Baba Mtakatifu Francisko amesikiliza shuhuda za vijana wa kizazi kipya nchini Ugiriki na kuwapatia wosia wake wa kitume ili kuwajenga ujasiri wa matumaini. Baba Mtakatifu Francisko amesikiliza shuhuda za vijana wa kizazi kipya nchini Ugiriki na kuwapatia wosia wake wa kitume ili kuwajenga ujasiri wa matumaini. 

Hija ya Kitume ya Papa Francisko Cyprus na Ugiriki: Ushuhuda Wa Imani ya Vijana

Maadhimisho ya Siku za Vijana ni nyenzo msingi katika mchakato wa safari ya imani inayopaswa kushuhudiwa kama kielelezo cha imani tendaji. Vijana wamemwelezea Baba Mtakatifu Francisko mashaka katika safari ya imani yao ili hatimaye, waweze kuandika historia katika maisha, ingawa inawawia vigumu kutambua huruma na upendo wa Mungu usiokuwa na mipaka kwa binadamu!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko kuanzia Jumamosi tarehe 4 hadi tarehe 6 Desemba 2021 amefanya hija yake 35 ya Kimataifa nchini Ugiriki kwa kunogeshwa na kauli mbiu “Jiwekeni Wazi Kwa Mshangao wa Mungu.” Hii ni sehemu ya ujumbe wa Baba Mtakatifu Francisko kwa maadhimisho ya Siku ya 36 ya Vijana Ulimwenguni. Baba Mtakatifu amehitimisha hija yake ya kitume nchini Ugiriki kwa kukutana na kuzungumza na vijana wa kizazi kipya nchini Ugiriki. Mkutano huu umefanyika kwenye Parokia ya Mtakatifu Dionisi “St. Dionysius School” katika shule inayoendeshwa na kusimamiwa na Shirika la Watawa wa Mtakatifu Ursula huko Maroussi mjini Athene nchini Ugiriki. Idara ya Utume wa Vijana Nchini Ugiriki inapania kuwajengea vijana matumaini ili hatimaye waweze kuwa ni vyombo na mashuhuda wa huruma na upendo wa Mungu kwa jirani zao. Maadhimisho ya Siku za Vijana katika ngazi mbalimbali ni nyenzo msingi katika mchakato wa safari ya imani inayopaswa kushuhudiwa kama kielelezo cha imani tendaji.

Vijana wamemwelezea Baba Mtakatifu Francisko mashaka katika safari ya imani yao kwa kumuuliza maswali yanayogusa ukuu wa Mungu na undani wa maisha ya ujana ili hatimaye, waweze kuandika historia katika maisha, ingawa inawawia vigumu kutambua huruma na upendo wa Mungu usiokuwa na mipaka kwa binadamu! Vijana wanasema, wakati mwingine wanashindwa kutambua uwepo angavu wa Mungu katika maisha yao, lakini kwa njia ya ushirikiano na mshikamano wa udugu wa kibinadamu, leo hii wamepata uzoefu na mang’amuzi mapya na imani imeendelea kuimarika zaidi. Kuna vijana ambao wamekumbana uso kwa uso na majanga ya vita, athari za myumbo wa uchumi kitaifa na Kimataifa, kiasi hata cha kuamua kuhatarisha maisha yao kwa kufanya maamuzi magumu ya kukimbia nchi na familia zao, leo hii wanaweza kusimulia mshangao wa Mungu katika maisha yao.

Mara baada ya shuhuda na hotuba ya Baba Mtakatifu Francisko kwa vijana hawa, walipata nafasi ya kusali, wakimwomba Mwenyezi Mungu kusikiliza sala na kilio chao, wanapopita katika giza na ukosefu wa matumaini; wanapokumbana na majanga katika maisha ili hatimaye, waweze kukua na kukomaa katika upendo kwa Mungu na jirani. Wamesali na kumwomba Mwenyezi Mungu ili aweze kuwajalia kuwa ni mashuhuda na vyombo vya huruma na upendo wake kwa jirani zao. Mwenyezi Mungu awasaidie vijana kupendana, kuheshimiana na kuthaminiana hata katika tofauti zao msingi, tayari kusikiliza na kuupokea Ukweli mfunuliwa ambao ni Kristo Yesu. Vijana wajifunze kushirikiana na kushikamana katika ujenzi wa udugu wa kibinadamu. Kanisa liwasaidie vijana kung’amua wito wao, tayari kuutolea ushuhuda wenye mvuto na mashiko!

Shuhuda za vijana

 

06 December 2021, 15:05