Hija ya Kitume ya Papa Francisko Cyprus Na Ugiriki: Toba Na Wongofu Chemchemi Ya Neema
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.
Baba Mtakatifu Francisko kuanzia Jumamosi tarehe 4 hadi Jumatatu tarehe 6 Desemba 2021 amefanya hija ya kitume nchini Ugiriki kwa kunogeshwa na kauli mbiu “Jiwekeni Wazi Kwa Mshangao wa Mungu.” Baba Mtakatifu Jumapili tarehe 5 Desemba 2021 amesafiri kutoka mjini Athene na kuelekea Kisiwani Lesvos kwenye Kambi ya Kuwapokea na Kuwatambua Wakimbizi na Wahamiaji. Jioni amerejea tena mjini Athene na kuadhimisha Ibada ya Misa takatifu kwenye Ukumbi wa “Megaron Concert Hall mjini Athene.” Ilikuwa ni “Mwaka wa kumi na tano wa kutawala kwake Kaisari Tiberio, Pontio Pilato alipokuwa liwali wa Uyahudi, na Herode mfalme wa Galilaya, na Filipo, ndugu yake, mfalme wa Iturea na nchi ya Trakoniti, na Lisania mfalme wa Abilene, wakati wa ukuhani mkuu wa Anasi na Kayafa, neno la Mungu lilimfikia Yohane, mwana wa Zakaria, jangwani. Akafika nchi yote iliyo karibu na Yordani, akihubiri ubatizo wa toba liletalo ondoleo la dhambi, kama ilivyoandikwa katika chuo cha maneno ya nabii Isaya; Sauti ya mtu aliaye nyikani…” Lk 3: 1-3.
Baba Mtakatifu Francisko katika tafakari yake, Dominika ya Pili ya Kipindi cha Majilio Mwaka C wa Kanisa, aliongozwa na sehemu hii ya Maandiko Matakatifu ambayo ni wito wa kinabii kutoka kwa Yohane Mbatizaji kwa kukazia zaidi dhana ya jangwa katika maisha ya waamini; toba na wongofu wa ndani, kwa kumpatia nafasi Mwenyezi Mungu chemchemi ya matumaini, ili aweze kuganga na kuponya madonda ya mwanadamu na katika ukame wa maisha ya kiroho, aweze kuwanyunyizia baraka ya matumaini. Mwinjili Luka analitambulisha Jangwa kwa namna ya pekee kabisa, huku akijikita katika historia na viongozi wa kisiasa waliokuwepo wakati ule. Lakini, jambo la kushangaza ni kuona kwamba, “Neno la Mungu lilimfikia Yohane, mwana wa Zakaria, jangwani” na wala si kwa viongozi wakuu wa kisiasa waliotajwa na Mwinjili Luka. Huu ndio mshangao wa Mwenyezi Mungu ambaye hafuati kamwe mantiki ya kibinadamu kwa kutoa kipaumbele cha kwanza kwa wenye nguvu na mamlaka na badala yake, Mwenyezi Mungu anawachagua wale walio wadogo na wanyenyekevu wa moyo.
Mwenyezi Mungu anaamua kuanzisha mchakato wa kazi ya ukombozi jangwani na wala si mjini Yerusalemu, Athene wala Roma. Ikumbukwe kwamba, kwa kuwa na madaraka, nguvu, uwezo na umaarufu hapa duniani, si kwamba, kila wakati watu wa namna hii wanampendeza Mwenyezi Mungu. Hatari kubwa kwa viongozi kama hawa kwani wanaweza kujijengea kiburi kiasi hata cha kumweka Mwenyezi Mungu pembezoni mwa vipaumbele vya maisha yao! Ni vyema kuwa mnyenyekevu na maskini wa roho au kama ilivyo kwa maskini jangwani. Inashangaza kuona kwamba, Yohane Mbatizaji aliamua kumwandalia Masiha njia jangwani, mahali penye utupu na mapambano makubwa ya maisha. Lakini ni jangwani ambapo Mwenyezi Mungu anapenda kuwafunulia watu utukufu wake, atakapokuja kuwaokoa watu wake kwa kujifunua jangwani. Rej. Isa 40:3-4. Hata leo hii, Mwenyezi Mungu anawatembelea na kujifunua kwa waja wake katika hali ya ukimya, mateso na mahangaiko makuu, jambo la msingi kwa mwamini ni kuhakikisha kwamba, anamwachia Mwenyezi Mungu nafasi katika moyo wake. Mwenyezi Mungu anapenda kujidhihirisha katika upweke wa nyoyo zao. Mwenyezi Mungu anakuja kuwaonesha ujirani mwema, huruma na mapendo thabiti. Msiogope kwani Mwenyezi Mungu anakuja kuwatembelea.
