka kuendeleza ukoloni katika masuala ya uchumi, utamaduni na masuala ya kijamii na matokeo yake demokrasia inadhoofika sana. Baba Mtakatifu anasema yeye kwa asili si mwana siasa lakini anasema jinsi mambo yalivyo.

Kanisa Katoliki katika sera na mikakati yake kuhusu huduma kwa wakimbizi na wahamiaji linapenda kukazia kwa namna ya pekee umuhimu wa: “Kuwapokea, kuwalinda, kuwaendeleza na kuwahusisha wakimbizi na wahamiaji” katika maisha ya jamii inayowapatia hifadhi. Kwa bahati mbaya sana, leo hii wakimbizi na wahamiaji wamekuwa kama “Mbwa koko”, hawapaswi kuonekana! Wanadhibitiwa kwa kujenga kuta zinazozungukwa kwa nyaya za umeme. Hizi ni siasa za ujenzi wa kuta za utengano. Kwa wale wanaojenga kuta za umeme watambue kwamba wanapoteza maana ya historia ya nchi zao. Kimsingi viongozi  wengi wenye mwelekeo kama huu, wanayo mang’amuzi ya utumwa. Viongozi wanapswa kuongoza nchi zao pamoja na kutambua haki msingi za wakimbizi na wahamiaji. Viongozi wa Jumuiya ya Kimataifa wajipange vyema ili kuweza kukabiliana na changamoto ya wimbi kubwa la wakimbizi na wahamiaji duniani. Cyprus, Ugiriki na Italia zinaelemewa kwa wingi wa wakimbizi. Wakimbizi na wahamiaji wasipoheshimiwa na kuthaminiwa, ni hatari sana kwa ustawi, maendeleo na mafao ya wengi kwa sasa na kwa siku za usoni.

Wakimbizi wapewe nafasi na masomo, fursa za ajira, tiba na ustawi wa jamii, vinginevyo watageuka na kuwa ni wapiganaji na wapambanaji watakaozamisha ustaarabu wa Jumuiya ya Umoja wa Ulaya. Baba Mtakatifu anakaza kusema, kuwapokea, kuwalinda, kuwaendeleza na kuwahusisha wakimbizi na wahamiaji ni mambo msingi yanayopaswa kuzingatiwa, vinginevyo, wakimbizi na wahamiaji hawa watatumbikia kwenye mikono ya wafanyabiashara biashara ya binadamu na viungo vyake watawadhalilisha na kuwakandamiza na hatimaye kuwauza kama bidhaa sokoni. Baba Mtakatifu Francisko tarehe 2 Desemba 2021 aliridhia uamuzi wa Askofu mkuu Michel Aupetit wa Jimbo kuu la Paris, Ufaransa kung’atuka kutoka madarakani kutokana na shutuma za kuwa na mahusiano tenge na mwanamke mmoja, kunako mwaka 2012. Askofu mkuu mstaafu Michel Aupetit anashutumiwa kwamba, kunako mwaka 2012 alimwandikia barua pepe katibu wake muhtasi na hatimaye, wakafanya mapenzi, shutuma ambazo Askofu mkuu mstaafu Michel Aupetit amezikana. Ili kuweza kudumisha amani, utulivu na ustawi wa roho za watu ameamua kung’atuka kutoka madarakani akiwa na umri wa miaka 70 tu.

Baba Mtakatifu Francisko anasema, kila zama inapaswa kupewa tafsiri sahihi bila ya kuchanganya mambo kwa Kanisa na jamii katika ujumla wake. Kesi za nyanyaso za kijinsia zinapaswa kupewa tafsiri sahihi kadiri ya nyakati. Leo hii mambo ni tofauti sana na jinsi yalivyokuwa miaka kadhaa iliyopita. Baba Mtakatifu anasema, anatarajia kukutana na Baraza la Maaskofu Katoliki Ufaransa, bila shaka ataweza kupata wasaa muafaka wa kusikiliza shutuma hizi. Askofu mkuu mstaafu Michel Aupetit alikuwa mdhambi, lakini uamuzi alioufanya ni dhamana kubwa sana kulinganisha na dhambi zake. Watu wote ni wadhambi, kama ilivyokuwa hata kwa Mtakatifu Petro Mtume aliyemkana Kristo Yesu mara tatu, lakini bado akaendelea na dhamana yake ya kuliongoza Kanisa. Pengine, waamini hawajazoea kuongozwa na mdhambi. Baba Mtakatifu anasema, ameridhia uamuzi huu kutokana na shutuma nzito zilizojaa unafiki dhidi ya Askofu mkuu mstaafu na wala si katika Altare ya Ukweli wa mambo.

Baba Mtakatifu kuhusu mchakato wa majadiliano ya kiekumene anasema, hivi karibuni anatarajia kukutana na kuzungumza na Patriaki Cyril wa Moscow na Urussi nzima na kwamba, yuko tayari kwenda nchini Urussi ili kutekeleza azma hii ya kiekumene, ili wote wawe wamoja chini Kristo Yesu mchungaji mkuu. Angependa kukutana na kuzungumza naye ana kwa ana kama ndugu wamoja. Mpasuko wa Kanisa wengine wameurithi na wengine ni sehemu ya historia, kumbe, kuna haja ya kuanza mchakato wa majadiliano ya kiekumene, ili wote waweze kuwa wamoja. Baba Mtakatifu anatambua nia njema ya viongozi wakuu wa Makanisa ya Kiorthodox wanaoendelea kujikita katika majadiliano ya kiekumene yaliyoanzishwa na Mtakatifu Paulo VI pamoja na Patriaki Anathegoras. Itakumbukwa kwamba, kunako tarehe 10 Agosti 1964, akachapisha Waraka wake wa kwanza wa kichungaji, unaojulikana kama "Ecclesiam suam” yaani "Kanisa la Bwana.” Huu ni Waraka unaonesha dira na mwelekeo wa Kanisa katika mapambazuko ya Millenia ya Tatu ya Ukristo, kwa kuzingatia changamoto zilizotolewa na Mababa wa Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican.

Ni katika mwelekeo huu, Mtakatifu Paulo VI akafanya hija ya kitume huko katika Nchi Takatifu ili kukutana na kusali na Patriaki Anathegoras, mwanzo wa mchakato wa majadiliano ya kiekumene kati ya Makanisa. Wanataalimungu wanalisaidia Kanisa kufahamu vyema mchakato wa majadiliano ya kiekumene ili kufikia umoja wa Kanisa. Uinjilishaji mpya unaotekelezwa na Mama Kanisa katika mapambazuko ya Millenia ya tatu ya Ukristo unajikita katika mchakato wa majadiliano ya kiekumene na kidini ili kujenga na kudumisha: utu, heshima, haki msingi za binadamu, ustawi, maendeleo na mafao ya watu wa Mungu katika ujumla wao. Baba Mtakatifu Francisko anakazia uekumene wa: damu, maisha ya kiroho, sala na huduma kwa maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii. Ikumbukwe kwamba, uekumene wa utakatifu wa maisha unafumbatwa katika toba na wongofu wa ndani; kwa kujikana na kujivika fadhila ya unyenyekevu; moyo wa ukarimu na udugu wa kibinadamu; upole, unyoofu, uvumilivu na kutumikia katika upendo bila ya kujibakiza.

Mahojiano
07 December 2021, 17:07