Yohane Mbatizaji alihubiri Ubatizo wa toba, wongofu wa ndani na maondoleo ya dhambi, huku akikikemea kizazi hiki cha nyoka. Wongofu wa ndani ni tema ambayo haiwafurahishi waamini wengi kwa kuonakena kana kwamba inapinga na furaha ya Injili. Hali inaweza kutokea ikiwa kama toba na wongofu wa ndani vitachukuliwa katika mtazamo wa kimaadili kana kwamba, ni matunda na juhudi zao binafsi. Hapa waamini wanaangalishwa kwamba, wasitegemee nguvu zao peke yao, kwani wanaweza kujikita wakiwa na huzuni katika maisha ya kiroho pamoja na kuchanganyikiwa. Toba na wongofu wa ndani ni muhimu kama sehemu ya mchakato wa kuratibu vilema na mapungu ya kibinadamu. Wema na ubaya ni mapambano endelevu katika maisha ya mwanadamu kama anavyosema Mtakatifu Paulo, Mtume na mwalimu wa Mataifa, kwa sababu ya utawala wa dhambi. Rej. Rum 7:18-19.
Baba Mtakatifu ametumia fursa hii kufafanua maana ya toba na wongofu wa ndani yaani “μετανοεῖν, metanoein.” Yaani kubadili mawazo na kwenda zaidi kwa kubadilisha mtindo wa kufikiri na kutenda kadiri ya vionjo vya mtu binafsi na kwa kudhani kwamba, wanajitosheleza. Huu ndio mwelekeo kwa watu wanaojifungia katika ubinafsi wao katika ugumu, woga na wasiwasi, daima wakisingizia kwamba, wamekuwa wakitenda kama hivi. Jangwa la maisha ya kiroho ni kielelezo cha maeneo ya kifo mahali ambapo hakuna uwepo wa Mungu. Yohane Mbatizaji anatoa wito na mwaliko wa toba na wongofu wa ndani, kwa kutambua ukweli kwamba, Mwenyezi Mungu ni mkuu. Toba na wongofu wa ndani ni mwanzo wa kujikita katika Injili ya matumaini na kwamba, katika maisha, kuna uwezekano wa toba na wongofu wa ndani. Hata katika shida, magumu na vishawishi vya maisha, hata katika muktadha huu, bado Mwenyezi Mungu yupo!
Jambo la msingi anasema Baba Mtakatifu kwa waamini ni kuhakikisha kwamba, wameacha malango ya nyoyo zao wazi, na kuendelea kumtumainia Mwenyezi Mungu muweza wa yote. Yote yanawezekana ikiwa kama Mwenyezi Mungu atapewa kipaumbele cha kwanza. Baba Mtakatifu anawaalika waamini na watu wote wenye mapenzi mema kumwomba Mwenyezi Mungu neema na baraka ya matumaini yanayoboresha imani na kuwasha moto wa mapendo. Walimwengu wana kiu ya matumaini. Kumbe, kuna haja kwa waamini kuwa ni vyombo na mashuhuda wa Injili ya matumaini katika ulimwengu mamboleo. Haya ni matumaini yanayopaswa kupyaishwa kila kukicha, kwani hii ni chemchemi ya neema na baraka za Mungu. Waamini wanapewa mwaliko wa kutubu na kumwongokea Mungu, ili fadhila ya matumaini iweze kuchanua tena na kuzaa matunda.